Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza katika Ibada ya Jumpili aliyoshiriki katika Usharika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Kisasa jijini Dodoma, Novemba 16, 2025.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwasisitiza Watanzania kuyaombea taifa ili amani, upendo na mshikamano viendelee kudumu nchini, akisema maombi ni nguzo muhimu ya utulivu wa taifa.
Wito huo umetolewa leo Jumapili, Novemba 16, 2025 na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, alipowasilisha salamu za Rais Samia kwa waumini na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kisasa mkoani Dodoma.
“Mheshimiwa Rais anawasalimu sana. Rai yake kwa Watanzania wote ni kuendelea kuiombea nchi yetu, tuwe watulivu na tuendelee kudumisha amani,” alisema Waziri Mkuu wakati akisoma salamu hizo.
Dkt. Mwigulu alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda amani ya nchi kwa sababu bila amani hakuna shughuli yoyote muhimu inayoweza kufanyika, ikiwemo ibada, maendeleo ya kijamii na utekelezaji wa mipango ya serikali.
“Pasipo amani hatuwezi kutekeleza majukumu yetu mengine. Pasipo amani hatuwezi hata kufanya ibada. Ndiyo maana tunapaswa kuiombea nchi yetu kila mara. Tukidumisha amani, tunaweza kukabiliana hata na mambo magumu,” alisema.
Ibada hiyo iliongozwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Dodoma, Dkt. Christian Ndossa, ambaye aliwahimiza waumini na Watanzania kwa ujumla kumtanguliza Mungu katika maisha yao, kuwa na matumaini na kujiepusha na matendo maovu.
Katika ibada hiyo, Waziri Mkuu aliambatana na mke wake, Mama Neema Mwigulu Nchemba, sambamba na viongozi mbalimbali wa serikali na Bunge akiwemo Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo; Mbunge wa Kilolo, Ritha Kabati; Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya; Mbunge wa Viti Maalumu, Balozi Dkt. Pindi Chana; Mbunge wa Itigi, Yohana Msita na Mbunge wa Kalenga, Jackson Kiswaga.
Ibada hiyo imeendelea kuwa sehemu ya mwamko wa viongozi kuitaka jamii kuenzi amani kama msingi wa maendeleo ya taifa.



Toa Maoni Yako:
0 comments: