Articles by "MAONI YA WASOMAJI"
Showing posts with label MAONI YA WASOMAJI. Show all posts
Napenda kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kugundua kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji Bw. Brighton Kilimba alitoa taarifa za uongo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Magufuli kuwa gari ya wagonjwa ya Kituo cha Afya Ikwiriri haiwezi kutembea kwa sababu ni mbovu na inahitaji matengenezo makubwa.

Nikiwa mtumishi wa Wilaya hii niliumia sana kwa sababu nilikuwa najua ni uongo wa mchana kweupe na niliumia zaidi kwa kuwa aliyekuwa anadanganywa ni Rais wangu ninayempenda Dk. John Pombe Magufuli.

Hata hivyo nilifurahi muda mfupi baadaye nilipomuona kwenye mitandao ya kijamii Bw. Brighton Eliud Kilimba, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji akiwa kwenye pingu na bango linaonesha anatuhumiwa kumdanganya Rais. Nikasema kweli vyombo vya ulinzi na usalama sasa hivi vipo makini na havijalala.

Ukweli ni kwamba gari ya wagonjwa ya Kituo cha Afya Ikwiriri ipo na viongozi waliamua tu kuipaki wakati wananchi wanahangaika kupeleka wagonjwa wao Jijini Dar es Salaam pale wanapohitaji matibabu ya rufaa. 

Gari hilo ni zuri, ni aina ya Toyota Landcruizer namba STL 940, ni gari imara na limekuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi kabla viongozi hawajaamua kulipaki na kuwaacha Wananchi wanahangaika kukodi magari kwa gharama kubwa na wakati mwingine kupanda bodaboda, ni jambo la kusikitisha sana kwa viongozi kutotekeleza wajibu wao kiasi hiki.

Kumbe siku ile Mheshimiwa Rais alipopita Rufiji na kulalamikiwa na wananchi juu ya ukosefu wa gari la wagonjwa, gari lilikuwepo na lilikuwa limetelekezwa katika Kituo cha Afya Ikwiriri likiwa halina tatizo lolote zaidi ya kuhitaji kufanyiwa service ya kawaida ya kubadilishwa oil na pengine kubadili matairi yake.

Kaimu Mkurugenzi Bw. Kilimba alipokuwa anamdanganya Rais kuwa gari ni bovu sana na haliwezi kutembea, Rais kwa machale akaamua kuagiza gari hilo lipelekwe TEMESA mara moja, nikajua hapa siri lazima itafichuka. 

Kwa kuwa gari halikuwa gereji kama Bw. Kilimba alivyosema hadharani, alichofanya Bw. Kilimba ni kupiga simu na kuagiza gari hilo lipelekwe gereji mara moja ili maafisa watakapofuatilia wakute lipo gereji, jamaa wa gereji waliposikia hivyo machale yakawacheza wakakataa kulipokea na ndipo maafisa wakagundua kuwa gari halikuwa gereji ambako Rais aliambiwa na halikuwa bovu kama Rais alivyoambiwa. Ni michezo tu ya viongozi.

Navipongeza sana vyombo vya ulinzi na usalama kwa kugundua mchezo huu, na kisha kumkamata na kumweka ndani Bw. Kilimba ambaye ni Afisa Kilimo wa Wilaya.

Aidha, nampongeza Rais Magufuli kwa hatua alizochukua siku ileile hata kabla hajafika Dar es Salaam kwa kumtumbua Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Bw. Juma Njwayo ambaye ndio alikuwa anaongoza kutoa taarifa za uongo kuhusu ubovu wa magari. Hawa wote ni tatizo kubwa sana hapa Rufiji na yapo mengi ya hovyo wanayafanya, endapo uchunguzi wa kina utafanyika yatabainika vizuri.

Naamini hili litakuwa funzo kwa viongozi wengine kuwajibika ipasavyo katika kuwatumikiwa wananchi kama ambavyo Mheshimiwa Rais Magufuli anasema kila siku, kuwatumikia wanyonge vizuri badala ya kuwaacha wanahangaika wakati Serikali inajitahidi kuhakikisha inapeleka huduma kwa wananchi.

Msimamo wa Mheshimiwa Rais wa kuagiza gari hilo litengenezwe ndani ya wiki 1 na wakati gari linatengenezwa gari la Mkurugenzi ndilo litumike kubeba wagonjwa ni ujumbe tosha kuwa sisi watumishi ni lazima tuweke maslahi ya wananchi mbele na tuwatumikie kama ambavyo tunapaswa kufanya.

Asante Mheshimiwa Rais kwa uongozi wako makini unaojali watu hasa wanyonge.

Ni mimi Mtumishi
Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji.
02 Agosti, 2020.
Nimebahatika kupata fursa kadhaa kukaa na kuzungumza na Mheshimiwa Rais Mstaafu Hayati Benjamin William Mkapa enzi za uhai wake.

Fursa ambayo sitaisahau ni ile ya masaa 10 ya mazungumzo kati yetu alipokuja shambani kwake Turiani Morogoro mwezi Novemba 2014, wakati huo nikiwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero.

Masaa 10 na Rais Mkapa, muda ambao ni nadra sana kwa yeye kumpatia mtu kwa mazungumzo yalinijenga na kunikomaza kiuongozi. Nilipata fursa ya kujifunza mengi kutoka kwake na kupata ufafanuzi juu ya maoni mengi juu yake niliyoyasoma kwenye magazeti. Tulizungumza mambo mengi sana yahusuyo uongozi na hatma ya nchi yetu.

Nilitumia wasaa huo kumuuliza ikiwa anayaona yale aliyoyazungumzia kwenye hotuba zake kabambe ikiwemo ile aliyoitoa kwenye Halmashauri Kuu ya CCM ya Agosti 2004 maarufu kama "Ushupavu wa Uongozi" (The Courage of Leadership); na ile hotuba yake aliyoitoa kwenye Mkutano Mkuu wa 2005 wa kuchagua Mgombea Urais wa CCM zitakidhi matakwa ya siasa za 2015.

Nilitaka pia kujua maoni yake kuhusu mtazamo na hisia juu ya uamuzi wa kuwaondoa wazee (Wenyeviti Wastaafu, Makamu Wenyeviti Wastaafu na Makatibu Wakuu Wastaafu) kwenye Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM. Jibu lake lilikuwa uamuzi ule ulitokana na mapendekezo yao wazee kuomba wapumzishwe kwenye vikao hivyo vya juu vya chama. Sababu zao kubwa zilikuwa mbili. Kwanza, waliona busara kumpatia Rais na Mwenyekiti wa Chama aliyeko madarakani uhuru zaidi wa kuongoza.

Pili, kuondoa dhana iliyokuwa ikijitokeza kila walipopata udhuru na kutohudhuria kuhisiwa na vyombo vya Habari kwamba wamesusia vikao vya Mwenyekiti. Ushauri wao ulikuwa ni kuundwa kwa Baraza la Wazee ili kukidhi dhima yao ya kutoa ushauri. Aidha, uamuzi ule uliwaondoa tu kuwa wajumbe wa kudumu wa vikao vya chama lakini haukuondoa uwezekano wa wao kualikwa kwenye vikao hivyo kwa mwaliko maalum.

Udadisi wangu haukuishia hapo. Nilimuuliza pia mtazamo wake juu ya maoni ya wengi dhidi ya mafanikio ya sera yake ya ubinafsishaji. Alinifurahisha kujua kuwa, amekuwa akisoma na kuona namna ambavyo jambo hilo lilivyopokelewa na wachambuzi mbalimbali.

Kilichomshangaza yeye ni namna ambavyo wapinzani wa sera hiyo ama kwa makusudi au kwa kupitiwa walijikita tu kwenye mifano ya maeneo ambayo ubinafsishaji haukwenda vizuri. Alishangaa kwa nini watu hao hawakutoa pia mifano mizuri ya ubinafsishaji kama ile ya Benki ya NBC iliyozaa Benki ya NMB, Kiwanda cha Sigara (TCC), baadhi ya viwanda vya sukari vinavyofanya vizuri na maeneo mengine. 

Tukiwa bado kwenye eneo hilo, nilimuuliza kwa nini aliamua kubadili noti na sarafu alipoingia madarakani. Jibu lake lilikuwa, uamuzi ule ulilenga kuwashawishi wale waliokuwa wamehodhi fedha majumbani mwao kuzirudisha benki. Kwa maelezo yake, uamuzi ule ulikuwa wa mafanikio kwani fedha iliyorudi benki ambayo ilikuwa nje ya mzunguko ilikuwa ni zaidi ya ile iliyokuwapo katika benki zetu.

Jambo lingine nililotaka kupata mtazamo wake ni ule utamaduni wa kukabidhi kofia ya uenyekiti wa Chama kwa Rais mpya (kuunganisha kofia mbili) kabla ya miezi 24 ya kwanza kuisha, yaani kabla ya Mkutano Mkuu wa Chama kikatiba. Maelezo yake yalikuwa kwamba kipindi hicho ndio muafaka zaidi wakati Rais mpya akiwa bado kwenye fungate ya kisiasa (political honeymoon). 

Baada ya muda huo, Rais huwa ameelemewa na mambo mengi. Nikataka pia kujua kwa nini hapendi kuongea chochote kama mzee mstaafu wakati ambao CCM walipitia mambo mengi kati ya 2008-2014. Jibu lake lilikuwa kwamba silaha nzuri kwa kiongozi mstaafu duniani ni kukaa kimya maana upo mstari mwembamba sana kati ya kushauri na kutoa maoni kwa upande mmoja, na kukosoa na kuingia kwa upande mwingine.

Mazungumzo yetu yaliendelea na kwa kweli sikumpatia wasaa wa kupumzika. Nikataka kujua iweje hakuwahi kumteua Comrade Abdulrahman Kinana katika nafasi yoyote ilihali alikuwa meneja wa kampeni zake za urais mara mbili. Jibu lake lilikuwa alitamani kumteua lakini Ndugu Kinana alimkatalia. Alifanya hivyo tena ilipofufuliwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kumuomba ampendekeze kuwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki jambo ambalo alilikubali. 

Tukaendelea, nikamuuliza, katika siku ya kwanza ya urais wake baada ya kuapishwa na kurejea Ikulu ni jambo gani la kwanza alilolifanya? Akaniambia, alimwandikia mtangulizi wake Rais Ali Hassan Mwinyi barua kwa mwandiko wa mkono wake bila kuichapa, akimshukuru sana kwa mchakato mzima wa kumpata Rais na kuahidi kuendelea kuomba ushauri wake katika kuendesha nchi.

Nilipomdadisi juu ya mtazamo wake kwenye kinyang’anyiro cha urais 2015 kilichokuwa mbele yetu wakati huo hakuwa tayari kufunguka. Pengine ni katika kuishi ile dhana ya kuwa ukistaafu unapaswa kujifunza kukaa kimya. Hata hivyo, nilimchokoza kwa kumtajia majina ya wagombea mbalimbali waliokuwa wakitajwa tajwa wakati huo. Nilimtajia majina 13. Wakati nikimtajia jina alikuwa anaitikia tu kwa kutikisa kichwa. 

Yapo majina ya wagombea ambayo hakuwa akiamini kama kweli watagombea na wapo wale alioshia kutabasamu na wapo ambao waliomsisimua. Utulivu wa mzee Mkapa ulikuwa unafanya kutojua hisia zake, lakini unapogusa mahala anapopapenda uliweza ona hata mishipa ya utosi wake ikifurahi. Nililiona hilo nilipolitaja jina la Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. Ni dhahiri Rais Mkapa alimpenda sana Dkt. Magufuli. Haikuhitajika tochi kuona mapenzi yake kwa Magufuli. Alichozungumza siku hiyo kilibaki funzo na darasa kwangu.

Tulizungumzia zaidi ya masuala ya siasa. Nilipenda pia kufahamu maisha yake nje ya siasa na uongozi. Mmoja wa wasaidizi wa Mzee Mkapa, wakati huo marehemu Mkude ambaye alikuwepo usiku ule hakusita kueleza hisia zake kwangu. Aliniambia kuwa mimi ni mwenye bahati kupata wasaa mrefu vile na Mzee Mkapa. Kuonyesha furaha yangu, nikamwambia kaka Mkude fursa ile itabaki kwenye kumbukumbu za maisha yangu kama Novemba Kuu (The Great November). Marehemu Mkude ndiye aliyenipiga picha na Mzee Mkapa usiku ule Mtaka wa mwezi Novemba baada ya mazungumzo yetu yaliyoanza saa kumi jioni na kumalizika saa saba usiku.

Mbali na mazungumzo yetu, nimekuwa msomaji mzuri wa hotuba zote za Mzee Mkapa alizotoa kila mwisho wa mwezi akiwa madarakani na zile alizotoa katika shughuli mbalimbali za kitaifa na kimataifa. Niliendelea kuwa mtoto na rafiki wa Mzee Mkapa hata nilipohamishiwa Wilaya ya Hai na baadae kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Bado nilipata nafasi ya kuzungumza naye kwa kirefu, japo sikuwahi kuyapata tena masaa 10 kama ilivyotokea Turiani. Mzee Mkapa aliendelea kuwa rafiki yangu, Mwalimu wangu na kila tulipoonana hatukuacha kuzungumza na kwa kweli nilimdodosa na kujifunza mengi.

Leo Mzee Mkapa hayupo nasi. Niseme nini zaidi? Nimempoteza baba, rafiki na mtu aliyependa kuniona nikifanya vizuri kwenye kazi zangu na hasa akinisisitiza kuwasaidia wananchi wanyonge kutoka kwenye umaskini na kuwatatulia shida zao.

Hakika nchi imepoteza mzee mwenye maono, msimamo na mwana mageuzi wa kweli aliyeipenda nchi yake kwa dhati ya moyo wake.

Miaka 10 ya utawala wake alitufikisha mahala pazuri, alijenga taasisi ambazo zitaishi daima mioyoni mwa Watanzania, aliipenda imani ya kanisa lake na kuheshimu imani za watu wengine.

Natoa pole kwa Mama Anna, watoto wake na nampa pole Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumpoteza Kiongozi Mashuhuri kwenye nchi na mlezi wake aliyemuamini na kumpa dhamana ya unaibu waziri akiwa na umri ulio chini ya miaka 40.Nampa pole kiongozi wangu wa zamani Ndugu William Erio, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF ambaye kupitia yeye, Mzee Mkapa alinipenda na kuniamini. Nampa pole nyingi dada yangu Dkt.Ellen Senkoro, Mtendaji Mkuu wa Mkapa Foundation ambaye wakati wote wa shughuli za Mzee Mkapa alipenda kunialika kwenye shughuli za Mzee wangu huyu.

Mwenyezi Mungu ampe pumziko la milele Mzee Mkapa. Hii dunia sisi ni wapitaji. Miaka yetu hakika ni ya kukopeshwa. Pumzika baba yangu, pumzika rafiki yangu, pumzika kiongozi wetu, Tutaonana kwenye ile asubuhi njema na iliyo kuu.

Mwanao
Anthony Mtaka.
Ni wazi Simba kwa sasa inabadilika na kila mchezaji anaonyesha thamani yake.
Kocha anawapa wengi nafasi ili kila mmoja aonyeshe kipaji chake na wanafanya hivyo.

Kikosi kichoanza mechi na Kmc ni wachezaji watatu walioanza mechi na Lipuli ndio walianza.

Hii ina maana pia ni ngumu kwa mpinzani wako kujua unakuja na kikosi gani ili apange mbinu za kukudhibiti.

Kmc walikuja tofauti sana. Walikuja wamekamia na wamedhamiria kupata chochote kwenye mechi ile. Ila mwisho tofauti ya Simba na Kmc ilionekana.

Bado Grayson Fraga alithibitisha waliomlipia nauli kutoka Brazil kuja Tanzania hawakukosea wala hawakutupa hela zao. Ni mchezaji wa kisasa. Hana Mambo mengi na kila analolifanya ni kwa faida ya Timu.

Hutamwona akipiga kanzu au chenga zisizo na sababu. Utamwona anapokonya mpira na haraka mno anaupeleka kinakotakiwa na utafika. Shida anayopata anapenda sana mpira wa kasi Ila wenzie bado hawajafikia kasi yake.

Simba inacheza vizuri mno Ila bado ni taratibu sana. Inatakiwa sasa wakivuka mstari wa katikati kuelekea kwa adui kuwe na kasi zaidi ili kuwachanganya mabeki wa timu pinzani.

Pia inabidi nafasi zinazotengenezwa wazifanyie kazi kuzigeuza magoli kwa pamoja na kufunga magoli mengi nafasi zinazopotea ni nyingi kuliko kuliko zinazokuwa magoli.

Hasan Dilunga ni mchezaji mzuri Ila kwa sasa hayupo kwenye kiwango chake kwa tunaomjua tunajua anaweza kufanya Mara mbili ya anachokifanya sasa. Pamoja na kwamba goli la kwanza lina mchango mkubwa sana kutoka kwake bado tunajua ana kitu cha ziada kuliko anachofanya sasa.

Chama ni Kama anazaliwa upya amejua kwamba yupo timu anapaswa kuendana na ukubwa wa Timu. Taratibu namuona Chama wa msimu uliopita anaanza kurejea. Kahata anathibitisha jicho lililomwona Gor mahia halikukosea.

Kuna watu wanahoji kiwango cha Kager. Kagere ni yule yule na kiwango ni kile kile Ila watu walishakariri kwamba mipira yote mbele lazima apewe Kagere kitu ambacho ilikuwa rahisi tu kwa wapinzani kwamba ukimkaba Kagere basi ni ngumu sana kufungwa goli na Simba na kocha ameliona hilo. Hivyo ametoa majukumu kwa watu wengine nao kutengeneza nafasi na kufunga. Hii inasaidia sana mabeki wote wanapowekeza kwa Kagere wengine wanakuwa huru wanafunga.

Tunakoelekea wapinzani watapata tabu sana kwamba wamkabe nani kwani kila mtu anafunga hii ndio mbinu mpya ya mwalimu na ninaamini kuna baadhi ya mechi ataruhusu Kagere asimame na wanzie wampe mipira afunge na atafunga. Ile Simba ya kuikariri na kujua inakuja kucheza kwa mfumo fulani haipo tena.

Hii ni Simba ya kubadilika kulingana na mechi. Hii ndio tafsiri sahii ya kikosi kipana. Huwezi kujua leo nani anacheza na nani anakaa benchi. Simba sio tena timu ya kugombea ubingwa wa Tanzania bara ni timu inayotakiwa sasa kuanza kutazama mbali. Huu ubingwa wa ligi hata kikosi Cha tatu kinaweza tu kutwaa ubingwa.

Tunaanza sasa kujenga timu ya kushindana Afrika ndani tushamaliza.
( Jicho la tatu la Mgalilaya).
Ndugu zangu,

Wakati huu tunapoungana na ndugu,  jamaa na rafiki zetu waliopoteza wapendwa wao katika ajali ya Moto hapa Morogoro ni vyema tukatambua kuwa :

- Si kila aliyeathirika na ajali hii ya Moto alikuwa anaenda KUIBA mafuta

- Kauli tunazozitoa zinaongeza MAJERAHA kwa waathirika wa ajali walionusurika na wale waliopoteza wapendwa wao

- Waathirika walionusurika wanahitaji FARAJA na MSAADA wetu wa kila namna hivyo shime kila mmoja kwa nafasi yake aone namna anavyoweza kushiriki katika hili jambo la kijamii

Hebu fikiri Mgonjwa mahututi ambaye muda huu yuko ICU na amejikuta akiwa muathirika wa hili kwa kuwa alikuwa akikimbilia KUMNUSURU MTOTO au MTU ambaye aliona ameelemewa na kutokana na kuwa na UHABA wa MAARIFA juu ya UOKOZI katika majanga ya moto akabeba NDOO YA MAJI na kwenda KUSAIDIA kunusuru MOTO usisambae au MTU ANAYEUNGUA apate kunusurika bila ya kujua kuwa MAJI hayafai kuzima Moto kwa kuwa yanaenda kuongeza OXYGEN na kufanya MOTO ukolee zaidi.

Nashauri ndugu zangu wapendwa,  tuweze kuachia kamati zilizoundwa kuchunguza zikafanya kazi zetu huku TUKICHUNGA NDIMI ZETU na kujizuia kutumia MAJANGA kama haya au yanayofanana na haya kujinufaisha ama KISIASA au kwa namna iwayo yoyote ile.

MUNGU aturehemu na kutuongezea maarifa na moyo wa uwajibikaji huku kila mmoja akiona anao wajibu wa KIZALENDO katika KUILINDA na KUIJENGA Nchi yetu pendwa ya TANZANIA.

Amen.

========== ASANTE ===========

Godwin D.  Msigwa
Morogoro
Tanzania
11 Agosti 2019
Tangu jana, nimeshuhudia umimi na ujinga mkubwa unaotaka kutamalaki hapa nchini kwamba akikamatwa mwandishi wa habari ni jambo la ajabu na kelele zinakuwa nyingi.

Baadhi ya Watanzania kama Ngurumo, mhariri aliyeondoka nchini kimkakati kwenda kutusi na kutukana nchi yake akiwa nje utawaona wakibadili hadi lugha ya kuandika kwa kiingereza ili mabwana zao wasome.

Cha ajabu wanahabari wanaopaswa kuwa "neutral" na nguzo ya nne ya utawala katika kazi yao akikamatwa mhasibu, mwalimu, mhandisi n.k kwa makosa yake binafsi au ya kitaaluma, sio habari na hata pale wanapoipa uzito habari hiyo kuwa ni kwa mbaaali ktk kurasa za ndani.

Lakini suala la Kabendera hata wanasiasa wanaharakati utashangaa wakiibuka akina Zitto n.k kusaka kiki kwa kusikika wakisema wameenda polisi kufustilia n.k.

Ushauri wangu tusijenge jamii ya ajabu hivi kwamba wanahabari hawakosei au wakikosea hatua zisichukuliwe. Eboo!

Polisi walisema mapema jana kuwa wanamshikilia hili si kosa kwa sheria zetu za jinai. Bado kelele zikaanza hadi nje ya nchi.

Kisheria, mtu anayeshikiliwa maana yake kuna tuhuma za jinai zinazohitaji ahojiwe na vyombo vinahitaji muda kupata ushahidi wake. Kosa ni lipi mwanahabari mwenye tuhuma akikamatwa kuhojiwa? Mbona hatuwaoni akina Zitto wakienda polisi kuulizia akikamatwa mhasibu, mkulima, na hata mwanachama wa vyama vyao?

Landa niulize kwa sisi tusiokuwa wa taaluma yenu, ninyi wanahabari ni mawakala wa agenda za wanasiasa? Wanawatumia kwa maslahi ya nani?

Nimeshukuru sasa Kamanda Mambosasa kaeleza tuhuma zinazomkabili Kabendera na ameeleza kuwa aliitwa kuhojiwa akagoma.

Hapo sheria zinakosa gani?

Naitwa John Kiligo, Mwanasheria
KAMA mtu ataandaa Tuzo kwa ajili ya taasisi yenye bahati mbaya zaidi hapa nchini kwa sasa, sina shaka taasisi hiyo itakuwa ni Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Na kama tuzo hiyo inatakiwa kushindaniwa na watu; basi mshindi atakuwa kati ya Rais wa TFF, Wallace Karia au Katibu Mkuu, Wilfred Kidao.

Kama kama viatu ambavyo nisingependa kuvivaa kwa sasa, basi vitakuwa ni viatu vya wawili hawa au taasisi hii.

Wao ndiyo viongozi wa kwanza katika muda wa miongo minne hapa Tanzania kufanikisha nchi yetu kushiriki katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2019) yaliyofanyika nchini Misri. Kwa kutumia Kiswahili kinachoeleweka, hawa ndiyo viongozi wa TFF ambao wamefanikisha hili baada ya miaka takribani 40 ya kutafuta fursa hii.

Kwa mtu ambaye hajui nini maana ya miaka 40, anatakiwa kujifunza kuhusu safari ya Waisraeli kutoka utumwani Misri (sadfa nyingine hii) kwenda Kanani.

Baada ya mafanikio hayo ya kujivunia, kuna watu leo wanapendekeza eti uongozi mzima wa TFF ujiuzulu kwa Stars kufanya vibaya kwenye mashindano hayo. Mojawapo
ya mambo yaliyonishangaza zaidi wiki hii ni hili. Tangu lini Watanzania wakaadhibiana kwa kufanya vizuri?

Na mfano unaotumika ni wa Misri. Eti tuige mfano wa Misri ambako kocha na Rais wa ‘TFF’ yao wamejiuzulu baada ya kutolewa na Afrika Kusini. Misri ni mabingwa wa kihistoria wa kombe hili na kwa sababu walikuwa wenyeji, kila mmoja alitaraji wangefanya vema. Hatua waliyochukua huko Misri ilitarajiwa.

Kuna mtu aliamini Tanzania ingetwaa ubingwa wa AFCON? Kuna mtu aliamini tungepenya katika kundi ambalo lilikuwa na timu za Senegal na Algeria? Senegal ilikuwa inapewa nafasi ya kutwaa kombe lakini kocha wao, Aliou Cisse, aliwaambia wanahabari katika mkutano wake wa kwanza walipofika Misri kwamba yeye alidhani Algeria wana nafasi kuliko wao.

Mpira huwa una matokeo ya ajabu na tungeweza kupenya lakini asilimia zaidi ya 80 tulijua kwamba tungeishia raundi ya kwanza tu. Tukaishia raundi ya kwanza hiyohiyo lakini ajabu ni kwamba watu wanadai tatizo ni TFF.

TFF ambayo imeita wachezaji wote waliotakiwa na mwalimu. TFF ambayo ilipeleka kambi ya timu katika nchi ambayo ilipendekezwa na mwalimu wa timu. TFF ambayo imepandisha hadhi ya Taifa kwa kuwaweka wachezaji katika hoteli za hadhi ya juu na hata kuwaongezea posho wachezaji wa timu hiyo?

TFF hii hii ambayo imetoka kufanikisha kufanyika kwa AFCON ya Vijana kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu? TFF hiihii ambayo imerejesha mashindano ya vijana ambayo yalitelekezwa katika miaka ya karibuni?

Ukimuuliza kila mpenda soka, atakwambia msingi wa maendeleo ya mchezo huu upo katika sehemu mbili; kukuza vijana na kufundisha walimu wa kutosha.

Nimemsikiliza Kidao mara nyingi katika mahojiano na waandishi wa habari na amekuwa akisisitiza kwamba sasa wanaelekeza nguvu zao katika maeneo hayo. Sasa hapo kosa la TFF, Karia, Kidao au Kamati ya Utendaji ya TFF ni ipi?

Mojawapo ya tatizo letu kama nchi ni kwamba mara nyingi tumekuwa hatujui tunachotaka. Tukipewa hiki, tunataka kile, tukipewa kile tunataka hiki. Mwaka mmoja uliopita, ungewauliza Watanzania wanataka nini, wangesema angalau tu watoe nuksi ya kwenda kushiriki Misri.

Wallace Karia na TFF yake leo walitakiwa wapongezwe kwa mafanikio yao. Kwenye uchaguzi ujao wa TFF, Karia angeweza kabisa kujitambulisha kama ‘RAIS WA AFCON’ na wenzake kumpa kura za kutosha. Hii ni kwa sababu amefanikisha mfupa uliowashinda wengi.

Wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, TFF ilipewa kila aina ya msaada ikiwamo kulipiwa kocha wa timu ya taifa lakini bado Taifa Stars haikufuzu. Leo hii, TFF inalipa gharama zote yenyewe na bado imefanikisha jambo ambalo hakuna aliyetalitarajia mwaka mmoja tu uliopita.

Mimi ningedhani Watanzania sasa wangejikita kwenye kuishauri TFF kuhusu mapungufu yaliyopo na lipi la kufanya ili sasa tuanze kuwaza kucheza Kombe la Dunia huko mbeleni.

Tushauri, tukosoe lakini tuwape nafasi watu ambao tayari wameweka rekodi na kuonyesha kwamba wanaweza kufanya makubwa zaidi endapo watapewa muda na nafasi ya kufanya waliyoyapanga.

Tuwape nafasi TFF wafanye kazi.

Ezekiel Kamwaga
Dar es Salaam
10 Juni 2019
Nianze kwa kutoa pongezi za dhati kwa Mtandao wa Vodacom Tanzania kwa kuweza kufanikisha zoezi la usajili wa alama za vidole likawa jepesi kwa kuwafuata wateja katika mitaa mbali mbali hapa jijini Dar es Salaam.

Hili jambo nimelishuhudia mwenyewe jinsi vijana wanavyoingia mtaani na kusajili wananchi bila ya kuwatoza pesa yeyote.

Jambo lililonishangaza ni baadhi ya mitandao ya simu za mkononi kuwatoza pesa wananchi pindi wanapotaka kukamilisha usajili wao kwa alama za vidole.

Hili sikubalini nalo nalipinga na ndiyo maana nimeandika waraka huu wa wazi kwa viongozi ili watambue vijana wao wanayoyafanya mtaani.

Inawezekanaje ukamtoza mwananchi Tsh 1,000 kwa mtandao mmoja wa simu alionao??? wakati hili zoezi lilitangazwa na serikali ni bure??? Jambo hili nimelishuhudia baada ya kuwaomba vijana wanisajili walipomaliza nikaambiwa nitoe Tsh 2,000 kwa vile walinisajilia laini zangu mbili nilikataa na wakaanza lalamika nikawambia hili zoezi halipaswi kutozwa mwananchi yeyote, waondoka shingo upande.

Basi niwaombe wahusika wa mitandao ya simu ya Airtel, Tigo na TTCL kuonya vijana waache kutoza pesa ili kuwakamilishia wananchi zoezi la alama za vidole.

Tunaiomba mamlaka husika hasa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kukemea mara moja mchezo unaofanywa na vijana ambao ameona ndiyo njia pekee ya kujipatia pesa.

Ni Mimi Blasio Kachuchu.
Mkazi wa Mbezi Makabe-Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Ijumaa tarehe 7 Juni 2019 aliendelea kudhihirisha kwa vitendo dhana nzima ya maslahi ya taifa kwa nchi yetu.

Kwa wale waliosoma na wanaosoma somo hili la maslahi ya taifa pale Chuo cha Diplomasia Kurasini au Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC) pale Kunduchi hakika watakuwa wamepata ile 'practical side' ya kile walichokisoma.

Ni imani yangu kuwa hata watanzania wengine pia wamenufaika mno na somo lile.

Mjengee picha yule mfanyabiashara ambaye alifanyiwa hila na baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu wa TRA ambaye sasa anatakiwa alipwe fidia ya hasara aliyopata!

Baada ya kumjengea picha huyo, mjengee picha Kilua na mpango wake uliokwama pale Kibaha.

Ni nani kati yetu alikuwa anafikiria kuhusu masharti yaliyowekwa na wachina kwenye ujenzi wa bandari ya Bagamoyo?

Nadhani Rais Magufuli ni mwanafunzi mzuri wa Niccolo Machiavelli.

Niccolo Machiavelli ambaye aliandika vitabu maarufu vya masuala ya maslahi ya taifa kama "The Prince" cha mwaka 1513 ambacho kilikuja kutafsiriwa kwa kingereza mwaka 1532 na "The Discourses" cha mwaka 1517 ambacho kilikuja kutafsiriwa mwaka 1531 kama 'The Discourses on Livy' ni miongoni mwa watu waliokuwa wakihusudiwa sana na hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kudhihirisha hilo, katika moja ya mahojiano yake Baba wa Taifa alipata kusikika akisema: "You want me to tell you what's a book I am reading now?... I'm reading Machiavelli!"

Akimaanisha, 'Unataka nimwambie ni kitabu gani nasoma sasa? Namsoma Machiavelli!'

KWA NINI NINASEMA RAIS MAGUFULI NI MWALIMU MZURI WA SOMO LA MASLAHI YA TAIFA?

Ili kufahamu sababu ni vema kwanza tukafahamu maana ya neno maslahi ya taifa japo kwa uchache.

Niccolo Machiavelli (1513) alitumia neno "Raison d' etat" au kwa Kingereza 'Reason of the State' kuelezea kwa kina namna nchi inavyoweza kufanya lolote liwezekanalo ili kupigania na kulinda maslahi ya taifa kwa kuwa rasilimali za taifa ndiyo sababu ya uhai wa dola.

Rasilimali za taifa zipo nyingi mno, kuna zile zinazoonekana na zisizoonekana kwa mfano bahari, mito, maziwa, milima, mabonde, mbuga, wanyama, ndege, samaki,misitu, mapori, madini, bandari na hata watu wenyewe.

Mimi hapa nitaongezea moja, nalo ni kodi. Kodi linabeba muktadha mpana wa maslahi ya taifa kwa wakati huu.

Hata waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki Profesa Paramagamba Kabudi alisema akiwanukuu waisrael na wamarekani kuwa wao (Marekani na Israel) wanaamini katika mambo mawili, *kuzifia nchi zao na kulipa kodi!*

Tukumbuke pia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusisitiza kwa kusema:

"Taifa lisilolipa kodi ni taifa mfu!"

Kwa nini Baba wa Taifa alisema vile?

Ritchie (2008:7) katika kitabu chake "US Nuclear Weapons Policy After the Cold War" alieleza:

"States constantly struggle for power because with power comes influence and a greater capacity to ensure national security and state survival in an uncertain and anarchic international environment."

Kwa tafsiri yangu:

'Madola hupambana kwa ajili ya nguvu kwa sababu kwa kuwa na nguvu hupelekea kuwa na ushawishi na uwezo mkubwa wa kuhakikisha usalama wa taifa na uhai wa dola katika mazingira ya kimataifa yasiyotabirika na yasiyo na serikali ya dunia.'

Kwa msingi huo kodi ndiyo uhai wa dola na ndiyo hupelekea dola kuwa na nguvu za kiuchumi na ushawishi.

Kutolipa kodi huweza kusababisha taifa kuanguka kama ilivyoanguka Ugiriki.

Rais Magufuli kwa kutambua hili la umuhimu wa kodi kwa uhai wa Dola alikutana na wafanya biashara kutoka wilaya zote 185 za Tanzania na kuwasisitiza kulipa kodi ili dola au nchi iweze kuishi (survive).

Kwa kusisitizia hili Burchill (2005:47) alieleza:

"Primary national interest of nation-states is the pursuit of national security usually defined as physical survival and territorial integrity."

Je Rais Magufuli si mwalimu mzuri wa maslahi ya Taifa?

Lingine linalothibitisha kuwa Rais Magufuli ni mwalimu mzuri wa Maslahi ya Taifa lilionekana kipindi cha mfungo wa mwezi wa Ramadhani.

Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alikuwa mgeni katika Mashindano ya 20 ya usomaji Qur'an Tukufu yaliyofanyika pale uwanja Mkuu wa Taifa (KwaMkapa) Jumapili tarehe 19 May, 2019.

Wapo walioshangaa hatua ya Rais Magufuli kuhudhuria mashindano yale, ni muhimu wafahamu kuwa alichofanya Mheshimiwa Rais kinabeba dhana nzima ya maslahi ya taifa.

Katika kuthibitisha hili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ilijipambanua wazi katika utangulizi, misingi ya Katiba kwamba:

KWA KUWA SISI Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na
amani:

Hivyo kitendo cha Rais kuhudhuria mashindano ya usomaji Quran ni sehemu ya kuimarisha Uhuru, haki, udugu baina ya waislamu na wakristo na kuimarisha amani inayotokana na kuimarika kwa udugu baina ya watanzania.

Kuonesha kuwa suala hili lilibeba sura ya umoja wa kitaifa wasaidizi wengi wa Mheshimiwa Rais nao waliamua kufanya matukio mbalimbali yakiwemo matukio kama hili la kuhudhuria usomaji wa Qur'an na wengine kufuturisha.

Kwa bahati mbaya moja wapo ya matukio ya kufuturisha lilileta taswira tofauti baada ya kiongozi kushika T-shirt iliyokuwa na maelezo ya imani yake huku tukio likiwa linalenga kufanya ibada kwa watu wa imani ya kiislamu.

Jambo hili lilizua mjadala kwa watu wa imani ya kiislamu kwa kuzingatia udugu baina ya watanzania.

Ni muhimu sana mambo kama haya yazingatiwe na yaepukwe ili wasaidizi wa Rais wasimuangushe Mheshimiwa Rais katika kuimarisha Uhuru, haki, udugu na amani ambayo ni maslahi msingi ya taifa kama ilivyoainishwa kwenye Katiba.

Kwa mujibu wa Hans Morgenthau (1951) katika kitabu chake "In Defense of the National Interest" alieleza kuwa, Uhuru, amani, usalama na umoja ni maslahi makuu ya taifa ambayo dola/nchi haiwezi kufanya maridhiano (compromise) ya mbadilishano na dola lingine lolote au taasisi yoyote ile ili kuviachia ama kuhatarisha.

Haya yameelezwa pia katika Sera ya Tanzania ya Mambo ya Nje kwenye msingi na malengo kuanzia ile ya mwaka 1964 iliyotolewa kwa Waraka wa Rais namba 2 na hii mpya iliyotolewa mwaka 2001 zilipoeleza:

Safeguarding the sovereignty, territorial integrity and
political independence of the United Republic of Tanzania;

Defence of freedom, justice, human rights, equality
and democracy

Nina hakika kabisa pia kuwa Rais Magufuli alimsoma Samuel Huntington katika The Clash of Civilization Remaking of World Order cha mwaka 1996 alipoeleza kuwa chanzo kikubwa cha migogoro katika kipindi hiki cha baada ya Vita Baridi (Post Cold War era) ni Utambulisho wa Tamaduni na Dini (Cultural and Religious Identity) ndiyo maana aliona umuhimu mkubwa wa kuhudhuria mashindano yale ili kuimarisha udugu, upendo baina ya waisalamu na wakristo, amani, Uhuru wetu kama watanzania na haki kama ilivyoelezwa kwenye Katiba yetu.

Je Rais Magufuli si mwalimu mzuri wa somo la maslahi ya taifa?

Raia Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ametuthibitishia pia kuwa yeye ni Strategic Negotiator kwa kutazama jinsi serikali yake ilivyoukataa mradi wa ujenzi wa Bandari wa Bagamoyo, mkataba wa Ujenzi wa Reli ya SGR uliokuwa ujengwe na wachina na namna alivyoshawishi bomba la mafuta liweze kujengwa kutoka Hoima, Uganda mpaka Chongoleani, Tanga.

Huu alikuwa mkakati thabiti wa kuifanya Bandari ya Tanga iweze kuketa mapato makubwa hasa kufuatia upanuzi unaoendelea.

Je Rais si strategic negotiator?

Hii sifa ya negotiator ni sifa mojawapo ya balozi, hivyo kuwa kwake mwanadiplomasia namba moja anatudhihirishia umahiri katika hili.

Kuthibitisha haya, Feltan aliainisha sifa 9 za balozi akizigawa katika mafungu mawili ya sifa za kiutendaji (functional skills) na sifa maalumu (special skills):

Kwa muktadha wa maslahi ya taifa nitaeleza sifa moja ambayo ni "cross-cultural skills" yaani ule uweledi wa kufahamu tamaduni mbalimbali.

Mfano mzuri katika hili ni pale Rais alipohudhuria kongamano la usomaji wa Qur'an pale uwanja wa Mzee Mkapa akiwa amevalia Kanzu nzuri sana ambayo binafsi ilinivutia mno na ile baraghashia yake ilivyokaa vema kichwani.

Kwa bahati mbaya sana sina hakika kama wengi wa watendaji waliopewa jukumu la kikatiba la kumsaidia Mheshimiwa Rais (tukiacha Makamu wa Rais na Waziri Mkuu) sijui kama wanamuelewa mheshimiwa Rais, sijui kwa kweli!

Jenga picha ya wale wafanya kazi wa TRA waliozuia mzigo tangu mwaka 2015 ili wapewe rushwa, jenga picha namna wafanyabiashara wanavyolalamika kuhusu kodi na tozo mbalimbali.

Unadhani wanamuelewa Rais anachotaka?

Ukimaliza kujiuliza hilo, jenga picha kile alichokisema Mkurugenzi Mkuu wa TIC bwana Godfrey Mwambe kuhusu "kukanyagana" kwa ofisi,taasisi na watendaji wa serikali kunavyokwamisha juhudi za dhati ya Mheshimiwa Rais za kuiletea maendeleo yatokanayo na viwanda nchi ya Tanzania.

Vipi kuhusu kutotambua misingi ya Katiba ya Uhuru, haki, udugu na umoja wa kitaifa?

Je wanamuelewa kweli!?

Rais Dkt, John Pombe Joseph Magufuli ni Mwalimu mzuri sana wa somo la maslahi ya Taifa, tusimuangushe!

Wenu:

Abbas Mwalimu

+255 719 25 8484

Uwanja wa Diplomasia (Facebook na WhatsApp).
Ameandika Askofu Benson Bagonza (PhD)

Kuna maswali magumu mbele yetu baada ya bunge kupitisha uamuzi wa kihistoria tarehe 2 Aprili 2019.

1. Je, Bunge limepitisha azimio la kutofanya kazi na Prof. Assad au na CAG?

2. Kama ni Prof Assad, basi Bunge bado linaweza kufanya kazi na CAG Assad.

3. Kama Bunge halitafanya kazi na CAG, linamuingiza Rais ktk mgogoro mkubwa wa Kikatiba, kwa sababu:

- Ndani ya siku 7 tangu kupokea Ripoti ya CAG, Rais anatakiwa kuipeleka Ripoti Bungeni iliyofanywa Kazi na CAG ambaye ni Prof. Assad.

4. Asipoileta atakuwa amevunja Katiba ya Nchi aliyoapa kuilinda.

5. Akiileta, atakuwa amelidharau Bunge wakati naye ni sehemu ya Bunge.

6. Akiteua CAG mwingine, huyo mpya hatakagua upya bali ataleta iliyokaguliwa na CAG Prof. Assad ambaye hatakiwi Bungeni.

7. Katiba inatamka kuwa; mchakato wa kumuondoa CAG ni mrefu na iko kimya kuhusu kuendesha mchakato wakati kuna Kaimu CAG.

Ukiwahi kuzaliwa unaona mengi. Ukiwahi kufa unakosa mengi.

Dumisha Uhuru na Umoja.
Kwenye Suala la ulipaji kodi TRA kupitia mashine za kielektroniki wadau wengi walishauri wananchi wapewe hiyo kazi ya ufuatiliaji kama sehemu ya time muone mapato yatakavyopanda.

Ushauri ulikuwa mdogo tu, mtu akipewa risiti ya mkono aipige picha na kuwe na namba za what'sup TRA ambapo atatuma, au namba ya simu.

Kila Wilaya iwe na namba zake. Mfanyabiashara afatiliwe na akitozwa faini basi aliyetoa taarifa apate asilimia yake (Motivation ) tena kupitia simu yake isigeuke kero. Au apate mrejesho nini kimetokea.

Ukitengeneza mfumo mzuri na Kitengo cha ufatiliaji (Carrot and Stick) itakuwa rahisi Sana. Ila Kitengo hicho na taarifa za malalamiko iwe na link huko juu kuhakikisha "Clear monitoring and evaluation".

Ni vizuri TRA ikafanya compliance decentralisation kwenye haya masuala. Wananchi waelewe wanachukua hatua gani wakiona mambo hayaendi vizuri.

Iwe njia nyepesi na rahisi na sio yenye urasimu kama iliyopo. Simu zenyewe ukipiga hazipokelewi.

Kwa sasa tumeona mabadiliko makubwa. Nichukue nafasi mimi kuwapongeza sana watendaji ingawa wanatakiwa kusikiliza maagizo ya Rais Magufuli ambapo ameyatoa kwa uchungu Mkubwa. "There is always a room for improvement"

Mfano Mdogo ni Vitambulisho vya wajasiriamali wadogo wadogo.

Vitambulisho hivyo vimesababisha kujua wafanyabiashara wasio na leseni. Kulikuwa na uhuni mwingi na uzembe wa wafuatiliaji. Watu wanafanya biashara hawana leseni na watendaji wa kata walikuwa wanapiga chao na TRA hivyo hivyo.

Kwa Gairo makusanyo ya mapato kupitia leseni yamepanda sana kwasababu ya Vitambulisho vya Magufuli.

Changamoto ninayoiona ni wafanyabiashara wengi kuimbilia kwenye kitambulisho badala ya leseni. Bila Rais Magufuli kulifumua nani alikuwa anajali?

Lazima mwakani orodha sahihi ya walipa kodi hata kama ni kidogo mtaa kwa mtaa, kitongoji kwa kitongoji, na kijiji kwa Kijiji. Kanzi data hiyo itasaidia nani ni wa kitambulisho na nani ni wa leseni.

Halmashauri, manispaa na majiji wawatumie wataalamu wao kuwaelimisha wafanyabiashara namna bora ya kufanya biashara na Elimu ili wainuke kimapato na kuingia uchumi wa Kati.

Uundwaji wa vikundi mbalimbali vya wafanyabiashara wadogo wadogo ni muhimu sana na utarahisisha compliance.

Mfano umoja wa mama Lishe, wauza Mbogamboga, wenye ma bucha, wachinjaji, madereva wa aina mbalimbali za usafiri n.k

Kwa wenzetu kila mtu ana "social security number" inasaidia kupitia mfumo kuona nini anafanya na Matokeo yake ni kodi aliyolipa. Tuna wachimba madini wengi sana wadogo wadogo, hata hivyo mfumo wao wa kulipa kodi hauko wazi hivyo Serikali inapoteza Pesa. Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko ameleta amsha amsha sasa wachimbaji wanashindana kulipa kodi baada ya masoko ya madini kuanza kufunguliwa.

Huu ni mwanzo mzuri tulione hili kizalendo kabisa na kwa moyo mkunjufu. Hakika TANZANIA sio masikini.

Kauli ya Rais Magufuli kuhusu TRA naiunga mkono kwani ni "naked truth". Wananchi wamepokea kwa furaha kubwa hotuba yake wanasubiri mpango kazi wa utekelezaji.

All the best TRA na Wizara ya Fedha kwa ujumla.

#Gairo Maendeleo Fasta kwa Mwendo Mdundo
*Tanzania na Taifa Stars kwa sasa tunahitaji watu wenye akili kubwa na sio watu maarufu wasio na utashi na maarifa .

Mawazo yangu juu ya Taifa Stars.

Nimefanya kazi National Microfinace Bank –(NMB) na nimefanya kazi Stanbic Bank, nimefanya kazi za Sales and Marketing kuuza maneno matamu kwa bei rahisi na kwa bidhaa ngumu kununulika.

Ni wakati sahihi Tanzania, kuwa na umoja na moyo wa kutoa kwa ajili ya Taifa Stars. Kwa uzoefu wangu wa kufanya kazi taasisi za fedha nimejua kitu kimoja kuhusu pesa. Pesa ukiitunza na wewe inakutunza ili tuitunze Taifa Stars lazima tuweke pesa.

Biblia takatifu ina vifungu 50 vinavyozungumzia pesa. Taifa Stars inahitaji pesa kuweza kuwa na maandalizi mazuri kuanzia trials matches, michuano yenyewe na mishahara ya wachezaji mizuri na posho maridhawa.

Tanzania, na Taifa Stars tunahitaji Simba ambaye ataongoza jeshi la kondoo kwa ubora, weredi na ubunifu na kwa uwazi mkubwa kwenye masuala ya pesa. Tunatakiwa tutumie science ya soccer na kuacha kila mtu kuwa msemaji na mlopokaji wa Taifa Stars.

Kwa takwimu tupo takribani wa Tanzania 57.31 million. Taifa Stars inahitaji Senior Director – Marketing, mwenye elimu bora na maarifa bora.

Taifa stars inahitaji Business manager mwenye maarifa na ubunifu kuifanya Taifa stars kuwa Branda Bora. Tunahitaji idadi ya wa-Tanzania 500,000 ambao watanunua jezi ya Taifa Stars.

Kwa mfano kama jezi ya Taifa Stars inauzwa Tshs 20,000/= kisha washabiki wa Taifa stars Tanzania, kwa idadi ya watu 500,000 wakanunua jezi kwa mwezi mmoja basi TFF watakuwa wameingiza kiasi cha Tsh 10,000,000,000 Bilion hii ni sawa na USD 4,266,158.6689 USD

TFF, yahitajika wawe na na product designer mzuri ambaye atabuni product za kike za Taifa Stars, product za kiume za Taifa Stars, product za watoto wa kike na wa kiume za Taifa Stars na sisi wananchi tunatakiwa kununua bidhaa za Taifa Stars, tuache kuongea tufanye matendo kuisaidia timu ya nchi yetu.

Timu ya taifa ya England ‘’Three Lions’’ wachezaji wanalipwa kama ifuatavyo. Ushindi wa mechi yeyote iwe ya kirafiki au michezo ya kufuzu kila mchezaji analipwa £1500 hii ni sawa na Tshs 4,638,710.72.

Wakitoka sale, kila mchezaji analipwa £1000 ambayo ni sawa na Tsh 3,092,096.14 na kama England akifungwa kila mchezaji analipwa £500 ambayo ni sawa na Tshs 1,545,429.90 yaani mmefungwa na bado mnalipwa pesa.

Kama tukiiga mfumo wa timu ya taifa ya England kuwalipa posho nono wachezaji wetu nafikili kila mchezaji atahitaji kulitumikia taifa lake kwa njia ya soka ili apate pesa nyingi kwa muda mfupi na kutengeneza njaa ya kila kijna kutaka kuchezea Taifa Stars.

Kwa sasa wa-Tanzania tunatakiwa kujitolea kwa machozi jasho na damu kwa ajili ya timu yetu ya Taifa. TFF tengenezeni Point of Sales (P.O.S) Mikoa yote na Wilaya zote na jezi zitolewe kwa idadi ya numbers na codes na ziuzwe kwenye Bank zote zilizopo wilayani na kila anayenunu a akibidhiwe risiiti ya Electronic Fiscal Device (EFD).

Tuzungumze umoja na uzalendo kwa vitendo na tutumia watu wenye weredi na maarifa ya soccer katika kipindi hiki.

Itaendelea sehemu ya pili...

Beberu Benjamini James.
“ This Isn’t Only Simba, It’s Astonishing Simba..!”
- Hii Sio Tu Simba, Ni Simba Ya Kushangaza..!

Ndugu zangu,

Matokeo yale yaliyoushangaza ulimwengu wa soka usiku wa juzi yalinifanya nirudi kwenye maktaba yangu kuona kama ilipata kutokea. Kuiangalia historia. Maana, nimekumbushia mara nyingi, kuwa historia ni Mwalimu Mzuri.

Ni hivi, Simba wale tuliowaona juzi walipata kutokea mwaka 1993. Tuliokuwepo tutakumbuka, Simba ya mwaka ule iliushangaza ulimwengu wa soka.

Mwaka ule Afrika kulikuwa na makombe matatu ya kugombania kwa ngazi ya vilabu; Kombe la Klabu Bingwa, Kombe la CAF na Kombe la Washindi.

Simba ilishiriki Kombe la CAF. Itakumbukwa, muasisi wa kombe lile alikuwa tajiri wa Nigeria, Mashoud Abiola. Huyu alikuwa swahiba wa Jenerali Ibrahim Babangida aliyetawala Nigeria enzi hizo.
Kuna wakati hata kombe lenyewe lilijulikana kama ‘ Kombe la Abiola’.

Simba ilianza mashindano yale kigoigoi. Lakini, cha kushangaza ikawa bora zaidi kwa kila mechi iliyofuata. Kama mwaka huu, kila timu iliyokanyaga Neshno kwa Mkapa ilipigwa. Na ikawa Simba iliyoshinda nyumbani na kukomaa ugenini. Simba ile ya kushangaza ilifika fainali ya Kombe la CAF.

Walivyoanza Simba wa 1993:

Walicheza na Flaviao ya Maputo nyumbani kwenye uwanja wa Kirumba, Mwanza. Wakatokw sare ya 0-0. Simba iliona mapema mapungufu yake. Kubwa kabisa wakandua kuwa Kirumba Stadium haukuwa uwanja wa nyumbani kwa Simba. Ilivyo Simba wako nyumbani wakiwa Neshno Kwa Mkapa. Faida za uwanja wa nyumbani kwa timu ni ile hali ya kuutawala uwanja ndani na nje. Simba hawajapata kuutawala uwanja wa Kirumba, Mwanza. Mechi ya marudiano Maputo Simba walishinda 1-0.

Mechi ya pili wakakutana na Mbabane Highlanders. Ugenini Simba wakashinda 1-0 na nyumbani hivyo hivyo.

Wakaja Al Haraach. Nyumbani Simba wakashinda 3-0 na ugenini wakafungwa 2-0.

Simba mechi iliyofuata wakawaribisha Club Aviacao ya Angola pale Neshno Kwa Mkapa. Aviacao walitisha, simulizi moja ya mjini wakati huo ni ukweli kuwa Aviacao kwenye mechi yao dhidi ya Gor Mahia, walitua Nairobi saa tano asubuhi kwenye siku ya mechi, jioni wakamfunga Gor Mahia.

Club Aviacao ya Angola hawakuamini macho yao walipolala 3-1 pale Neshno Edward Chumila alipachika mawili na Malota Soma ‘ Ball Jagler’ akatupia moja.

Ikaja mechi ya fainali dhidi Stella Abidjan. Simba walipambana ugenini wakatoa sare ya 0-0.

Nyumbani ilihitaji goli moja tu. Mfadhili wa Simba enzi hizo, Azim Dewji, akaahidi kila mchezaji kupewa gari aina ya Canter, mpya, Simba ikibeba kombe.

LAKINI, kuna mchezaji wa Stella Abidjan kila mpenzi wa Simba aliyekuwepo wakati huo hatamsahau, na atawasimulia wanawe. Aliitwa Boli Zozo.

Alipachika magoli mawili pale Neshno Kwa Mkapa na yaliyozima ndoto za Simba.

Mwaka huu 2019 nawaona Simba wa 1993. Wanaweza kuushangaza ulimwengu wa soka na kufuka nusu fainali na hata fainali.

This Is Astonishing Simba!

Maggid Mjengwa.

Whatsapp: 0688 37 36 52