Articles by "BURUDANI"
Showing posts with label BURUDANI. Show all posts
Na Mwandishi Wetu, Beijing

Katika hatua muhimu za kuendeleza sekta ya filamu na kuitumia kama nyenzo madhubuti ya kutangaza utalii wa Tanzania, Bodi ya Filamu Tanzania imeshiriki mafunzo maalumu ya mbinu za kisasa za utayarishaji na uendelezaji wa filamu yaliyofanyika jijini Beijing, China. Mafunzo hayo ya siku 14 yalihudhuriwa na Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uhakiki wa Filamu, Bi. Boppe David Kyungu, kwa udhamini wa Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China chini ya uongozi wa Balozi Chen Mingjian.

Kupitia mafunzo hayo, Bi. Boppe alipata fursa ya kujifunza teknolojia mpya, mbinu za kubuni maudhui ya kuvutia kimataifa, pamoja na njia za kutumia filamu kama chachu ya kuendeleza utalii na utamaduni. Aidha, alitembelea maeneo muhimu ya kimkakati ya utamaduni, uzalishaji wa filamu na vivutio vya utalii nchini China, hatua iliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na taasisi kubwa za filamu za nchini humo.

Bodi ya Filamu Tanzania imesema kuwa ushiriki huo unaendana moja kwa moja na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anayesisitiza kufunguliwa kwa milango ya kimataifa na kuitumia filamu kama chombo cha kuitangaza Tanzania katika majukwaa ya dunia. Kwa mujibu wa Bodi, mafanikio ya mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza ujuzi, ubunifu na ushindani wa wanatasnia wa filamu nchini.
Aidha, Bodi imeendelea kuwahimiza wadau wote wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza kujisajili ili watambuliwe na kuunganishwa na fursa za mafunzo, masoko na ushirikiano wa kimataifa unaoendelea kupanuka kupitia mikakati inayotekelezwa.

Kwa mujibu wa Bodi, jitihada hizi si za muda mfupi bali ni sehemu ya mpango mpana wa mageuzi ya sekta ya filamu nchini, unaolenga kuifanya kuwa injini muhimu ya uchumi wa ubunifu na chombo mahususi cha kuitangaza Tanzania katika anga la kimataifa kupitia kazi bora, zenye ubora wa kisasa na ushindani.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga (PhD), amempongeza John Elisha, maarufu kama Boneka, kwa kushinda Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Mwaka 2025 kupitia tamthiliya maarufu ya Kombolela inayorushwa katika chaneli ya Sinema Zetu ya Azam TV.

Tuzo hiyo imetolewa na East Africa Youth Panel Awards tarehe 19 Oktoba 2025, ikitambua mchango wa Elisha katika kukuza ubunifu na ubora wa tasnia ya filamu Afrika Mashariki.

Akiwa katika ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania, Kivukoni jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 23, 2025, Elisha aliwasilisha rasmi tuzo hiyo kwa Bodi kama ishara ya heshima na ushirikiano kati ya wasanii na taasisi hiyo.

“Tuzo hii ni matokeo ya jitihada, ubunifu na kujituma kwa wasanii wetu. Tunampongeza John kwa mafanikio haya na tunamhimiza aendelee kufanya kazi kwa weledi na ubunifu,” alisema Dkt. Kasiga.
Aidha, Dkt. Kasiga aliwataka wasanii wote wa filamu nchini kuhakikisha wanajisajili na Bodi ya Filamu Tanzania, na kuwasilisha kazi zao kwa ukaguzi na vibali ili kujenga sekta ya filamu yenye nidhamu na mazingira bora ya kazi.

“Bodi itaendelea kuwatambua na kuwapongeza wasanii wanaofanya vizuri, pamoja na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za kukuza soko la filamu zetu,” aliongeza Dkt. Kasiga.

Kwa upande wake, John Elisha alishukuru Bodi ya Filamu kwa kumtambua, akisema tuzo hiyo ni motisha kwake na kwa wasanii wengine kuendelea kutangaza utamaduni wa Tanzania kupitia sanaa ya filamu.
Dar es Salaam/Ujerumani, Septemba 19, 2025 – Leo ni siku maalum kwa mashabiki wa muziki wa dansi duniani kote, kwani kiongozi wa bendi maarufu ya Ngoma Africa Band ya Ujerumani, Ebrahim Makunja, anayejulikana zaidi kama Kamanda Ras Makunja au “Anunnaki Alien”, anasherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwake.

Ras Makunja, ambaye alizaliwa jijini Dar es Salaam, ni mtoto wa kwanza wa marehemu Jumanne Saleh Makunja Ngayonga na mama yake Moza Hassan Seifu Mpili. Kwa zaidi ya miaka 33, msanii huyu amekuwa mtunzi na mwimbaji mahiri wa muziki wa dansi, akitikisa majukwaa ya kimataifa na kuifanya Ngoma Africa Band kujulikana kwa jina la utani “FFU-Ughaibuni”.
Safari yake ya muziki

Ras Makunja ameendelea kuwa nembo ya muziki wa dansi barani Ulaya na Afrika kwa mtindo wake wa kipekee unaochanganya sauti, midundo na ujumbe mzito wa kijamii. Umaarufu wake kama “mkuu wa viumbe wa ajabu” umewavutia mashabiki wengi, huku akibaki kinara wa kusambaza muziki wa Tanzania nje ya mipaka ya nchi.
Kumbukumbu ya miaka

Sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake mwaka huu imepewa uzito mkubwa na mashabiki wa Ngoma Africa Band, ambao wamekuwa wakimtumia salamu za pongezi kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo ukurasa rasmi wa Facebook wa bendi hiyo: facebook.com/ngomaafricaband

Aidha, mashabiki pia wanakaribishwa kusherehekea naye kupitia muziki wake unaopatikana katika ukurasa wa bendi hiyo kwenye ReverbNation: www.reverbnation.com/ngomaafricaband
Salamu kwa mashabiki

Akizungumzia siku yake ya kuzaliwa, baadhi ya wanamuziki wenzake wamempongeza kwa mchango wake mkubwa katika kukuza muziki wa dansi kimataifa. “Kamanda Ras Makunja ni alama ya ubunifu na uthubutu. Bila yeye, muziki wa dansi ungekuwa tofauti kabisa kwenye ramani ya kimataifa,” alisema mmoja wa wanabendi.

Mwisho wa habari

Kwa sasa, shangwe na burudani zinaendelea kambini kwao FFU-Ughaibuni, huku mashabiki wakiungana kumtakia maisha marefu, afya njema na mafanikio zaidi katika safari yake ya muziki.

Happy Birthday Kamanda Ras Makunja! 🎉🎶

 
Na Mwandishi Wetu.

Msanii nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Mbwana Yusuph maarufu kama Mbosso, amewashukuru uongozi na mashabiki wa Simba Sports Club kwa kumpa nafasi ya kipekee kuwa headliner wa Tamasha la kihistoria la SIMBA DAY lililofanyika hivi karibuni.

Kupitia barua yake ya wazi aliyoiandika kwenye mtandao wa Instagram, Mbosso alisema uongozi wa Simba SC uliweza kumpa nafasi hiyo adhimu ambayo ingeweza kupewa msanii mwingine yeyote, lakini badala yake walimchagua yeye kuongoza burudani ya tamasha hilo kubwa.

“Kwangu mimi hili ni tamasha langu kubwa la kwanza kufanyia kwenye uwanja linalohusiana na mpira wa miguu katika maisha yangu ya muziki. Ndiyo maana nilijitahidi kwa uwezo wangu wote kuhakikisha nawapa furaha mashabiki na wadau wa Simba SC,” aliandika Mbosso.

Ameeleza kuwa SIMBA DAY kwake haikuwa tu tamasha, bali pia jukwaa la kuonyesha vipaji vyake vingine ambavyo huenda havijawahi kuonekana, ikiwemo kuigiza kwa uhalisia, kuimba na kuwasilisha ubunifu kwa kiwango cha juu.

Aidha, Mbosso alibainisha kuwa licha ya kutumia gharama kubwa kuhakikisha onyesho lake linafanikiwa, hakufanya hivyo kwa faida binafsi bali kwa mapenzi yake makubwa kwa Simba Sports Club na mashabiki wake.

“Nina imani mlifurahi, na kama kulikuwa na sehemu nilikosea au kulikuwa na mapungufu, naomba mnisamehe kwa kuwa mimi ni mwanadamu na siwezi kufanya vyote kwa ukamilifu,” alisema Mbosso huku akimalizia barua yake kwa kutia sahihi ya jina lake la kisanii Mad Max Mbosso Khan.

Tamasha la SIMBA DAY ni tukio la kila mwaka la Simba SC linalokutanisha mashabiki kutoka maeneo mbalimbali nchini, likiwa na lengo la kutambulisha kikosi kipya cha wachezaji na kutoa burudani ya muziki.

Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC imeadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake kwa kuandaa bonanza la michezo jijini Arusha mwishoni mwa wiki, likikusanya wateja, mashabiki wa michezo na familia mbalimbali kusherehekea robo karne ya mafanikio.

Katika shamrashamra hizo, mpira wa miguu ulikuwa kivutio kikuu ambapo timu ya Kuza FC ilitwaa ubingwa baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Kitambi Noma FC. Kapteni wa Kuza FC, Gabriel Mwandembwa, alipokea kombe la ushindi kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Arusha (ARFA), Jame Rugagila.
Mbali na soka, bonanza hilo liliibua burudani nyingine ikiwemo michezo ya video ya FIFA, mashindano ya magari yanayoendeshwa kwa simu, kuvuta kamba, pamoja na mbio za magunia, hali iliyoongeza shamra shamra na kufurahisha washiriki wa rika zote.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Vodacom, George Venanty, pamoja na Meneja Masoko na Mikakati, Hamida Hamad, walibainisha kuwa lengo la kampuni hiyo ni kuendelea kujenga ukaribu na jamii kupitia shughuli za kijamii na burudani sambamba na huduma bora za mawasiliano.

“Sherehe hizi ni sehemu ya kusherehekea safari yetu ya miaka 25 ya kuunganisha Watanzania. Tunataka tuendelee kushirikiana na wateja wetu si tu kupitia huduma za kidijitali, bali pia kwa kutengeneza kumbukumbu za pamoja za furaha na mshikamano,” alisema Venanty.

Vodacom imesisitiza kuwa itaendelea na mfululizo wa matukio ya kusherekea miaka 25 yake katika mikoa mbalimbali nchini, ikilenga kuimarisha uhusiano wa karibu na wateja wake.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wamesaini makubaliano ya ushirikiano kwa lengo la kulinda kazi za sanaa nchini, kupitia usajili wa kazi na miradi ya ubunifu pamoja na kutumia haki za ubunifu kama mtaji wa maendeleo.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo Agosti 12, 2025, jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, na Katibu Mtendaji wa BASATA, Dk.Kedmon Mapana na kushuhudiwa Waandishi wa Habari.

Akizungumza katika hafla hiyo,Nyaisa amesema makubaliano hayo yanalenga kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu kisheria na kiuendeshaji kupitia kubadilishana taarifa kwa njia za TEHAMA, ili kurahisisha utoaji huduma, kutoa elimu na kuongeza uelewa kwa wasanii kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara na kulinda kazi zao.

Ameeleza kuwa makubaliano hayo pia yatawezesha urasimishaji wa shughuli za burudani, ikiwemo kumbi za muziki na burudani (night clubs), kwa kuzingatia vigezo vya kibunifu na kibiashara, sambamba na kusukuma mbele kazi za sanaa za asili na utamaduni wa Kitanzania ili zipate nafasi katika soko la ndani na kufikia viwango vya kimataifa.

“Ni ukweli usiopingika kuwa sekta ya ubunifu na sanaa inakua kwa kasi, na inazidi kuwa nyenzo muhimu ya ajira, utambulisho wa taifa na chanzo cha mapato. Ni jukumu letu kama taasisi kuhakikisha tunaunda mazingira bora ya kisera, kisheria na kiutendaji ili kusaidia ukuaji huo. Hivyo, utiaji saini wa makubaliano haya ni hatua ya kwanza muhimu kuelekea ndoto hiyo,” amesema Nyaisa.

Kwa upande wake, Dk. Mapana amebainisha kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria kwani urasimishaji wa kazi za sanaa kupitia usajili wa alama zinazowatambulisha wasanii kabla ya kuziingiza sokoni, utawapa ulinzi unaowezesha ukuaji wao wa kiuchumi.

“Sekta inayoongoza katika ukuaji wa uchumi ni Sekta ya Sanaa na Burudani kwa asilimia 17. Ukuaji huu unatokana na kazi kubwa ya wasanii, na kupitia urasimishaji wa kazi zao watapata elimu ya bure ya kisheria na fursa za mikopo kupitia Mfuko wa Utamaduni, ili waweze kukua kiuchumi,” amesema Dk. Mapana.

Aidha, ametoa wito kwa wanamuziki wanaotarajia kushiriki katika Tuzo za Kitaifa za Muziki Tanzania (TMA) zitakazofanyika Septemba 2025, kuhakikisha wanasajili alama zinazowatambulisha ili kulinda haki zao za kisanaa.

Wito huo pia unawahusu washiriki wa mashindano ya ulimbwende mwaka 2027, ambayo Tanzania itaandaa.
Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Katika kuunga juhudi za kukuza sekta ya utalii na kuongeza idadi ya watalii nchini, kampuni ya utalii ya Meru Eco Camp imezindua mkakati kabambe wa maboresho ya huduma unaolenga kuvutia wageni wa ndani na nje ya Tanzania.

Kampuni hiyo inayotoa huduma ndani ya Hifadhi ya Shamba la Miti la Meru, wilayani Arumeru mkoani Arusha, sasa inajivunia kuwa na vivutio vya kipekee vikiwemo maporomoko ya maji ya Napuru (Napuru Waterfalls), malazi ya kisasa na rafiki kwa mazingira, pamoja na michezo ya kusisimua ikiwemo zipline yenye urefu wa mita 800 – zipline ndefu zaidi Afrika Mashariki – inayokatiza kutoka msituni hadi mto Themi uliopo katikati ya jiji la Arusha.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wadau wa Utalii, Mkurugenzi Mtendaji wa Meru Eco Camp, Catherine Loy, alisema:

“Tumejipanga kuifanya Meru Eco Camp kuwa kitovu cha utalii wa asili na burudani kwa wageni wote. Tunaongeza michezo ya kipekee kama gofu, kurusha mishale, baiskeli, na pikipiki kwa ajili ya watalii wanaopenda kujichanganya na mazingira.”

Kwa upande wake, Nsajigwa Victor, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, alieleza kuwa wanatarajia kujenga eco lodges – malazi ya kiasili yanayozingatia utunzaji wa mazingira – ili kuongeza idadi ya watalii wanaolala hifadhini.
Lucas Christopher, mtaalamu wa masuala ya fedha wa Meru Eco Camp, alisema maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza ajira kwa vijana na kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa kupitia utalii endelevu.

Naye Colins James, Mkurugenzi Msaidizi wa New Meru Camp, aliongeza kuwa mbali na malazi, wameandaa michezo mingi ya kuvutia, hasa kwa familia na vijana, ikiwa ni sehemu ya kuvutia wageni wapenda burudani za mazingira.
Kwa upande wake, Fredy Msaki, Mratibu wa kampuni ya utalii ya FOCA, alibainisha kuwa kuna programu maalum za malazi kwa bei nafuu kwa familia na watalii wote watakaotembelea Hifadhi ya Shamba la Miti la Meru.

Mpango huu mkubwa unatajwa kuwa ni sehemu ya jitihada za kuifanya Arusha kuendelea kuwa kitovu cha utalii Afrika Mashariki huku ukiibua matumaini mapya kwa jamii inayozunguka msitu wa Meru.
Eneo la Malazi ya kisasa...
Zipline... Moja ya mchezo unaopendwa na Watalii.
Eneo la Maporomoko ya Maji ya Napuru
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam.

Mashabiki wa urembo nchini sasa watapata fursa ya kipekee kushuhudia safari ya warembo wanaowania taji la Miss Universe Tanzania 2025, kupitia vipindi maalum vinavyotarajiwa kuanza kurushwa leo, Julai 25, 2025, kupitia king’amuzi cha Startimes Tanzania katika Chaneli ya ST Swahili.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kipindi hicho, Mkurugenzi wa Kampuni ya Millen Privé & Co. Lifestyle Bespoke Luxury Lifestyle & Hospitality Management, ambaye pia ni Mwanamitindo wa Kimataifa, Millen Happiness Magese, alisema mwaka huu mashabiki wataweza kuona kwa mara ya kwanza mchakato mzima wa maandalizi ya Miss Universe Tanzania.
“Watu wengi wamekuwa wakiona warembo wanaingia kambini na kutoka bila kuelewa kilichojiri kati ya hapo. Mwaka huu tumeamua kufungua milango. Mtashuhudia jinsi tulivyowachagua, tulivyowafundisha, na namna walivyokuja kuiva mpaka siku ya mwisho,” alisema Millen.

Alibainisha kuwa vipindi hivyo vitatoa nafasi kwa Watanzania kuona kwa karibu namna tasnia ya urembo inavyoendeshwa kwa weledi, nidhamu na maadili ya hali ya juu.

Lengo kuu, kwa mujibu wa Millen, ni kuwapa wananchi uelewa mpana wa mchango wa mashindano ya urembo katika kuibua vipaji, kuhamasisha uthubutu kwa vijana na kuchochea maendeleo ya sekta ya mitindo na burudani nchini.

Mashindano ya Miss Universe Tanzania kwa mwaka huu yanatarajiwa kuvuta hisia za wengi si tu kwa uzuri wa washiriki, bali pia kwa maudhui ya vipindi ambavyo vinajielekeza katika kukuza thamani ya mwanamke, kujenga uwezo binafsi na kukuza taswira ya Tanzania kimataifa.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) leo, tarehe 23 Julai 2025, imetoa rasmi leseni ya mwaka mmoja kwa Kampuni ya Society of Music Advocacy Limited (SOMA) kwa ajili ya ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha ya kazi za muziki nchini.

Leseni hiyo inahusu kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, ambapo kampuni hiyo itakuwa na jukumu la kukusanya na kugawa mirabaha kwa niaba ya wamiliki wa kazi za muziki, huku COSOTA ikiendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa majukumu hayo kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa leseni, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa COSOTA, Ndugu Philemon Kilaka, aliitaka SOMA kuanza kazi mara moja kwa kuhakikisha ukusanyaji wa mirabaha unafanyika katika maeneo yote yanayotumia kazi za muziki ikiwemo hoteli, baa, migahawa, kumbi za starehe na maeneo mengine husika.

Aidha, alisisitiza kuwa utekelezaji wa jukumu hilo unapaswa kuzingatia Sheria ya Hakimiliki pamoja na Kanuni za Usimamizi wa Kampuni ya Ugawaji wa Mirabaha ya mwaka 2023, ili kulinda haki za wasanii na wadau wote wa kazi za muziki nchini.

Kwa hatua hii, Tanzania imepiga hatua muhimu katika kuhakikisha wasanii wananufaika ipasavyo na kazi zao kupitia mfumo rasmi wa ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe. George Simbachawene akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chipogolo, Kata ya Chipogolo wakati wa hafla ya kugawa vifaa vya michezo ya mashindano ya ligi Samia Cup.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe. George Simbachawene akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chipogolo, Kata ya Chipogolo wakati wa hafla ya kugawa vifaa vya michezo ya mashindano ya ligi Samia Cup.


Wananchi wa Kijiji cha Chipogolo, Kata ya Chipogolo wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati wa ugawaji vifaa vya michezo ya mashindano ya ligi Samia Cup.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe. George Simbachawene (kulia) akimpatia mpira mmoja wa wawakilishi wa wachezaji wa timu za mpira kwa ajili ya mashindano ya ligi Samia Cup yanayotarajiwa kufanyika katika Kata ya Chipogolo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe. George Simbachawene (aliyevaa miwani) akisalimiana na baadhi ya wananchi wa Kata ya Chipogolo wakati alipowasili kwa ajili ya hafla ya kugawa vifaa vya michezo ya mashindano ya ligi Samia Cup.
Wananchi wa Kijiji cha Chipogolo, Kata ya Chipogolo wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati wa hafla ugawaji vifaa vya michezo ya mashindano ya ligi Samia Cup.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe. George Simbachawene (aliyeshika mpira) akiteta jambo na Mwenyekiti wa CCM Chipogolo, Bw. Msafiri Mgonela (wa kwanza kulia) wakati wa hafla ya ugawaji vifaa vya michezo ya mashindano ya ligi Samia Cup.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe. George Simbachawene (wa tatu kutoka kulia) akifurahia jambo wakati wa hafla ya ugawaji vifaa vya michezo ya mashindano ya ligi Samia Cup. Kulia kwake ni Diwani wa Kata ya Chipogolo, Mhe. Kayanda Mwanika


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe. George Simbachawene akifurahia jambo na mmoja wa wawakilishi wa timu ya mpira ya wanawake wakati wa hafla ya ugawaji vifaa vya michezo ya mashindano ya ligi Samia Cup.


Wananchi wa Kijiji cha Chipogolo, Kata ya Chipogolo wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati wa hafla ugawaji vifaa vya michezo ya mashindano ya ligi Samia Cup.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe. George Simbachawene akifurahia jambo na mwananchi wa Kata ya Chipogolo aliyehudhuria hafla ya ugawaji vifaa vya michezo ya mashindano ya ligi Samia Cup.

Na Mwandishi Wetu-Chipogolo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe ameunga mkono mashindano ya ligi Samia Cup na kugawa vifaa vya michezo huku akiahidi kutoa zawadi kwa mshindi wa kwanza kiasi cha fedha shilingi 500,000/=, mshindi wa pili 250,000/= na mshindi wa tatu 150,000/= kuelekea mashindano ya ligi Samia Cup yanayotarajiwa kufanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Kata Chipogolo.

Mhe. Simbachawene ameunga mkono mashindano hayo alipokuwa mgeni rasmi kwenye hafla maalum iliyolenga kugawa vifaa hivyo vilivyonunuliwa na Diwani wa Kata ya Chipogolo, Mhe. Kayanda Mwanika.

Mhe. Diwani ninakupongeza sana, kwenye baadhi ya maeneo mimi ndiye ninayeombwa kutoa vifaa vya michezo, lakini leo ni tofauti na nilivyozoea nimekuja kugawa vifaa hivi vilivyonunuliwa nawe, hongera kwa kujitolea na huo ndio uongozi, nami nitaongeza fedha kuanzia mshindi wa kwanza hadi wa tatu. Amesema Waziri Simbachawene.

Akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Chipogolo, Waziri Simbachawene ametoa pongezi kwa Mhe. Diwani Kayanda kwa kutoa vifaa hivyo na kutumia fursa ya Mashindano ya Ligi Samia Cup kuwafahamisha wananchi maendeleo ambayo yamefanyika katika kipindi cha miaka mitano chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo kujengwa kwa vituo vya afya, usambazaji wa umeme, kutatua changamoto ya maji na miundombinu ikiwemo ujenzi wa Barabara kwenye baadhi ya maeneo.

Aidha, Waziri Simbachawene amesema michezo inatoa ajira, inaimarisha afya, inajenga undugu na inaleta furaha kwa jamii hivyo ni vema wananchi wa Chipogolo wakashiriki kwa wingi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Chipogolo, Mhe. Kayanda Mwanika amemshukuru Waziri Simbachawene kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kugawa vifaa hivyo vya michezo na kuunga mkono mashindano hayo kwa kutoa fedha kwa washindi.

Vilevile, Mhe. Kayanda amemshukuru Waziri Simbachawene kwa kushughulikia masuala mbalimbali ya maendeleo katika Kata ya Chipogolo.
Na Mwandishi Wetu.

UONGOZI wa Mac D umetangaza tarehe ya kufanyika bonanza lake katika awamu ya pili ambapo litaanza asubuhi saa 12:00 kutakuwa na mbio za kujifurahisha 'Fun Run' zitakazojulikana kwa jina la 'Mac D Fun Run 2025' .

Akizungumza na Waandishi wa Hbari leo tarehe 01 Mei 2025 kwenye Ukumbiwa EB Twenty Five uliopo Mbezi Makonde Jijini Dar es Salaam Mratibu wa bonanza hilo Denzel Deogratius Rweyunga amesema kuwa bonanza hilo linalofanyika kwa msimu wa pili litafanyika tarehe 07 Juni 2025 ambapo pia mbio hizo zitaanza katika Viwanja vya Chuo Cha Taifa Cha Jeshi (National Defence CollageNDC) Kunduchi Jijini Dar es Salaam.

"Washiriki wa mbio za KM 10 na KM5 wataanza mbio majira ya saa moja asubuhi kutoka Chuo Cha NDC wataelekea uelekeo wa kwenda Ununio na watakapofika katika Uwanja wa mpira unaofahamika kama Ununio Playground karibu na Kanisa la Roman Catholic watageuza hapo na kurejea katika uwanmja wa NDC.

Amesema kuwa lengo kuu la mbio hizi kwa mwaka huu ni kuunganisha jamii katika kuboresha afya na na kuwa wakakamavu katika kufanya mazoezi na kulenga kutokomeza magonjwa yasiyoambukiza kufahamiana na kutengeneza marafiki wapya.

"Tunawaalika watu wote mtu mmoja mmoja, vikundi vya wakimbiaji na taasisi mbalimbali kushiriki pamoja nasi na baada ya kujisajili mshiriki atapata Tshirt bure na kwa yeyote anayependa kushiriki ajisajili kupitia www.macdbonanza .co.tz, vituo vingine vya usajili ni pamoja na EB Twenty Five Mbezi Makonde, Mac D Wines & Spirits Kunduchi, Zaks Bay Boko Magengeni na Leather Men Mabatini Kijitonyama Dar es Salaam.

"Msimu wa pili wa bonanza letu tutaanza na Fun Run hizi ni mbio za kujifurahisha na kuweka miili yetu katika hali nzuri ya kiafya ambapo hakuna mshindi wala zawadi yeyote itakayoshindaniwa bali washiriki wote watapatiwa fulana na namba ya kukimbia bure pia Kituo cha ITV kitarusha matangazo hayo mubashara" amesema Rweyunga.

Mratibu huyo ameongeza kwa kusema kuwa baada ya Fun Run kumalizika jioni kuanzia saa 10 timu mbili ambazo ni Mac D FC na IPP Media watashuka dimbani na katika mchuano wa mwaka huu mshindi ataondoka na Kombe na mechi hii itatangazwa mubashara na kituo cha Radio One.

Wakati huohuo Rweyunga ametoa shukrani kwa wadhamini wa bonanza hilo sambamba na kuwatambulisha katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam.

"Bonanza la mwaka huu limeandaliwa katika viwango vya juu , tunawashukuru sana wadhamini wetu ambao wamejitokeza kutuunga mkono ambao ni ITL, Bonite Bottlers (Kilimanjaro Drinking Water),Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Isumba Trans Limited , Zaks Bay Liquar na Pwani Inland Clearance and Depot (PICD).
Na Mwandishi Wetu.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Wakili Patrick Kipangula ameshiriki Kikao Kazi cha Kimkakati cha Maafisa Utamaduni na Maafisa Maendeleo ya Michezo Tanzania akiwa sehemu ya wadau muhimu waliopewa dhamana ya kusimamia maadili katika Taaluma ya Habari nchini.

Moja ya mada zilizopewa kipaumbele katika Kikao Kazi hicho kilichozinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ni Mmomonyoko wa Maadili ya Mtanzania.
Kikao Kazi hicho cha siku 4 cha Mafundo na Mazingativu kilichoandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kinafanyika katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam kuanzia leo tarehe 22 hadi 25 Aprili, 2025.
Mbali na kuwashirikisha Maafisa Utamaduni na Maafisa Maendeleo ya Michezo Kikao Kazi hicho kimewakutanisha Wakuu wa Taasisi na viongozi wa vyama vya Michezo, Sanaa na Utamaduni.

Kauli Mbiu ya Kikao Kazi hicho ni "Utamaduni, Sanaa na Michezo, Msingi wa Maadili ya Mtanzania, Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025".
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Wakili Patrick Kipangula (pichani) ameshiriki Kikao Kazi cha Kimkakati cha Maafisa Utamaduni na Maafisa Maendeleo ya Michezo Tanzania