Articles by "MICHEZO"
Showing posts with label MICHEZO. Show all posts
Na Mwandishi Wetu, Mtwara

Benki ya Exim imejitokeza kuwa mdhamini mkuu wa mbio za Kilomita 5 katika msimu wa nne wa Korosho Marathon, tukio kubwa la michezo lililofanyika mkoani Mtwara likilenga kuhamasisha afya, ustawi wa vijana na mshikamano wa jamii.

Akizungumza wakati wa mbio hizo, mgeni rasmi ambaye pia ni Waziri wa Vijana, Mheshimiwa Joeli Nanauka, alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wadau mbalimbali katika kukuza afya na maendeleo ya kijamii kupitia michezo. Alisema kuwa michezo ni nyenzo muhimu katika kuibua vipaji, kujenga umoja na kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli chanya za maendeleo.
“Tunazo fursa nyingi kupitia michezo—si tu kuongeza afya zetu, bali pia kujenga mahusiano bora na kuimarisha mshikamano wa kijamii. Tunapongeza Exim kwa kuonesha mfano wa kujitoa katika kuunga mkono juhudi hizi,” alisema Waziri

Kwa upande wake, Exim Bank ilieleza kuwa udhamini huo ni sehemu ya nafasi yake ya kuchangia maendeleo ya jamii na kuunga mkono shughuli zinazowagusa wananchi moja kwa moja. Benki hiyo imerejea dhamira yake ya kuendelea kushiriki miradi yenye manufaa kwa jamii, ikisisitiza kuwa michezo ni jukwaa muhimu katika kuhamasisha maisha bora, kukuza vipaji na kuimarisha umoja wa wananchi.
Kipa wa Simba SC, Moussa Camara, ametuliza mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi baada ya kuthibitisha kuwa upasuaji wa goti lake umefanyika kwa mafanikio. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Camara aliweka picha ikionyesha mguu wake ukiwa umefungwa bandeji na kueleza kuwa hatua hiyo muhimu imeenda vyema.

“Alhamdulillah, upasuaji wa goti langu umekamilika kwa mafanikio. Asante kwa uongozi wa Simba SC Tanzania na wakala wangu VISMA kwa juhudi na weledi wao. Tutaonana hivi karibuni nikiendelea na kazi,” ameandika Camara.

Ujumbe huo umetuliza hisia za mashabiki waliokuwa na hofu juu ya maendeleo ya jeraha lake, hususan baada ya sintofahamu iliyojitokeza awali kuhusu kusita kwake kufanyiwa upasuaji. Sasa, taarifa hii mpya inaashiria kuwa kurejea kwake uwanjani kunaweza kuanza kuhesabika.

Taarifa hizo zimepokelewa kwa hamasa kubwa na mashabiki wa Simba SC ambao wamejaa matumaini ya kumuona mlinda mlango wao namba moja akirejea kwa nguvu mpya kuelekea michezo ijayo ya ligi na michuano ya kimataifa.

Camara amehitimisha ujumbe wake kwa kuashiria kuwa yuko kwenye maandalizi ya kurejea uwanjani mara tu atakapomaliza hatua za awali za matibabu na mazoezi ya kuimarisha goti lake.
Kipa namba moja wa Simba, Moussa Camara, hatimaye ameondoa sintofahamu iliyokuwa ikizunguka mustakabu wa jeraha lake baada ya kukubali kusitisha mgomo na kuridhia kufanyiwa upasuaji wa goti lake nje ya nchi. Hatua hii imehitimisha mvutano wa wiki kadhaa kati yake na uongozi wa klabu, ambao ulianza mara baada ya madaktari kupendekeza kuwa jeraha lake linahitaji upasuaji wa moja kwa moja ili arejee kwenye ubora wake.

Camara alikuwa anasita kukubali mapendekezo hayo licha ya vipimo kuonyesha wazi kuwa jeraha lake halitapona bila upasuaji. Msimamo wake huo uliiacha Simba kwenye wakati mgumu, hasa kutokana na umuhimu wa mchezaji huyo katika mechi kubwa za ligi na michuano ya kimataifa. Mgomo huo ulisababisha kukosa michezo kadhaa na kuleta presha kwa benchi la ufundi lililotaka suala hilo likamilishwe haraka.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya klabu, mazungumzo ya faragha na viongozi wa juu wa Simba yameleta muafaka, na sasa taratibu zote za safari na matibabu yake zimekamilishwa. Inatarajiwa kuwa upasuaji utafanyika katika siku chache zijazo, huku ripoti za kitabibu zikionyesha matumaini makubwa ya Camara kurejea katika ubora wake mara baada ya programu ya ukarabati.

Kutokuwepo kwa kipa huyo kumeigharimu timu, na mashabiki wengi wamekuwa na hamu kubwa ya kuona suala hilo linamalizika ili kurejesha utulivu langoni. Wadau wa soka ndani ya klabu wanaamini kurejea kwake baada ya matibabu kutaimarisha ushindani ndani ya kikosi na kuongeza uimara katika mbio za ubingwa msimu huu.

Benchi la ufundi limeelezea faraja kubwa kufuatia uamuzi huo, likisema kuwa Camara ni sehemu muhimu ya mfumo wa timu, na kurejea kwake kutaleta mabadiliko makubwa katika matokeo ya timu.
Na Mwandishi Wetu, Michezo

Nyota wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, amezungumza kwa uwazi kuhusu hali yake ya kifedha, akisema licha ya kutajwa kuwa bilionea, bado anajiona “maskini” kwa sababu ya majukumu makubwa anayobeba kwa familia na jamii inayomtegemea.

Akihojiwa na mwandishi maarufu Morgan, Ronaldo alifichua kuwa alifikia hadhi ya kuwa bilionea akiwa na umri wa miaka 39, lakini bado anaendelea kutafuta fedha kwa bidii kila siku.

“Mwezi mmoja uliopita watu walisema mimi ni bilionea, lakini ukweli ni kwamba nilikuwa bilionea nikiwa na miaka 39,” alisema Ronaldo. “Ninaheshimu mali zangu, fedha zangu na kila kitu ninachomiliki. Nina HR wangu ambaye tunawasiliana mara mbili kwa siku — asubuhi na usiku — kujua nini kimeingia, kimepungua na nini cha kufanya kuongeza zaidi.”

Hata hivyo, Ronaldo alisisitiza kuwa pamoja na utajiri huo, bado hajitoshelezi kifedha kwa sababu ana wajibu mkubwa wa kusaidia watu wengi wanaomtegemea.

“Mimi ni baba, lakini pia nina jamii kubwa nyuma yangu. Kila mwezi nachangia zaidi ya milioni 450 za Tanzania kusaidia familia na watu wanaonihitaji. Hivyo, siwezi kusema nina pesa nyingi, maana bado nina kazi ya kutafuta zaidi,” alisema nyota huyo wa Al-Nassr.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, Ronaldo ndiye mchezaji anayelipwa zaidi duniani, akiwa na mkataba wa mamilioni ya dola kwa mwaka, lakini kauli yake imeonyesha upande wa utu na uwajibikaji wa kijamii unaokwenda mbali zaidi ya umaarufu na fedha.

Mashabiki wengi mitandaoni wameitafsiri kauli hiyo kama somo muhimu kuhusu unyenyekevu na kujituma, huku wengine wakisema Ronaldo amethibitisha kwamba “tajiri wa kweli ni yule anayejua kutumia utajiri wake kusaidia wengine.”

Dar es Salaam — Klabu ya Azam FC imepiga hatua kubwa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya KMKM ya Zanzibar katika mchezo wa marudiano wa Hatua ya 32 Bora uliopigwa jioni ya jana katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Ushindi huo umeifanya Azam FC kufuzu hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 9-0, baada ya awali kushinda 2-0 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Oktoba 18 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Katika mchezo wa jana, Azam FC ilionekana kutawala dakika zote, ikicheza soka la kasi na kushambulia kwa mpangilio ambao uliwaweka KMKM katika wakati mgumu. Mabao yalipatikana kutokana na umakini wa safu ya ushambuliaji na nidhamu ya kiufundi iliyoongozwa na benchi la ufundi la timu hiyo.

Wamiliki wa klabu hiyo, Yussuf Bakhresa, Omar Bakhresa na Abubakar Bakhresa, walikuwepo jukwaani kushuhudia ushindi huo mkubwa, wakionekana kufurahishwa na kiwango kilichooneshwa na timu yao huku wakishangilia kila bao lililofungwa.

Kocha wa Azam FC aliipongeza timu yake kwa kujituma na kuonesha nidhamu ya mchezo, akisema ushindi huo ni mwanzo wa safari ndefu katika michuano hii. “Tumepambana, tumeonesha ubora, lakini safu ya ushindani inaendelea kuwa ngumu kadri tunavyoingia hatua ya makundi. Tunatakiwa kuongeza umakini zaidi,” alisema.

Kwa matokeo haya, Azam FC sasa inaungana na klabu nyingine 15 za Afrika kwenye hatua ya makundi ambayo itaanza kutimua vumbi hivi karibuni, ambapo droo ya upangaji wa makundi inasubiriwa kutangazwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Mashabiki wa Azam FC wametajwa kuongeza ari kwa wachezaji huku wengi wakiamini mwaka huu huenda klabu hiyo ikafanya historia kubwa katika michuano ya kimataifa.

NAIROBI, KENYA – Rais William Ruto ameipongeza timu ya taifa ya soka ya wanawake, Harambee Starlets, kwa ushindi wa mabao 3-1 walioupata dhidi ya Gambia katika mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) unaotarajiwa kufanyika nchini Morocco mwaka 2026.

Kupitia ujumbe wake kwa taifa, Rais Ruto alisema ushindi huo ni ushahidi wa nidhamu, vipaji na ari ya kupambana iliyooneshwa na wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

"Hongera kwa Harambee Starlets kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Gambia, ushindi unaotuvusha hatua moja karibu zaidi na kufuzu WAFCON 2026," alisema Rais Ruto.
Aidha, alisifu uwekezaji na usimamizi wa timu, akibainisha kuwa mafanikio ya Starlets ni sehemu ya kuimarika kwa nafasi ya Kenya katika michezo ya wanawake barani Afrika.

"Ushindi huu unaonesha nidhamu, kipaji na dhamira ya wachezaji wetu, pamoja na uongozi madhubuti wa benchi la ufundi. Mmeliletea taifa letu heshima na kutuonesha ukuaji wa nguvu ya michezo ya wanawake nchini," aliongeza.

Rais Ruto aliwahimiza wachezaji kuendeleza ari hiyo wanapojiandaa kwa mchezo wa marudiano, akisisitiza kuwa taifa lote lipo nyuma yao.
"Tunaposubiri mchezo wa marudiano, tambueni kwamba taifa zima lipo pamoja nanyi. Ushindi wenu ni fahari yetu. Endeleeni kung’ara, endeleeni kushinda, na roho ya Harambee iendelee kutuunganisha kama taifa," alisema.

Rais alimalizia kwa ujumbe wa hamasa, akisema: "Hongera Starlets! Kama nilivyoahidi, nitacheza kama mimi."
NAIROBI, KENYA – Rais William Ruto ameongoza hafla ya kihistoria katika Ikulu ya Nairobi kuadhimisha kuwasili kwa Ngao ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), tukio ambalo linatajwa kuwa ishara ya nafasi muhimu ambayo Kenya inazidi kuchukua katika ramani ya michezo ulimwenguni.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Ruto alisema kuwa Kenya imejaa vijana wenye vipaji na uwezo wa kuleta heshima ya kimataifa endapo watawekewa mazingira bora kupitia uwekezaji makini katika miundombinu ya michezo.

"Sisi ni taifa lenye vipaji vya kiwango cha juu vinavyostahili jukwaa la dunia. Vijana wetu wana uwezo mkubwa, na jukumu letu kama serikali ni kuhakikisha tunawawezesha kufikia kilele cha mafanikio," alisema Rais Ruto.
Rais alibainisha kuwa serikali yake imeanza na inaendelea kuboresha viwanja vikubwa na madogo kote nchini. Alisema ujenzi wa viwanja vipya, ukarabati wa vile vilivyopo na uwekezaji katika programu za mafunzo kwa vijana ni sehemu ya mpango mpana wa kuandaa mabingwa wa kesho.

"Tunajenga miundombinu ya kisasa ya michezo katika kila kona ya nchi. Hii ni pamoja na viwanja, vituo maalum vya mafunzo, na ushirikiano na mashirika ya kimataifa ili kuhakikisha vijana wetu wanapata fursa sawa na wenzao duniani," aliongeza.

Kuwasili kwa kombe hilo nchini kumetajwa kama tukio linalolenga kuongeza hamasa miongoni mwa vijana na wadau wa michezo, huku likiwaalika kuona kwamba mafanikio ya kiwango cha kimataifa yanapatikana kupitia nidhamu, mafunzo bora, na juhudi za pamoja.

Wadau wa michezo wamepongeza hatua za serikali wakisema ni ishara ya mwelekeo mpya unaotegemea matokeo, hali inayoweza kuifanya Kenya kuwa kitovu cha vipaji barani Afrika.
Rais wa Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (BD) Bw. Shendu Hamis Mwagalla, akikabidhi cheti cha kutambua mchango wa udhamini kwa Bi. Gemma Kamara, Mkuu wa Idara ya Bei za vifurushi na makundi maalumu ya wteja kutoka Vodacom Tanzania PLC, kama ishara ya kuthamini mchango wa kampuni hiyo katika kuendeleza mchezo wa mpira wa kikapu nchini. Kupitia udhamini huo, Vodacom imeboresha uwanja wa Don Bosco Oysterbay, kudhamini zawadi za washindi wa kwanza, pili na tatu, na kuendeleza programu za kuwawezesha vijana kupitia michezo. Tukio hilo limefanyika katika hafla ya utoaji tuzo za Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Dar es Salaam (BDL) 2025, mwanzoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam, 13 Oktoba 2025: Vodacom Tanzania PLC kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (BDL) waliandaa hafla ya tuzo maalum jijini Dar es Salaam, ikiwa ni kilele cha msimu wa Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Dar es Salaam (BDL) 2025.

Hafla hiyo ilikusudia kusherehekea mafanikio ya wachezaji, timu na wadau walioshiriki msimu mzima, huku ikiangazia athari chanya za uwekezaji wa Vodacom katika kukuza michezo na vijana nchini.

Ligi ya mwaka huu ilihusisha jumla ya timu 277, kwa upande wa wanawake na wanaume zilizoshiriki katika mashindano yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Don Bosco Oysterbay, ambao umekarabatiwa na Vodacom kama sehemu ya dhamira yake ya kukuza vipaji na kuinua ari ya vijana kupitia michezo. Tuzo na zawadi zilitolewa kwa mabingwa wa msimu huu pamoja na wachezaji bora wa kike na wa kiume, waliodhihirisha nidhamu na ubunifu uwanjani.
Akizungumza katika halfa hiyo Mkuu wa Idara ya bei za vifurushi na makundi maalum ya wateja, Gemma Kamara Alisema “Kwa Vodacom, ushirikiano huu na BD ni zaidi ya udhamini wa michezo. Ni njia ya kushirikiana na jamii katika kuwawezesha vijana kutambua uwezo wao. Tumejifunza mengi kupitia ligi hii, kuona vijana wakikua, wakijiamini, na kutumia michezo kama nguzo ya maendeleo binafsi na kijamii. Vodacom itaendelea kuwa mstari wa mbele kuwawezesha vijana kupitia michezo, elimu, na teknolojia kama nguzo kuu za kuwasaidia kufikia ndoto zao.

Kwa upande wake, Mpoki Mwakipake, Katibu wa Shirikisho la Mpira wa kikapu, aliishukuru Vodacom kwa mchango wake mkubwa katika kuendeleza mchezo wa mpira wa kikapu nchini. “Ushirikiano kati ya BD na Vodacom umeleta mabadiliko makubwa katika mchezo huu.

Tumeshuhudia ongezeko la ari, nidhamu na ushindani wa kweli. Ni heshima kubwa kuona vijana wetu wakifikia viwango vya juu zaidi” alisema Mpoki Mwakipale, Katibu wa Shirikisho la Mpira wa kikapu.
“Moja ya changamoto kubwa tunayokutana nayo kama wachezaji ni ukosefu wa miundombinu bora ya michezo,” alisema Nadia Samir, mchezaji wa Don Bosco Troncatti. “Lakini mwaka huu tumefarijika kuona mabadiliko makubwa uwanja wa Don Bosco umeboreshwa kwa udhamini wa Vodacom, ligi imekuwa ya ushindani zaidi. Tungependa kuona wadhamini wengine wakijitokeza ili kuendelea kuboresha mpira wa kikapu nchini Tanzania.”

Kwa upande wa wanaume, Dar City Basketball Team waliibuka mabingwa baada ya ushindani mkali katika michezo ya fainali dhidi ya wapinzani wao JKT, wakijinyakulia zawadi ya shilingi milioni 10 kutoka Vodacom. Kwa upande wa wanawake, DB Lioness Basketball Team walitawala uwanjani na kutwaa taji la ubingwa wa BDL 2025, nao wakipokea zawadi ya shilingi milioni 10 kama sehemu ya kutambua jitihada na mafanikio yao.
Kupitia miradi kama hii, Vodacom inaendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuwa mshirika wa maendeleo kwa vijana wa Kitanzania ikitumia michezo, elimu na teknolojia kama nyenzo za kujenga kizazi kinachojiamini, chenye dira na matumaini ya kesho iliyo bora.

Hafla ya utoaji tuzo ilihudhuriwa na Vodacom, BD, wadau wa michezo, familia za wachezaji na waandishi wa habari. Usiku huo ulipambwa na muziki, furaha na shangwe za vijana waliotimiza ndoto zao kupitia mchezo wa mpira wa kikapu.
Washindi wa Vodacom Tanzania Open 2025 wakiwa katika picha ya pamoja jijini Arusha, wakiwemo Njoroge Kibugu (Kenya) kwa upande wa wanaume na Madina Idd (Tanzania) kwa upande wa wanawake. Mashindano haya yalishirikisha wachezaji zaidi ya 150 kutoka nchi nane barani Afrika, yakionyesha vipaji vya kipekee na ushindani wa hali ya juu.

Na Mwandishi Wetu. 

Arusha, 5 Oktoba 2025: Mashindano maarufu ya Vodacom Tanzania Open 2025 yamehitimishwa katika mandhari ya kuvutia ya Kilimanjaro Golf & Wildlife Estate (Kiligolf) jijini Arusha kwa hafla ya utoaji wa zawadi iliyoambatana na shamrashamra. Mashindano haya ya siku nne yaliwaleta pamoja wachezaji wa golf wa rika na viwango tofauti kutoka maeneo mbalimbali ya Africa, yakifungua ukurasa muhimu katika kalenda ya golf hapa nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Vodacom Tanzania PLC, Bw. David Tarimo, aliyaelezea mashindano hayo kuwa ya mafanikio makubwa, “tumekuwa na siku nne za kipekee. Tumeshuhudia ushindani wa kusisimua, vipaji vya kustaajibsha na shauku kubwa kwa michezo. Kuanzia wachezaji wa kitaalamu hadi wale wanaochipukia, mashindano haya yamewaleta pamoja washiriki wa aina mbalimbali wapatao 150, na kuyafanya kuwa miongoni mwa mashindano ya kukumbukwa zaidi.”

Aliendelea kusisitiza dhamira ya Vodacom katika michezo na teknolojia akisema, “golf inaakisi maadili yetu tunayoyathamini, usahihi, nidhamu na fikra za kimkakati. Kama mdhamini kwa mwaka wa tatu mfululizo, tunawekeza katika jukwaa linaloinua vipaji vya ndani, linakuza ushirikiano wa kikanda, na kuiweka Tanzania kama kituo cha matukio ya michezo ya kiwango cha kimataifa. Mwaka huu, tumeunganisha teknolojia ya kisasa katika mashindano haya kuanzia taarifa za matokeo ya moja kwa moja hadi uzoefu wa mashabiki unaoendeshwa na mtandao wa Vodacom.”
Mashindano ya Vodacom Tanzania Open 2025 yamesajiliwa katika viwango vya World Amateur Golf Ranking (WAGR) na yanaendana na dhamira pana ya Vodacom ya kuwawezesha jamii kupitia michezo, ujumuishaji na matokeo chanya endelevu.

Akiongeza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Golf nchini Tanzania (TGU), Bw. Gilman Kasiga, alisifia ushirikiano huo na mchango wa mashindano hayo katika mchezo wa huo nchini, “tunajivunia kushirikiana na Vodacom Tanzania kwa mashindano ya mwaka huu. Dhamira yao ya ubora na ubunifu imepandisha kiwango cha mashindano ya golf nchini. Tukio hili limeonyesha vipaji vya hali ya juu na pia limeonyesha jinsi ushirikiano wa kimkakati unavyoweza kukuza michezo na kuhamasisha jamii. Kwa mwaka wa tatu mfululizo, Vodacom imesimama nasi, ikionyesha kujitolea kwake katika kukuza michezo na vipaji hapa nchini.”
Mashindano haya yametoa zawadi kubwa kwa washindi wa makundi ya kitaalamu na ya ridhaa, ambapo washindi wa juu wa kitaalamu walipokea hadi shilingi 8.2 milioni, huku zawadi za fedha zikitolewa kwa washiriki 22 wa juu. Mshindi wa juu wa ridhaa pia alitunukiwa zawadi ya shilingi 2.5 milioni, ikionyesha dhamira ya mashindano haya ya kusherehekea ubora katika viwango vyote vya mchezo.

Washindi walipatikana kwa kuzingatia matokeo ya siku nne za mchezo wa stroke play, kwa mujibu wa kanuni za Golf zilizopitishwa na R&A na USGA, na zikisaidiwa na kanuni za ndani za Kiligolf.

Kadri Vodacom inavyosherehekea miaka 25 ya kuwaunganisha Watanzania, kampuni hiyo inaendelea kujenga urithi wa ubora katika uwanja wa golf, ndani ya jamii na katika ukanda mzima wa Afrika mashariki.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) limetangaza kikosi cha timu ya taifa ya mabondia 26 pamoja na benchi la ufundi lenye watu 9, kitakachoiwakilisha nchi katika Mashindano ya Kanda ya 3 Afrika yatakayofanyika Nairobi, Kenya kuanzia Oktoba 14 hadi 25, 2025.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga, imeeleza kuwa kikosi hicho kimeteuliwa kufuatia mashindano ya Klabu Bingwa ya Taifa yaliyomalizika hivi karibuni, na sasa kiko tayari kupambana ili kuipatia Tanzania heshima katika jukwaa la kimataifa.

Mashindano ya Nairobi yanatarajiwa kuwa jaribio la kwanza la kimataifa kuelekea maandalizi ya michezo ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth Games) yatakayofanyika Glasgow, Scotland kuanzia Julai 23 hadi Agosti 2, 2026, ambapo Tanzania itashiriki rasmi.

Kwenye orodha ya mabondia walioteuliwa, upande wa wanaume unaongozwa na Juma Athumani (MMJKT) atakayepigania uzito wa 46-48kg (minimumweight), Azizi Chala (Ngome) uzito wa 48-51kg, na Faki Issa wa Jeba Tanga (bantamweight). Pia wamo bondia machachari kama George Costantino (Ngome), Ezra Paulo (Ngome), Rashid Mrema (Polisi), pamoja na Maximillian Patrick (MMJKT) atakayepigania uzito wa juu kabisa, super heavyweight (92kg+).

Kwa upande wa wanawake, timu inajivunia vipaji vya mabondia kama Martha Kimaro (Ngome), Aisha Hamisi (JKT), Sarafina Fusi (Ngome), pamoja na Veronica Ebroni (Magereza) ambaye atawakilisha taifa kwenye uzito wa juu (heavyweight).

Aidha, benchi la ufundi linaongozwa na Samwel Kapungu (Mwalimu Mkuu - BFT) akisaidiana na Mzonge Hassani (Ngome), pamoja na walimu wengine kutoka MMJKT, Ngome na Polisi. Pia kuna waamuzi, matron Fatuma Manzi (MMJKT) na daktari wa timu Mussa Magolima (BFT).

Akizungumzia maandalizi hayo, Mashaga alisema kuwa Tanzania ina matarajio makubwa kutokana na maandalizi mazuri na ari ya wachezaji waliochaguliwa.

“Tunakwenda Nairobi tukiwa na dhamira ya dhati ya kupima kiwango chetu na kuhakikisha tunaandaa timu imara kuelekea michezo ya Jumuiya ya Madola 2026. Kikosi hiki kina wachezaji wenye vipaji na uzoefu wa kutosha,” alisema.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa kivutio kikubwa, huku Tanzania ikitarajia kufanya vizuri na kushinda medali ili kuendelea kujijengea heshima katika ramani ya ngumi za kimataifa.

Dar es Salaam, 23 Septemba 2025: Vodacom Tanzania Plc kwa kushirikiana na Chama cha Gofu Tanzania, imejitokeza kama mdhamini mkuu wa mashindano ya Vodacom Tanzania Open, yanayotarajia ushiriki wa wachezaji zaidi ya 150 wa gofu kutoka Tanzania na nchi za mashariki na kusini mwa Afrika.

Ushirikiano huu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuendeleza michezo ya gofu katika msimu wa tatu hapa jijini Dar es Salaam na visiwani Zanzibar. Vodacom ikiwa inaadhimisha miaka 25 inalenga kujikita kama mtandao namba moja unaounga mkono mchezo wa gofu nchini Tanzania.

Tanzania Open si mashindano pekee, bali ni jukwaa la kuonesha vipaji, mshikamano katika michezo na ubunifu wa kidijitali. Kupitia ubia huu, Vodacom inaleta mapinduzi katika mchezo wa gofu kwa kuunganisha urithi wa mchezo huu na teknolojia ya kisasa, huku ikikuza ushirikishwaji wa jamii na ujumuishi kwenye michezo.
Akizungumza katika uzinduzi wa mashindano haya, Mkuu wa idara ya masoko na uwezeshaji Vodacom Business, Joseph Sayi, alisema:


“Ushirikiano wetu na Tanzania Open unaonyesha dhamira ya Vodacom katika kukuza michezo nchini Tanzania huku tukionesha namna teknolojia inavyoweza kuboresha maisha ya wananchi hata kupitia michezo. Kuanzia huduma za mtandao hadi huduma za malipo kwa kutumia M-Pesa, tunahakikisha kila mmoja anapata uzoefu wa kipekee ndani na nje ya uwanja.”

Pia, mwenyekiti wa Chama cha Gofu Tanzania, Gilman Kasiga, alisema:
Mashindano ya Vodacom Tanzania Open 2025 ni tukio la kihistoria kwa mchezo wa gofu na kwa taifa letu. Kwa mwaka wa tatu mfululizo, Vodacom imeendelea kuwa bega kwa bega nasi kama mdhamini mkuu, jambo linalodhihirisha dhamira yao ya kuendeleza michezo na kukuza vipaji nchini. Kama mashindano makuu ya Chama cha Gofu Tanzania, Vodacom Tanzania Open siyo tu jukwaa la kuonesha umahiri wa wachezaji wetu wa kulipwa na wale wa kiwango cha juu, bali pia ni chanzo cha hamasa na matumaini kwa kizazi kipya cha wachezaji.

Tunajivunia kuona vijana, wanawake, na wachezaji chipukizi wakishiriki kwa pamoja, jambo linaloashiria dhamira ya dhati ya TGU katika kukuza ushirikishwaji, maendeleo, na ukuaji endelevu wa mchezo huu. Kupitia ushirikiano wetu naVodacom, tunaonesha namna ambavyo gofu si mchezo pekee bali ni nyenzo ya kukuza utalii, uwekezaji, ajira na fursa nyingi za kijamii na kiuchumi nchini Tanzania. Mashindano haya ni ya ubora wa kimataifa, na tunawaalika wadau wote wa gofu pamoja na umma kushiriki nasi katika kusherehekea mchezo huu wa heshima na hadhi ya kipekee.
Kwa kuhitimisha, Mkuu wa idara ya masoko na uwezeshajiVodacom Business, Joseph Sayi, alieleza:

“Vodacom Tanzania Open ni mfano halisi wa kuunganisha urithi wa michezo na ubunifu wa teknolojia ya kisasa. Sisi Vodacom tunajivunia kuwa sehemu ya mashindano haya. ”

Ushirikiano kati ya Vodacom Tanzania na Chama cha Gofu Tanzania ni hatua kubwa katika kuimarisha nafasi ya Tanzania kwenye ramani ya gofu ya kikanda, huku ikisukuma mbele dhamira ya Vodacom ya jamii iliyounganishwa kidijitali.
Mwanariadha mahiri wa Tanzania, Alphonce Felix Simbu, ameandika historia mpya kwa kuipa nchi medali ya kwanza ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya riadha yanayoendelea jijini Tokyo, Japani.

Simbu alitinga kileleni baada ya kukimbia kwa muda wa saa 2:09:48, akiwashinda wapinzani wake kwa ushindani mkubwa. Alimzidi kwa sekunde chache tu mkimbiaji kutoka Ujerumani, Amanol Petros, ambaye alimaliza wa pili kwa tofauti ndogo ya sekunde 0.03.

Ushindi huu umeweka Tanzania kwenye ramani ya dunia ya riadha na kumfanya Simbu kuwa shujaa mpya wa michezo nchini.
RAIS SAMIA ATOA PONGEZI

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliandika:

“Hongera sana Simbu! Ushindi huu si wa kwako pekee bali ni wa Watanzania wote. Umeonyesha uthubutu, nidhamu na moyo wa kizalendo unaoipa heshima nchi yetu. Serikali itaendelea kukuunga mkono pamoja na wanariadha wengine ili michezo iwe chanzo cha heshima na furaha ya taifa letu.”

Aidha, Rais Samia alimtaja Simbu kama kielelezo cha matumaini kwa kizazi kipya cha wanamichezo na akasisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya bidii na kujituma.

TAIFA LAJIVUNIA

Kwa mara ya kwanza katika historia, bendera ya Tanzania imepepea juu kwenye mashindano ya dunia ya riadha jijini Tokyo. Ushindi wa Simbu umepokewa kwa shangwe na matumaini mapya ya kuwa taifa la ushindani katika michezo ya kimataifa.