Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

KAMISHNA wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Lyabwene Mtahabwa (Pichani) amesema uwekezaji katika elimu ya awali ni msingi muhimu wa kujenga rasilimali watu bora kwa maendeleo ya Taifa, akibainisha kuwa changamoto kubwa iliyopo nchini ni uelewa mdogo wa jamii kuhusu mahitaji halisi ya mtoto katika umri wa awali.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya elimu ya awali nchini, Dkt. Mtahabwa alisema uzoefu wake wa muda mrefu katika taaluma hiyo umeonesha wazi kuwa hatua za mwanzo za maisha ya mtoto, hususan kuanzia miaka sifuri hadi nane, zina mchango mkubwa katika kumjenga mtoto ambaye baadaye anakuwa rasilimali yenye tija kwa Taifa.

“Nimezeekea katika taaluma ya elimu ya awali na nina Shahada ya Tatu katika fani hiyo. Changamoto kubwa ninayoiona hapa Tanzania, hasa kwa watoto wa elimu ya awali, Darasa la Kwanza na la Pili, ni jamii kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu kile ambacho mtoto anatakiwa kupewa ili baadae awe na faida kubwa kwa Taifa,” alisema Dkt. Mtahabwa.

Alifafanua kuwa utu uzima wa mtu ni matokeo ya malezi, mazingira na elimu aliyopitia akiwa mtoto mdogo, akisisitiza kuwa umri wa miaka 0 hadi 8 ni kipindi nyeti kinachohitaji uangalizi, malezi sahihi na uwekezaji wa makusudi.

Dkt. Mtahabwa alieleza kuwa jitihada za Serikali za kujenga rasilimali watu bora haziwezi kufanikiwa endapo jamii haitatambua umuhimu wa kuwekeza ipasavyo katika maendeleo ya watoto wachanga. Alisisitiza kuwa elimu ya awali si suala la hiari, bali ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa kwa muda mrefu.

Aidha, aliitaka jamii kushirikiana na Serikali na wadau wa elimu kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunza, malezi yenye upendo, lishe bora, afya njema na misingi imara ya maadili tangu wakiwa wadogo.

Alimalizia kwa kusisitiza kuwa dhana ya kujenga rasilimali watu bora inaanza na kujenga rasilimali watoto bora, akihimiza uwekezaji wa dhati katika elimu ya awali kama mkakati wa uhakika wa maendeleo endelevu ya Taifa.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: