Mkutano huo, unaofanyika kuanzia tarehe 10 hadi 12 Juni, 2026, umewakutanisha viongozi, wanadiplomasia waandamizi na wadau wa masuala ya amani, diplomasia na usuluhishi kutoka nchi mbalimbali zenye ushawishi duniani.
Na Beda Msimbe, TBN, aliyekuwa Petersburg, Urusi
Ulimwengu wa sasa wa diplomasia ya kijiografia unatawaliwa na ushindani mkubwa wa nguvu za kisiasa na kiuchumi kati ya mataifa makubwa ya Magharibi na yale ya Mashariki.
Katika mazingira haya, mataifa yanayoendelea mara nyingi hujikuta yakitazamwa kwa darubini ya shaka pale yanapochukua hatua za kimkakati kupanua wigo wa washirika wao wa kimaendeleo.
Ziara ya hivi karibuni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi, imezua minong'ono na hisia mbalimbali miongoni mwa wachambuzi wa mambo, wengi wao wakihofia kuwa huenda Tanzania sasa inabadili mwelekeo wake wa sera ya mambo ya nje kwa kuitupa mkono Magharibi na kugeukia upande wa Mashariki.
Hofu hii haina msingi wowote, kwani majibu thabiti na ya kizalendo aliyoyatoa Rais Samia mbele ya waandishi wa habari pembezoni mwa Jukwaa la Kimataifa ya Uchumi la St. Petersburg (SPIEF) nchini Urusi, yanadhihirisha ukomavu wa diplomasia ya Tanzania inayojali maslahi ya taifa kwanza kabisa.
Katika mazungumzo hayo maalum yaliyowashirikisha waandishi wa habari 13 walioambatana naye, akiwemo mwakilishi kutoka Mtandao wa Bloggers Tanzania (TBN), Rais Samia alikuwa wazi na alinyoosha maelezo bila kusita.
Alifafanua kuwa Tanzania haihamishi nguvu zake kutoka upande mmoja kwenda mwingine, bali inaongeza wigo wa washirika ili kuhakikisha malengo ya maendeleo ya kiuchumi yanatimizwa kwa faida ya wananchi wake.
Hii ina maana kwamba wale wote wenye hofu au mashaka kuhusu ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na Urusi wanapaswa kuondoa shaka hiyo mara moja, kwani serikali haifuati mtu au upande wowote wa kiitikadi, bali inafuata yeyote mwenye nia njema ya kushirikiana katika kuinua maisha ya Watanzania.
Msimamo huu wa Rais Samia si jambo geni wala la kubahatisha, bali ni muendelezo wa misingi imara ya kihistoria iliyowekwa na Muasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Miaka 57 iliyopita, Mwalimu Nyerere alipotembelea Urusi (wakati huo ikiwa Muungano wa Sovieti), alitamka maneno yaleyale yanayosikika leo kutoka kwa Rais Samia: kwamba Tanzania ni nchi isiyofungamana na upande wowote. Mwalimu alisisitiza kuwa Tanzania itajichanganya na marafiki zake kwa jinsi marafiki hao wanavyotaka kuwa na Tanzania, mradi tu hawataingilia uhuru na mamlaka ya nchi. Falsafa hiyo ya kihistoria ndiyo inayomwongoza Rais Samia hadi leo katika ulimwengu huu unaozidi kuwa na vitovu vingi vya nguvu ya kiuchumi na kiteknolojia.
Sera ya Tanzania ya kutofungamana na upande wowote (Non-Aligned Policy) imekuwa silaha kuu ya kulinda uhuru wa Tanzania wa kufanya maamuzi ya kimkakati. Katika kile kinachoitwa Diplomasia ya Maslahi ya Kitaifa (National-Interest Diplomacy), kigezo kikuu cha kupima ubora wa uhusiano wa kimataifa si itikadi za kisiasa, bali ni mchango gani uhusiano huo unaingiza katika uchumi wa nchi, ajira kwa vijana, na uhamishaji wa teknolojia.
Rais Samia alifafanua kuwa ziara yake nchini Urusi ilikuja na maombi saba ya kimkakati kutoka Tanzania, na wenyeji wao wa Urusi wakavutiwa kiasi cha kuongeza maombi mengine mawili na kufanya jumla ya maeneo tisa ya ushirikiano. Hii inadhihirisha kuwa pande zote mbili zinazungumza lugha moja inayolenga ustawi wa kiuchumi na maendeleo ya jamii.
Ili kuelewa kwa nini Tanzania inapaswa kuendelea kushirikiana na Urusi pamoja na ulimwengu mzima, ni lazima kuangalia uwiano wa washirika wetu duniani kote.
Serikali ya Awamu ya Sita haijafunga milango kwa mataifa ya Magharibi; badala yake washirika wetu wa kitamaduni wanaendelea kuwa nguzo muhimu. Kwa mfano, Marekani bado ni mshirika mkubwa sana wa kiuchumi na kibiashara nchini Tanzania, ikiongoza katika kuleta watalii wengi na kuwekeza kupitia kampuni kubwa zaidi ya 500 zilizopo nchini, hususan katika sekta ya madini na uwekezaji mbalimbali wa kimkakati. Vivyo hivyo, mataifa ya Ulaya yameendelea kuwa washirika wakuu katika biashara na utoaji wa misaada pamoja na uwezeshaji wa kifedha. Uhusiano huu wa karibu na Magharibi haujatikisika, na unazidi kuimarika kila uchao.
Wakati huo huo, Tanzania imeendelea kunufaika na uhusiano mkubwa na mataifa ya Asia. China imekuwa mshirika mkuu wa kihistoria na wa sasa katika kuwezesha miradi mikubwa ya miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi, huku India nayo ikiwa miongoni mwa washirika wakubwa wa kibiashara .
Japan haikuachwa nyuma, kwani imeendelea kuwekeza kwa nguvu katika sekta za nishati, elimu, na ujenzi wa miundombinu ya kijamii. Hata mataifa mengine kama Australia, Uingereza, na Ufaransa yamekuwa yakija nchini kwa kasi kupitia mipango mbalimbali kama vile mpango wa Matei wa Ufaransa ili kuwezesha maendeleo ya kiuchumi.
Kwa mtazamo huu, Urusi inaingia kama mshirika mwingine muhimu wa kimkakati baada ya Tanzania kumaliza changamoto zilizotokana na masharti magumu ya mabadiliko ya kiuchumi ya Benki ya Dunia katika miaka ya 1980, ambayo wakati huo yalilazimu Tanzania kuangalia upande mmoja tu wa mlango.
Ni dhahiri kuwa Diplomasia ya sasa ya Tanzania inatawaliwa na ukomavu na uhuru wa kuchagua. Kama alivyowahi kunukuu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, kuhusu methali maarufu ya kiuchumi: "Tanzania haihitaji kujua rangi ya paka, mradi tu paka huyo ana uwezo wa kukamata panya."
Maneno haya yana maana kwamba Tanzania haichagui wala haibagui mshirika kwa kuangalia sura au mfumo wake wa kisiasa, bali inaangalia uwezo na utayari wa mshirika huyo kushirikiana nayo katika kutatua changamoto za umaskini na kukuza uchumi. Kila taifa linaloheshimu mamlaka ya Tanzania na liko tayari kuchangia katika ustawi linakaribishwa kwa mikono miwili.
Mkakati huu wa kutafuta washirika wengi kwa wakati mmoja una umuhimu mkubwa sana katika kulinda usalama wa kiuchumi wa Tanzania. Hakika kuweka mayai yote kwenye kikapu kimoja ni hatari kubwa katika ulimwengu wa sasa uliopasuka kutokana na vikwazo vya kiuchumi na migogoro ya kikanda. Kuwa na washirika mbalimbali kunatoa nguvu kubwa ya majadiliano (bargaining power) kwenye meza za kimataifa, kwani hatutegemei chanzo kimoja tu cha mitaji au teknolojia. Kama soko moja likiyumba au kukiwa na mabadiliko ya kisiasa upande mmoja, Tanzania inaweza kuendelea kusonga mbele kwa kutumia milango mingine iliyo wazi.
Kwa kuwa, dira yetu ya maendeleo ya taifa ya 2050 ndiyo dira kuu inayoongoza Tanzania hivi sasa ni vyema kama taifa kutumia diplomasia ya kiuchumi kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, lengo likiwa ni kukuza uchumi kwa kiwango kikubwa na kufikia thamani ya uchumi wa dola bilioni 1,000 (trilioni moja) ifikapo mwishoni mwa utekelezaji wake.
Ili kufikia lengo hili kubwa la kihistoria, serikali inahitaji mitaji mikubwa, miundombinu ya kisasa, na teknolojia ya hali ya juu kutoka kila kona ya dunia. Tanzania haiwezi kufikia malengo hayo makubwa kwa kujifungia milango au kwa kuchagua upande mmoja wa kidunia. Ndiyo maana Rais Samia anapiga hatua kwa ujasiri, akifungua milango kila mahali—iwe ni Washington, Beijing, Brussels, au Moscow—kuhakikisha kuwa maslahi ya taifa yanalindwa na fursa za kiuchumi zinawafikia wananchi wote.
Kwa miaka mingi, chapa nyingi nchini Tanzania zipo kila mahali lakini ni ngumu mtu kuzikumbuka. Nembo kubwa jukwaani, DJ’s maarufu, vinywaji kwa bei nafuu, na watengeneza maudhui wa mitandoni wakituma video zisizofikisha ujumbe kamili kwenye mitandao ya kijamii ( Instagram). Baada ya hapo, kila mtu anarudi nyumbani kwake, hadi kufikia jumatatu tukio lote limesahaulika.
Huo umekuwa ni ukweli mchungu kwa chapa nyingi zaidi barani Afrika. Kampuni inatumia fedha nyingi zaidi kujitangaza, lakini hushidwa kuacha historia isiyofutika kwa wateja na walaji wake. Kibaya zaidi, walaji nao wamegundua hilo.
Siku hizi, watumiaji wana ladha tofouti. Hawavutiwi tena na uwepo wa chapa ya kampuni peke yake, bali ubunifu uliopo nyuma ya uwepo wa chapa hiyo.
Ndiyo maana, tukio walilolifanya Heineken hivi karibuni la Kuonesha fainali za ligi ya Mabingwa barani Ulaya limeacha historia ya kipekee. Tukio hilo liliibua gumzo kitaifa, sio kwa sababu ya mpira wa miguu tu, bali ni kwa sababu ilionesha kiwango kikubwa cha fursa ambazo bado watu wengi hawajazijua katika kubadilisha namna tunavyotengeneza burudani kwa watumiaji wetu nchini Tanzania.
Kwa usiku mmoja watanzania walipewa burudani kubwa yenye hadhi ya Kimataifa, yenye mvuto wa kisasa na mazingira yaliyobuniwa kwa hali ya juu na kukosha mioyo ya walaji wengi. Muonekano wa eneo lenyewe ilikuwa ni kivutio tosha. Makontena yaligeuka kuwa chanzo cha kivutio, ubunifu wa njia za juu uliwashangaza maelfu ya watu waliohudhuria. Skrini kubwa ilitawala na kufananisha uwoneshaji wa fainali hizo na tamasha kubwa la muziki kimataifa.
Watu hawakuhudhuria tu bali walishiriki historia.
Tofouti hiyo ni muhimu sana, kwa sababu inawafanya walaji kujisikia umuhimu sana kuwepo katika tukio hilo kubwa. Kwa sababu hiyo itabaki kama historia kwenye maisha yao na sehemu ya utambulisho wao. Watu wanapenda kushiriki matukio yanaoakisi utu wao wa ndani, na mtindo wa maisha wanaoutamani.
Hali hii inaonekana zaidi kwa vijana wa mijini ambao sasa wanaishi katika ulimwengu uliounganishwa kidijitali. Wanatazama maisha ya usiku ya Lagos kupitia TikTok. Wanafuatilia tamasha za Amsterdam au London kupitia Instagram. Kila siku wanakutana na viwango vya kimataifa vya ubunifu na mandhari ya kisasa. Matarajio yao yamebadilika sana zaidi ya chapa za kampuni nyingi walipofikia.
Hata hivyo kuna Chapa za Kampuni nyingi zaidi bado zinafanya kazi zikiwa na maono ya 2015. Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na dhana ya kwamba walaji wengi wa Afrika Mashiriki hawaitaji utekelezaji wa kiwango cha Kimataifa. Ndio maana wanafanya uzalishaji mdogo, ubunifu mdogo, miundombinu ya kawaida na sauti zisizoridhisha. Nembo za chapa ya kampuni kila mahali bila kuwa na hadithi ya kusimulia. Kauli yao maarufu huwa ni kuwa “hiki kinatosha kwa soko letu”
.Lakini, pengine soko halikuwa tatizo hata siku moja, huenda tatizo lilikuwa ni ukosefu wa Ubunifu.
Kwa sababu mwitikio ulioonekana siku ile ulithibisha jambo moja muhimu ambalo ni wananchi wana kiu na ubunifu wa viwango, wanataka vitu vipya, muonekano unaovutia na mradi utekelezwe kwa viwango vinavyohitajika.
Mitandao ya kijamii ililipuka kwa maudhui ya video. Video za drone zilisambaa kila mahali. Watu hawakushiriki tu mechi yenyewe, bali walionyesha mazingira, usanifu wa eneo, nguvu ya umati na ukubwa wa tukio. Hata watu ambao hawakuwa mashabiki wakubwa wa mpira walitamani kuhudhuria kwa sababu mazingira yenyewe yalikuwa kivutio cha kitamaduni.
Hilo linapaswa kuwafanya wataalamu wa masoko wengi kutafakari! Kwa sababu linaashiria mabadiliko makubwa katika namna walaji wanavyohusiana na chapa. Kwa sasa, uzoefu wenyewe unaanza kuwa bidhaa. Si kinywaji, si tiketi wala si udhamini bali ni uzoefu wenyewe. Na hapo ndipo chapa nyingi zinaanza kupoteza umuhimu wake.
Bajeti nyingi za masoko bado zimejikita katika kupima kiwango cha mwonekano badala ya athari za kihisia. Aktivisheni nyingi bado zinaundwa kwa lengo la kuridhisha ripoti za ‘PowerPoint’ na taratibu za manunuzi, badala ya kuunda nyakati ambazo watumiaji watazikumbuka kwa miaka mingi.
Matokeo yake ni sekta yenye matukio makubwa kwa ukubwa, lakini matupu kihisia. Yenye watu wengi, lakini yasiyokumbukwa.
Watumiaji wanaweza kutambua tofauti hiyo mara moja. Wanajua chapa inapojaribu kwa dhati kuunda utamaduni mpya na wanajua inapojaribu tu kujitangaza ndani ya utamaduni uliopo.
Ndiyo maana uzoefu huu wa Heineken ulipokelewa vizuri sana. Ulionekana kuwa wa makusudi. Uliundwa kwa umakini. Uliandaliwa kwa viwango vya juu. Uliwatendea watumiaji kama watu wanaostahili uzoefu wa kiwango cha kimataifa, si kama jambo la mwisho kufikiriwa.
Lakini hadhira ya leo haitoi tu pongezi kwa jitihada. Inatambua na kuthamini ubora. Na hilo linabadilisha kila kitu.
Kwa sababu mara tu watumiaji wanapopata uzoefu wa mazingira ya kuvutia, ya kiwango cha juu na yenye kuamsha hisia, huwa ni vigumu kuridhika tena na aktivisheni za kawaida zilizojaa viti vya plastiki, msongamano wa watu, mifumo dhaifu ya sauti na mbinu zilezile zinazojirudia kila mwaka.
Kiwango kimepandishwa rasmi, na chapa ambazo zitashindwa kutambua mabadiliko haya zinaweza kuanza kupotea polepole katika mazungumzo ya kitamaduni na kijamii.
Hili si suala la burudani pekee. Ni suala la mustakabali wa masoko. Chapa zitakazoongoza katika miaka kumi ijayo si lazima ziwe zile zenye bajeti kubwa zaidi za matangazo bali zitakuwa zile zinazoweza kujenga ulimwengu ambao watu wanatamani kuwa sehemu yake.
Mustakabali ni wa chapa zinazoelewa umuhimu wa mazingira, simulizi, hisia na kujenga jamii zinazowaunganisha watu. Chapa zinazokoma kuingilia utamaduni na badala yake kuanza kuutengeneza.
Hicho ndicho kilichoufanya uzoefu huu kuwa wa kipekee. Kwa usiku mmoja, ulizipa changamoto dhana zilizokuwepo kwa muda mrefu kuhusu kile ambacho hadhira ya Tanzania inapaswa kutarajia kutoka kwa matukio ya hapa nchini. Ulionyesha wazi kwamba soko hili liko tayari kwa mawazo makubwa, ubunifu wa kiwango kikubwa na utekelezaji unaoweza kushindana na viwango vya kimataifa.
Na pengine ndiyo sababu mjadala wake ulisambaa kwa haraka kote nchini. Si kwa sababu watu walikuja kutazama mpira wa miguu, bali kuona taswira ya kile ambacho uzoefu wa chapa nchini Tanzania unaweza kuwa pale ambapo ubunifu unapopewa nafasi yake stahiki.
Swali la msingi sasa ni hili:
Je, chapa nyingine ziko tayari kuwa jasiri vya kutosha kufuata njia hiyo?
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Asha-Rose Migiro, leo Ijumaa Juni 5,2026 amefanya mazungumzo na Mheshimiwa Marianne Young, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, katika Makao Makuu ya CCM, Dodoma.
Mazungumzo hayo yalihusu maeneo ya ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Uingereza, kwa kuzingatia vipaumbele vilivyobainishwa katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya mwaka 2025–2030, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Viongozi hao walijadili fursa za kuendeleza ushirikiano kwenye maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hususan katika kuwawezesha vijana na wanawake kupitia elimu, ujuzi, ubunifu na uwekezaji. CCM inaendelea kuthamini ushirikiano wa kimataifa unaochangia maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi wa Tanzania.

Na Beda Msimbe, TBN – Moscow, Urusi
Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin, amesema nchi yake itaendelea kufungua fursa mbalimbali za uwekezaji na ushirikiano kwa Tanzania ili kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya mataifa yote mawili.
Rais Putin alitoa kauli hiyo jijini Moscow baada ya kufanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye yuko nchini humo kwa ziara ya kiserikali ya kihistoria.
Amesema Urusi imekuwa ikifuatilia kwa karibu mageuzi ya kiuchumi na kijamii yanayotekelezwa Tanzania na kuridhishwa na hatua kubwa za maendeleo zinazopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia.
“Tumekuwa tukifuatilia kwa karibu maendeleo ya Tanzania na tunafurahishwa na mageuzi yanayofanyika katika sekta mbalimbali za uchumi na ustawi wa jamii. Tunaamini ushirikiano wetu utaendelea kuleta manufaa makubwa kwa wananchi wa nchi zetu,” alisema Putin.
Aliongeza kuwa mazungumzo yake na Rais Samia yamekuwa na tija kubwa na yamefungua ukurasa mpya wa kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya biashara, uwekezaji, elimu, teknolojia, nishati na maendeleo ya rasilimali watu.
Putin amesema Urusi itatumia pia Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi unaotarajiwa kufanyika nchini humo kutangaza na kuhamasisha fursa mbalimbali za uwekezaji zinazoweza kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, kwa sasa Urusi ina miradi takribani 70 nchini Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani milioni 434.22, ambayo imechangia kutoa ajira kwa zaidi ya Watanzania 3,000.
Kwa upande wake, Rais Samia amesema ziara yake nchini Urusi ni ya kihistoria kwa Tanzania kutokana na ukweli kwamba ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa Tanzania kufanya ziara ya kiserikali nchini humo baada ya zaidi ya nusu karne.
“Ziara yangu ina umuhimu wa pekee wa kihistoria kwangu binafsi na kwa nchi yangu. Imepita zaidi ya nusu karne tangu kufanyika kwa ziara ya mwisho ya kiserikali ya Tanzania nchini Urusi. Hivyo, kwangu hii ni safari ya kihistoria sana kuja Urusi kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa pande mbili pamoja na maendeleo endelevu kwa wananchi wetu,” alisema Rais Samia.
Rais Samia pia alimshukuru Rais Putin na Serikali ya Urusi kwa mwaliko pamoja na mapokezi na ukarimu aliopatiwa tangu kuwasili kwake nchini humo.
Katika mazungumzo hayo, Rais Samia alikumbusha mchango wa Urusi katika harakati za Tanzania za kupigania uhuru na kujenga taifa, huku akimpongeza Rais Putin kwa maadhimisho ya miaka 81 ya Ushindi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia yaliyofanyika Mei 9 mwaka huu.
Ziara hiyo ya Rais Samia nchini Urusi ni ya kwanza kufanywa na kiongozi wa Tanzania katika kipindi cha zaidi ya miaka 50, jambo ambalo linaipa uzito mkubwa wa kidiplomasia katika historia ya mahusiano ya nchi hizo mbili.
Viongozi hao walieleza kuwa mazungumzo yao yamelenga kuimarisha zaidi uhusiano wa kirafiki uliodumu kwa miongo mingi pamoja na kujadili masuala muhimu ya kikanda na kimataifa yanayoendelea duniani.
Ziara ya Rais Samia inatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi, hususan katika sekta za uwekezaji, biashara, elimu, sayansi na teknolojia, huku ikichochea fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mataifa hayo mawili.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladmir Putin katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow, tarehe 03 Juni, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladmir Putin katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow, tarehe 03 Juni, 2026.



.jpg)
Na Mwandishi Maalum
MOSCOW, URUSI – Kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuweka shada la maua katika Kaburi la Askari Asiyejulikana (Tomb of the Unknown Soldier) jijini Moscow kimeelezwa kuwa ni hatua yenye uzito mkubwa wa kidiplomasia inayobeba ujumbe wa amani, heshima kwa historia na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.
Rais Samia aliweka shada hilo katika mnara wa kumbukumbu uliopo karibu na Kremlin kama sehemu ya ratiba ya ziara yake ya kitaifa nchini Urusi, hatua iliyotafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya kimataifa kuwa ishara ya kuthamini mchango wa mashujaa waliopigania uhuru na usalama wa mataifa yao.
Katika diplomasia ya kisasa, viongozi wa mataifa wanaposhiriki shughuli za kuenzi mashujaa wa kitaifa wa nchi mwenyeji huwa wanatoa ujumbe wa kuheshimu historia ya taifa husika, kuthamini sadaka za waliopoteza maisha kwa ajili ya amani na kuimarisha urafiki kati ya mataifa.
Kwa kushiriki hafla hiyo ya heshima katika Kaburi la Askari Asiyejulikana jijini Moscow, Rais Samia ameonesha kuwa Tanzania inaungana na jumuiya ya kimataifa katika kutambua mchango wa mashujaa waliolinda uhuru wa mataifa yao kwa gharama ya maisha yao.
Hatua hiyo pia inaendana na historia ya Tanzania ambayo tangu kupata uhuru wake mwaka 1961 imeendelea kujijengea sifa ya kuwa miongoni mwa mataifa yaliyokuwa mstari wa mbele kuunga mkono harakati za ukombozi wa Afrika, kulinda amani na kusisitiza matumizi ya mazungumzo katika kutatua migogoro.
Kaburi la Askari Asiyejulikana ni moja ya maeneo yenye hadhi kubwa ya kitaifa nchini Urusi. Mnara huo ulijengwa kuwakumbuka askari waliopoteza maisha wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia bila kutambulika majina yao.
Katika eneo hilo kuna kauli maarufu inayosema, “Jina lako halijulikani, lakini ushujaa wako hautakufa,” ambayo imeendelea kuwa alama ya heshima kwa mashujaa wote waliotoa maisha yao kwa ajili ya mataifa yao.
Wachambuzi wa diplomasia wanaeleza kuwa uwepo wa Rais Samia katika eneo hilo unaonesha kiwango cha heshima ambacho Tanzania inaipa historia ya Urusi pamoja na mchango wake katika matukio muhimu ya dunia.
Aidha, hatua hiyo imeonekana kuongeza uzito wa ziara ya Rais Samia nchini humo kwa kuonesha kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi haujajikita tu katika nyanja za uchumi na biashara, bali pia katika kuthamini historia, urafiki na maadili ya pamoja yanayounganisha mataifa hayo mawili.
Katika kipindi ambacho dunia inaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali za usalama na migogoro, ujumbe wa Rais Samia katika tukio hilo umeonekana kukumbusha umuhimu wa kujifunza kutokana na madhara ya vita na kuendelea kuwekeza katika amani, maridhiano na ushirikiano wa kimataifa.
Kwa mtazamo mpana, tukio hilo limeendelea kuiweka Tanzania katika nafasi ya taifa linalothamini historia, kuenzi mashujaa na kujenga mahusiano ya kirafiki na mataifa mengine kwa lengo la kuimarisha maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi wake.
Hivyo, kitendo cha Rais Samia kuweka shada la maua katika Kaburi la Askari Asiyejulikana jijini Moscow hakipaswi kuonekana kama tukio la kawaida la kiitifaki, bali kama sehemu ya diplomasia ya kisasa inayolenga kuimarisha hadhi ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa huku ikiendeleza misingi ya amani, mshikamano na ushirikiano wa kimataifa.
Balozi
wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, akiwasilisha nakala
za hati za utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Mhe. Ahmed
Attaf, jijini Algiers, leo tarehe 26 Mei, 2026.
Balozi
wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, akiwa katika
mazungumzo mafupi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Mhe. Ahmed
Attaf, mara baada ya kuwasilisha nakala za hati za utambulisho jijini
Algiers, leo tarehe 26 Mei, 2026. Mazungumzo hayo yalihusu uimarishaji
wa ushirikiano na uhusiano baina ya nchi hizi mbili.
Pichani, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja
na sehemu ya wajumbe wa makundi yaliyoshiriki mikutano hiyo, yakiwemo
United People’s Alliance (UPA), SSOMA, SPLM-IO, pamoja na People’s
Coalition for Civil Action na Federal Democratic Party. Picha na Issa
Michuzi
Na Mwandishi Wetu.
Mikutano ya ngazi ya juu iliyohusisha makundi
mbalimbali ya upinzani nchini Sudan Kusini imefanyika jijini Dar es
Salaam tarehe 21 na 22 Mei, 2026 ikiwa ni sehemu ya juhudi mpya za
kufufua mchakato wa amani jumuishi baada ya kusuasua kwa utekelezaji wa
makubaliano ya amani ya mwaka 2018.
Mazungumzo hayo yaliongozwa
na Rais wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye ni Mwakilishi
Maalum wa Umoja wa Afrika kwa Ukanda wa Pembe ya Afrika na Bahari ya
Shamu.
Majukumu yake makuu yanajumuisha: Upatanishi wa Amani:
Kusimamia diplomasia ya kuzuia migogoro na kuongoza mazungumzo jumuishi
ili kutatua changamoto za kisiasa na kiusalama katika ukanda huo.
Ushirikiano
wa Kikanda: Kufanya kazi kwa karibu na jumuiya na taasisi mbalimbali
kama vile IGAD na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kujenga misingi
thabiti ya amani na usalama.
Kwa ujumla, mikutano hiyo
ilionyesha dhamira ya Umoja wa Afrika na wadau wa kikanda katika
kuimarisha mazungumzo ya kisiasa na kuhakikisha mazingira ya amani na
utulivu yanaimarishwa kuelekea uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu nchini
Sudan Kusini.
Mikutano hiyo pia ililenga kuisaidia Umoja wa
Afrika kupata picha kamili ya hali ya kisiasa na kiusalama nchini Sudan
Kusini kabla ya uchaguzi uliotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huo wa
2026.









































