Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM — Waumini wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania, Stanslaus Thobias Nyakunga na Elia Phaustine Kabote, wamewasilisha rasmi barua kwa Balozi wa Vatican nchini, Archbishop Angelo Accattino, wakiomba kufanyika kwa uchunguzi wa kichungaji na kiutawala kuhusu mwenendo wa Padri Dkt. Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).

Kwa mujibu wa waumini hao, ombi hilo limetokana na malalamiko na mitazamo iliyodaiwa kuenea kwa muda mrefu katika jamii, ikihusisha Padri Kitima na masuala ya siasa za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hususan madai ya kuingilia au kushiriki katika migogoro ya ndani ya chama hicho—hali ambayo, wamesema, haijaonekana kwa vyama vingine vya siasa.

Nyakunga na Kabote wamesema kuwa mitazamo hiyo, iwe ni ya kweli au la, imeanza kuibua sintofahamu miongoni mwa waumini na kuliweka Kanisa katika mazingira yanayoweza kutafsiriwa kama ya upendeleo wa kisiasa. Hali hiyo, wamedai, inaweza kuhatarisha nafasi ya Kanisa kama taasisi ya amani, upatanisho na mwongozo wa kimaadili kwa jamii.

Katika barua yao kwa Balozi wa Vatican, waumini hao wamesisitiza kuwa hawakusudii kutoa hukumu wala kumshambulia mtu binafsi, bali wanaiomba mamlaka ya Kanisa kulishughulikia suala hilo kwa busara ya kichungaji ili kulinda umoja wa waumini na taswira ya Kanisa kwa ujumla.


Waumini hao wamerejea Maandiko Matakatifu wakisisitiza wajibu wa viongozi wa Kanisa kuwa nguzo za amani na maridhiano. Katika barua hiyo, wamenukuu kauli ya Biblia isemayo: “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mathayo 5:9), pamoja na “Kwa maana Mungu si wa machafuko bali wa amani” (1 Wakorintho 14:33). Aidha, wametaja onyo la Mtume Paulo dhidi ya mgawanyiko miongoni mwa waumini (1 Wakorintho 1:10).

Hatua ya waumini hao imekuja katika kipindi ambacho taifa linapitia mjadala mpana wa kisiasa na kijamii, ambapo taasisi za dini zinatarajiwa kuwa nguzo za utulivu, maridhiano na mshikamano wa kitaifa, badala ya kuonekana kuvutwa katika mvutano wa vyama vya siasa.

Katika maombi yao, Nyakunga na Kabote wameomba mambo matatu makuu: kufanyika kwa uchunguzi wa mwenendo wa Padri Kitima, kutolewa kwa mwelekeo wa wazi unaohakikisha uongozi wa Kanisa unabaki huru dhidi ya siasa za vyama, na kuchukuliwa kwa hatua zozote zitakazolinda umoja wa waumini, amani ya jamii na mamlaka ya kimaadili ya Kanisa.

Waumini hao wamesema wanaliamini Holy See kuwa na busara na mamlaka ya kushughulikia suala hilo kwa maslahi mapana ya Kanisa na jamii kwa ujumla.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: