Na Mwandishi Wetu, Beijing

Katika hatua muhimu za kuendeleza sekta ya filamu na kuitumia kama nyenzo madhubuti ya kutangaza utalii wa Tanzania, Bodi ya Filamu Tanzania imeshiriki mafunzo maalumu ya mbinu za kisasa za utayarishaji na uendelezaji wa filamu yaliyofanyika jijini Beijing, China. Mafunzo hayo ya siku 14 yalihudhuriwa na Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uhakiki wa Filamu, Bi. Boppe David Kyungu, kwa udhamini wa Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China chini ya uongozi wa Balozi Chen Mingjian.

Kupitia mafunzo hayo, Bi. Boppe alipata fursa ya kujifunza teknolojia mpya, mbinu za kubuni maudhui ya kuvutia kimataifa, pamoja na njia za kutumia filamu kama chachu ya kuendeleza utalii na utamaduni. Aidha, alitembelea maeneo muhimu ya kimkakati ya utamaduni, uzalishaji wa filamu na vivutio vya utalii nchini China, hatua iliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na taasisi kubwa za filamu za nchini humo.

Bodi ya Filamu Tanzania imesema kuwa ushiriki huo unaendana moja kwa moja na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anayesisitiza kufunguliwa kwa milango ya kimataifa na kuitumia filamu kama chombo cha kuitangaza Tanzania katika majukwaa ya dunia. Kwa mujibu wa Bodi, mafanikio ya mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza ujuzi, ubunifu na ushindani wa wanatasnia wa filamu nchini.
Aidha, Bodi imeendelea kuwahimiza wadau wote wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza kujisajili ili watambuliwe na kuunganishwa na fursa za mafunzo, masoko na ushirikiano wa kimataifa unaoendelea kupanuka kupitia mikakati inayotekelezwa.

Kwa mujibu wa Bodi, jitihada hizi si za muda mfupi bali ni sehemu ya mpango mpana wa mageuzi ya sekta ya filamu nchini, unaolenga kuifanya kuwa injini muhimu ya uchumi wa ubunifu na chombo mahususi cha kuitangaza Tanzania katika anga la kimataifa kupitia kazi bora, zenye ubora wa kisasa na ushindani.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: