Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

TUME ya Taifa ya Mipango (NPC) imetangaza kukamilika kwa hatua muhimu za maandalizi ya kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sambamba na kuanza utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/2027 kuanzia rasmi Julai 1, 2026.

Akitoa taarifa kwa umma, Katibu Mtendaji wa NPC, Dkt. Fred Msemwa, amesema mipango hiyo imepitia ngazi zote za maamuzi ya Serikali na inatarajiwa kuwasilishwa bungeni tarehe 2 Februari, 2026 jijini Dodoma kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye kupitishwa.

Dkt. Msemwa amesema maandalizi hayo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyefungua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 tarehe 17 Julai, 2025, ikiwa ni dira itakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka 25 kuanzia mwaka wa fedha 2026/2027 hadi 2050/2051.

Kwa mujibu wa NPC, maandalizi makuu matatu ya kuanza utekelezaji wa Dira 2050 yamekamilishwa, yakiwemo kuandikwa kwa Mpango Elekezi wa Muda Mrefu (2026/2027–2050/2051), kukamilika kwa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/2027–2030/2031), pamoja na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/2027.

Aidha, Dkt. Msemwa amesema Tume imeandaa nyenzo mbalimbali zitakazosaidia utekelezaji mzuri wa dira hiyo, ikiwemo Muongozo wa Kitaifa wa Upangaji wa Mipango (National Planning Guideline) utakaosaidia Wizara, Idara, Taasisi za Umma, Mikoa, Halmashauri, Manispaa na Majiji kutafsiri na kutekeleza Dira ya Taifa kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine, NPC imekamilisha maandalizi ya Mfumo wa Kitaifa wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Miradi (National Project Management Information System – NPMIS), unaolenga kuimarisha uwajibikaji, matokeo ya kazi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo kuanzia Julai 2026.

Katibu Mtendaji huyo ametoa wito kwa wananchi na wadau wote kufuatilia kwa karibu uwasilishaji wa mipango hiyo bungeni, akisisitiza kuwa ni fursa muhimu kwa kila Mtanzania kuelewa mustakabali wa Taifa na kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wake.

Alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeandaliwa kwa kuzingatia matumaini ya Watanzania wote, ikisisitiza ustawi wa pamoja, ushiriki wa wananchi katika maendeleo, umoja wa kitaifa na dhamira ya kutomwacha Mtanzania hata mmoja nyuma.

“Ni muhimu kwa kila Mtanzania kuwa na taarifa kamili ya kinachoendelea katika mipango ya maendeleo ya Taifa letu, kwani Dira 2050 ni mwelekeo wa kizazi cha sasa na vijavyo,” amesema Dkt. Msemwa.

Mwisho, NPC imewahimiza Watanzania kushiriki kikamilifu katika kujadili na kufuatilia utekelezaji wa mipango hiyo mikubwa ya maendeleo kwa maslahi ya Taifa na vizazi vijavyo.

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: