Mwanariadha mahiri wa Tanzania, Alphonce Felix Simbu, ameandika historia mpya kwa kuipa nchi medali ya kwanza ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya riadha yanayoendelea jijini Tokyo, Japani.
Simbu alitinga kileleni baada ya kukimbia kwa muda wa saa 2:09:48, akiwashinda wapinzani wake kwa ushindani mkubwa. Alimzidi kwa sekunde chache tu mkimbiaji kutoka Ujerumani, Amanol Petros, ambaye alimaliza wa pili kwa tofauti ndogo ya sekunde 0.03.
Ushindi huu umeweka Tanzania kwenye ramani ya dunia ya riadha na kumfanya Simbu kuwa shujaa mpya wa michezo nchini.

RAIS SAMIA ATOA PONGEZI
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliandika:
“Hongera sana Simbu! Ushindi huu si wa kwako pekee bali ni wa Watanzania wote. Umeonyesha uthubutu, nidhamu na moyo wa kizalendo unaoipa heshima nchi yetu. Serikali itaendelea kukuunga mkono pamoja na wanariadha wengine ili michezo iwe chanzo cha heshima na furaha ya taifa letu.”
Aidha, Rais Samia alimtaja Simbu kama kielelezo cha matumaini kwa kizazi kipya cha wanamichezo na akasisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya bidii na kujituma.
TAIFA LAJIVUNIA
Kwa mara ya kwanza katika historia, bendera ya Tanzania imepepea juu kwenye mashindano ya dunia ya riadha jijini Tokyo. Ushindi wa Simbu umepokewa kwa shangwe na matumaini mapya ya kuwa taifa la ushindani katika michezo ya kimataifa.








Toa Maoni Yako:
0 comments: