Jimbo Kuu la Archdiocese of Dar es Salaam limetoa ratiba kamili ya mazishi ya aliyekuwa Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo hilo, Polycarp Kardinali Pengo, pamoja na maelekezo maalum ya maegesho ya magari ili kuhakikisha ibada zinafanyika kwa utulivu na mpangilio mzuri.
Kwa mujibu wa tangazo rasmi, siku ya Ijumaa Februari 27, 2026, mwili wa marehemu utawasili katika Kanisa Kuu la Mt. Yosefu Cathedral, jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 3:00 asubuhi kwa ajili ya heshima za mwisho hadi alasiri, kabla ya kufanyika Misa ya kumuaga jioni.
Waumini watakaofika kwa magari madogo wataelekezwa kuegesha katika eneo la GSM nyuma ya Shule ya St. Joseph’s Millennium, huku mabasi kutoka mikoani yakielekezwa kuegesha katika viwanja vya Karimjee na Mnazi Mmoja.
Siku ya Jumamosi Februari 28, 2026, ibada ya mazishi itafanyika katika Kituo cha Hija Pugu. Maegesho ya magari yatafanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Pugu, huku magari mengine yakielekezwa katika eneo la Parokia ya Pugu kadiri yatakavyoongozwa na wasimamizi.
Aidha, Kanisa limeeleza kuwa magari binafsi hayataruhusiwa kuingia ndani ya kituo cha hija isipokuwa yale ya viongozi wa Kanisa na Serikali, hatua inayolenga kudhibiti msongamano na kurahisisha usalama wa waumini.
Uongozi wa Kanisa umewahimiza waamini kufuata maelekezo yote yaliyotolewa ili kuhakikisha mazishi ya kiongozi huyo yanaheshimiwa kwa utulivu na mshikamano unaostahili.



Toa Maoni Yako:
0 comments: