Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za makusudi kuimarisha uhuru wa Mahakama ili iweze kutekeleza wajibu wake kikamilifu katika ujenzi wa Taifa na kuchochea ustawi wa maendeleo ya nchi.
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli, jijini Dodoma.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama katika ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, kuimarisha rasilimali watu, kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama na kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi. Alibainisha kuwa jitihada hizo zitahusisha mpango wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo katika kata zote nchini zisizo na Mahakama hizo.
Hata hivyo, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa uhuru wa Mahakama usitumiwe vibaya kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki, akisisitiza kuwa uhuru huo ni dhamana ya kutenda haki kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia Katiba na Sheria za nchi.
Ameeleza kuwa Mahakama ina wajibu mkubwa wa kulinda utawala wa sheria, kusimamia utekelezaji wa mikataba, kulinda rasilimali za Taifa na kuhakikisha maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wote kwa usawa.
Aidha, amesema Mahakama ina mchango muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia kulinda haki na misingi ya Katiba, kutatua migogoro ya kiuchumi, kibiashara na kijamii kwa haraka na haki, pamoja na kujenga imani ya wananchi na wawekezaji katika mfumo wa kisheria wa nchi
Makamu wa Rais ameongeza kuwa Mahakama ina nafasi ya kuzuia migogoro inayoweza kusababisha migawanyiko ya kijamii au kisiasa, kuimarisha uwajibikaji na nidhamu katika utumishi wa umma na sekta binafsi, kuchangia mapambano dhidi ya rushwa na kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa kwa kuwahakikishia ulinzi wa haki zao za kisheria.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewaasa viongozi, wanasiasa, wanaharakati na wananchi kuheshimu tume iliyoundwa na Rais kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, kwa kuacha kuyajadili masuala hayo nje ya mfumo wa kisheria. Kauli hiyo imetolewa kufuatia ombi la Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, aliyeeleza kuwa mijadala hiyo imekuwa ikiathiri wananchi.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa George Masaju, amesema Mahakama inaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi wa utoaji haki. Amesema kwa sasa Mahakama inaandaa mfumo wa kisasa unaotumia Akili Unde (AI) kwa ajili ya kurekodi mwenendo wa mashauri na hukumu mahakamani.
Jaji Mkuu amefafanua kuwa katika mfumo huo, Jaji, Hakimu, Wakili na Shahidi wanapozungumza mahakamani, mfumo huo utatafsiri lugha iliyotumika na kuiandika kwa lugha iliyochaguliwa kwa wakati huo huo. Amesema mfumo huo ukianza kutumika utaondoa ucheleweshaji na changamoto za upotoshaji zinazoweza kujitokeza katika kuchukua kumbukumbu kwa njia ya maandishi ya mkono au kompyuta, hivyo kuongeza ufanisi na uaminifu wa shughuli za Mahakama.










Toa Maoni Yako:
0 comments: