Articles by "HABARI ZA KIJAMII"
Showing posts with label HABARI ZA KIJAMII. Show all posts
Dar es Salaam. Tarehe 27 Aprili 2024: Katika kuunga mkono juhudi za kuboresha elimu nchini, Benki ya CRDB imeasaini mkataba wa ushirikiano na Chama cha Wawekezaji katika Elimu Tanzania (TAPIE) utakaowawezesha wanachama wake kupata mikopo nafuu ya kuboresha miundombinu na kuwezesha uendeshaji wakati wote.


Mkataba huo umesainiwa tarehe 27 Aprili 2024 kwenye mkutano mkuu wa 5 wa mwaka wa TAPEI uliofunguliwa na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt Doto Biteko na kuhudhuriwa na wadau wa elimu nchini.
Akizungumza na wajumbe waliohudhuria mkutano mkuu huo, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema Benki inatambua changamoto wanazokutana nazo wamiliki binafsi wa shule hivyo imechukua hatua za kusaidia kuzitatua ili kuwa na mazingira rafiki kwa wanafunzi kusoma na kujifunza.


“Ni ukweli usiopingika kuwa elimu ndio msingi wa maendeleo ya Taifa lolote lile duniani kwani husaidia kujenga maarifa, ujuzi na kuongeza ufanisi hivyo kuwa kichocheo muhimu katika ukuaji wa uchumi. Kwa kuyatambua haya yote, Benki ya CRDB imeiweka sekta ya elimu katika moja ya vipaumbele vyake vya uwezeshaji. Tunafanya hivi ikiwa ni sehemu za kusaidia jitihada za Serikali pamoja na wadau wa sekta hii kutoa elimu bora itikayozalisha rasilimali watu bora katika nyanja mbalimbali,” amesema Raballa.


Kwa kuzitambua changamoto zilizopo ukiwamo ukweli kwamba uendeshaji wa shule unategemea mapato yatokanayo na ada ambayo mara nyingi hukusanywa shule zinapofunguliwa hivyo kuwa na uhaba pindi zinapofungwa, Benki ya CRDB imewaletea mkopo wa uendeshaji ili kukidhi mahitaji yanayopaswa kulipiwa wakati mapato mengine yakisubiriwa indi muhula mpya utakapoanza.
Raballa pia amesema shule nyingi zipo kwenye maeneo ambayo hayajarasmishwa jambo linalowanyima wamiliki uwezo wa kukopa kutokana na kutokidhi vigezo vya dhamana hivyo Benki ya CRDB imewaletea suluhisho kwa kuwaruhusu kukopa fedha zitakazowezesha urasmishaji wa maeneo yao ili kupata hati ya wizara itakayowaruhusu kukopa ili kuimarisha biashara zao.


“Tunawaruhusu wamiliki wa shule kukopa mpaka shilingi milioni 10 kwa ajili ya kurasmisha maeneo ya shule. Fedha hizi ni kwa ajili ya kutafuta hati ya wizara hivyo kuyatambulisha maeneo yao ya kisheria. Vilevile, tunayo mikopo kwa dhamana zisizo rasmi yaani maeneo ya shule ambayo hayana hati. Benki yetu inamruhusu mmiliki kuja kukopa mpaka shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya shule. Tunaamini kwa utaratibu huu rahisi na rafiki, tutasaidia kuwezesha uwekezaji wa shule katika sekta binafsi,” amesema Raballa.
Wakati wamiliki wakipewa mkopo wa uwekezaji wanaoweza kuurejesha mpaka kwa miaka 7, Raballa amesema walimu na wafanyakazi wa shule binafsi nao wanaweza kupata mkopo kwa ajili ya kufanikisha mambo yao binafsi. Mikopo ya wafanyakazi hawa, amesema inajumuisha ‘salary advance’ ambao ni mahsusi kwa wale ambao mishahara yao inapitia Benki ya CRDB ambao wanaweza kupata mpaka asilimia 50 ya mshahara wao na wakalipa ndani ya siku 30 pamoja na mkopo wa binafsi unaofika mpaka shilingi milioni 100 zinazoweza kurejeshwa kwa mpaka miaka 8.


”Kwa miaka mitatu iliyopita, kiwango cha mikopo ya eimu tuliyoitoa kwa kundi hili imekuwa ikiongezeka. Mwaka 2021 Benki yetu ya CRDB ilikopesha zaidi ya shilingi bilioni 78.66 ambazo zilipanda mpaka shilingi bilioni 86 mwaka 2022 na mwaka jana zikawa shilingi bilioni 97.17. Nitumie fursa hii kuweka wazi kwamba mikopo hii tunayotoa kwa wamiliki wa shule binafsi hasa wanachama wa TAPIE, inaweza kurejeshwa mpaka kwa miaka 7,” amesisitiza Raballa.
Kwa upande wake, rais wa TAPIE, Mahmoud Mringo amesema hadi sasa kuna zaidi ya shule 6,362 zinazojumisha za awali 2,364, za msingi 2,270 na sekondari 1,728 zinazomilikiwa na watu binafsi, mashirika ya dini na yasiyo ya dini, majeshi, na jumuiya za wazazi ambazo zimedahili takriban wanafunzi 1,020,772 kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita ambazo zimeajiri takribani walimu 59,445 na wataalamumwengine zaidi ya 100,000 wenye taaluma na ujuzi mbalimbali kama wahasibu, madereva, wasimamizi na walezi wa wanafunzi, walinzi na wapishi. Ajira hizi zimesaidia kuinua hali za kimaisha kwa watu husika na kupanua wigo wa kodi mbalimbali na hivyo kukuza uchumi wa taifa.


“Ukitaka kujenga darasa, maabara au kuboresha miundombinu mingine ya shule, ni lazima uende kukopa benki lakini tatizo ni riba kubwa. Kujenga shule ndogo tu kwa sasa unahitaji walau shilingi bilioni 2 lakini kuwa na shule yenye kila kitu basi unahitaji shilingi bilioni 10. Ukizikopa hizi kutoka benki na ukalipa kwa riba iliyopo, itakuchukua miaka 20 ya kumaliza deni ambalo ni lazima lilipwe na mwanafunzi.


Bado kuna kodi na tozo 16 ambazo shule inatakiwa kulipa. Haya mambo yote yanaifanya elimu yetu kuwa ghali na kusoma shule zisizo za serikali inaonekana ni anasa,” amesema Mringo akiiomba serikali iangalie namna ya kupunguza riba ya mikopo tozo pamoja na kodi.
Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko amepongeza juhudi za sekta binafsi kuchangia kuboresha elimu nchini kwamba zinaifanya jamii iwe na mchango zaidi katika kukuza uchumi. "Niwapongeze kwa ushirikiano na mkataba wa makubaliano mnayosaini leo na Benki ya CRDB. Ili kufanikisha mambo, ushirikiano na wadau wengine ni muhimu sana. Hivi mnavyofanya, ndio namna nzuri ya kukabiliana na changamoto zetu," amesema Dkt Biteko.






Benki ya CRDB kupitia sera yake ya uwekezaji kwa jamii, Aprili 24 - 25, 2024 ilikabidhi madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Kikilo na madarasa mengine mawili katika Shule ya Msingi Isabe zote za wilayani Kondoa, mkoa wa Dodoma yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki hiyo.

Hafla ya kukabidhi madarasa hayo, iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi ambaye aliambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa pamoja na Maafisa Elimu Sekondari na Msingi.

Katika hafla zote mbili Dkt. Khamis Mkanachi ameishukuru Benki ya CRDB kwa kukubali maombi ya ujenzi wa madarasa katika Wilaya ya Kondoa, ambayo yapo katika vijiji vya Kikilo na Bukulu. Huku akitoa rai kwa wanafunzi kusoma kwa bidii kwani mazingira ya shule yanaendelea kuboreshwa.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa, Mashauri Vicent aliyekabidhiwa madarasa hayo ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya elimu pia kuahidi kuwa watahakikisha madarasa hayo yanakuwa ni sehemu ya kuchagiza ongezeko la wanufaika ambayo ni watoto kwenye jamii ya Kondoa.

Kwa upande wa Benki ya CRDB, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay aliyeongozana na Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji kwa Jamii pamoja na Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati, amesema kuwa Benki ya CRDB imeweka sera ya uwekezaji kwa jamii inayolenga kuchangia maendeleo mbalimbali katika jamii hasa katika swala la Elimu, Mazingira, Afya, Vijana na Wanawake. Aidha, ametoa rai kwa wazazi wa shule hizo kuendelea kushirikiana kwa karibu na uongozi wa shule katika kuboresha miundombinu ya shule.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay wakiwa pamoja na viongozi wengine pamoja na Wanafunzi katika moja ya madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 katika Shule ya Msingi Isabe, iliyopo katika kijiji cha Bukuru, Wilayani Kondoa, katika hafla  iliyofanyika Aprili 25, 202.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi (wanne kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay muda mfupi baada ya kukaidhi madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 kwa uongozi wa Halmashauri ya Kondoa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay (katikati) akiwa pamoja na viongozi wengine wa Benki ya CRDB pamoja na wa Halmashauri ya Kondoa wakiwa katika picha ya paamoja na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kikilo, muda mfupi baada ya kukaidhi madarasa mawili katika shule hiyo
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi akizungumza wakati wa hafla kukaidhi madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 kwa uongozi wa Halmashauri ya Kondoa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay akizungumza wakati wa hafla kukaidhi madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 kwa uongozi wa Halmashauri ya Kondoa.












Stanley Kafu, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Exim Bank, akizungumza wakati wa mahafali ya pili ya mpango endelevu wa kuwainua kiuchumi wanawake wajasiriamali ujulikanao kama WEP yaliyofanyika tarehe 23 Aprili, 2024, Mjini Arusha.
Mshindi wa kwanza Beatrice Alban Msafiri (wa pili kulia), Zainab Nungu Mkuu wa Kitengo cha Mikopo, Exim Bank (wa kwanza kushoto), na Faraja Nyalandu, Mkurugenzi Mtendaji wa Ndoto Hub (wa kwanza kulia) wakifurahi pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Exim Bank, Stanley Kafu wakati wa mahafali ya mafunzo ya ujasiriamali, biashara na uwezeshaji kwa wanawake wajasiriamali chini ya mradi wa benki hiyo yajulikanayo kama WEP katika tukio lililofanyika tarehe 23 Aprili 2024 mjini Arusha.
Mshindi wa tatu Rukia Said Mohamed (wa pili kulia), Zainab Nungu Mkuu wa Kitengo cha Mikopo, Exim Bank (wa kwanza kushoto), na Faraja Nyalandu, Mkurugenzi Mtendaji wa Ndoto Hub (wa kwanza kulia) wakifurahi pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Exim Bank, Stanley Kafu wakati wa mahafali ya mafunzo ya ujasiriamali, biashara na uwezeshaji kwa wanawake wajasiriamali chini ya mradi wa benki hiyo yajulikanayo kama WEP katika tukio lililofanyika tarehe 23 Aprili 2024 mjini Arusha.
Mshindi wa pili Catherine Assenga (wa pili kulia), Zainab Nungu Mkuu wa Kitengo cha Mikopo, Exim Bank (wa kwanza kushoto), na Faraja Nyalandu Mkurugenzi Mtendaji wa Ndoto Hub (kulia) wakifurahi pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Exim Bank, Stanley Kafu wakati wa mahafali ya mafunzo ya ujasiriamali, biashara na uwezeshaji kwa wanawake wajasiriamali chini ya mradi wa benki hiyo yajulikanayo kama WEP katika tukio lililofanyika tarehe 23 Aprili 2024 mjini Arusha.
Washindi na baadhi ya washiriki wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Exim Bank wakati wa mahafali ya kumaliza mafunzo ya biashara, ujasiriamali, na uwezeshaji kwa wanawake wajasiriamali. Mafunzo hayo yalitolewa na Exim Bank chini ya mpango wake wa Kuwainua Kiuchumi Wanawake (WEP) na mahafali hayo yamefanyika tarehe 23 Aprili, 2024 mjini Arusha.
---
Exim Bank, kupitia Mpango wake wa Kuwawezesha Kiuchumi Wanawake (WEP), imetoa mafunzo kuhusu masuala ya ujasiriamali, biashara, na uwezeshaji kwa wanawake wajasiriamali kama sehemu ya kuunga mkono ujumuishwaji wa watu wote, wakiwemo wanawake, katika mipango mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.

Kupitia mpango wake wa ‘Exim Cares’, mwaka jana (2023) Exim Bank ilizindua Mpango wa Kuwakwamua Kiuchumi Wanawake ujulikanao ‘Women Empowerment Program (WEP)‘ wenye lengo la kuongeza ushirikishwaji na kuleta usawa kwa wanawake barani Afrika, hasa katika nchi ambazo zina matawi ya benki hiyo ikiwemo Tanzania, Comoros, Djibouti na Uganda.

Akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Exim Bank, Stanley Kafu, anasema, “Ukiwa mwaka wa pili mfululizo wa mpango wa Kuwakwamua Wanawake Kiuchumi (WEP), Exim Bank tunafuraha kubwa kuwa sehemu ya mafanikio haya na tunawapongeza washiriki wote kwa kuanza na kumaliza salama mafunzo haya kuhusu ujasiriamali, uwezeshaji, na biashara.”

Washindi watatu, wa awamu hii ya kwanza mwaka huu, walipata zawadi za pesa taslimu zilitolewa kwa washindi watatu ambapo mshindi wa kwanza, Beatrice A. Msafiri, akizawadiwa kiasi cha TZS 8,000,000, mshindi wa pili, Catherine Assenga akipata TZS 5,000,000 na mshindi wa tatu, Rukia S. Mohamed akiondoka na TZS 3,000,000. Pia, wahitimu wote walipata fursa ya kuweza kupata mikopo bila riba kutoka Exim Bank ili waweze kujiendeleza kiuchumi.

Exim Bank inaamini uwezeshaji wa wanawake na ujasiriamali unabaki kuwa sehemu muhimu ya mipango ya maendeleo nchini Tanzania na barani Afrika kijumla. Hii inadhihirishwa na ongezeko la idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi katika sekta mbalimbali kama siasa, kijamii na kiuchumi.

Akielezea kuhusu malengo ya mradi, Kafu alisema, “Mpango huu utakuwa ni endelevu kwa muda wa miaka mitano na tunatarajia kuwafikia wanawake zaidi ya 600,000 ifikapo mwaka 2028.”

Kafu anasisitiza kuwa Mpango wa WEP ni sehemu ya mkakati mkubwa na wa kina unaolenga kutengeneza jukwaa la wanawake ili waweze kufanikiwa na kustawi katika maisha yao, hasa kwenye eneo la uchumi.

Exim Bank imekuwa na itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo kwa Watanzania wote. Programu hii inawiana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 na itakuwa chachu katika kuimarisha ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa wanawake.

Mkurugenzi wa Lamata Village entertainment, Bi. Leah Mwendamseke ‘Lamata’ akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa tamthilia mpya iitwayo EZRA (Ukweli Upe Muda) itakayokuwa ikirushwa katika vituo mbali mbali vya Televisheni na Online app ya VTV inayomilikiwa na Vodacom Tanzania.
Akizungumza leo Aprili 23, 2024 katika Uzinduzi wa app mpya ya VTV ambapo ndani yake unaweza kustream tamthilia mpya kabisa ya EZRA inayoandaliwa na kampuni ya Lamata Village entertainment, Lamata amesema kuwa tamthilia EZRA ndani yake kuna visa na mikasa, story ya aina yake ambayo itawaacha watazamaji na wasikilizaji mdomo wazi huku ukitaka kujua yaliyojiri.

Pia alitoa shukrani zake za kipekee kwa Uongozi wa Bodi ya Filamu kwa kushirikiana nao katika uzinduzi huo, huku akiwamwagia maua ya pekee kwa Kampuni ya Vodacom Tanzania kwa kuweza kuwashika mkono na kufanikisha kazi hiyo.Mshehereshaji Bw. Evance Bukuku akizungumza katika halfa ya uzinduzi wa Tamthilia ya EZRA na app ya VTV.Kwa upande wao Vodacom Tanzania wamewaalika watazamaji kuweza kupakua app ya VTV ili kuweza kuiona tamthilia hiyo kidijitali zaidi.

Usibaki nyuma! pakua app ya VTV leo google play au Appstore ufaidi mchapo mzima wa Ezra na burudani nyingine mbalimbali.

Wageni waalikwa.
Meneja wa Lamata Village entertainment, Bw. Danny Nyalusi akitoa machache.
Waigizaji waliopo katika tamthilia ya EZRA.
Viongozi mbali mbali wakiwa na waigizaji.
Wasanii mbali mbali waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa tamthilia mpya iitwayo EZRA itakayokuwa ikirushwa katika vituo mbali mbali vya Televisheni na Online app ya VTV inayomilikiwa na Vodacom Tanzania.