
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya uapisho wa Mawaziri pamoja na Naibu Mawaziri, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 18 Novemba, 2025.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaingia katika kipindi chake cha pili ikiwa na mkakati mahsusi wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kupunguza utegemezi wa fedha kutoka nje, kwa kutumia rasilimali zilizopo ndani ya nchi.
Rais Samia ameyasema hayo leo wakati akiwaapisha Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino, Dodoma, ambapo amewataka viongozi hao kuhakikisha wanatoa matokeo ndani ya muda mfupi, kwa kuzingatia uwajibikaji na uadilifu.

Amesisitiza kuwa dhamana waliyopewa haina nafasi ya uzembe, na kwamba Serikali haitasita kuwawajibisha watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Ameongeza kuwa jukumu kubwa lililo mbele ya Mawaziri na Manaibu ni kuhakikisha kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inaenda sambamba na matarajio ya wananchi.
Katika kuelekea utekelezaji wa mpango wa siku 100 wa Serikali, Rais Samia amewaagiza Mawaziri kushirikiana kwa karibu na Makatibu Wakuu wa Wizara zao ili kuanza mara moja kutimiza majukumu waliyopewa. Ameeleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuhakikisha miradi ya Serikali inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia thamani halisi ya matumizi ya fedha.

Vilevile, Rais Samia amewataka viongozi walioteuliwa kuwa mfano wa utendaji bora, nidhamu na uadilifu, akisema kuwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla wanatazama namna wanavyoongoza na kusimamia majukumu yao.
Akiwapongeza viongozi waliomaliza muda wao katika awamu ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Sita, Rais Samia amesema wametoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kuhakikisha maendeleo hayakwami licha ya changamoto za upatikanaji wa fedha kutoka nje.
Mwisho, Rais Samia amewatakia heri Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya walioteuliwa, akiwataka kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha Serikali inaendelea kuleta matokeo chanya kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.



































.jpeg)











