Articles by "HABARI"
Showing posts with label HABARI. Show all posts

  Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Wananchi waliotembelea banda la Wakala wa Vipimo (WMA) katika Maonesho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park, Dodoma, wameeleza kufurahishwa na elimu wanayoipata kuhusu matumizi sahihi ya vipimo na kuahidi kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhakiki vipimo katika shughuli za kila siku.

Siku ya tatu ya maonesho hayo yaliyofunguliwa Juni 16 na yanayotarajiwa kuhitimishwa Juni 23, 2026, banda la WMA limeendelea kuvutia idadi kubwa ya wananchi wanaotaka kujifunza namna Serikali inavyohakikisha vipimo vinavyotumika katika biashara na huduma mbalimbali vinakuwa sahihi na vya kuaminika.

Mmoja wa wananchi hao, Bw. Bilson Vedastus, alisema elimu aliyopata imemsaidia kuelewa mambo muhimu ya kuzingatia anaponunua mafuta, gesi ya kupikia na bidhaa nyingine zinazopimwa.

“Awali sikuwa naelewa mambo haya kwa kina, lakini sasa najua ninachopaswa kuangalia ninapojaza mafuta, kununua sukari au gesi ya kupikia,” alisema.

Kwa upande wake, Bi. Asha Siyaya alisema elimu hiyo imewapa uwezo wa kutambua udanganyifu unaoweza kufanywa kupitia vipimo visivyo sahihi na kuahidi kutoa taarifa pale watakapobaini ukiukwaji.

“Tumeona jinsi pampu za mafuta, mizani na vifaa vingine vinavyohakikiwa ili kuhakikisha vinapima kwa usahihi. Hatuwezi kukaa kimya tukiona mteja anadhulumiwa. Tutawaeleza wengine na kuripoti udanganyifu popote tutakapouona,” alisema.

Wataalamu wa WMA, Albogast Kajungu, Mbwana Amani na Said Ibrahim, waliwaeleza wananchi kuwa huduma za uhakiki wa vipimo zinagusa sekta nyingi zinazohusiana moja kwa moja na maisha ya kila siku ya wananchi.

Walifafanua kuwa pampu za mafuta huhakikiwa na kuwekewa alama za uthibitisho, huku mizani inayotumika sokoni na madukani kupimia bidhaa mbalimbali ikikaguliwa mara kwa mara ili kuhakikisha watumiaji wanapata kiwango stahiki cha bidhaa wanazonunua.

Aidha, mita za maji na umeme zinazotumika majumbani na katika biashara huhakikiwa ili kuhakikisha wateja wanalipia matumizi halisi, huku mitungi ya gesi ya kupikia, bidhaa zilizofungashwa pamoja na mizani za kupimia uzito wa magari barabarani nazo zikiendelea kufanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara.

Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja Mawasiliano wa Wakala wa Vipimo, Bi. Veronica Simba, alisema lengo la WMA ni kuhakikisha kila mwananchi anapata thamani halisi ya fedha anayolipia bidhaa na huduma mbalimbali.

Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutembelea banda la WMA katika maonesho hayo ili kupata elimu zaidi kuhusu haki zao na umuhimu wa matumizi ya vipimo sahihi katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Dar es Salaam, Juni 17, 2026 – Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), imewahimiza waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini kuendelea kuwasilisha kazi zao za kuwania Tuzo za Samia Kalamu 2026 kabla ya kufungwa kwa dirisha la maombi mwishoni mwa mwezi huu.

Taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam imeeleza kuwa hadi Juni 15, 2026, jumla ya kazi 624 zilikuwa zimewasilishwa kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, huku vyombo vya habari mtandaoni vikiongoza kwa idadi kubwa ya kazi zilizowasilishwa.

Takwimu zinaonyesha kuwa vyombo vya habari mtandaoni vimewasilisha kazi 276, sawa na asilimia 44 ya kazi zote zilizopokelewa. Magazeti yamewasilisha kazi 178 (asilimia 29), televisheni kazi 102 (asilimia 16), redio kazi 60 (asilimia 10), huku majarida yakichangia kazi nane pekee, sawa na asilimia moja ya jumla ya mawasilisho.

Waandaaji wa tuzo hizo wameeleza kuwa Samia Kalamu Awards zinalenga kuhamasisha ubora, weledi na uwajibikaji katika uandishi wa habari za maendeleo, kwa kutambua mchango wa wanahabari katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kazi zinazostahili kushindanishwa ni zile zilizochapishwa au kurushwa katika vyombo vya habari kati ya Julai 1, 2025 na Juni 30, 2026.

Aidha, waandishi na taasisi za habari zimekumbushwa kuwa dirisha la kuwasilisha kazi litafungwa rasmi Juni 30, 2026 saa 5:59 usiku, hivyo zinapaswa kutumia muda uliobaki kuhakikisha kazi zao zinawasilishwa kwa wakati kupitia tovuti rasmi ya tuzo hizo.

Tuzo za Samia Kalamu zilianzishwa mwaka 2025 na zimekuwa jukwaa muhimu la kutambua na kuenzi mchango wa waandishi wa habari katika kuendeleza taifa kupitia kaulimbiu ya “Kalamu kwa Maendeleo.”

Kwa mujibu wa waandaaji, waandishi na vyombo vya habari vinakaribishwa kuendelea kushiriki ili kuhamasisha uandishi wenye tija kwa maendeleo ya Tanzania.
Na Mwandishi Wetu.

Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeanza kutoa huduma mbalimbali za ithibati katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma na kutatua changamoto zinazowakabili waandishi wa habari.

Kupitia banda la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, maafisa wa JAB wanaendelea kuhudumia waandishi wa habari na wananchi kwa kutoa elimu kuhusu mchakato wa ithibati, kusaidia usajili kwa waombaji waliokwama kutumia mfumo wa TAI HABARI pamoja na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu Sheria ya Huduma za Habari.
Aidha, waandishi wa habari ambao maombi yao yameidhinishwa wanaendelea kupokea vitambulisho vyao vya ithibati katika maonesho hayo, hatua inayowawezesha kupata huduma kwa haraka bila kulazimika kufika katika ofisi za JAB.

Maafisa wa JAB, Mawazo Kibamba na Happiness Chindiye, wamekuwa wakitoa huduma hizo moja kwa moja kwa wadau wanaotembelea banda hilo, sambamba na kupokea maoni, maswali na changamoto zinazohusu utekelezaji wa mfumo wa ithibati nchini.

Huduma hizo ni sehemu ya jitihada za JAB za kuimarisha uwajibikaji, kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa kuhakikisha waandishi wa habari wanapata msaada kwa wakati, sambamba na kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo "Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu."

Na Mwandishi Wetu

Waandishi wa habari nchini wamehimizwa kuwekeza zaidi katika elimu, mafunzo na kujisomea ili kujenga uwezo wa kufanya uandishi wa uchambuzi unaolenga kuibua hoja za maendeleo na kutoa ukosoaji wa kujenga wenye manufaa kwa jamii.

Wito huo umetolewa tarehe 16 Juni, 2026 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Hello Tanzania kinachorushwa na Uhuru FM, ambapo alisema maendeleo ya sekta ya habari yanahitaji waandishi wenye uwezo wa kuchambua masuala kwa kina na kuyawasilisha kwa usahihi, weledi na uwajibikaji.

Amesema moja ya malengo ya Mpango Mkakati wa miaka mitano wa JAB ni kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari, kuboresha maslahi ya waandishi na kuwajengea uwezo unaowawezesha kushindana kitaaluma na kada nyingine za kitaalamu ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Wakili Kipangula, ili Tanzania iweze kufikia viwango vya kimataifa katika tasnia ya habari ni lazima kuwe na msingi imara wa elimu na mafunzo unaozalisha waandishi wenye uwezo wa kufanya uchambuzi wa kina, kuuliza maswali sahihi na kutoa ukosoaji wenye lengo la kujenga na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Amesisitiza kuwa sheria za nchi zinatoa nafasi ya kukosoa sera, mifumo na utendaji wa taasisi mbalimbali ikiwemo serikali, lakini ukosoaji huo unapaswa kufanyika kwa kuzingatia ukweli, maadili na maslahi ya umma bila kugeuka kuwa matusi, kejeli au vitendo vya kudhalilisha watu.

Kwa upande wake, Mtangazaji wa Uhuru FM, Lilian Madelemo, amesema tangu kuanzishwa kwa JAB, watangazaji wengi wameongeza umakini katika kuzingatia weledi na maadili wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, hatua inayosaidia vyombo vya habari kufanya kazi kwa kujiamini na kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na ukiukwaji wa misingi ya taaluma.
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kikundi cha Vicoba cha Diamond Divas Group, Mhe. Janeth Elias Mahawanga, akizungumza katika semina iliyoandaliwa na kikundi hicho ikihusu elimu ya kifedha na jinsi ya kuwekeza katika mifuko ya uwekezaji iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Katibu wa Kikundi cha Vicoba cha Diamond Divas Group, Bi.Noryne Mmasi, akizungumza katika semina iliyoandaliwa na kikundi hicho ikihusu elimu ya kifedha na jinsi ya kuwekeza katika mifuko ya uwekezaji iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Mkufunzi wa Masuala ya kifedha, uchumi na uwekezaji, Bw. Emilian Busara, akitoa elimu ya fedha na uwekezaji katika semina iliyoandaliwa na Kikundi cha Vicoba cha Diamond Divas Group ikihusu elimu ya kifedha na uwekezaji iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Baadhi ya wanachama wa Kikundi cha Vicoba cha Diamond Divas Group wakisikiliza mada iliyokuwa ikitolewa na Mkufunzi wa Masuala ya kifedha, uchumi na uwekezaji, Bw. Emilian Busara katika semina kuhusu elimu ya kifedha na jinsi ya kuwekeza katika mifuko mbalimbali ya uwekezaji, iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Wanachama wa Kikundi cha Vicoba cha Diamond Divas Group, wakipozi mbele ya wapigapicha mara baada ya kumalizika kwa semina iliyoandaliwa na kikundi hicho kuhusu elimu ya kifedha na jinsi ya kuwekeza katika mifuko mbalimbali ya uwekezaji, iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Na Mwandishi Wetu.

WITO umetolewa kwa wanawake nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji katika mifuko mbalimbali ya uwekezaji, Ili kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na kuliwezesha Taifa kuwa na uchumi shirikishi wa viwanda unaowezeshwa na ushirikishwaji mpana wa huduma za kifedha.

Wito huo umetolewa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake cha Huduma ndogo za kifedha cha Diamond Divas, Mhe. Janeth Elias Mahawanga wakati wa semina kuhusu Uwekezaji wa wanawake katika mifuko ya uwekezaji akisema uwekezaji huo utawasaidia kuongeza Mitaji ya biashara zao hivyo kujiinua kiuchumi.

“Tunapozungumzia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kwa upande wa wanawake, Dira inasema Uchumi wa wananchi mmoja mmoja unakwenda kuongezeka, na Uchumi wa Taifa, lakini pia viwanda vidogo vidogo, Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa na maono ya kuwa na dira ya Taifa, utekeleza wa dira unatutegemea sisi wananchi, sisi wanawake tunataka kuingia moja kwa moja katika utekelezaji wa dira, tunataka kuingia katika uchumi wa viwanda tukawe wawekezaji katika Taifa letu.

“Kupitia semina kama hizi, ili kuwaandaa wanawake kushiriki kikamiifu, ni lazima kuwajengea uwezo kufahamu elimu ya fedha, biashara, fursa mbalimbali na uwekezaji, na ndio maana kwenye elimu hii sisi kama kikundi cha Diamond Divas tunataka kuwa wawekezaji, tunataka kuanzisha viwanda, tuanzishe taasisi yetu ndogo ya fedha, ili tuweze kuyafanya yote haya lazima tujikite zaidi katika elimu ya fedha, biashara, fursa na uwekezaji,” alisema Mhe Janeth.

Akizungumzia nini kifanyike Ili kuongeza kasi ya watanzania hususan wanawake kuwekeza katika mifuko ya uwekezaji na Masoko ya mitaji, Mkufunzi wa Masuala ya kifedha, uchumi na uwekezaji, Bw. Emilian Busara alitaja suala la utoaji wa elimu kuhusu mifuko hiyo kupewa kipaumbele zaidi Ili wanaotaka kuwekeza wachague ni aina gani ya mfuko unawafaa.

“Cha kwanza watanzania wanahitaji elimu ya fedha, bila kuwapa watu elimu, hakuna namna nyingine ambayo watu wanaweza kuijua mifuko ya uwekezaji, jinsi ya kuwekeza na manufaa yake, na la pili ni kuchukua hatua ya kuwekeza, huwezi kujifunza kuendesha baisketi kwa kusoma kwenye vitabu, lakini tatu ni yule anayejua basi amuelimisha mwingine, yakifanyika haya, sina shaka idadi ya watanzania hususan wanawake watakaojiunga na mifuko hii itaongezeka,” alisema Bw. Busara akitoa pongezi kwa kikundi cha Diamond Divas kwa kuonesha njia.

Kwa upande wake, mmoja wa washiriki katika semina hiyo, Bi. Hellen Siria alitoa ushauri kwa wanawake walio katika vikundi vya kuwezeshana katika Jamii kuvirasimisha Ili viweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa ikiwemo fursa za kupata mitaji, mikopo ya aina mbalimbali na fursa nyinginezo zitakazowasaidia kuinua biashara na maisha yao.

“Wito wangu kwa wanawake wenzangu, hasa kwenye vile vikundi vilivyopo katika jamii, tuvirasimishe ili iwe rahisi kunufaika na fursa mbalimbali zinazojitokeza zinazowahusu wanawake wajasiriamali, lakini kilicho muhimu zaidi kwa wanawake tuhakikishe tunajikita katika uwekezaji,” alisema Bi. Hellen.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Mwakilishi wa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga Maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, amesisitiza umuhimu wa vyuo vikuu kuendelea kuimarisha tafiti na ubunifu unaotoa suluhisho kwa changamoto za jamii na kuchochea maendeleo ya taifa yanayoongozwa na maarifa.

Dkt. Nungu aliyasema hayo Juni 11, 2026, katika Ukumbi Mpya wa Maktaba wa UDSM jijini Dar es Salaam, alipomsomea hotuba mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Ignatius Nombo, wakati wa kufunga rasmi Maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya chuo hicho.
Katika hotuba hiyo, ilielezwa kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unategemea uwepo wa mfumo imara wa elimu unaozalisha wataalamu wenye ujuzi, maadili, fikra bunifu na uwezo wa kutumia teknolojia kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii.

 Aidha, hotuba hiyo ilibainisha kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, inasisitiza elimu jumuishi na yenye ubora, matumizi ya TEHAMA, mafunzo kwa vitendo pamoja na ujifunzaji unaozingatia umahiri, hivyo vyuo vikuu vinapaswa kuandaa wahitimu wenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya taifa.
Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu isemayo, "Kuutumia Utajiri wa Madini wa Tanzania kwa Nishati Jadidifu, Mabadiliko ya Kidijitali na Usalama wa Jamii," Dkt. Nungu alisema taasisi za elimu ya juu zina jukumu la kuzalisha watafiti na wabunifu watakaosaidia taifa kujenga uwezo wa ndani katika sekta za sayansi, nishati, teknolojia za kidijitali na usimamizi wa rasilimali.

Aliongeza kuwa ni muhimu tafiti na bunifu zinazozalishwa vyuoni ziwafikie wananchi na sekta za uzalishaji ili ziweze kuchangia moja kwa moja kuboresha maisha ya Watanzania na kuimarisha ushindani wa uchumi wa taifa.
Dkt. Nungu pia aliipongeza UDSM kwa kuendelea kuwa kitovu cha maarifa, utafiti na ushauri wa kitaalamu nchini, huku akiwapongeza washindi wa tuzo mbalimbali zilizotolewa wakati wa maadhimisho hayo kwa mchango wao katika kuendeleza sayansi na ubunifu.

Kwa niaba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, hotuba hiyo iliahidi kuendelea kushirikiana na vyuo vikuu katika kuimarisha elimu ya juu, tafiti na matumizi ya sayansi na teknolojia, kabla ya Dkt. Nungu kutangaza rasmi kufungwa kwa Maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mheshimiwa Balozi Mobhare Matinyi akisalimiana na Mheshimiwa Abdelmadjid Tebboune, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, mara baada ya kukabidhi hati za utambulisho wa kibalozi katika hafla iliyofanyika kwenye Ikulu ya Algiers tarehe 10 Juni, 2026. Katikati ni Mheshimiwa Ahmed Attaf, Waziri wa Mambo wa Nje wa Algeria.
Mheshimiwa Balozi Mobhare Matinyi akizungumza na waandishi wa habari wa Algeria mara baada ya kukabidhi hati zake za utambulisho wa kibalozi kwa Mheshimiwa Abdelmadjid Tebboune, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, katika hafla iliyofanyika kwenye Ikulu ya Algiers tarehe 10 Juni, 2026. Kushoto kwake ni Mwambata wa Ulinzi Kanali Nassoro Kapolo na kushoto kwake ni Afisa wa Ubalozi, Maryam Kilongo.

Na Mwandishi Wetu

Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, amekabidhi hati zake za utambulisho wa kibalozi kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Abdelmadjid Tebboune, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Algiers, Juni 10, 2026, kuashiria kuanza rasmi kwa majukumu yake ya kuiwakilisha Tanzania nchini humo.

Baada ya hafla hiyo, Balozi Matinyi alimfikishia Rais Tebboune salamu na shukrani kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuthamini uhusiano wa kindugu na ushirikiano uliodumu kwa zaidi ya miaka 60 kati ya Tanzania na Algeria.

Akizungumza na waandishi wa habari, Balozi Matinyi alisema mazungumzo yao yalijikita katika namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo, hasa baada ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta za ulinzi na elimu ya juu. Alisema pande hizo mbili zimekubaliana kuweka msukumo mpya katika sekta nyingine zenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya wananchi.

Alitaja maeneo ya kipaumbele yaliyopatiwa msisitizo kuwa ni kilimo, viwanda, utengenezaji wa dawa, nishati, madini na utalii, pamoja na kuendeleza ushirikiano katika sekta za sayansi, teknolojia, utafiti, utamaduni na elimu ili kuimarisha mahusiano baina ya mataifa hayo mawili.

"Nimepewa jukumu na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha ushirikiano wa Tanzania na Algeria unawanufaisha wananchi wa pande zote mbili. Kwa kutumia umahiri wa viongozi wetu, tunaamini tutafanikisha azma hiyo," alisema Balozi Matinyi.

Kwa upande wake, Rais Tebboune alieleza utayari wa Algeria kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo, akibainisha kuwa nchi yake iko tayari kufikia makubaliano mapya kupitia vikao vya pamoja na ziara za viongozi wa ngazi za juu.

Balozi Matinyi anakuwa balozi wa nne wa Tanzania nchini Algeria, akitanguliwa na Balozi Omari Yussuf Mzee, Meja Jenerali Jacob Kingu na Balozi Imani Njalikai. Mbali na Algeria, Ubalozi wa Tanzania uliopo Algiers unahudumia pia nchi za Tunisia, Mauritania, Niger na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahrawi (SADR).
Na Mwandishi Wetu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amewasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27 akisisitiza vipaumbele vitano vya utekelezaji wake.

Akitaja vipaumbele hivyo, amesema mosi ni kuimarisha utawala bora, demokrasia, amani, na utulivu na pili ni kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani na kipaumbele cha tatu ni, kuimarisha uwezo wa watu na maendeleo ya jamii.

Akiendelea kufafanua vipambele hivyo, Mhe. Waziri amesema kipaumbele cha nne ni kuimarisha uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu kwa mabadiliko ya tabianchi na cha tano kikiwa kusimamia utekelezaji wa vichocheo vya mageuzi ambavyo ni pamoja na nishati, miundombinu ya usafiri na usafirishaji, utafiti na maendeleo, na mageuzi ya kidigitali.

Prof Kitila amesesema utekelezaji wa vipaumbele hivyo ni hatua za kuyatekeleza malengo makuu ya Dira 2050, na vimezingatia Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/27 – 2030/31 wenye dhima ya “Mageuzi kwa ajili ya Ukuaji Jumuishi wa Uchumi na Uzalishaji Ajira” ambao ni wa kwanza katika utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/27 – 2050/51.

Aidha katika kutekeleza maeneo ya vipaumbele hivyo, Serikali imepanga kuanza kutekeleza programu na miradi mbalimbali ikiwemo miradi shikizi 38 kati ya 51 iliyopo katika programu saba (7) za kielelezo zilizoainishwa katika Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

Africa Global Logistics (AGL), kupitia kampuni dada ya EALS, imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na Shule ya Sekondari Mabibo kwa kukabidhi madumu 12 ya kuhifadhia taka, vizima moto 3 vya CO2 (kg 9), vizima moto 24 vya ABC (kg 9), pamoja na king'ora kimoja cha tahadhari ya moto kinachotumia mfumo wa mkono. Mchango huu ni sehemu ya dhamira endelevu ya kampuni katika kuimarisha usalama, kuhifadhi mazingira na kuchangia maendeleo ya jamii, kufuatia ujenzi wa miundombinu ya vyoo shuleni hapo mwaka 2025.
Na Mwandishi Wetu

Kampuni ya AGL Tanzania imezindua mpango wa “Plastic-Less” unaolenga kupunguza matumizi ya plastiki zinazotumika mara moja, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kulinda mazingira na kuhamasisha jamii kuzingatia matumizi endelevu ya rasilimali.

Kupitia mpango huo, kampuni imegawa chupa za maji zinazoweza kutumika tena kwa wafanyakazi wake wote na kuweka visambaza maji katika vyumba vya mikutano pamoja na maeneo mbalimbali ya kazi, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa chupa za plastiki zinazotupwa baada ya matumizi.

Kwa wageni wanaotembelea ofisi za kampuni hiyo, AGL imeanza kutumia glasi zinazoweza kuoshwa na kutumika tena badala ya vyombo vya plastiki vya matumizi ya mara moja, ikiwa ni mkakati wa kupunguza uzalishaji wa taka zinazochafua mazingira.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo uliofanyika Juni 5 sambamba na maadhimisho ya juhudi za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Meneja wa Masuala ya Sheria wa AGL, Angeline Mtulia, alisema uendelevu ni sehemu ya utamaduni wa kampuni na wajibu wa pamoja kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

“Kupitia mpango wa ‘Plastic-Less’, tunaonesha kuwa mabadiliko madogo ya tabia yanapoungwa mkono na miundombinu sahihi na ushirikiano wa kijamii yanaweza kuleta matokeo makubwa katika uhifadhi wa mazingira na ustawi wa jamii,” alisema Mtulia.

Katika kuimarisha uelewa wa wafanyakazi, timu ya QHSE kwa kushirikiana na kundi la urejelezaji taka la The Recyclers ilitoa mafunzo kuhusu usimamizi wa taka na athari za matumizi ya plastiki kwa mazingira, huku ikisisitiza umuhimu wa kubadili mtindo wa maisha ili kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Mbali na shughuli za ndani ya kampuni, AGL kupitia kampuni dada ya EALS ilitekeleza programu za uwajibikaji kwa jamii kwa kutembelea Shule ya Sekondari Mabibo na kukabidhi mapipa 12 ya kuhifadhia taka, vizima moto 27 pamoja na king'ora cha tahadhari ya moto kwa lengo la kuimarisha usafi wa mazingira na usalama shuleni.

Wanafunzi wa shule hiyo pia walipatiwa elimu kuhusu madhara ya taka za plastiki, mbinu za kutenganisha taka kwa usahihi na umuhimu wa kuhifadhi mazingira, sambamba na mafunzo ya kujikinga na majanga ya moto.

AGL imesema itaendelea kufuatilia utekelezaji wa mpango huo kwa kupima kiwango cha matumizi ya plastiki kabla na baada ya utekelezaji wake ili kutathmini mafanikio yake katika kupunguza taka na kuchangia uhifadhi wa mazingira.

Kupitia mpango wa “Plastic-Less”, kampuni hiyo imeonesha dhamira ya kuunga mkono Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa kuunganisha uhifadhi wa mazingira, matumizi bora ya rasilimali na maendeleo ya jamii, huku ikijenga utamaduni wa uwajibikaji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa katika picha ya pamoja na Bw. Massad Boulos, mwanadiplomasia na Mshauri Mwandamizi wa Rais Donald Trump kuhusu masuala ya Afrika, nchi za Kiarabu na Mashariki ya Kati, baada ya kufanya mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa Oslo Forum unaofanyika Oslo, Norway.

Mkutano huo, unaofanyika kuanzia tarehe 10 hadi 12 Juni, 2026, umewakutanisha viongozi, wanadiplomasia waandamizi na wadau wa masuala ya amani, diplomasia na usuluhishi kutoka nchi mbalimbali zenye ushawishi duniani.

Na Mwandishi Wetu

Weledi, maadili na uelewa wa sheria kwa waandishi wa habari vimetajwa kuwa nyenzo muhimu katika kulinda haki za wananchi na kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi kuhusu masuala ya kisheria, haki za binadamu na ukatili wa kijinsia.

Hayo yameelezwa na Mjumbe wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Ladislaus Komanya, tarehe 09 Juni 2026 wakati akiwasilisha mada kuhusu "Uhuru wa Vyombo vya Habari katika Enzi ya Kidijiti: Wajibu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari" katika mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria wilayani Tarime, mkoani Mara.

Wakili Komanya amesema uhuru wa vyombo vya habari unaenda sambamba na uwajibikaji wa mwandishi katika kuthibitisha taarifa, kuzingatia maadili ya taaluma na kuheshimu sheria za nchi. 

Ameongeza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na teknolojia za kidijiti kwa kuzingatia weledi na maadili ili kuhakikisha taarifa wanazozitoa zinachangia upatikanaji wa haki, maendeleo ya jamii na ustawi wa wananchi.

"Mwandishi wa habari anapaswa kuzingatia misingi ya taaluma, maadili na sheria ili kuhakikisha taarifa anazozitoa zinachangia upatikanaji wa haki na maendeleo ya jamii," amesema Wakili Komanya.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuthibitisha taarifa kabla ya kuzichapisha au kuzirusha, hususan wanaporipoti masuala yanayohusu sheria, haki za binadamu na makundi maalumu katika jamii. 

Amesema matumizi ya teknolojia za kidijiti yanapaswa kwenda sambamba na uwajibikaji ili kulinda hadhi ya taaluma ya habari na maslahi ya umma.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amesema mafunzo hayo yataongeza tija katika utoaji wa habari za kisheria na kusaidia wananchi kutambua haki zao kupitia vyombo vya habari.

Amesema pia kuwa ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia yanayoripotiwa katika vyombo vya sheria linahitaji ushiriki mkubwa wa waandishi wa habari katika kutoa elimu na taarifa sahihi kwa wananchi ili kusaidia juhudi za kuyatokomeza.

"Endapo mtatumia mafunzo haya kwa ufasaha, yataongeza tija katika kuhabarisha wananchi kuhusu mafanikio ya huduma za msaada wa kisheria pamoja na changamoto zinazojitokeza katika jamii zetu," amesema Gowele.

Kwa upande wake, Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wakili wa Serikali Athumani Msosole, amesema mafunzo hayo yatawawezesha waandishi wa habari kutambua namna bora ya kuripoti masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu, changamoto za kisheria pamoja na hatua zinazochukuliwa na mamlaka mbalimbali katika kutatua matatizo hayo ndani ya jamii.

Msosole amesema uandishi sahihi wa habari za masuala ya sheria una mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao na huduma mbalimbali za msaada wa kisheria zinazotolewa nchini.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Tarime, Jacob Karoli, amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani yatawajengea waandishi wa habari uwezo wa kuandika habari za kisheria kwa usahihi zaidi na hivyo kuongeza manufaa ya habari hizo kwa wananchi.

Jumla ya waandishi wa habari 40 kutoka Wilaya ya Tarime wanashiriki mafunzo hayo yanayolenga kuwawezesha kuwa mabalozi wa elimu ya sheria, haki za binadamu na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.

Na Beda Msimbe, TBN, aliyekuwa Petersburg, Urusi

Ulimwengu wa sasa wa diplomasia ya kijiografia unatawaliwa na ushindani mkubwa wa nguvu za kisiasa na kiuchumi kati ya mataifa makubwa ya Magharibi na yale ya Mashariki. 

Katika mazingira haya, mataifa yanayoendelea mara nyingi hujikuta yakitazamwa kwa darubini ya shaka pale yanapochukua hatua za kimkakati kupanua wigo wa washirika wao wa kimaendeleo. 

Ziara ya hivi karibuni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi, imezua minong'ono na hisia mbalimbali miongoni mwa wachambuzi wa mambo, wengi wao wakihofia kuwa huenda Tanzania sasa inabadili mwelekeo wake wa sera ya mambo ya nje kwa kuitupa mkono Magharibi na kugeukia upande wa Mashariki. 

Hofu hii haina msingi wowote, kwani majibu thabiti na ya kizalendo aliyoyatoa Rais Samia mbele ya waandishi wa habari pembezoni mwa Jukwaa la Kimataifa ya Uchumi la St. Petersburg (SPIEF) nchini Urusi, yanadhihirisha ukomavu wa diplomasia ya Tanzania inayojali maslahi ya taifa kwanza kabisa.

Katika mazungumzo hayo maalum yaliyowashirikisha waandishi wa habari 13 walioambatana naye, akiwemo mwakilishi kutoka Mtandao wa Bloggers Tanzania (TBN), Rais Samia alikuwa wazi na alinyoosha maelezo bila kusita. 

Alifafanua kuwa Tanzania haihamishi nguvu zake kutoka upande mmoja kwenda mwingine, bali inaongeza wigo wa washirika ili kuhakikisha malengo ya maendeleo ya kiuchumi yanatimizwa kwa faida ya wananchi wake. 

Hii ina maana kwamba wale wote wenye hofu au mashaka kuhusu ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na Urusi wanapaswa kuondoa shaka hiyo mara moja, kwani serikali haifuati mtu au upande wowote wa kiitikadi, bali inafuata yeyote mwenye nia njema ya kushirikiana katika kuinua maisha ya Watanzania.

Msimamo huu wa Rais Samia si jambo geni wala la kubahatisha, bali ni muendelezo wa misingi imara ya kihistoria iliyowekwa na Muasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. 

Miaka 57 iliyopita, Mwalimu Nyerere alipotembelea Urusi (wakati huo ikiwa Muungano wa Sovieti), alitamka maneno yaleyale yanayosikika leo kutoka kwa Rais Samia: kwamba Tanzania ni nchi isiyofungamana na upande wowote. Mwalimu alisisitiza kuwa Tanzania itajichanganya na marafiki zake kwa jinsi marafiki hao wanavyotaka kuwa na Tanzania, mradi tu hawataingilia uhuru na mamlaka ya nchi. Falsafa hiyo ya kihistoria ndiyo inayomwongoza Rais Samia hadi leo katika ulimwengu huu unaozidi kuwa na vitovu vingi vya nguvu ya kiuchumi na kiteknolojia.

Sera ya Tanzania ya kutofungamana na upande wowote (Non-Aligned Policy) imekuwa silaha kuu ya kulinda uhuru wa Tanzania wa kufanya maamuzi ya kimkakati. Katika kile kinachoitwa Diplomasia ya Maslahi ya Kitaifa (National-Interest Diplomacy), kigezo kikuu cha kupima ubora wa uhusiano wa kimataifa si itikadi za kisiasa, bali ni mchango gani uhusiano huo unaingiza katika uchumi wa nchi, ajira kwa vijana, na uhamishaji wa teknolojia. 

Rais Samia alifafanua kuwa ziara yake nchini Urusi ilikuja na maombi saba ya kimkakati kutoka Tanzania, na wenyeji wao wa Urusi wakavutiwa kiasi cha kuongeza maombi mengine mawili na kufanya jumla ya maeneo tisa ya ushirikiano. Hii inadhihirisha kuwa pande zote mbili zinazungumza lugha moja inayolenga ustawi wa kiuchumi na maendeleo ya jamii.

Ili kuelewa kwa nini Tanzania inapaswa kuendelea kushirikiana na Urusi pamoja na ulimwengu mzima, ni lazima kuangalia uwiano wa washirika wetu duniani kote. 

Serikali ya Awamu ya Sita haijafunga milango kwa mataifa ya Magharibi; badala yake washirika wetu wa kitamaduni wanaendelea kuwa nguzo muhimu. Kwa mfano, Marekani bado ni mshirika mkubwa sana wa kiuchumi na kibiashara nchini Tanzania, ikiongoza katika kuleta watalii wengi na kuwekeza kupitia kampuni kubwa zaidi ya 500 zilizopo nchini, hususan katika sekta ya madini na uwekezaji mbalimbali wa kimkakati. Vivyo hivyo, mataifa ya Ulaya yameendelea kuwa washirika wakuu katika biashara na utoaji wa misaada pamoja na uwezeshaji wa kifedha. Uhusiano huu wa karibu na Magharibi haujatikisika, na unazidi kuimarika kila uchao.

Wakati huo huo, Tanzania imeendelea kunufaika na uhusiano mkubwa na mataifa ya Asia. China imekuwa mshirika mkuu wa kihistoria na wa sasa katika kuwezesha miradi mikubwa ya miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi, huku India nayo ikiwa miongoni mwa washirika wakubwa wa kibiashara .

Japan haikuachwa nyuma, kwani imeendelea kuwekeza kwa nguvu katika sekta za nishati, elimu, na ujenzi wa miundombinu ya kijamii. Hata mataifa mengine kama Australia, Uingereza, na Ufaransa yamekuwa yakija nchini kwa kasi kupitia mipango mbalimbali kama vile mpango wa Matei wa Ufaransa ili kuwezesha maendeleo ya kiuchumi. 

Kwa mtazamo huu, Urusi inaingia kama mshirika mwingine muhimu wa kimkakati baada ya Tanzania kumaliza changamoto zilizotokana na masharti magumu ya mabadiliko ya kiuchumi ya Benki ya Dunia katika miaka ya 1980, ambayo wakati huo yalilazimu Tanzania kuangalia upande mmoja tu wa mlango.

Ni dhahiri kuwa Diplomasia ya sasa ya Tanzania inatawaliwa na ukomavu na uhuru wa kuchagua. Kama alivyowahi kunukuu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, kuhusu methali maarufu ya kiuchumi: "Tanzania haihitaji kujua rangi ya paka, mradi tu paka huyo ana uwezo wa kukamata panya." 

Maneno haya yana maana kwamba Tanzania haichagui wala haibagui mshirika kwa kuangalia sura au mfumo wake wa kisiasa, bali inaangalia uwezo na utayari wa mshirika huyo kushirikiana nayo katika kutatua changamoto za umaskini na kukuza uchumi. Kila taifa linaloheshimu mamlaka ya Tanzania na liko tayari kuchangia katika ustawi linakaribishwa kwa mikono miwili.

Mkakati huu wa kutafuta washirika wengi kwa wakati mmoja una umuhimu mkubwa sana katika kulinda usalama wa kiuchumi wa Tanzania. Hakika kuweka mayai yote kwenye kikapu kimoja ni hatari kubwa katika ulimwengu wa sasa uliopasuka kutokana na vikwazo vya kiuchumi na migogoro ya kikanda. Kuwa na washirika mbalimbali kunatoa nguvu kubwa ya majadiliano (bargaining power) kwenye meza za kimataifa, kwani hatutegemei chanzo kimoja tu cha mitaji au teknolojia. Kama soko moja likiyumba au kukiwa na mabadiliko ya kisiasa upande mmoja, Tanzania inaweza kuendelea kusonga mbele kwa kutumia milango mingine iliyo wazi.

Kwa kuwa, dira yetu ya maendeleo ya taifa ya 2050 ndiyo dira kuu inayoongoza Tanzania hivi sasa ni vyema kama taifa kutumia diplomasia ya kiuchumi kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, lengo likiwa ni kukuza uchumi kwa kiwango kikubwa na kufikia thamani ya uchumi wa dola bilioni 1,000 (trilioni moja) ifikapo mwishoni mwa utekelezaji wake. 

Ili kufikia lengo hili kubwa la kihistoria, serikali inahitaji mitaji mikubwa, miundombinu ya kisasa, na teknolojia ya hali ya juu kutoka kila kona ya dunia. Tanzania haiwezi kufikia malengo hayo makubwa kwa kujifungia milango au kwa kuchagua upande mmoja wa kidunia. Ndiyo maana Rais Samia anapiga hatua kwa ujasiri, akifungua milango kila mahali—iwe ni Washington, Beijing, Brussels, au Moscow—kuhakikisha kuwa maslahi ya taifa yanalindwa na fursa za kiuchumi zinawafikia wananchi wote.

Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetumia Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu-KiliFair 2026 kutangaza mafanikio ya mpango wa bima ya lazima kwa wasafiri, ikieleza kuwa umeimarisha usalama wa wageni na kuchangia ukuaji wa sekta ya afya pamoja na mapato ya utalii visiwani humo.

Mpango huo ulioanza kutekelezwa rasmi Oktoba 1, 2024, unawataka wageni wote wa kimataifa wanaoingia Zanzibar kuwa na bima ya usafiri kabla ya kuwasili. Tangu kuanzishwa kwake, mpango huo umeendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato, ukiingiza wastani wa dola za Marekani milioni moja, sawa na zaidi ya Sh bilioni 2.6 kila mwezi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) kwenye viwanja vya Magereza jijini Arusha, Ofisa Mauzo wa shirika hilo, Abdul-Halim Muhammad, alisema maonesho hayo yamewapa fursa ya kutoa elimu kwa watalii, wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii kuhusu umuhimu wa bima hiyo.

“Tunashiriki Karibu-KiliFair kuongeza uelewa kuhusu bima hii ya lazima na kueleza namna inavyowanufaisha wageni huku ikichangia maendeleo ya huduma muhimu Zanzibar,” alisema.

Kwa mujibu wa utaratibu huo, wageni wengi wa kimataifa hulipa dola 44 za Marekani kwa kila safari ya kuingia Zanzibar, huku wageni kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakilipia dola 22 pekee. Watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi 17 hulipa dola 22, huku walio chini ya umri huo wakisamehewa.

Muhammad alisema bima hiyo inawawezesha wageni kupata huduma za matibabu ya dharura na msaada mwingine muhimu wanapokuwa Zanzibar, hatua inayopunguza changamoto za kifedha na kuhakikisha wanapata huduma kwa haraka wanapozihitaji.

Alisema sehemu ya mapato yanayokusanywa kupitia mfuko huo hutumika kugharamia huduma za afya kwa wageni waliokatiwa bima, huku fedha zinazobaki zikielekezwa katika kuimarisha huduma za afya kwa wananchi na wageni kwa ujumla.
“Mpango huu ulianzishwa baada ya mamlaka kubaini kuwepo kwa matukio ya mara kwa mara ya watalii na wawekezaji kuhitaji matibabu ya dharura huku kukiwa na sintofahamu kuhusu nani angegharamia huduma hizo. Sasa mfumo huu umeondoa changamoto hiyo,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa KiliFair Promotions, Dominic Shoo, alisema Karibu-KiliFair 2026 imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama maonesho makubwa ya utalii na biashara Afrika Mashariki kwa kuwakutanisha wadau kutoka zaidi ya nchi 40 duniani.

Alisema maonesho hayo yamevutia zaidi ya waoneshaji 500 na wanunuzi wa huduma za utalii wapatao 20,000, hatua inayochochea uwekezaji, ushirikiano wa kibiashara na upanuzi wa masoko ya utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Karibu-KiliFair ni jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania na Afrika Mashariki kimataifa. Kadri wadau wanavyoongezeka kushiriki, ndivyo fursa za biashara, uwekezaji na ukuaji wa sekta ya utalii zinavyozidi kuongezeka,” alisema Shoo.