Articles by "HABARI NA MATUKIO"
Showing posts with label HABARI NA MATUKIO. Show all posts

Na Mwandishi Wetu

Wadau wa sekta ya usafiri wa majini katika mikoa ya Mwanza, Kigoma na Kagera arehe 16 Aprili, 2026 wamejitokeza na kutoa maoni yao kuhusu athari za ongezeko la bei ya mafuta, wakisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua stahiki zitakazolinda maslahi ya wananchi pamoja na uendelevu wa huduma hiyo.

Wakizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), maafisa waratibu wa vikao hivyo, wamesema kuwa vikao hivyo vimeandaliwa kwa lengo la kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufikia uamuzi wowote kuhusu marekebisho ya nauli za usafiri wa majini.

Wameongeza kuwa vikao hivyo vimeitishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 29 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura 415, kinachoitakaTASAC kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kupata maoni katika michakato mbalimbali inayohitaji maoni ya wadau.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika mkoani Kagera, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Mkoa wa Kagera, Bw. Isaya Tendega, ameipongeza TASAC kwa kuandaa vikao hivyo ambavyo vimefanyika katika wakati muafaka kufuatia mabadiliko ya bei ya mafuta yaliyoanza kutumika hivi karibuni, hali inayoweza kuongeza gharama za uendeshaji wa vyombo vya usafiri majini na kuathiri maisha ya wananchi.
Baadhi ya wadau walioshiriki mkutano huo walieleza kuwa ni muhimu kwa mamlaka husika kuzingatia uwiano kati ya gharama za uendeshaji na uwezo wa wananchi kumudu nauli ili kuepusha kuwaongezea mzigo wananchi, hususan wale wanaotegemea usafiri wa majini kwa shughuli zao za kila siku.

Aidha, wadau wengine walipendekeza kuwepo kwa mikakati mbadala ya kupunguza gharama za uendeshaji, ikiwemo matumizi ya nishati mbadala na kuboresha ufanisi wa vyombo vya usafiri, badala ya kutegemea zaidi ongezeko la nauli.

TASAC imebainisha kuwa itaendelea kupokea maoni hadi tarehe 26 Aprili, 2026 kabla ya kukamilisha mchakato wa kufanya maamuzi ambao utakuwa shirikishi na wa uwazi, ukizingatia maoni ya wadau wote pamoja na hali halisi ya soko.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa - Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Ndg. Rabia Abdalla Hamid, amefanya Kikao kazi na Kansela wa Chama Cha Kikomunisti (CPC), Ubalozi wa China nchini Tanzania Ndg. Xu Sujiang leo tarehe 16.04.2026, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam.

Lengo la kikao hicho ni kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha uhusiano na itikadi za vyama hivyo.





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wadau wa Sekta ya Afya pamoja na wageni mbalimbali kabla ya kufungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wadau wa Sekta ya Afya pamoja na wageni mbalimbali kabla ya kufungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2026.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima ya Kibinadamu ya Upasuaji wa Ubongo kutoka kwa Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Tanzania (TNS) Dkt. Othman Kiloloma kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2026.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima ya Kibinadamu ya Upasuaji wa Ubongo kutoka kwa Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Tanzania (TNS) Dkt. Othman Kiloloma kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2026.
Wafanyakazi wa Sekta ya Afya wakiwa kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2026.
Wadau wa Sekta ya Afya wakiwa kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2026.


 Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Aprili 15, 2026, akupewa maelezo juu ya mradi wa jengo la maabara ya TEHAMA ambayo ni ‘Smart Class’ alipokuwa Mgeni rasmi katika Mahafali ya 59 ya Shule ya Sekondari Kibaha (KSS) kama mgeni rasmi, katika hafla iliyofanyika shuleni hapo, Tumbi, Kibaha Mji, mkoani Pwani.
Janjaa: Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Aprili 15, 2026, akikagua na kupewa maelezo juu ya maabara ya TEHAMA ambayoni ‘Smart Class” na Mkuu wa Shule hiyo alipokuwa Mgeni rasmi katika n Mahafali ya 59 ya Shule ya Sekondari Kibaha (KSS) kama mgeni rasmi, katika hafla iliyofanyika shuleni hapo, Tumbi, Kibaha Mji, mkoani Pwani.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Aprili 15, 2026, akimpongeza na kumshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Viwanja vya Ndege (TAA) Bw. Abdul Mombokaleo kwa kujitolea computer zenye thamani ya shilingi milioni 170 kama mchango wake yeye na Alumni wengine kwa kuboresha elimu ya Sayansi katika shule hiyo.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Aprili 15, 2026, akiwatambulisha baadhi ya Alumni walio katika kamati ya mradi wa ujenzi wa jengo la maabara ya TEHAMA ambayo ni ‘Smart Class’ katika Mahafali ya 59 ya Shule ya Sekondari Kibaha (KSS) kama mgeni rasmi, katika hafla iliyofanyika shuleni hapo, Tumbi, Kibaha Mji, mkoani Pwani. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Viwanja vya Ndege (TAA) Bw. Abdul Mombokaleo, akifuatiwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO Nchini Prof. Hamisi Malebo.
Sehemu ya wahitimu wa kidato cha sita katika Mahafali ya 59 ya Shule ya Sekondari 
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Aprili 15, 2026, amehudhuria Mahafali ya 59 ya Shule ya Sekondari Kibaha (KSS) kama mgeni rasmi, katika hafla iliyofanyika shuleni hapo, Tumbi, Kibaha Mji, mkoani Pwani.

Akiwa katika mahafali hayo, Dkt. Kikwete amezindua harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo la ghorofa la maabara ya TEHAMA na masomo mengine, ambalo linatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 3.

Amesema ujenzi huo ni muhimu katika kuendeleza ubunifu na uwezo wa wanafunzi katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).

Aidha, Dkt. Kikwete amekubali kuwa mlezi wa kamati ya kukusanya michango kwa ajili ya mradi huo mkubwa ambao kwa sasa umefikia hatua ya msingi.

Pia, Rais Mstaafu ameishukuru jumuiya ya wanafunzi wa zamani (alumni) wa shule hiyo, wakiuongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Abdul Mombokaleo, kwa kuchangia kompyuta zenye thamani ya Shilingi Milioni 170 kwa ajili ya “Darasa Janja” (Smart Class) lililoanzishwa shuleni hapo.

Darasa hilo litakuwa ni kituo cha mafunzo kwa wanafunzi wa shule hiyo na shule nyingine zitakazounganishwa kupitia mfumo wa mtandao, ambapo mwalimu anaweza kufundisha madarasa yaliyoko nje ya Kibaha kwa wakati mmoja kwa njia ya kidigitali.

Katika ziara yake, Dkt. Kikwete alipata fursa ya kutembelea na kukagua Darasa Janja hilo, akipokea maelezo kutoka kwa Mkuu wa Shule kuhusu namna teknolojia hiyo inavyotumika kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji shuleni hapo.

Shule ya Sekondari Kibaha, inayomilikiwa na Shirika la Elimu Kibaha na kusimamiwa na Kurugenzi ya Hud uma za Elimu, ilianzishwa mwaka 1965 kupitia ushirikiano kati ya Serikali ya Tanganyika ya wakati huo na nchi za Nordic – Denmark, Finland, Norway, na Sweden. Wakati inaanzishwa, shule ilikuwa na wanafunzi 110 wa Kidato cha Kwanza na 60 wa Kidato cha Tano.

Kwa sasa, shule hiyo ya bweni kwa wavulana ina uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 800 na imeendelea kuwa miongoni mwa taasisi kongwe na zenye heshima kubwa katika sekta ya elimu nchini.

Dkt. Kikwete ni miongoni mwa alumni mashuhuri wa Shule ya Sekondari Kibaha, alikosoma zaidi ya miaka 60 iliyopita. Wengine waliopitia shule hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Bw. Peter Ulanga, Balozi Lazaro Nyalandu, Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO Nchini Prof. Hamisi Malebo, Mkurugenzi Mkuu wa Viwanja vya Ndege Bw. Abdul Mombokaleo, na Mwenyekiti Mstaafu wa CHADEMA Mhe. Freeman Mbowe, miongoni mwa wengine wengi.

Aidha, kwa kutambua mchango mkubwa wa alumni wake, Shule ya Sekondari Kibaha inaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa elimu ili kuhakikisha inaendelea kuwa kinara katika utoaji wa elimu ya ubora nchini.
Kibaha, Katika hafla iliyofanyika shuleni hapo, Tumbi, Kibaha Mji, mkoani Pwani. (Picha na Habari na Issa Michuzi)
mm
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Jiji la Dar es Salaam linatarajia kuandika historia mpya katika tasnia ya burudani baada ya kutangazwa kwa uzinduzi wa tamasha la kwanza la kimataifa la vichekesho, Punchline International Comedy Festival (PICF) 2026, litakalofanyika kuanzia Mei 25 hadi Juni 1, 2026.

Tamasha hilo lililotangazwa na Punchline Africa, linatarajiwa kuwakutanisha wachekeshaji kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa kipindi cha wiki moja, likijumuisha maonesho ya jukwaani, shughuli za vyombo vya habari pamoja na ubadilishanaji wa utamaduni. Kilele cha tamasha hilo kitakuwa Grand Finale itakayofanyika katika ukumbi wa The Superdome.

PICF 2026 itahusisha maonesho ya vichekesho kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, hatua inayolenga kuonesha utofauti wa vipaji vya wacheshi barani Afrika. Waandaaji wamesema mbali na burudani, tamasha hilo lina lengo la kuhamasisha umuhimu wa vichekesho katika kuboresha afya ya akili kwa kuwapa watu nafasi ya kucheka, kupunguza msongo wa mawazo na kuunganishwa kijamii.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwanzilishi Mwenza wa Punchline Africa, Evans Bukuku, alisema tamasha hilo ni jukwaa muhimu la kuleta watu pamoja na kuwapa nafuu ya kihisia kupitia sanaa ya uchekeshaji.“Comedy siyo kuchekesha tu, ni njia ya kuelewa maisha na kupunguza msongo wa mawazo. Kupitia PICF tunataka watu waondoke wakiwa na nafuu hata kama changamoto bado zipo,” alisema.

Kwa upande wake, Balozi wa Ufaransa nchini, Anne Sophie Ave, alisema wameamua kuunga mkono tamasha hilo kutokana na mchango wa sanaa katika kukuza vipaji vya vijana na kuwajengea kujiamini.

Aliongeza kuwa Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji kutokana na nafasi yake kama kitovu cha Afrika Mashariki na historia yake katika harakati za Pan-Afrika, akisisitiza kuwa sanaa ya vichekesho inaweza kuwa daraja la kuunganisha bara hilo.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Filamu nchini, Emmanuel Ndumukwa, alisema serikali inaunga mkono juhudi hizo na kuona kuwa tamasha hilo linaweza kuwa chachu ya kukuza tasnia ya uchekeshaji nchini.

Kwa upande wa wasanii, mchekeshaji Humphrey Richard alisema PICF 2026 ni fursa adhimu kwa wacheshi kujifunza, kubadilishana uzoefu na kufikia masoko ya kimataifa.
Tamasha hilo linaandaliwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo Alliance Française Dar es Salaam, Tanzania Film Board pamoja na SGA Security.

Aidha, PICF ni sehemu ya mradi wa Création Africa unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ufaransa, unaolenga kuwawezesha wasanii na taasisi za ubunifu nchini.

Tamasha hilo linatarajiwa kuvutia maelfu ya washiriki na kufikia zaidi ya watu milioni moja kupitia majukwaa ya kidigitali, huku taarifa za wasanii watakaoshiriki na ratiba kamili zikitolewa katika siku zijazo.

Dar es Salaam/Zanzibar

Kituo cha wanyamapori cha Serval Wildlife kimetoa tamko rasmi kufuatia taarifa za kifo cha mwanahabari na mtengeneza maudhui mtandaoni, Ashley, kikieleza masikitiko yake na kufafanua kuhusu tukio hilo lililozua mjadala mkubwa mitandaoni.

Kupitia taarifa hiyo, Serval Wildlife ilieleza kuwa inatoa pole za dhati kwa familia, ndugu na marafiki wa marehemu, ikisisitiza kuwa wako pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

Aidha, taasisi hiyo imeweka wazi kuwa tukio la kifo hicho halikutokea katika eneo lao, bali lilitokea visiwani Zanzibar, jambo lililothibitishwa pia na Zanzibar Police Force kupitia taarifa yao rasmi.

Serval Wildlife imefafanua kuwa marehemu Ashley aliwahi kutembelea kituo hicho na kupata uzoefu mzuri, huku akiondoka katika hali njema. Imeongeza kuwa video zinazosambaa mtandaoni kwa sasa zinatokana na ziara yake katika kituo hicho, hali iliyosababisha mkanganyiko kuhusu eneo halisi la tukio.

Katika hatua nyingine, taasisi hiyo imesema haitashiriki wala kuchapisha tena picha au video za marehemu kwenye kurasa zake, kwa heshima na kuepuka kuonekana kama inatumia tukio hilo kwa masoko.

Tamko hilo limehitimishwa kwa kuomba uelewa kutoka kwa umma pamoja na kuendelea kuiombea familia ya marehemu katika kipindi hiki cha majonzi.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele leo Aprili 14, 2026 amekutana na kuzungumza na mjumbe maalum Jumuiya ya Madola (Commonwealth) Rais wa zamani wa Malawi Mhe.Lazarus McCarthy Chakwera ambaye alitembelea ofisi za Tume Njedengwa jijini Dodoma. Ziara hiyo maalum ya mjumbe huyo wa Jumuia ya Madola ililenga kuangalia namna Uchaguzi Mkuu wa 2025 ulivyofanyika. (Picha na INEC).

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Washindi wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2026 wametangazwa rasmi katika hafla iliyofanyika ukumbi wa The Superdome, Masaki jijini Dar es Salaam, huku waandishi mbalimbali wakitunukiwa kwa mchango wao katika kukuza na kuendeleza fasihi ya Kiswahili nchini.

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali, wasomi, pamoja na wadau wa sekta ya fasihi, ilishuhudia washindi wakikabidhiwa tuzo na mfano wa hundi za fedha kama ishara ya kuthamini ubunifu na juhudi zao katika uandishi.
Katika kipengele cha riwaya, Bishop John Hiluka aliibuka mshindi wa kwanza kupitia kazi yake “Waraka kutoka Gerezani”, akifuatiwa na Halfani Sudi aliyeshika nafasi ya pili kwa riwaya “Mnara wa Posta”. Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Enock Maregesi kwa kazi yake “Alama za Bluu”.

Kwa upande wa ushairi, Abdalaj Salum Ngereza alitwaa ushindi wa kwanza kupitia diwani ya “Muwinda Elimu”, huku Kombo Abdalah Omar akishika nafasi ya pili kwa “Tunu ya Taifa”. Nafasi ya tatu ilikwenda kwa Hafidh Makame kwa diwani yake “Naisubiria Faraja”.
Katika kipengele cha hadithi za watoto, Amina Abdulrahman Mohamed aliibuka mshindi wa kwanza kwa kazi “Shumi na Vitungule”, wakati Fatma Suleiman akishika nafasi ya tatu kupitia hadithi “Kidau cha Panya”.

Kwa upande wa tamthilia, Hamis Kibari alitwaa nafasi ya kwanza kwa kazi yake “Ufalme wa Mabadiliko”, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Esther Nyawale kwa tamthilia “Jiko la Ukombozi”.
Akizungumza katika hafla hiyo, mmoja wa waandaaji alieleza kuwa tuzo hizo zinaendelea kuwa chachu ya kuhamasisha ubunifu miongoni mwa waandishi wa Kiswahili, hususan kizazi kipya, na kuchangia kukuza lugha na utamaduni wa Mtanzania.

Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ni miongoni mwa tuzo muhimu nchini zinazolenga kuenzi mchango wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, katika kukuza lugha ya Kiswahili na fasihi yake.

Uharibifu wa Ziwa Victoria: Matokeo ya Shughuli za Kibinadamu Yaanza Kuonekana Wazi

Katika miaka ya karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la shughuli za kibinadamu kandokando ya Ziwa Victoria, hali ambayo sasa imeanza kuleta athari zinazoonekana wazi katika mfumo wa ikolojia wa ziwa hilo.
Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (TRAMEPRO), ukiongozwa na Katibu Mkuu wake, Boniventura Mwalongo, umebaini changamoto kadhaa zinazolikumba ziwa hilo. Ziara hiyo ilifanyika katika eneo la Kigoto, Mwanza, kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki za Binadamu (TAHURI).

Miongoni mwa changamoto zilizobainika ni pamoja na uwepo wa magugu vamizi, matumizi holela ya rasilimali za ziwa, pamoja na uchafuzi wa maji unaotokana na majitaka yasiyodhibitiwa.

Aidha, kupungua kwa kina cha maji kumetajwa kuwa matokeo ya moja kwa moja ya uharibifu wa maeneo ya kinga ya fukwe, jambo linalochangia kuongezeka kwa tope na mchanga ndani ya ziwa. Hali hii inaathiri kwa kiasi kikubwa mazalia ya samaki na kusababisha kupungua kwa uzalishaji wa rasilimali hiyo muhimu.

Wataalamu wanaonya kuwa endapo hali hii itaendelea, usalama wa chakula, ajira za wavuvi na uchumi wa maeneo yanayozunguka ziwa hilo vitakuwa hatarini.


Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Tanzania Breweries Limited (TBL) imetoa wito kwa wadau mbalimbali nchini kushirikiana kwa karibu katika kukabiliana na changamoto ya pombe haramu, ikisema tatizo hilo linaendelea kuhatarisha afya ya wananchi, kudhoofisha uchumi na kuathiri biashara halali.

Akizungumza katika taarifa yake, kampuni hiyo imepongeza juhudi za Serikali zinazoendelea kuchukuliwa dhidi ya biashara haramu, hususan operesheni za kukamata na kuondoa bidhaa bandia sokoni, ambazo zimeelezwa kuwa zinaonesha dhamira ya kulinda watumiaji na kuhakikisha ushindani wa haki.

Hata hivyo, TBL imebainisha kuwa pombe haramu bado imeenea kwa kiwango kikubwa nchini, hali inayowaweka wananchi wengi katika hatari ya kutumia vinywaji visivyo salama na visivyodhibitiwa. Imeelezwa kuwa hali hiyo pia inaongeza shinikizo kwa sekta ya afya na kudhoofisha uchumi rasmi.

Kwa upande wa afya, imeelezwa kuwa pombe haramu mara nyingi hutengenezwa bila kufuata viwango vinavyotakiwa, jambo linaloweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo uharibifu wa viungo vya mwili, kupoteza uwezo wa kuona na hata vifo.

Kiuchumi, TBL imeeleza kuwa Tanzania inapoteza zaidi ya shilingi trilioni moja kila mwaka kutokana na mapato yasiyokusanywa yanayotokana na biashara hiyo haramu. Fedha hizo zingeweza kusaidia kuboresha huduma za jamii kama afya, elimu na miundombinu.

Aidha, kampuni hiyo imeeleza kuwa uwepo wa pombe haramu unaathiri ushindani wa haki sokoni, kwani wafanyabiashara wanaofuata sheria hukumbana na ushindani kutoka kwa wale wanaokwepa kodi na kuuza bidhaa kwa bei ya chini, hali inayopunguza uwekezaji na kuathiri ajira.

Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, amesema kuwa suluhisho la kudumu linahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii kwa ujumla. Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha utekelezaji wa sheria, kuweka mifumo madhubuti ya udhibiti, pamoja na kuendesha kampeni za elimu kwa umma kuhusu madhara ya pombe haramu.

“Mapambano dhidi ya pombe haramu ni jukumu la pamoja. Kila mdau ana nafasi ya kuhakikisha bidhaa zisizo salama zinapungua sokoni na wananchi wanatumia bidhaa zilizo salama na zinazokidhi viwango,” alisema Kilpin.

TBL imeeleza kuwa itaendelea kujikita katika uzalishaji wa bidhaa bora pamoja na kushirikiana na wadau wengine katika kulinda afya ya watumiaji na kukuza matumizi ya uwajibikaji.

Imeelezwa kuwa pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa, bado kuna haja ya kuweka mikakati ya muda mrefu itakayohakikisha tatizo la pombe haramu linadhibitiwa kikamilifu, hasa kwa kuzingatia kuwa upatikanaji wake kwa urahisi na bei nafuu unaendelea kuchochea matumizi yake kwa baadhi ya makundi ya wananchi.

Mapambano dhidi ya pombe haramu yameainishwa kuwa muhimu katika kulinda afya ya jamii, kuongeza mapato ya Serikali na kuhakikisha soko la pombe linakuwa salama, lenye ushindani wa haki na endelevu.