Articles by "TEKNOLOJIA"
Showing posts with label TEKNOLOJIA. Show all posts
Mkuu wa Idara ya Usalama wa Mtandaoni kutoka Vodacom Tanzania Plc Bw. Joel Kazoba akizungumza katika uzinduzi wa klabu ya usalama wa mitandao uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam cha Tehama kilichopo Kijitonyama. Klabu hiyo imezinduliwa kwa ushirikiano baina ya Vodacom na chuo hicho cha Tehama yenye madhumuni ya kuhamasisha wanafunzi kujiunga katika masomo ya usalama mtandaoni na kuwapa uzoefu wa vitendo katika kukabiliana na vitisho vya usalama wa kidijitali. Pembeni ni Mkuu wa Kitengo cha mafunzo ya kielectroniki Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Baraka Maiseli.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni Bi. Warda Obathany (Kushoto) akimkabidhi cheti mshindi wa kwanza mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam cha Tehama Alexus Samson (Kulia) wa michezo ya vitendo maarufu kama “capture the flag”. wa mashindano ya kudukua mifumo (capture the flag) Mashindano hayo yalifanyika katika uzinduzi wa klabu ya usalama Chuoni hapo wiki hii. Uzinduzi huo ulifanywa na Vodacom Tanzania plc kwa kushirikiana na chuo cha Tehama UDSM klabu hii inaenda kuhamasisha wanafunzi kujiunga katika masomo ya usalama mtandaoni na kuwapa uzoefu wa vitendo katika kukabiliana na vitisho vya usalama wa kidijitali.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni Bi. Warda Obathany (Kushoto) akimkabidhi zawadi mshindi wa tatu mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar Es Salaam cha Tehama UDSM Rafia Maganga (Kulia) wa mashindano ya kudukua mifumo (capture the flag) Mashindano hayo yaliofanyika katika uzinduzi wa klabu chuoni hapo wiki hii. Uzinduzi huo ulifanywa na Vodacom Tanzania plc kwa kushirikiana na chuo cha Tehama UDSM klabu hii inaenda kuhamasisha wanafunzi kujiunga katika masomo ya usalama mtandaoni na kuwapa uzoefu wa vitendo katika kukabiliana na vitisho vya usalama wa kidijitali.

Na Mwandishi Wetu.

Vodacom Tanzania Plc, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wameanzisha Klabu ya Usalama wa Mitandao katika Chuo Kikuu ch dar es Salaam na kuzindua siku ya michezo kwa vitendo maarufu kama “Capture the Flag (CTF)”. Uzinduzi huu wa pamoja, ulimefanyika katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam cha Tehama (CoICT) kilichopo Kijitonyama.

Klabu hii imeanzishwa mahsusi ili kuhamasisha wanafunzi wa Kitanzania kujiunga na masomo ya usalama wa mitandao, kutoa uzoefu kwa vitendo katika kukabiliana na vitisho vya usalama wa kidijitali na kukuza ushirikiano kati ya wataalamu wa sekta, wanafunzi na viongozi wa serikali.

Kuundwa kwa Klabu ya Usalama wa Mitandao ya UDSM ni hatua muhimu katika kukabiliana na mahitaji yanayokua ya wataalamu wenye ujuzi katika usalama wa mitandao nchini Tanzania. Klabu hii itawapa wanafunzi fursa za mafunzo ya vitendo na kuwapa uzoefu kuhusu changamoto zinazoikabili sekta ya usalama wa kidijitali leo na hatimaye kusaidia kulinda mustakabali wa dijitali hapa nchini.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Usalama Mtandaoni Joel Kazoba kutoka Vodacom aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Tehama wa Kampuni hiyo, Athuman Mlinga alisema, “Tunafuraha kushirikiana na CoICT kuzindua Klabu ya Usalama wa Mitandao na kuandaa michezo hii ya CTF, tunawapa wanafunzi zaidi ya maarifa ya nadharia pekee. Capture the Flag (CTF) ni aina ya mashindano ambapo watu wanatatua mafumbo na matatizo yanayohusiana na usalama wa mtandao ili kupata vidokezo vilivyofichwa katika mifumo.”

Kazoba aliongeza kwamba mchezo huu unasaidia kuboresha ujuzi katika udukuzi wa mifumo na kulinda kompyuta. Kila changamoto, au kidokezo inawakilisha udhaifu wa usalama katika mifumo ambao timu inapaswa kugundua na kushughulikia, hii inahimiza fikra za kina na ukuzaji wa ujuzi. Kwa kushiriki katika michezo hii ya CTFs, wanafunzi wanajifunza kufikiri kama wataalamu wa usalama wa mtandao wakichambua udhaifu, kutathmini hatari na kuunda suluhu za kujihami dhidi ya mashambulizi halisi katika mifumo ya kompyuta.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Katibu Tawala wa wilaya ya Kinondoni Warda Obathany aliyemwakilisha mgeni rasmi Mh Naibu Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Patrobas Katambi alisisitiza umuhimu wa mpango huu, akisema, “Klabu za usalama wa mtandao ni zaidi ya shughuli za ziada; ni njia ya mafunzo kwa walinzi wa kidijitali wa kesho.”

Mh aliongeza kwamba, “hivi sasa kuna ongezeko la matumizi ya dijitali nchini, Hivyo kuna haja kubwa ya wataalamu wa usalama wa mitandao wa ndani ya nchi wanaoelewa changamoto za mifumo zinazoikabili Tanzania. Na mpango huu ni maendeleo makubwa katika kukabiliana na mahitaji yanayokua ya Tanzania ya wataalamu wenye ujuzi katika usalama wa mtandao,” aliongezea.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo ya Elekroniki na Mawasiliano Profesa Baraka Maiseli aliyemwakilisha Mkuu wa chuo cha Tehama cha UDSM, Profesa Joel Mtebe, alifafanua kwamba “Mbali na ujuzi wa vitendo, ushirikiano huu unawapa wanafunzi wetu njia ya kuelekea kwenye sekta ya usalama wa mitandao, ukitoa maarifa watakayopata, ushauri, na uhusiano ambao utasaidia katika nyanja zao za kazi. Tunawashukuru Vodacom kwa uwekezaji katika mpango huu, unaoakisi maono ya muda mrefu kwa Tanzania yenye usalama wa kidijitali, na viongozi vijana walio tayari kukabiliana na changamoto za usalama wa mtandao zinazo endelea kuibuka,” aliongeza.

Kadri vitisho vya mtandao vinavyoendelea kuibuka, umuhimu wa mafunzo ya awali na ukuzaji wa ujuzi utaendelea kukua. Kwa mpango huu, Vodacom Tanzania na UDSM sio tu kwamba wanakuza wataalamu wenye ujuzi wa usalama wa mtandao bali pia wanachangia katika mustakabali salama na thabiti wa dijitali kwa Watanzania wote. Shughuli za klabu na michezo ijayo ya CTF zitaendelea kuwahamasisha, kuwafundisha na kuwapa nguvu wanafunzi kuwa viongozi katika usalama wa mtandao na pia kuhakikisha Tanzania inabaki salama katika enzi hizi za kidijitali.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewahimiza vijana nchini kuchangamkia fursa za kidijitali ikiwemo akili bandia (Artificial Intelligence), kwa kubuni mifumo itakayotatua changamoto za kijamii na hivyo kujipatia kipato.

Meneja TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali ametoa rai hiyo Ijumaa Oktoba 11, 2024 wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana 2024 yanayofanyika katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza kuanzia Oktoba 08-14, 2024 yakiwa na kaulimbiu ya "vijana na matumizi ya fursa za kidijitali kwa maendeleo endelevu".

Amesema mamlaka hiyo inawawezesha vijana kunufaika na matumizi ya kidijitali kwa kutoa rasilimali za mawasiliano ili kufanikisha mawazo yao ya kibunifu ikiwemo kupata masafa na namba za kuwafikia wateja bure.

"Vijana wenggi wamekuwa na kasumba ya kupuuzia fursa mbalimbali za kimaendeleo zinazotangazwa mpaka waone watu wengine wamefanikiwa, tunapaswa kuchangamkia soko la kidijiti ili kujikwamua kiuchumia" amesema John Waronga ambaye ni mmoja wa vijana waliotembelea banda la TCRA.

Maonesho ya wiki ya vijana yamefunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye amewataka vijana kutumia mitandao kujiajiri na kukuza uchumi ili kuwa na taifa lenye uchumi imara huku akiwataka kutotumia maendeleo hayo ya kidijitali kwa matumizi mabaya ikiwemo kuchochea chuki, kueneza taarifa za uongo na picha ama video zisizo na maadili katika jamii.


Majaliwa amesema ili kufikia dira ya maendeleo ya taifa 2050, teknolojia ya kidijitali ina fursa muhimu na maadhimisho hayo ni jukwaa muhimu kwa vijana kuwa chachu ya maendeleo na kwamba Serikali itaendelea kuwajengea vijana uwezo ili kufanikisha bunifu zao.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali (kulia) akitoa ufafanuzi wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na mamlaka hiyo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete (kushoto) alipotembelea banda la TCRA.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali (kulia) akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete (kushoto) alipotembelea banda la TCRA.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali (kulia) akitoa elimu kwa mwananchi aliyetembelea maonesho ya wiki ya vijana kuhusu kampeni ya 'Ni Rahisi Sana' inayoendeshwa na TCRA kwa lengo la kuhamasisha jamii kutambua fursa za kidijiti nk.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali (kulia) akioa elimu kwa mwananchi aliyeembelea banda la TCRA.
Tazama Video hapa chini

Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa akiagana na Mwenyekiti
Mgeni rasmi Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa akiwasili katika Ukumbi wa Hazina, kufungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji la Taifa - TBC na kupokelewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Stephen Kagaigai na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Dkt. Ayub Rioba Chacha leo tarehe 20 Septemba, 2024 Jijini Dodoma.

Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa akiwa katika picha ya pamoja na makundi mbalimbali ya Wajumbe wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji la Taifa - TBC kilichofanyika leo tarehe 20 Septemba, 2024 katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.

Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa akiwa katika picha ya pamoja na makundi mbalimbali ya Wajumbe wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji la Taifa - TBC kilichofanyika leo tarehe 20 Septemba, 2024 katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.

Picha mbalimbali za wajumbe wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji la Taifa - TBC kilichofanyika leo tarehe 20 Septemba, 2024 katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine kimemchagua Katibu wa Baraza Bi. Anna Malimbo na Kamati ya maazimio ya baraza hilo.

Picha mbalimbali za wajumbe wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji la Taifa - TBC kilichofanyika leo tarehe 20 Septemba, 2024 katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine kimemchagua Katibu wa Baraza Bi. Anna Malimbo na Kamati ya maazimio ya baraza hilo.

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma.

Serikali imelihakikishia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kwamba inafanya kila linalowezekana kuhakikisha shirika hilo linatekeleza majukumu yake muda wote, na itaendelea kutatua na hatimaye kumaliza changamoto zote zinazolikabili, zikiwemo za kifedha, vifaa na raslimali watu.

Ahadi hiyo ya Serikali imetolewa tarehe 19 Septemba, 2024 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa (Mb), wakati akifungua Kikao cha Pili cha Baraza la Wafanyakazi wa TBC kilichofanyika katika Ukumbi wa Kambarage (Hazina) Jijini Dodoma.

"Naomba niwahakikishie kuwa Serikali inafanya kila linalowezekana ili TBC itekeleze majukumu yake muda wote, na Wizara itahakikisha changamoto zote zinazowakabili zinatatuliwa kwa wakati kwani Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha mnawezeshwa kifedha, vifaa na raslimali watu ili kutekeleza dhima yake kwa umma wa Watanzania," amesema Mhe. Silaa.

Mhe. Silaa amesema, Serikali inatambua juhudi mbalimbali zinazofanywa na TBC kuhakikisha kunakuwa na fedha za kutosha na kwamba kwa kutambua changamoto za kifedha kwa Shirika, Wizara inasimamia kwa karibu mchakato wa kutungwa kwa Sheria ya TBC, aliyosema, pamoja na mambo mengine, itaiwezesha kupata vyanzo vya mapato vya uhakika, endelevu na toshelevu.

"Waraka wa Sheria hii umeshasomwa kwa mara ya kwanza Bungeni na hatua inayofuata ni kupitishwa na Bunge baada ya kupata maoni ya wadau kama taratibu zinavyoelekeza," amesema Mhe. Silaa.

Aidha, ameipongeza TBC kwa maendeleo makubwa yaliyofikiwa ya kufunga mifumo ya TEHAMA katika miundombinu ya studio za redio na televisheni, upanuzi wa usikivu uliofikia asilimia 92 mwaka huu, na maendeleo ya ujenzi wa Makao Makuu ya TBC eneo la Vikonje Dodoma uliofikia asilimia 26 hadi sasa.

Awali akimkaribisha Waziri, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Stephen Kagaigai amewashauri watanzania kufuatilia maudhui yanayotolewa na Shirika hilo kwani ndicho chombo cha Umma wa Watanzania.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Dkt. Ayub Rioba Chacha ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa unaowezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa licha ya changamoto ndogo ndogo ikiwemo ya upungufu wa watumishi wenye ujuzi kwani waliokuwepo wengi sasa wamefikia umri wa kustaafu.
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania-TANAPA kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imeanza kutoa Anwani za Makazi katika kambi, makazi, hoteli na vivutio vya utalii katika maeneo ya Hifadhi zake zote 21.

Zoezi hilo ambalo litafanyika kwa awamu linaenda sambamba na kusajili taarifa za Anwani za Makazi katika Mfumo wa Kidigitali unaojulikana kwa jina la NaPA, hatua inayolenga kuboresha shughuli za utalii katika hifadhi hizo.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo kwa mazungumzo na makubaliano baina ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambayo ni Mratibu wa Utekelezaji na Matumizi ya Mfumo; Wizara ya Maliasili na Utalii na TANAPA.

Akitoa tamko la kuanza kutoa na kusajili Anwani za Makazi katika Hifadhi hizo, leo tarehe 27 Agosti, 2024, Naibu Kamishna wa Uhifadhi - Maendeleo ya Biashara wa TANAPA, Kamishna Massana Mwishawa amesema lengo ni kurahisisha shughuli za utalii hususan kuwawezesha watalii kufika maeneo mbalimbali ya utalii kwa urahisi.

Kamishna Mwishawa ambaye alimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Bw. Juma Kuji, amesema utoaji na usajili wa Anwani za Makazi litaanzia na Hifadhi na mbuga tatu zilizo ndani ya Mikoa ya Arusha na Manyara ambazo ni Hifadhi ya Taifa Arusha, Hifadhi ya Taifa Tarangire na Hifadhi ya Taifa Manyara.
Mratibu wa Anwani za Makazi Taifa, kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Jampyon Mbugi ameipongeza TANAPA kwa utayari wao wa kutumia Mfumo katika kuboresha huduma za utalii.

Amesema kuwa, Mfumo wa Anwani za Makazi ni Mfumo wa Utambuzi ambao pamoja na masuala mengine utachochea jitihada zilizoanzishwa na Serikali katika kutangaza utalii na kwamba utatumiwa na Sekta zote za Kijamii na Kiuchumi zikiwemo za utalii, biashara, ulinzi, usalama na uokoaji.

Awali wakiwasilisha mada kuhusu mfumo huo unavyotumika na faida zake mbele ya Menejimenti ya TANAPA, wataalamu wa Mfumo huo kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wameainisha faida ambazo TANAPA itazipata kwa hifadhi zake kutambuliwa na mfumo.
Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Tanzania inajivunia hatua ilizochukua za kuziba pengo la kidijitali nchini kwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za mtandao wa kasi kwa taasisi za Serikali na kwa umma kwa ujumla kupitia utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla ameyasema hayo leo Agosti 27, 2024 akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi huo kinachofanyika kwa wiki nzima jijini Arusha.

Aidha, amesema kuwa anatambua mchango mkubwa wa Benki ya Dunia wa kuwezesha mapinduzi ya uchumi wa kidijitali nchini kupitia ufadhili wa mradi wa Tanzania ya kidijitali ambao pamoja na mambo mengine unahakikisha jamii zote za watanzania haziachwi nyuma katika zama hizi za kidijitali.
“Kupitia mradi huu hatujengi tu miundombinu bali tunatengeneza fursa za kidijitali kwa watanzania kwa kuwaunganisha na huduma za kidijitali na kuweka msingi imara wa bunifu za TEHAMA zitakazolipeleka taifa letu mbele.”, amezungumza Katibu Mkuu Abdulla.

Bwana Abdulla amesema lengo la Serikali kupitia Wizara hiyo ni kukuza uchumi wa kidijitali kwa kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa chini ya mradi wa Tanzania ya kidijitali inafanyika kwa ubora na kasi inayotakiwa ili kuijenga Tanzania yenye uwezo mkubwa wa matumizi ya teknolojia ya kidijitali.

Ameizungumzia miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa minara 758 Tanzania Bara na Zanzibar, itakayowezesha mawasiliano vijijini na kuwezesha upatikanaji wa huduma ya mtandao wa kasi kwa ofisi 968 za umma ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi.
Eneo jingine alilolizungumzia ni kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA 500 kwa kufadhili mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi ambapo mpaka sasa watumishi wa umma 50 tayari wanaendelea na mafunzo ya muda mrefu nje ya nchi maeneo ya teknolojia zinazoibukia.

Kwa upande wake Bw. Paul Seaden, Kiongozi wa Kikosi kazi kutoka Benki ya Dunia amesema kuwa kikao hicho cha tathmini ya mradi ni muhimu ili kufanya mapitio na kuhakikisha mradi unaendelea kutekelezwa kwa ufanisi na matokeo chanya.

Aidha, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa inayoutoa na wapo tayari kumalizia miaka miwili iliyobakia ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa Tanzania ya Kidijitali.
Na Mwandishi Wetu.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) inaendelea kuunda Mfumo wa Jamii X-Change ambao ukikamilika utakuwa umetekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan la mifumo kusomana na kubadilishana taarifa.

Hayo yamezungumzwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Mohammed Khamis Abdulla leo Agosti 27, 2024 baada ya kuzindua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya Kidijitali kinachofanyika katika Hoteli ya Kibo Palace jijini Arusha.

Amesema Wizara hiyo imeelekeza fedha nyingi katika ujenzi wa mfumo huo kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali ambao utawezesha mifumo ya TEHAMA ya kisekta kusomana na kubadilishana taarifa utakaojumuisha moduli tatu ambazo ni Jamii Namba, Jamii Kadi na Jamii Malipo.

“Tunategemea mradi huu ukikamilika kila mtanzania atakuwa na Jamii Namba ambayo ni namba ya NIDA itakayokuwa ndio utambuzi wa kila mtanzania na kumwezesha kupata huduma za kijamii”, amesema Bw. Abdulla na kuongeza;

"Baada ya kila mtanzania kupata Jamii Namba, Serikali itaitambulisha Jamii Kadi ambayo itakuwa ni kadi ya kielektroniki itakayojumuisha huduma kadhaa za kielektroniki ndani ya kadi moja kwa sababu itaunganisha taarifa za kadi za benki, vitambulisho vya kitaifa, kadi za kusafiria, bima na nyingine nyingi".

Amefafanua kuhusu Jamii Malipo kuwa ni programu itakayotengenezwa na kuunganishwa na Jamii Kadi na pia itaunganishwa na Mfumo wa Malipo ya Haraka Tanzania (TIPS) unaoruhusu miamala kufanyika kielektroniki kati ya benki na taasisi mbalimbali za kifedha nchini Tanzania.

Ameongeza kuwa kupitia Jamii Malipo kila mwananchi ataweza kufanya miamala kupitia akaunti yake ya benki, M-Pesa, Airtel Money, Paypal na nyingine nyingi kwa kutumia Jamii Kadi, simu ya mkononi au kompyuta ikiwa ni pamoja na kufanya manunuzi na kulipia huduma mbalimbali za kijamii.
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha

Serikali imesema imekusanya taarifa za Anwani za Makazi Milioni 12.3 nchi nzima, zinazotakiwa kuhuishwa kila wakati ili ziendelee kuwa taarifa sahihi wakati wote kwa kuwa zinabadilika mara kwa mara kutokana na sababu mbalimbali.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholaus Merinyo Mkapa, tarehe 14 Agosti, 2024 wakati wa ufunguzi wa Zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi mkoani Arusha.
Bw. Mkapa amesema, ni lazima iwepo mikakati endelevu ya kuhakikisha Mfumo wa Anwani za Makazi yaani NaPA unakuwa na taarifa sahihi kila wakati kwa kuwa nyumba mpya zinajengwa kila siku, upimaji wa viwanja unaoendelea katika maeneo mbalimbali pamoja, watu kuhama kutoka eneo moja Kwenda lingine na matumizi yanabadilika na sababu nyingine kadhaa.

“Katika kufanikisha suala hilo, wizara imeandaa mkakati wa kufanya uhakiki wa taarifa katika halmashauri zote nchini (Mass Data Cleaning), unaokwenda sambamba na kujenga uwezo kwa Waratibu, Wataalamu Wenyeviti na watendaji wa Kata na Mitaa ili waweze kuendelea kutekeleza shughuli za Mfumo wa Anwani za Makazi katika maeneo yao”, amesema Bw. Mkapa.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema hadi sasa, wizara imeshafanya zoezi la uhakiki na kujenga uwezo katika Halmashauri 31, kati ya hizo, 19 ni za Tanzania Bara na 11 za Tanzania Zanzibar.

Amesema, katika uhakiki huo, wizara imefanikiwa kuhuisha zaidi ya taarifa za anwani Milioni 2.3, kutoa anwani mpya zaidi ya 500,000 na kujenga uwezo kwa wataalamu, wenyeviti na watendaji wapatao 6,621.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano wa Wizara hiyo, Bw. Mulembwa Munaku amesema kuwa zoezi la Uhakiki linafanyika baada ya wizara kufanya tathmini na kubainisha mapungufu mbalimbali yakiwemo baadhi ya taarifa zilizokusanywa kukosa sifa, kutoa majina ya Barabara bila kuzingatia miongozo na baadhi ya wananchi kutofikiwa na zoezi.

Wenyeviti wa mitaa,watendaji wa kata na mitaa, Wakurugenzi wa halmashauri, Makatibu tawala wilaya pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi za umma na binafsi wakishiriki mafunzo maalum ya zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi kutoka Mkoa wa Arusha tarehe 14 Agosti, 2024.
---
Bw. Munaku amesema ufunguzi uliofanyika leo unakwenda sambamba na Utoaji wa Mafunzo kwa washiriki ambapo Mada mbalimbali zitatolewa kama vile Utambuzi na utoaji wa majina ya barabara na namba za Anwani, Mfumo wa kidijitali wa Anwani za Makazi, kupata uelewa wa maswali yanayotumika kukusanya taarifa za Anwani na Utaratibu wa Kusajili na Kuhakiki majina wa Barabara.