Dar es Salaam, 1 Oktoba 2025: Dunia imegubikwa na simanzi kufuatia kifo cha mtafiti mashuhuri wa wanyamapori, Dkt. Jane Goodall, aliyefariki dunia na kuacha urithi mkubwa katika historia ya uhifadhi wa mazingira na sokwe.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, akimtaja marehemu Dkt. Goodall kama rafiki wa dhati wa Tanzania na mtu aliyebadilisha sura ya uhifadhi duniani kupitia kazi yake ya utafiti katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe.
“Kwa huzuni kubwa nimepokea taarifa za kifo cha Dkt. Jane Goodall. Kazi yake ya kipekee katika Gombe National Park ilibadilisha historia ya uhifadhi wa wanyamapori na kuiweka Tanzania katikati ya jitihada za kimataifa za kulinda sokwe na mazingira. Urithi wake utaendelea kuishi,” alisema Rais Samia.
Historia ya Jane Goodall
Dkt. Jane Goodall alizaliwa tarehe 3 Aprili 1934, jijini London, Uingereza. Tangu akiwa mtoto, alipenda sana wanyama na kusoma vitabu kuhusu maisha ya wanyama, ikiwemo simulizi za Tarzan na Dr. Dolittle.
Mwaka 1957, akiwa na ndoto ya kuishi barani Afrika na kujifunza zaidi kuhusu wanyamapori, alisafiri kwenda Kenya. Huko alikutana na mtafiti maarufu wa visukuku na anthropolojia, Dr. Louis Leakey, ambaye alitambua ari yake na kumhimiza kuanza utafiti wa sokwe katika Ziwa Tanganyika, mkoani Kigoma.
Mnamo 14 Julai 1960, akiwa na umri wa miaka 26, Jane Goodall alifika Gombe, ambako alianza utafiti uliokuja kuwa wa kipekee duniani. Ndani ya miezi michache, aligundua tabia nyingi mpya za sokwe, zikiwemo matumizi ya zana – jambo lililobadilisha mtazamo wa kisayansi kuhusu tofauti kati ya binadamu na wanyama.
Utafiti wake wa zaidi ya miongo sita uliiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia kama kitovu cha tafiti za sokwe na uhifadhi wa wanyamapori. Pia, alianzisha Taasisi ya Jane Goodall (Jane Goodall Institute), ambayo imekuwa mstari wa mbele katika elimu ya uhifadhi na kulinda mazingira.
Mbali na mchango wake wa kisayansi, Dkt. Goodall aliweka msisitizo mkubwa juu ya uhusiano kati ya binadamu na mazingira, akihimiza vizazi vijavyo kulinda misitu na wanyama kwa manufaa ya dunia nzima.
Mashirika ya kimataifa ya uhifadhi na watetezi wa mazingira wamesema watandeleza kazi yake, huku Tanzania ikiendelea kufaidika na historia aliyoiacha katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe, Kigoma.




.jpg)

Toa Maoni Yako:
0 comments: