Articles by "DINI"
Showing posts with label DINI. Show all posts
Askofu Philemon Nyika wa Kanisa la International Evangelism Church Ikungi, mkoani Singida, akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini Wilaya ya Ikungi walipokuwa wakitoa tamko la kuwaomba wananchi kushiriki kikamilifu uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho Oktoba 29, 2025.

Na Mwandishi Wetu, Ikungi

Ikungi,  Singida Oktoba 28, 2025: VIONGOZI wa Dini Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wametoa tamko la kuwaomba wananchi wote wa wilaya hiyo kushiriki kikamilifu kwa Amani uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho Oktoba 29, 2025.

Tamko hilo wamelitoa Oktoba 27, 2025 wakati wakizungumza na waandishi habari na kueleza kuwa Oktoba 29 kila mwaka ni siku ya uchaguzi mkuu wa kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini wenzake Askofu Philemon Nyika wa Kanisa la International Evangelism Church Ikungi alisema wakiwa kama walezi wa maadili, amani na mshikamano katika jamii wanatoa tamko hilo kuhamasisha wananchi wote wa Wilaya ya Ikungi na Tanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.

“ Kupiga kura ni haki ya kila mtu kikatiba na ni wajibu wa kizalendo, tunawasihi wananchi wote waliojiandikisha wajitokeze kwa wingi kesho Oktoba 29, 2025 kwenda kupiga kura,” alisema Askofu Nyika.

Aidha Askofu Nyika aliwataka wananchi kufanya maamuzi ya busara na ya haki kwa kuchagua viongozi wanaoamini watawatumikia kwa uadilifu huku wakitambua kwamba kura ni haki yao na kulinda amani ya nchi ni wajibu wa kila mmoja wetu.

Askofu Nyika alisema kudumisha amani ni msingi wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiroho, hivyo wanawakumbusha wananchi wote kwamba tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa chanzo cha chuki, migawanyiko, maandamano na vurugu siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi na visipewe nafasi kwa sababu amani ni zawadi kutoka kwa Mungu isichezewe hata kidogo.

“Sisi Viongozi wa dini kutoka Wilaya ya Ikungi tutaendelea kuliomba taifa letu liendelee kuwa na utulivu, mshikamano, upendo na tunawasihi waumini wetu waendelee kuiombea nchi yetu ya Tanzania,” alisema Askofu Nyika.

Kwa upande wake Sheikh wa Wilaya ya Ikungi, Abdi Selemani alisema tunapoenda kupiga kura kesho jambo la kwanza ni kuangalia amani ya nchi yetu kwani amani ni tamko la lililotoka kwa Mungu na ni jambo kubwa sana.

“Tuna wasihi wananchi wa Wilaya ya Ikungi na Tanzania kwa ujumla kuendelea kuitunza amani hii tuliyopewa na Mwenyezi Mungu, “ alisema Sheikh Selemani.

Sheikh Selemani aliwaomba wananchi wote waliojiandikisha kupiga kura kesho Oktoba 29, 2025 kwenda kufanya hivyo kwani ni haki yao na wasipofanya hivyo watakuwa wamejinyima haki hiyo.

Naye Askofu Jeremia Samuel wa Kanisa la The Free Pentecostal Church Of Tanzania Jimbo la Ikungi, alisema kesho Oktoba 29, 2025 ni jukumu la kila Mtanzania aliyejiandikisha kujitokeza kwenda kupiga kura kwa ajili ya kumchagua Rais wetu, wabunge na madiwani.

“Kwa bahati nzuri vyama vyote vilivyoshiriki kampeni tumewaona wagombea wao walivyoshiriki kunadi sera za vyama vyao hivyo imetupa urahisi wa kujua ni nani wa kuweza kutuongoza katika taifa letu hivyo ni wito wetu viongozi wa dini kwenu kesho Oktoba 29, 2025 mjitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura,” alisema Askofu Samuel.

Viongozi wa dini walioshiriki katika mkutano huo ni kutoka Jumuiya Zawwiyyatul Qaadiriyya Tanzania (JZQT) ambayo,ni muungano wa mazawiyya yote ya Tanzania, Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), The Free Pentecostal Church Of Tanzania, Kanisa la CPCT na Aswar Suna
Sheikh wa Wilaya ya Ikungi, Abdi Selemani akizungumza kwenye mkutano huo.
Askofu Jeremia Samuel wa Kanisa la The Free Pentecostal Church Of Tanzania Jimbo la Ikungi, akichangia jambo kwenye mkutano huo.
Viongozi wa dini Wilaya ya Ikungi wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano huo.
Viongozi wa dini wa Wilaya ya Ikungi waliopata fursa ya kuzungumza kwa niaba ya wenzao. Kutoka kushoto ni Sheikh wa Wilaya ya Ikungi, Abdi Selemani, Askofu Philemon Nyika wa Kanisa la International Evangelism Church Ikungi na Askofu Jeremia Samuel wa Kanisa la The Free Pentecostal Church Of Tanzania Jimbo la Ikungi.
Viongozi wa dini wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano huo ukiendelea.
Viongozi wa dini wakiwa kwenye mkutano huo.
Viongozi wa dini wakiuombea uchaguzi uchanyike kwa Amani hapo kesho Oktoba 29, 2025.

Vatican, Roma — Hija ya kiroho ya Mwaka wa Jubilei Kuu 2025 imekuwa tukio la kipekee kwa Mtanzania mmoja ambaye amefanikisha ndoto yake ya kukutana na Baba Mtakatifu, Papa Leo XIV, na kupata baraka kuu na rehema kamili kutoka kwake.

Irenca Mama Gees, Mtanzania na Mkristo wa Kanisa Katoliki, ameeleza kuwa ni changamoto kubwa kueleza hisia zake baada ya tukio hilo: “Nimepoteza maneno, moyo wangu umejaa shukrani za dhati. Yote ninayoyafanya na kila kitu katika maisha yangu, nakitupa sifa kwa Mungu… na kwa Mungu tu,” alisema kwa unyenyekevu mkubwa.

Safari hii ya kiroho, inayojulikana kama Mahujaji wa Matumaini, ni sehemu ya Mwaka wa Jubilei Kuu 2025, na inahusisha ibada maalumu, sala, na kutafuta rehema na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu. Mama Gees amesisitiza shukrani zake kwa wote waliomsaidia kwa hali na mali kuhakikisha ndoto yake ya kiroho inatimika.
“Tukio hili ni ndoto iliyotimia, kukutana na Papa Leo XIV kwenye Vatican. Nimejawa na furaha isiyoelezeka na shukrani zisizo na kifani kwa Mungu,” aliongeza.

Mama Gees ameeleza kuwa safari hii ni kumbukumbu isiyosahaulika na kuwa alitazama tukio hilo kama baraka kubwa katika maisha yake ya kiroho. Picha za tukio hilo zimesambaa katika mitandao ya kijamii zikionyesha furaha na unyenyekevu wake akiwa ndani ya Basilica ya Mt. Petro Vatican, Roma.

Hija hii imehimiza wengi katika jamii ya Watanzania wa Kanisa Katoliki kuendeleza imani na kufanya safari za kiroho ili kupata karibu na imani yao. Irenca Mama Gees amesisitiza kwamba kila mtu anapaswa kutunza na kuthamini nafasi za kiroho kama hizi zinazofungua njia ya baraka na rehema.
Dar es Salaam, Oktoba 13, 2025: Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limekanusha vikali waraka ulioenezwa kwenye mitandao ya kijamii ukidai umetolewa na Baraza hilo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Katika taarifa iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa TEC, Rev. Fr. Charles Kitima, Baraza hilo limesema waraka wenye kichwa cha habari “Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Kuhusu Amani kwa Taifa Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Utakaofanyika Tarehe 29 Oktoba 2025” siyo halali na haujatolewa na TEC.

“Tunapenda kuwatangazia Waamini na Watanzania wote kwa ujumla kuwa waraka huo si wa kweli, na Baraza halihusiki na maudhui yaliyomo ndani yake,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

TEC imeeleza kusikitishwa na tabia ya baadhi ya watu kutumia jina la Taasisi hiyo kusambaza jumbe zisizotokana na Baraza, na kuwataka wahusika kuacha mara moja.

“Tabia hii mbaya ya kutumia Taasisi ya Maaskofu kupitia jumbe za uongo lazima ikome,” iliongeza taarifa hiyo.

Baraza hilo limewataka Watanzania kupuuza taarifa hiyo feki na kusisitiza kuwa tamko lolote rasmi kutoka kwa TEC litatolewa kupitia vyanzo vyake halali.
Iringa, Septemba 30, 2025: Kanisa Katoliki Jimbo la Mafinga limeweka wazi sintofahamu kuhusu Padre Jordan Kibiki, aliyeripotiwa kujiteka wiki iliyopita, na kufafanua kuwa tukio hilo lilitokana na changamoto ya afya ya akili, hususan msongo wa mawazo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kanisa hilo, Jeshi la Polisi limefuta tuhuma dhidi ya Padre Kibiki na kumwachia huru baada ya uchunguzi kuthibitisha ukweli huo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Askofu wa Jimbo la Mafinga, Mhashamu Vicent Mwagala, alisema Padre Kibiki ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Afya Nyololo na Paroko Msaidizi wa Parokia hiyo, alitarajiwa Septemba 18, 2025 kuhudhuria kikao cha afya katika ofisi za Halmashauri ya Mufindi, lakini hakuwasili licha ya kuondoka nyumbani asubuhi.

Askofu Mwagala alieleza kuwa gari lake lilipatikana limeegeshwa barabarani bila dereva na juhudi za kumpata ziligonga mwamba, hali iliyosababisha hofu kubwa miongoni mwa waumini na viongozi wenzake.

Kwa mujibu wa maelezo ya Polisi, Padre Kibiki alikiri kujitenga kutokana na msongo wa mawazo uliosababishwa na shinikizo la kifedha baada ya kupoteza fedha alizokuwa amekopa kwenye biashara ya mtandao (online scam).

“Baada ya uchunguzi wa kitabibu, madaktari walithibitisha kuwa Padre Kibiki alikuwa anakabiliwa na depression. Kwa ushauri wa wataalamu, amepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Tosamaganga kwa uangalizi wa karibu na matibabu ya afya ya akili,” alisema Askofu Mwagala.

Aliongeza kuwa Jimbo la Mafinga linaendelea kufuatilia afya ya Padre Kibiki ili aweze kurejea katika hali ya kawaida na kuendelea na majukumu yake ya kiroho.

“Tunawaomba waumini na jamii kwa ujumla waendelee kumwombea Padre Jordan ili apone haraka,” alisema, huku akilishukuru Jeshi la Polisi na vyombo vya habari kwa ushirikiano katika kipindi hicho kigumu.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO, 2023), msongo wa mawazo ni moja ya changamoto kubwa za kiafya duniani, na unaweza kumpata mtu yeyote bila kujali nafasi, kazi au wito wake wa kidini.

Vatican.
Misa ya mazishi ya Askofu Mkuu Novatus Rugambwa imefanyika Septemba 25 katika Basilika ya Mtakatifu Petro, ikiendeshwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican. Katika hotuba yake, Kardinali Parolin alimsifu marehemu kwa maisha ya uchaji, unyenyekevu na uadilifu aliouonyesha katika safari yake ndefu ya kuhudumu katika diplomasia ya Vatican.

Kardinali Parolin alikumbusha safari ya maisha ya Askofu Rugambwa, aliezaliwa Bukoba, Tanzania, tarehe 1 Oktoba 1957, na kupewa daraja la upadre mwaka 1986. Kuanzia mwaka 1991, aliutumikia muda mrefu utumishi wa diplomasia ya Vatican, akiacha alama kubwa ya upendo na imani.

Katika hotuba yake, Kardinali alisisitiza ushuhuda wa marehemu wakati wa ugonjwa alioupitia, akisema kuwa aliukabili kwa imani na moyo wa upendo, na hivyo kugeuza mateso yake kuwa fursa ya kumtegemea Mungu na kuimarisha imani ya watu wa Mungu waliomzunguka.
Mfano wa upendo na uaminifu wa kidiplomasia

Kardinali Parolin alieleza kuwa Askofu Rugambwa alitoa mfano bora wa utumishi katika diplomasia ya Kanisa, ambayo aliiita “njia ngumu ya kichungaji inayodai uaminifu wa Injili na heshima ya watu wa mataifa mbalimbali.” Alisema marehemu alitenda kwa uchaji, busara na uthabiti katika kutetea haki na heshima ya binadamu, mambo ambayo ni nguzo ya amani ya kweli.
Kwa mujibu wa Kardinali, Askofu Rugambwa aliweza kutengeneza uhusiano thabiti na wa kujenga, akiwa na moyo wa kichungaji uliojaa subira na upendo wa kibaba.

Mshuhuda wa kweli wa maisha matakatifu

Aidha, Kardinali Parolin aliongeza kuwa sifa nyingine kubwa ya marehemu ilikuwa ni “uadilifu wa maisha” uliomfanya kuwa shahidi wa kweli na anayeaminika wa ukweli aliohubiri. Akinukuu maneno ya Mtakatifu Paulo VI, alisema: “Binadamu wa leo husikiliza zaidi mashahidi kuliko walimu.”

Alisisitiza kuwa mfano bora wa maisha matakatifu ni silaha muhimu zaidi kwa wachungaji wa Kanisa, hasa wale wanaotumikia kama mabalozi wa Papa.
Urithi wa upendo na unyenyekevu

Kardinali pia aligusia huruma na mshikamano wa marehemu na maskini, akisema ulikuwa ni “mzizi wa maisha yake ya kikristo na njia ya pekee ya kukutana na Mungu.”

Alihitimisha mahubiri yake kwa maneno ya Mtakatifu Leo Mkuu, akisema kwamba wale wanaokaa katika upendo na umoja wa Roho hawatashindwa na vikwazo vyovyote, bali baada ya mapambano ya maisha ya duniani, watapata pumziko la amani ya Mungu.

Kardinali Parolin aliomba neema hiyo itimizwe kwa Askofu Rugambwa, na pia kwa waamini wote, ili kwa unyenyekevu na mshikamano, wawe vyombo vya wokovu kwa kila mmoja, hadi watakapokutana tena nyumbani mwa Baba wa mbinguni.
Tabora, Septemba 21, 2025 – Maelfu ya waamini wa Kanisa Katoliki kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania walijitokeza jijini Tabora kushiriki Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre wa Askofu Mkuu Mstaafu, Mhashamu Paulo Runangaza Ruzoka. Sherehe hizo, zilizofanyika katika Viwanja vya Solomoni, nje ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, zilihudhuriwa na viongozi wa Kanisa, makasisi, watawa, na waamini wa kawaida.

Katika maandamano ya heshima, watumishi wa altare, mashemasi, mapadre, mafrateri na maaskofu waliongoza msafara, huku wakisindikizwa na nyimbo za shukrani na heshima. Kardinali Polycarp Pengo na maaskofu wengine wa majimbo jirani walihudhuria ibada hiyo, iliyoashiria nusu karne ya huduma ya kichungaji ya Askofu Ruzoka.

Nukuu na Ushuhuda

Akitoa homilia, Askofu Mkuu wa Tabora alisema: “Waliomfahamu Askofu Ruzoka hakuona aibu na hakuwa na uoga kuishuhudia imani ya Kristo kwa kuitangaza.”

Askofu Ruzoka mwenyewe, akizungumza kwa unyenyekevu, alishukuru kwa zawadi ya maisha ya upadre na wito wa kuongoza Kanisa kwa miaka mingi, akisisitiza mshikamano na mshikikano wa Kikristo. “Utumishi wa kweli ni kielelezo cha upendo wa Kristo kwa binadamu,” alisisitiza katika hotuba yake fupi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)

Katika salamu zake za pongezi, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) liliupongeza mchango wa Askofu Mkuu Mstaafu Ruzoka, likisema ameacha alama kubwa katika historia ya Kanisa na Taifa:

Alitambulika kwa malezi na makuzi katika Seminari Ndogo ya Itaga na kusimamia Sinodi ya kwanza ya Jimbo Katoliki Kigoma na baadaye Tabora.

Ni miongoni mwa waasisi wa Kamati ya Haki na Amani ya Viongozi wa Dini Tanzania, iliyolenga kudumisha mshikamano wa kitaifa, haki na upendo miongoni mwa Watanzania.

TEC ilimsifu kama gwiji wa historia ya Kanisa na Tanzania, aliyesimama kidete kulinda haki, amani na ustawi wa jamii.

Askofu Flavian Kassala wa Geita, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa TEC, alisema:
“Askofu Ruzoka ni kiongozi aliyeacha urithi wa kipekee – alisimama kulinda imani, alitunza historia na alihimiza mshikamano wa kitaifa kupitia kazi yake ya kichungaji na kijamii.”

Historia yake kwa kifupi

1948: Alizaliwa Nyakayenzi, Kigoma.

20 Julai 1975: Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre na Askofu Alphons Daniel Nsabi – akiwa Padre wa sita mzalendo wa Kigoma.

10 Novemba 1989: Alichaguliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Kigoma; aliwekwa wakfu Januari 6, 1990 mjini Vatican.

25 Novemba 2006: Aliteuliwa na Papa Benedikto XVI kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, na kusimikwa rasmi Januari 28, 2007.

10 Novemba 2023: Papa Francisko akaridhia ombi lake la kung’atuka, na kumteua Kardinali Protase Rugambwa kumrithi Tabora.

Kwa jumla, amehudumu kama Padre kwa miaka 48 na Askofu kwa miaka 33, akifundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Urithi wake

Askofu Mkuu Mstaafu Ruzoka ataendelea kukumbukwa kama mchungaji na mlezi wa imani, aliyekuwa daraja kati ya Kanisa na jamii. Urithi wake wa maendeleo, mshikamano na uadilifu wa kiroho utaendelea kuwa dira kwa vizazi vijavyo.
Askofu Mkuu Novatus Rugambwa alizaliwa tarehe 8 Oktoba 1957 huko Bukoba, Tanzania. Alijiunga na masomo ya upadre na baada ya mafunzo ya kidini, alipewa daraja la upadre mwaka 1986.

Baada ya miaka ya utumishi wa kichungaji, alijiunga na Shule ya Kidiplomasia ya Vatican (Pontifical Ecclesiastical Academy), ambapo alifundishwa masuala ya kidiplomasia na sheria za kanisa.

Mnamo 1991, alianza rasmi kutumikia Huduma ya Kidiplomasia ya Vatican, akihudumu katika balozi mbalimbali za kitume duniani, ikiwemo Sudan, Turkey, Pakistan, na Indonesia.

Mwaka 2010, Papa Benedict XVI alimteua kuwa Askofu Mkuu na Balozi wa Vatican (Apostolic Nuncio) nchini Angola na Sao Tome and Principe. Baadaye alihamishiwa Honduras (2015), kisha New Zealand, Fiji, Tonga na Samoa (2019).

Mbali na jukumu la kidiplomasia, Askofu Mkuu Rugambwa alikuwa pia mjumbe wa kudumu wa Vatican katika mashirika mbalimbali ya kimataifa.

Kote alikopita, alijulikana kwa unyenyekevu wake, hekima ya kidiplomasia na moyo wa upendo, uliomfanya kuwa daraja kati ya Vatican, makanisa ya eneo husika na serikali.

Urithi wake

Kifo cha Askofu Mkuu Rugambwa kimeacha pengo kubwa, lakini mchango wake katika Kanisa na katika kuliletea taifa heshima kwenye meza ya kidiplomasia ya kimataifa utabaki kuwa sehemu ya urithi wake.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza na Mwenyekiti wa Bodi ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Renatus Nkwande,akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 88 wa Chama cha Madaktari Tanzania (TCMA) jijini Dodoma.

Na Alex Sonna - Dodoma.

KATIKA kuunga mkono jitihada za serikali kwenye sekta ya afya zaidi ya vituo 900 vya afya nchini ikiwemo hospitali 105, vituo vya afya 134 na zahanati 697 vinaendeshwa na makanisa, mchango unaokadiriwa kufikia asilimia 42 ya huduma za Afya nchini.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Renatus Nkwande, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 88 wa Chama cha Madaktari Tanzania (TCMA).

Amesema kuwa Kanisa linasimamia hospitali 105, ambapo tatu kati yake ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (Mwanza), Kituo cha Tiba ya Rufaa ya Kanda ya KCMC (Moshi), na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC)—zinatoa huduma za rufaa ngazi ya kanda.

Aidha, hospitali 12 za rufaa za mikoa na hospitali 37 zilizoteuliwa za wilaya (Council Designated Hospitals – CDH) zinaendeshwa kwa makubaliano rasmi na mamlaka za serikali za mitaa.

“Bila shaka mchango huu ni mkubwa na unapaswa kutambuliwa rasmi katika sera ya taifa ya afya,” amesisitiza Askofu Mkuu Renatus Nkwande.

Hata hivyo ameitaka Serikali kuelekeza moja kwa moja mgao wa fedha za basket fund kwenye hospitali za Kanisa badala ya kupitisha fedha hizo kupitia akaunti za halmashauri, akibainisha kuwa ucheleweshaji umekuwa chanzo cha changamoto kubwa za uendeshaji.

“Pia kuna changamoto ya ucheleweshaji wa fedha za mfuko wa pamoja (Basket fund) kunakosababishwa na utaratibu wa serikali kuzipitisha kwenye akaunti ya halmshauri badala ya kuzipeleka moja kwa moja kwenye taasisi za afya za dini kama inavyofanywa kwenye vituo vya serikali.

“Tunaomba uongozi wa makanisa kupitia makatibu wakuu na makatibu wa afya wa majimbo na Dayosisi kwa kushirikiana na Christian Social Services Commission (CSSC) kufuatilia kwa karibu jambo hili kwenye wizara husika,”amesema Askofu Mkuu Nkwande

Aidha, ametoa wito wa kuwepo kwa mgawanyo wa haki wa rasilimali watu, akieleza kuwa hospitali nyingi zinazomilikiwa na taasisi za dini zimekosa wataalamu bingwa, hali inayosababisha kushuka kwa ubora wa huduma.

Kadhalika, alisema hospitlai nyingi za kanisa ni za muda mrefu na nyingine zina zaidi ya miaka 100 miundombinu na vifaa vingi vimechakaa na kupitwa na wakati,

Alisema hali hiyo inachangia huduma duni ambazo zinashindwa kuhimili soko la ushindani.

“Tunashauri kuwepo na mkakati thabiti wa kuzifanyia ukarabati hospitali na vituo vya kutolea huduma ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa vifaa tiba ili kuongeza ufanisi na tija katika vituo vya kanisa na hivyo kuhimili ushindani wa soko,”amesema

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA) Dk. Gresmus Ssebuyoya amesema vituo vya afya vya makanisa nchini vinakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo uhamishaji wa watumishi kutoka vituo vya kanisa kwenda serikalini bila kufuata utaratibu.

Amesema, hali hiyo inasababisha uhaba wa watumishi unaochangia kuzorota kwa huduma katika vituo husika.

“Kama tulivyotangulia kusema, hospitali na vituo vingi vya kanisa hufanya kazi na serikali kupitia mikataba na halmshauri husika. Pamoja na nia njema ya serikali ya kufanya kazi na taasisi kupitia mpango wa PPP, utekelezajia wa mikataba hii umekuwa na changamoto kadhaa ikiwemo baadhi ya halmshauri kusita kuendelea kusaini mikataba inapoisha hata kama vituo husika vinaendelea kutumia rasamimali za serikali na kutoa huduma kama awali,”amesema Dk. Ssebuyoya

Amesema, hali hiyo inasabaisha uwapo wa hoja za kiukaguzi kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (CAG) zinazohitaji vituo vya kanisa kutoa ufafanuzi.

Aidha, alisema vituo vingi vya kutolea huduma za afya vya makanisa vipo vijijini sehemu ambazo ndiko waliko wananchi wengi na walio na uwezo mdogo wa kumudu hali ya maisha.

“Hadi mwishoni mwa mwaka jana, makanisa kwa pamoja yanaendesha vituo takriban 900 vya huduma za afya zikiwamo hospitali 105 ambapo hospitali tatu ni za rufaani ngazi ya kanda , ambazo ni Bugando Medical Center (BMC) ya Mwanza, Kilimanjaro Christian Medical Center (KCMC) ya Moshi na Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) ya Arusha na hospili 12 zikiwa na huduma za rufaa ngazi ya mkoa,”alisisitiza


Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza na Mwenyekiti wa Bodi ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Renatus Nkwande,akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 88 wa Chama cha Madaktari Tanzania (TCMA) jijini Dodoma.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza na Mwenyekiti wa Bodi ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Renatus Nkwande,akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 88 wa Chama cha Madaktari Tanzania (TCMA) jijini Dodoma.


Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA) Dk. Gresmus Ssebuyoya,akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 88 wa Chama cha Madaktari Tanzania (TCMA) jijini Dodoma.


Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza na Mwenyekiti wa Bodi ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Renatus Nkwande (hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 88 wa Chama cha Madaktari Tanzania (TCMA) jijini Dodoma.


Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza na Mwenyekiti wa Bodi ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Renatus Nkwande (hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 88 wa Chama cha Madaktari Tanzania (TCMA) jijini Dodoma.


Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza na Mwenyekiti wa Bodi ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Renatus Nkwande (hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 88 wa Chama cha Madaktari Tanzania (TCMA) jijini Dodoma.


Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza na Mwenyekiti wa Bodi ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Renatus Nkwande (hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 88 wa Chama cha Madaktari Tanzania (TCMA) jijini Dodoma.
Dar es Salaam: Benki ya CRDB hivi karibuni ilizindua ‘CRDB Al Barakah Sukuk,’ hatifungani inayokusanya fedha ili kuwezesha biashara bila riba nchini na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

Hatifungani hiyo inayofuata misingi ya Kiislamu, inakusudia kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 30 pamoja na dola za Marekani milioni 5 huku kukiwa na uwezekano wa kuongeza kiasi hicho mpaka shilingi bilioni 40 na dola milioni 7. Uzinduzi huo unaifanya CRDB Al Barakah Sukuk kuwa hatifungani yenye thamani kubwa zaidi kutolewa na taasisi ya fedha nchini tena ikiruhusu uwekezaji wa sarafu nyingi.
Akizindua hatifungani hiyo mwishoni mwa wiki, Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete ameipongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kuhamasisha ujumuishaji kiuchumi wa wananchi wote.

"Hatifungani hii inaleta mapinduzi katika masoko yetu ya mitaji nchini. Inatoa nafasi kwa watu ambao awali walikuwa wameachwa nje ya mfumo rasmi ya fedha kutokana na imani za kidini kwa kuileta fursa hii ya uwekezaji usio na riba unaoendana na misingi ya sharia. Hii ni hatua kubwa katika kuwajumuisha wananchi kiuchumi na maendeleo ya maadili yetu. Ninao uhakika kwamba hatifungani hii itavutia wawekezaji wengi kuliko matarajio mliyonayo kwa sasa,” amesema Rais Kikwete.
CRDB Al Barakah Sukuk ni toleo la tatu la hatifungani za Benki ya CRDB chini ya Mkakati wa Muda wa Kati (Medium Term Strategy) wa 2023–2027 wenye thamani sawa na dola za Marekani milioni 300 uliothibitishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).

Hatifungani hii imekuja baada ya Hatifungani ya Kijani (Green Bond) na Hatofungani ya Miundombinu ya Samia (Samia Infrastructure Bond) ambazo zote zilivutia wawekezaji wengi kuliko ilivyotarajiwa hali inayothibitisha imani waliyonayo wawekezaji wa ndani na nje ya nchi juu ya ufanisi wa Benki ya CRDB.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela amesema: "Hatifungani hii inathibitisha imani yetu kwamba uwezeshaji lazima uwe jumuishi na ukidhi mahitaji ya kila Mtanzania. Kupitia hatifungani hii tunafungua milango kwa watu wengi zaidi kushiriki uwekezaji kupitia masoko yetu ya mitaji bila kuathiri imani zao za kidini. Ni kichocheo cha kuwezesha miradi na biashara zinazozingatia maadili, zilizo endelevu na zinazoinufaisha jamii.”

Nsekela amesema fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo ya hatifungani hii zitaelekezwa kuwezesha miradi inazingatia maadili na biashara zisizo na madhara kwa binadamu kulingana na misingi ya sharia ikiwamo inayolenga kutoa huduma za afya, kilimo na ufugaji, elimu na uzalishaji usioathiri mazingira.
“Hatifungani hii inatoa faida ya asilimia 12 kwa mwaka kwa watakaowekeza kwa shilingi na asilimia 6 kwa watakaowekeza kwa dola ya Marekani kwa mwaka. Faida hii italipwa kwa mwekezaji mara nne kwa mwaka yaani kila baada ya miezi mitatu. Mtu binafsi, kampuni au taasisi anaweza kuwekeza kuanzia shilingi 500,000 au dola 1,000 za Marekani. Dirisha la uwekezaji litakuwa wazi kuanzia sasa mpaka Septemba 12,” amesema Nsekela.

British International Investment (BII), kampuni ya uwekezaji kutoka nchini Uingereza ndio mwekezaji mkuu katika hatifungani hii na Balozi wa uingereza nchini, Mheshimiwa Marianne Young amesema CRDB Al Barakah Sukuk itaimarisha diplomasia ya kiuchumi kati ya Tanzania na Uingereza.
“Uingereza inajisikia fahari kushirikiana na Tanzania kuwezesha uwekezaji endelevu. Kupitia BII tunaiunga mkono Benki ya CRDB kutambulisha hatifungani ya kwanza isiyo na riba nchini. Mafanikio haya yanadhihirisha ushirikiano wetu wenye faida kwa pande zote mbili katika mkakati huu wa kufanikisha ukusanyaji paundi bilioni 1 kwa ajili ya uwekezaji mpaka mwaka 2030. Hii ni hatifungani kwanza ye Kiislamu ambayo BII imewekeza duniani na ni fuaraha kuona uwekezaji huo umefanyika Tanzania. Sukuk hii itatoa fursa ya uwezeshaji wa biashara zinazochangia kukua kwa uchumi,” amesema Mheshimiwa Marianne Young.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Sharia, Abdul Van Mohammed amesema imani ya dini ni kati ya vitu muhimu ambavyo huongoza uamuzi wa wawekezaji wengi.
“Hatifungani hii inafuata misingi ya Sharia lakini ipo kwa ajili ya kila Mtanzania. Tunamkaribisha kila mwekezaji aliye tayari kuwekeza katika CRDB Al Barakah Sukuk ili kwa Pamoja tuujenge Uchumi wetu,” amesema Mohammed.

Akieleza namna CRDB Al Barak Sukuk ilivyovutia macho ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa BII, Jumai Mohammed amesema: “Tuna furaha kuwa mwekezaji mkuu wa CRDB Al Barakah Sukuk inayoendana na misingi yetu ya uwekezaji wezeshi na kukuza upatikanaji wa mitaji barani Afrika. Sukuk inadhihirisha umuhimu wa masoko ya mitaji na dhamana katika kukuza uchumi,” amesema Mohammed.

Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA Nicodemus Mkama pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela wamesema uzinduzi wa CRDB Al Barakah Sukuk unaonyesha kukua na kuimarika kwa masoko ya dhamana na mitaji nchini.