Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari za mitandaoni kutoka vyama vya Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari (kulia) akizungumza na waandishi wa habari za mitandaoni kutoka vyama vya Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari akifafanua jambo katika kikao kazi na waandishi wa habari za mitandaoni kutoka vyama vya Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari akipokea maoni ya Tanzania Bloggers Network (TBN) kuhusu changamoto za wanachama wake toka kwa, Mwenyekiti wa TBN Taifa, Bw. Beda Msimbe.
Kikao kikiendelea.
Na Mwandishi Wetu.
Dar es Salaam Desemba 18, 2025: Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeahidi kushughulikia changamoto na vikwazo vinavyowakabili waandishi wa habari za mitandaoni na bloga ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, wakati wa kikao kazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam, kikishirikisha TCRA na waandishi wa habari za mitandaoni kutoka Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA).
Bw. Msigwa alisema Serikali iko tayari kufanya marekebisho ya sera na kanuni endapo zitabainika kuwa zimepitwa na wakati au kuwa kikwazo kwa waandishi wa habari za mitandaoni, mradi tu marekebisho hayo yafanywe kwa ushirikiano na kwa kuzingatia maslahi ya taifa.
“Kama kuna sera au taratibu zinaonekana kuwa kikwazo kwa waandishi wa habari za mitandaoni, tunaweza kukaa pamoja tukazipitia na kuzifanyia marekebisho. Lakini ni muhimu nanyi katika kazi zenu mtangulize maslahi ya taifa,” alisema Msigwa.
Alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa waandishi wa habari za mitandaoni, huku akisisitiza kuwa kundi hilo lina wajibu wa kutumia fursa hiyo kwa uzalendo na kulinda maslahi ya nchi.
“Tusitegeane. Haiwezekani Serikali ijenge mazingira mazuri ya kazi halafu ninyi mnatumika kulidhuru taifa. Rais ndiye kiongozi Mkuu wa Serikali anayewaunga mkono, na ndio maana mnaalikwa katika matukio ya Serikali kama wanahabari wengine,” alisema.
Aidha, aliipongeza TCRA kwa kupokea maoni ya waandishi wa habari hao na kuonesha utayari wa kuyafanyia kazi, akibainisha kuwa ada na leseni siyo kikwazo kikubwa kuliko umuhimu wa kazi wanayoifanya kwa taifa.
“Leseni na ada tusiziogope. Ni ulinzi na utambulisho wa kazi zenu. Kinachotakiwa ni kuhakikisha taarifa mnazozitoa zina manufaa kwa taifa letu,” alisisitiza.
Bw. Msigwa alieleza kuwa uwepo wa utaratibu wa kuwatambua waandishi wa habari za mitandaoni ni muhimu ili kulinda taaluma hiyo dhidi ya watu wasiokuwa na sifa, hali inayoweza kudhoofisha tasnia ya habari.
Kutokana na hilo, aliwahimiza waandishi wa habari za mitandaoni na bloga kujisajili katika Bodi ya Ithibati ya Wanahabari Tanzania ili waweze kutambulika rasmi na kunufaika na mafunzo maalum yatakayoratibiwa na Serikali.
“Nawaomba mjisajili kwenye Bodi ya Ithibati ya Wanahabari. Mafunzo yakianza, mtakuwa miongoni mwa wanufaika na mtakuwa bora zaidi katika kazi zenu,” alisema.
Kuhusu malalamiko ya kodi, Bw. Msigwa alisema suala hilo limeshachukuliwa na Serikali, huku akiahidi kuzungumza na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuandaa mazungumzo ya pamoja yatakayolenga kupata muafaka.
“TRA ni taasisi makini na ina maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwezesha sekta mbalimbali kufanya kazi. Ninaamini mtapata suluhu ya changamoto hizi,” alisema.
Aliongeza kuwa kazi za waandishi wa habari zina mchango mkubwa katika kukuza mapato ya taifa kwa kuhamasisha ulipaji kodi, uwekezaji na utalii, akisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa chanya kuhusu usalama na fursa zilizopo nchini.
“Habari zako zinaweza kuhamasisha uwekezaji, utalii na hata kuongeza mapato ya kodi. Waambieni watalii kuwa Tanzania ni nchi salama na iko tayari kuwakaribisha,” alisema.
Pia aliwataka waandishi wa habari za mitandaoni kupuuza taarifa za uzushi na uchochezi zinazolenga kulichafua taifa, akisisitiza kuwa uzalendo ni nguzo muhimu ya maendeleo ya sekta ya habari.
Kwa upande mwingine, Bw. Msigwa alisema Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeanza mchakato wa kuanzisha mfuko wa waandishi wa habari utakaosaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanahabari katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Tumeanza mchakato wa kuanzisha mfuko wa waandishi wa habari. Tuombeeni dua ili ufanikiwe na ufanye kazi kama ulivyokusudiwa. Lazima tuwe wazalendo ili jitihada hizi zifanikiwe,” alisema.








Toa Maoni Yako:
0 comments: