Articles by "UTALII"
Showing posts with label UTALII. Show all posts

Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetumia Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu-KiliFair 2026 kutangaza mafanikio ya mpango wa bima ya lazima kwa wasafiri, ikieleza kuwa umeimarisha usalama wa wageni na kuchangia ukuaji wa sekta ya afya pamoja na mapato ya utalii visiwani humo.

Mpango huo ulioanza kutekelezwa rasmi Oktoba 1, 2024, unawataka wageni wote wa kimataifa wanaoingia Zanzibar kuwa na bima ya usafiri kabla ya kuwasili. Tangu kuanzishwa kwake, mpango huo umeendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato, ukiingiza wastani wa dola za Marekani milioni moja, sawa na zaidi ya Sh bilioni 2.6 kila mwezi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) kwenye viwanja vya Magereza jijini Arusha, Ofisa Mauzo wa shirika hilo, Abdul-Halim Muhammad, alisema maonesho hayo yamewapa fursa ya kutoa elimu kwa watalii, wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii kuhusu umuhimu wa bima hiyo.

“Tunashiriki Karibu-KiliFair kuongeza uelewa kuhusu bima hii ya lazima na kueleza namna inavyowanufaisha wageni huku ikichangia maendeleo ya huduma muhimu Zanzibar,” alisema.

Kwa mujibu wa utaratibu huo, wageni wengi wa kimataifa hulipa dola 44 za Marekani kwa kila safari ya kuingia Zanzibar, huku wageni kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakilipia dola 22 pekee. Watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi 17 hulipa dola 22, huku walio chini ya umri huo wakisamehewa.

Muhammad alisema bima hiyo inawawezesha wageni kupata huduma za matibabu ya dharura na msaada mwingine muhimu wanapokuwa Zanzibar, hatua inayopunguza changamoto za kifedha na kuhakikisha wanapata huduma kwa haraka wanapozihitaji.

Alisema sehemu ya mapato yanayokusanywa kupitia mfuko huo hutumika kugharamia huduma za afya kwa wageni waliokatiwa bima, huku fedha zinazobaki zikielekezwa katika kuimarisha huduma za afya kwa wananchi na wageni kwa ujumla.
“Mpango huu ulianzishwa baada ya mamlaka kubaini kuwepo kwa matukio ya mara kwa mara ya watalii na wawekezaji kuhitaji matibabu ya dharura huku kukiwa na sintofahamu kuhusu nani angegharamia huduma hizo. Sasa mfumo huu umeondoa changamoto hiyo,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa KiliFair Promotions, Dominic Shoo, alisema Karibu-KiliFair 2026 imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama maonesho makubwa ya utalii na biashara Afrika Mashariki kwa kuwakutanisha wadau kutoka zaidi ya nchi 40 duniani.

Alisema maonesho hayo yamevutia zaidi ya waoneshaji 500 na wanunuzi wa huduma za utalii wapatao 20,000, hatua inayochochea uwekezaji, ushirikiano wa kibiashara na upanuzi wa masoko ya utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Karibu-KiliFair ni jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania na Afrika Mashariki kimataifa. Kadri wadau wanavyoongezeka kushiriki, ndivyo fursa za biashara, uwekezaji na ukuaji wa sekta ya utalii zinavyozidi kuongezeka,” alisema Shoo.
 

Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Zanzibar imeendelea kutumia Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Kili Fair kama jukwaa la kutangaza vivutio vyake vya utalii, utamaduni na urithi wa kihistoria, huku ikiwakaribisha wageni na wadau wa sekta hiyo kushiriki Siku Maalumu ya Zanzibar itakayofanyika Jumapili.

Akizungumza katika maonesho hayo yanayoendelea jijini Arusha, Meneja wa Uhusiano wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Hakimu Kimara, alisema siku hiyo itatoa fursa kwa washiriki kujifunza na kushuhudia mambo mbalimbali yanayoifanya Zanzibar kuwa moja ya vivutio vikubwa vya utalii nchini na duniani.

Alisema Zanzibar imebeba historia ndefu ya mwingiliano wa watu kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa karne nyingi, hali iliyochangia kujengwa kwa utamaduni wa kipekee unaoakisi mchanganyiko wa tamaduni za Kiafrika, Kiarabu na Kibantu.

Kwa mujibu wa Kimara, wageni watakaotembelea banda la Zanzibar watapata nafasi ya kujifunza kuhusu historia ya visiwa hivyo, tamaduni za Wazanzibari na urithi wake mkubwa wa kihistoria unaoifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya utamaduni na historia katika Afrika Mashariki.

Aidha, alisema washiriki watajionea vyakula vya asili vya Kizanzibari vinavyojulikana kwa ladha na mapishi yake ya kipekee yaliyoathiriwa na tamaduni mbalimbali zilizokutana katika visiwa hivyo kwa miaka mingi.

“Ukitembelea Zanzibar utakutana na vyakula vyenye mchanganyiko wa tamaduni za Kiarabu na Kibantu, jambo ambalo limeifanya Zanzibar kuwa na utambulisho wake wa kipekee katika utalii wa utamaduni,” alisema Kimara.

Pia kutakuwa na maonesho ya muziki wa asili ikiwemo taarab, ambapo wageni watapata fursa ya kufahamu historia ya muziki huo, mageuzi yake na namna ulivyoendelea kuhifadhi utambulisho wake wa asili licha ya mabadiliko ya nyakati.

Kimara alisema sekta ya utalii imeendelea kuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya uchumi kwa kuingiza mapato makubwa na kuchochea ukuaji wa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Alifafanua kuwa utalii ni sekta mtambuka inayogusa maeneo mengi ya uchumi ikiwemo biashara, usafirishaji, malazi, huduma za chakula, sanaa na shughuli za wajasiriamali, huku ikiwaunganisha watu kutoka mataifa mbalimbali duniani.

“Utalii unawakutanisha watu wa mataifa tofauti, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Kupitia maonesho kama haya tunapata nafasi ya kutangaza vivutio vyetu na kuwafikia watu wengi zaidi,” alisema.

Aliongeza kuwa Maonesho ya Kili Fair yameendelea kutoa elimu muhimu kwa wageni na wadau wa utalii kuhusu vivutio mbalimbali vya Tanzania, hali inayowasaidia wengi kufahamu maeneo mapya na kupanga kuyatembelea siku zijazo.

Kwa upande mwingine, alisema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kukuza biashara kwa kuwawezesha wadau wa sekta ya utalii kutangaza huduma na bidhaa zao pamoja na kujenga ushirikiano wa kibiashara na taasisi za ndani na nje ya nchi.

Kimara alitoa wito kwa mikoa mingine yenye vivutio vya utalii kuandaa maonesho yanayofanana na Kili Fair ili kuongeza juhudi za kuitangaza Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Alisema kutokana na kuongezeka kwa idadi ya washiriki kila mwaka, kuna umuhimu wa kuendelea kupanua eneo la maonesho hayo ili kutoa nafasi kwa wadau wengi zaidi kushiriki.

“Matarajio yetu ni kuona mwakani washiriki wengi zaidi wakihudhuria maonesho haya. Kadri tunavyoongeza majukwaa ya kutangaza utalii ndivyo tunavyoongeza fursa za biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisema.

Maonesho ya Kili Fair yameendelea kujidhihirisha kuwa moja ya majukwaa makubwa ya utalii nchini kwa kuwakutanisha wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania, huku yakichangia kutangaza vivutio vya utalii, kuimarisha biashara na kufungua fursa mpya za uwekezaji katika sekta hiyo.

Na Mwandishi Wetu

Jumba la sanaa la Rangi Gallery la jijini Dar es Salaam limeandika historia baada ya kuwa taasisi ya kwanza kutoka Tanzania kushiriki katika maonesho ya kimataifa ya sanaa ya Art OnO 2026 yaliyofanyika jijini Seoul, Korea Kusini.

Maonesho hayo yaliyofanyika kuanzia Aprili 2 hadi 5 mwaka huu katika kituo cha maonesho cha SETEC, yameelezwa kuwa miongoni mwa majukwaa makubwa na yenye hadhi ya juu barani Asia yanayowakutanisha wadau wa sanaa kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Kupitia ushiriki huo, Rangi Gallery ilisimama sambamba na majumba makubwa ya sanaa kutoka nchi 12 zikiwemo Japan, Ujerumani, Uswisi na mataifa mengine, hatua iliyotajwa kuiweka Tanzania katika ramani ya sanaa ya kisasa duniani.

Katika maonesho hayo, Rangi Gallery iliwasilisha kazi za wasanii wanne wanawake kutoka Tanzania ambao ni Theresia Venance, Tulsi Patel, Valerie Asiimwe Amani na Turakella Editha Gyindo.

Kazi za wasanii hao zilionesha upekee wa sanaa ya kisasa ya Kitanzania, zikigusa masuala ya utambulisho, mila, mabadiliko ya kijamii, uzoefu wa mwanamke pamoja na uhusiano wa binadamu na mazingira.

Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Rangi Gallery, Lorna Mashiba Albou, alisema ushiriki huo ni ushahidi kuwa sanaa ya Tanzania ina uwezo mkubwa wa kushindana kimataifa.

“Wasanii wetu wameiwakilisha vyema Tanzania katika jukwaa hili la kimataifa. Hii inaonesha vipaji vya Kitanzania vinaweza kufika mbali vikipewa nafasi sahihi,” alisema Lorna.

Aliongeza kuwa licha ya wasanii wote waliowasilishwa kuwa wanawake, jambo hilo halikupangwa mahsusi bali lilitokana na ubora wa kazi zao.

Ushiriki wa Rangi Gallery pia umepewa uzito wa kidiplomasia baada ya Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Togolani Edriss Mavura, kuhudhuria maonesho hayo na kushuhudia kazi zilizooneshwa.

Wadau wa sanaa wameeleza kuwa hatua hiyo ni mwanzo wa safari kubwa kwa Tanzania katika soko la kimataifa la sanaa, huku baadhi ya wasanii walioshiriki wakitarajiwa kuiwakilisha nchi katika maonesho makubwa ya Venice Biennale 2026 nchini Italia.

Rangi Gallery ilianzishwa jijini Dar es Salaam na Lorna Mashiba Albou, ambaye awali alikuwa mwanasheria kabla ya kuhamia katika sekta ya uchumi wa ubunifu.

Mbali na kuonesha kazi za wasanii wa ndani, jumba hilo linaendesha programu ya Rangi Nyumbani Residency, inayolenga kuwaunganisha wasanii wa Tanzania na mitandao ya kimataifa.

Wachambuzi wanasema Tanzania imekuwa na vipaji vingi vya sanaa kwa miaka mingi, lakini changamoto kubwa imekuwa ukosefu wa majukwaa ya kuvitangaza. Kupitia juhudi za taasisi kama Rangi Gallery, sasa mlango wa dunia umeanza kufunguka kwa wasanii wa Kitanzania.

Na Mwandishi Wetu

Zaidi ya mastaa na watengeneza maudhui 30 wamesafirishwa kwa ndege binafsi kutoka Dar es Salaam hadi Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kushiriki uzinduzi wa kinywaji kipya cha Serengeti Premium Apple, kilichoelezwa kuwa cha kwanza cha aina ya premium (RTD) kutengenezwa nchini Tanzania na kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL).

Uzinduzi huo wa siku tatu mfululizo umefanyika kwa mtindo wa kipekee uliolenga kuunganisha burudani, ubunifu, utalii pamoja na ladha mpya ya kinywaji hicho.
Safari hiyo ilianza kwa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kabla ya wageni hao kusafirishwa kwa ndege binafsi hadi Serengeti, ambako walipokelewa kwa hafla maalumu ndani ya hifadhi hiyo maarufu duniani.

Wakiwa Serengeti, mastaa hao walipata nafasi ya kutembelea vivutio vya utalii, kushiriki chakula cha mchana na jioni katika mazingira ya kuvutia, sambamba na burudani mbalimbali zilizopangwa kwa ustadi.

Katika siku iliyofuata, wageni hao walishiriki tukio maalumu la “Toast in the Sky”, lililofanyika angani kupitia puto maalumu la moto (hot air balloon), tukio lililoibua hisia na kuvutia wengi.

Kwa mujibu wa waandaaji, uzinduzi huo umeakisi misingi ya chapa mpya ya Serengeti Premium Apple ikiwemo ladha laini na ya kuburudisha ya apple, ubunifu wa Kitanzania, maisha ya kisasa pamoja na mafanikio ya Mtanzania wa leo.

Aidha, kampuni ya Serengeti Breweries Limited imesema uzinduzi huo unaonyesha uwezo wa Tanzania kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango vya kimataifa huku ikitumia vivutio vya ndani kuitangaza nchi na ubunifu wake.

Uzinduzi huo umevutia hisia za wengi huku ukiweka historia mpya katika sekta ya vinywaji na burudani nchini.

Moshi, Kilimanjaro: Mwanamke mwenye umri wa miaka 86, Jutta kutoka jimbo la Florida, Marekani, ameandika historia kwa kufanikiwa kufika kileleni mwa Mlima Kilimanjaro na kuwa mwanamke wa pili mwenye umri mkubwa zaidi kufanya hivyo duniani.

Jutta alifanikiwa kufika katika kilele cha Uhuru Peak chenye urefu wa mita 5,895 juu ya usawa wa bahari, akionesha kuwa umri si kikwazo pale dhamira na uthubutu vinapokutana. Rekodi hiyo inamfanya afuate nyayo za Anne Lorimor ambaye ndiye mwanamke aliyeshikilia rekodi ya kuwa wa kwanza kwa umri mkubwa zaidi kupanda mlima huo.
Kwa mujibu wa waongozaji wa safari hiyo, Jutta alishiriki katika msafara maalum uliomwezesha pia kufika katika eneo la Crater Camp, ambalo liko katika urefu wa takriban futi 18,800 juu ya usawa wa bahari, likiwa miongoni mwa kambi za juu zaidi duniani.

Mlima Kilimanjaro ni mlima mrefu zaidi barani Afrika na una sifa ya kuwa miongoni mwa milima michache mikubwa duniani inayoweza kupandwa bila kuhitaji ujuzi wa kiufundi wa kupanda miamba au barafu, jambo linalowapa watu wengi nafasi ya kujaribu kufikia kilele chake.

Akizungumza baada ya ushindi huo, Jutta alisisitiza kuwa mafanikio hayo ni ushahidi kuwa ndoto hazina kikomo cha umri, na kwamba mtu yeyote mwenye nia, uvumilivu na maandalizi sahihi anaweza kufanikisha malengo yake.

Tukio hilo limeendelea kuvutia watalii na wapenda milima duniani, huku likitoa somo kwa jamii kuwa mafanikio hayategemei umri bali dhamira na juhudi binafsi.

 

Na Mwandishi Wetu.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Conservation Area imeendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya barabara ndani ya hifadhi hiyo ili kuhakikisha huduma bora kwa watalii, wawekezaji na wananchi wanaozunguka eneo hilo.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Uhifadhi, Abdul-Razaq Badru, baada ya kufanya ziara ya kukagua ukarabati wa barabara mbalimbali ndani ya hifadhi, akisisitiza kuwa hakuna kulala katika utekelezaji wa majukumu ya kuboresha mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 646.

Akiwa katika kijiji cha Endulen, Badru amesema barabara zinazoendelea kuimarishwa ni pamoja na ile ya geti la Loduare hadi Golini (km 88), View Point hadi Naiyobi (km 76), Kimba–Endulen hadi Makao Makuu (km 77) inayosimamiwa na TANROADS, pamoja na Endulen hadi Ndutu (km 52), Ndutu–Golini (km 23), Makumbusho ya Olduvai hadi Nasera (km 54) na barabara za ndani ya kreta ya Ngorongoro zenye urefu wa km 110.

Amesema lengo la maboresho hayo ni kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote wa mwaka, hatua itakayorahisisha shughuli za utalii na uchumi kwa ujumla.
“Tunataka viwango vya utoaji huduma kwa wateja wetu viwe juu. Ndiyo maana muda wote tupo eneo la kazi kuhakikisha mitambo inafanya kazi na kila barabara inapitika bila kujali majira,” alisisitiza Badru.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuongeza ubora wa huduma katika hifadhi hiyo, ambayo ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii nchini.

Na Mwandishi Wetu

Katika zama hizi za utandawazi, Watanzania wengi huamini kuwa uzuri wa dunia uko nje ya mipaka yetu. Hata hivyo, uzoefu mmoja mdogo wa safari ya utalii nje ya nchi unaweza kubadili kabisa mtazamo huo na kutufundisha thamani ya tulichonacho nyumbani.

Hivi karibuni, Glorie Ngahyoma alipata fursa ya kutembelea kinachoitwa “National Park” katika moja ya nchi za Asia akiwa na rafiki yake kutoka China. Alipokea mwaliko huo kwa furaha kubwa, akiwa na matumaini ya kuona hifadhi ya wanyama wa porini kama zile tulizo nazo nyumbani. Walianza safari mapema asubuhi, wakasafiri kwa takribani masaa matatu hadi kufika eneo hilo.

Hata hivyo, walipoingia ndani ya hifadhi hiyo, alianza kugundua tofauti kubwa. Badala ya mandhari ya pori na wanyama wakubwa wa asili, alikuta wanyama wengi wa kufugwa kama kondoo, punda, sungura, farasi na ndege. Mnyama pekee aliyemvutia sana, kwa sababu hakuwahi kumuona kabla, alikuwa panda. Safari hiyo ilimfanya aanze kutafakari kwa kina juu ya namna tulivyo na bahati kubwa nchini kwetu.

Cha kushangaza zaidi, wakati wa ziara hiyo aligundua kuwa yeye mwenyewe alikuwa kivutio cha utalii. Wageni wengi walikuwa wakimshangaa, wakimuomba kupiga picha naye na wengine wakivutiwa na nywele zake za rasta. Hali hiyo ilimfanya atambue jinsi watu wengine wanavyothamini utofauti wa tamaduni na muonekano wetu wa Kiafrika.

Waliporudi nyumbani, alimwonesha rafiki yake picha na video za Serengeti National Park kupitia mtandao, akamweleza kuhusu vivutio mbalimbali vya Tanzania. Rafiki yake alishangazwa sana na ukubwa wa wanyama pori, uhamaji wa nyumbu na mandhari ya asili. Ndani ya muda mfupi, alitangaza kuwa ana ndoto ya kuitembelea Serengeti.

Kutokana na uzoefu huo, alijifunza mambo matatu muhimu.

Kwanza, Tanzania imebarikiwa kwa rasilimali za asili na vivutio vya kipekee vinavyoweza kuvutia dunia nzima.

Pili, ni muhimu kwa Watanzania kujivunia nchi yao na kuacha kudharau kile walichonacho. Kauli za kudhani maisha bora yako nje pekee mara nyingi hutokana na kutokujua thamani ya nyumbani.

Tatu, utalii haupaswi kuwa wa kutazama pekee bali wa kuhifadhi. Kila mtalii anapaswa kuwa balozi wa mazingira kwa kuchangia uhifadhi, hata kama ni kupanda mti mmoja.

Ni wakati sasa kwa Watanzania kuanza kuutazama utalii wa ndani kama fursa ya kujifunza, kujivunia na kuchangia maendeleo ya taifa. Kwa kufanya hivyo, tutahakikisha kuwa utajiri wa asili tulionao leo unaendelea kuwapo kwa vizazi vijavyo.

Na Sixmund Begashe, Dodoma

DODOMA: Serikali imewataka wadau wa uwindaji wenyeji na bucha za nyamapori kuendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuimarisha mchango wa sekta ya Maliasili na Utalii katika uchumi wa taifa na kuhakikisha manufaa yake yanawafikia Watanzania kwa upana zaidi.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dodoma kati ya Wizara hiyo na wadau wa sekta ya uwindaji wenyeji pamoja na bucha za nyamapori, kilicholenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu nafasi ya sekta hizo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Dkt. Kijaji amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejipanga kuhakikisha rasilimali za maliasili zinasimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji ili ziwe chachu ya ajira, uwekezaji na ustawi wa wananchi.

Ameeleza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi katika kusimamia na kuendeleza urithi wa maliasili, huku akisisitiza kuwa haitamvumilia mtumishi yeyote atakayekwaza juhudi za Serikali za kukuza sekta hiyo na kuwakwamisha wananchi kunufaika na fursa zilizopo.
Aidha, amewapongeza wadau hao kwa uzalendo wao na mchango wao katika uchumi, akiwataka kuendelea kushikamana na Wizara ili kufungua fursa zaidi za uwekezaji na ajira, hususan kwa vijana, kupitia sekta ya Maliasili na Utalii.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Bw. Nkoba Mabula, amesema ofisi yake itasimamia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri, ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua na kutoa matokeo chanya kwa taifa na wananchi.