ZANZIBAR: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, kufuatia kifo cha Mbunge wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Halima Idd Nassor.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, marehemu Halima Idd Nassor amefariki dunia leo Januari 18, 2026, alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili – Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mazishi ya marehemu yamefanyika leo Januari 18, 2026 katika eneo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Katika salamu zake, Rais Samia ameeleza masikitiko makubwa kwa msiba huo na kusema marehemu alikuwa kiongozi mahiri aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa ujumla, hususan kupitia majukumu yake ya kibunge na ndani ya chama.

Rais pia ametoa pole kwa familia ya marehemu, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), wanachama wa CCM, Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wote walioguswa na msiba huo.

Aidha, Rais Samia amewaomba Watanzania kuendelea kuwa na subira, mshikamano na kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.

Taarifa hiyo imesainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: