Kipa wa Simba SC, Moussa Camara, ametuliza mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi baada ya kuthibitisha kuwa upasuaji wa goti lake umefanyika kwa mafanikio. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Camara aliweka picha ikionyesha mguu wake ukiwa umefungwa bandeji na kueleza kuwa hatua hiyo muhimu imeenda vyema.
“Alhamdulillah, upasuaji wa goti langu umekamilika kwa mafanikio. Asante kwa uongozi wa Simba SC Tanzania na wakala wangu VISMA kwa juhudi na weledi wao. Tutaonana hivi karibuni nikiendelea na kazi,” ameandika Camara.
Ujumbe huo umetuliza hisia za mashabiki waliokuwa na hofu juu ya maendeleo ya jeraha lake, hususan baada ya sintofahamu iliyojitokeza awali kuhusu kusita kwake kufanyiwa upasuaji. Sasa, taarifa hii mpya inaashiria kuwa kurejea kwake uwanjani kunaweza kuanza kuhesabika.
Taarifa hizo zimepokelewa kwa hamasa kubwa na mashabiki wa Simba SC ambao wamejaa matumaini ya kumuona mlinda mlango wao namba moja akirejea kwa nguvu mpya kuelekea michezo ijayo ya ligi na michuano ya kimataifa.
Camara amehitimisha ujumbe wake kwa kuashiria kuwa yuko kwenye maandalizi ya kurejea uwanjani mara tu atakapomaliza hatua za awali za matibabu na mazoezi ya kuimarisha goti lake.



Toa Maoni Yako:
0 comments: