Articles by "UCHUMI"
Showing posts with label UCHUMI. Show all posts
Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), CPA (T) Moremi Marwa, amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali kupitia shirika hilo imepanga kujenga zaidi ya minara 1,400 ya mawasiliano nchini, ikianza na minara 600 mwaka huu, na mingine 850 kufuata mwaka 2026/2027.

CPA Marwa ameyasema hayo Agosti 24, 2025, katika banda la TTCL kwenye Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs Forum 2025) kinachoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha AICC jijini Arusha, kilichofunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdori Mpango.

Amesema TTCL ndiyo taasisi pekee nchini inayomiliki Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, huku Serikali ikiendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa ili kufanikisha ajenda ya uchumi wa kidijitali.

“Hatua hii inalenga kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na yenye changamoto ambazo kwa kawaida watoa huduma binafsi hawawezi kufika kutokana na kutolipa kibiashara,” alisema CPA Marwa.

Aidha, amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mpango huu miezi sita iliyopita, zaidi ya minara 100 imekwishajengwa, na matarajio ni kwamba ifikapo Juni 2026, minara yote 620 iliyopangwa kwa mwaka huu itakuwa imekamilika.

Ameongeza kuwa TTCL imejipanga kuhakikisha minara hiyo inaunganishwa moja kwa moja na Mkongo wa Taifa, ili wananchi wapate huduma za intaneti yenye kasi na uhakika.

Vilevile, CPA Marwa amekumbusha kuwa mwaka jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua mkakati wa kidijitali unaolenga kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kidijitali, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo imeweka msisitizo mkubwa katika eneo hilo.

Mbali na Mkongo wa Taifa, TTCL pia ina kituo cha Data Center kinachowezesha mifumo ya kidijitali nchini kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Uwekezaji huu unaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya teknolojia, huku wananchi wakinufaika na huduma bora za mawasiliano, ikiwemo intaneti ya kasi kubwa inayosaidia kukuza uchumi wa kidijitali nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Soko la Madini la Tanzanite Trading Centre lililopo Mirerani, Simanjiro.
Na Mwandishi Wetu, Simanjiro.

● Ujenzi wa soko la madini Mirerani umefikia 98%.

● Shilingi bilioni 5.5 zimetolewa na Rais Samia kukamilisha mradi

● Shughuli za biashara kuanza rasmi Septemba 15, 2025.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amemtaka mkandarasi Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha unakamilisha mapema ujenzi wa jengo la soko la madini la Tanzanite Trading Centre lililopo Mirerani, kufikia mwishoni mwa Agosti mwaka huu.

RC Sendiga alitoa agizo hilo jana Agosti 18, 2025 wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi huo, ambapo hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 98 ya utekelezaji.
Jengo la Soko la Madini la Tanzanite Trading Centre lililopo Mirerani, Simanjiro mkoani Manyara, likiwa katika hatua za mwisho za ujenzi.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, akikagua maendeleo ya ujenzi wa Soko la Madini la Tanzanite Trading Centre lililopo Mirerani, Wilaya ya Simanjiro
Jiwe la Msingi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Bi. Mariam Muhaji, akizungumza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Soko la Madini la Tanzanite Trading Centre lililopo Mirerani, Wilaya ya Simanjiro.
---
“Hakuna sababu ya kuchelewesha mradi huu, hasa ikizingatiwa kuwa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan tayari ametoa zaidi ya shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya kukamilisha soko hili,” alisema Sendiga.

Aidha, alielekeza kuwa kufikia Septemba 15, 2025 shughuli rasmi za uuzaji na uchakataji wa madini zianze katika soko hilo, akisisitiza kuwa litakuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Mirerani na Wilaya ya Simanjiro kwa ujumla.

Katika kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa bora, RC Sendiga alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Simanjiro kusimamia maboresho ya ndani na nje ya eneo la soko, huku akisisitiza viwanja vya biashara vinavyozunguka eneo hilo vitolewe bila urasimu.
“Viwanja hivi ni mali yetu wananchi wa Mirerani. Tuelezwe wazi masharti ni yapi ili wananchi wajipange mapema. Tunataka faida ya kwanza ibaki kwa wananchi wa hapa,” alisisitiza.

Vile vile, RC Sendiga aliwataka viongozi na wananchi kuendelea kulitangaza soko hilo ili liwe kitovu cha biashara na uwekezaji wa madini aina ya Tanzanite.

Katika hatua nyingine, aliwakumbusha wakazi wa Mirerani na Simanjiro kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Dar es Salaam: Benki ya CRDB hivi karibuni ilizindua ‘CRDB Al Barakah Sukuk,’ hatifungani inayokusanya fedha ili kuwezesha biashara bila riba nchini na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

Hatifungani hiyo inayofuata misingi ya Kiislamu, inakusudia kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 30 pamoja na dola za Marekani milioni 5 huku kukiwa na uwezekano wa kuongeza kiasi hicho mpaka shilingi bilioni 40 na dola milioni 7. Uzinduzi huo unaifanya CRDB Al Barakah Sukuk kuwa hatifungani yenye thamani kubwa zaidi kutolewa na taasisi ya fedha nchini tena ikiruhusu uwekezaji wa sarafu nyingi.
Akizindua hatifungani hiyo mwishoni mwa wiki, Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete ameipongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kuhamasisha ujumuishaji kiuchumi wa wananchi wote.

"Hatifungani hii inaleta mapinduzi katika masoko yetu ya mitaji nchini. Inatoa nafasi kwa watu ambao awali walikuwa wameachwa nje ya mfumo rasmi ya fedha kutokana na imani za kidini kwa kuileta fursa hii ya uwekezaji usio na riba unaoendana na misingi ya sharia. Hii ni hatua kubwa katika kuwajumuisha wananchi kiuchumi na maendeleo ya maadili yetu. Ninao uhakika kwamba hatifungani hii itavutia wawekezaji wengi kuliko matarajio mliyonayo kwa sasa,” amesema Rais Kikwete.
CRDB Al Barakah Sukuk ni toleo la tatu la hatifungani za Benki ya CRDB chini ya Mkakati wa Muda wa Kati (Medium Term Strategy) wa 2023–2027 wenye thamani sawa na dola za Marekani milioni 300 uliothibitishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).

Hatifungani hii imekuja baada ya Hatifungani ya Kijani (Green Bond) na Hatofungani ya Miundombinu ya Samia (Samia Infrastructure Bond) ambazo zote zilivutia wawekezaji wengi kuliko ilivyotarajiwa hali inayothibitisha imani waliyonayo wawekezaji wa ndani na nje ya nchi juu ya ufanisi wa Benki ya CRDB.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela amesema: "Hatifungani hii inathibitisha imani yetu kwamba uwezeshaji lazima uwe jumuishi na ukidhi mahitaji ya kila Mtanzania. Kupitia hatifungani hii tunafungua milango kwa watu wengi zaidi kushiriki uwekezaji kupitia masoko yetu ya mitaji bila kuathiri imani zao za kidini. Ni kichocheo cha kuwezesha miradi na biashara zinazozingatia maadili, zilizo endelevu na zinazoinufaisha jamii.”

Nsekela amesema fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo ya hatifungani hii zitaelekezwa kuwezesha miradi inazingatia maadili na biashara zisizo na madhara kwa binadamu kulingana na misingi ya sharia ikiwamo inayolenga kutoa huduma za afya, kilimo na ufugaji, elimu na uzalishaji usioathiri mazingira.
“Hatifungani hii inatoa faida ya asilimia 12 kwa mwaka kwa watakaowekeza kwa shilingi na asilimia 6 kwa watakaowekeza kwa dola ya Marekani kwa mwaka. Faida hii italipwa kwa mwekezaji mara nne kwa mwaka yaani kila baada ya miezi mitatu. Mtu binafsi, kampuni au taasisi anaweza kuwekeza kuanzia shilingi 500,000 au dola 1,000 za Marekani. Dirisha la uwekezaji litakuwa wazi kuanzia sasa mpaka Septemba 12,” amesema Nsekela.

British International Investment (BII), kampuni ya uwekezaji kutoka nchini Uingereza ndio mwekezaji mkuu katika hatifungani hii na Balozi wa uingereza nchini, Mheshimiwa Marianne Young amesema CRDB Al Barakah Sukuk itaimarisha diplomasia ya kiuchumi kati ya Tanzania na Uingereza.
“Uingereza inajisikia fahari kushirikiana na Tanzania kuwezesha uwekezaji endelevu. Kupitia BII tunaiunga mkono Benki ya CRDB kutambulisha hatifungani ya kwanza isiyo na riba nchini. Mafanikio haya yanadhihirisha ushirikiano wetu wenye faida kwa pande zote mbili katika mkakati huu wa kufanikisha ukusanyaji paundi bilioni 1 kwa ajili ya uwekezaji mpaka mwaka 2030. Hii ni hatifungani kwanza ye Kiislamu ambayo BII imewekeza duniani na ni fuaraha kuona uwekezaji huo umefanyika Tanzania. Sukuk hii itatoa fursa ya uwezeshaji wa biashara zinazochangia kukua kwa uchumi,” amesema Mheshimiwa Marianne Young.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Sharia, Abdul Van Mohammed amesema imani ya dini ni kati ya vitu muhimu ambavyo huongoza uamuzi wa wawekezaji wengi.
“Hatifungani hii inafuata misingi ya Sharia lakini ipo kwa ajili ya kila Mtanzania. Tunamkaribisha kila mwekezaji aliye tayari kuwekeza katika CRDB Al Barakah Sukuk ili kwa Pamoja tuujenge Uchumi wetu,” amesema Mohammed.

Akieleza namna CRDB Al Barak Sukuk ilivyovutia macho ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa BII, Jumai Mohammed amesema: “Tuna furaha kuwa mwekezaji mkuu wa CRDB Al Barakah Sukuk inayoendana na misingi yetu ya uwekezaji wezeshi na kukuza upatikanaji wa mitaji barani Afrika. Sukuk inadhihirisha umuhimu wa masoko ya mitaji na dhamana katika kukuza uchumi,” amesema Mohammed.

Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA Nicodemus Mkama pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela wamesema uzinduzi wa CRDB Al Barakah Sukuk unaonyesha kukua na kuimarika kwa masoko ya dhamana na mitaji nchini.

Dodoma, Agosti 7, 2025: Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet R. Lekashingo, ameongoza ujumbe wa Tume kutembelea Banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (Nane Nane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Dkt. Lekashingo ameambatana na Makamishna wa Tume, Mhandisi Theonestina Mwasha na Dkt. Theresia Numbi, pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo. 

Wakiwa katika banda hilo, wamepata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Tume, ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini, taratibu za upatikanaji wa leseni, biashara ya madini, uongezaji thamani madini, pamoja na usimamizi wa mazingira katika shughuli za uchimbaji.

Akizungumza na maafisa wa Tume na wananchi waliotembelea banda hilo, Dkt. Lekashingo amewapongeza watumishi wa Tume kwa kazi nzuri ya kutoa elimu na huduma kwa umma.

Amesisitiza umuhimu wa kutumia maonesho hayo kama jukwaa la kuelimisha na kuhamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu katika Sekta ya Madini, hususan kupitia uongezaji thamani madini na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo.

“Ni muhimu wananchi wakapata uelewa mpana kuhusu namna wanavyoweza kunufaika na rasilimali za madini zilizopo nchini iwe ni kupitia uchimbaji, biashara, uongezaji thamani au utoaji wa huduma kwenye migodi. Sekta hii ina mchango mkubwa katika Pato la Taifa na ajira kwa Watanzania,” amesisitiza Dkt. Lekashingo.

Kwa upande wao, Makamishna wa Tume wameeleza kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi kutembelea banda la Tume na kuonesha dhamira ya kujifunza zaidi kuhusu Sekta ya Madini, jambo linalodhihirisha hamasa na mwamko chanya wa Watanzania kushiriki kwenye sekta hiyo muhimu.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amewataka maafisa wa Tume kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kulingana na mahitaji ya wadau waliopo katika maonesho mbalimbali nchini.

“Yapo madini yanayotumika kama mbolea, na pia zipo fursa nyingi za usambazaji wa bidhaa za kilimo kwenye migodi. Ni muhimu wananchi wakafahamu fursa hizi na kushiriki kikamilifu ili Sekta ya Madini iendelee kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na mchango wake katika Pato la Taifa uongezeke,” amesema Mhandisi Lwamo.

Tume ya Madini ni miongoni mwa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini zinazoshiriki kikamilifu katika Maonesho ya Nane Nane mwaka huu, ikiwa na lengo la kuelimisha umma kuhusu Sekta ya Madini, kuonesha mafanikio yaliyopatikana, pamoja na kuhamasisha uwekezaji zaidi katika sekta hiyo kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizindua Kiwanda cha Majaribio cha Kuchenjua Urani cha Mantra Tanzania Limited kilichopo katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, tarehe 30 Julai, 2025.















●Ajira 8,700 zatarajiwa; Tanzania yajiimarisha kuwa kinara wa rasilimali za nishati safi Afrika

Na Mwandishi Wetu, Ruvuma.

Ruvuma, Tanzania – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Kiwanda cha Majaribio cha Uchenjuaji wa Madini ya Urani kilichopo Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, mradi unaoendeshwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited. Uzinduzi huu ni hatua kubwa katika dira ya taifa kufikia maendeleo ya viwanda ifikapo mwaka 2050.

Akihutubia wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia alisema kuwa mradi huo unaonesha dhamira ya Serikali kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa, teknolojia na rasilimali za ndani. “Tunataka Watanzania waone manufaa ya moja kwa moja kutoka mradi huu. Ni wajibu wetu kuhakikisha ajira zinatolewa kwa wananchi, hasa kutoka maeneo yanayozunguka mradi, na kwamba mapato yake yanaimarisha huduma za kijamii,” alisema Rais Samia.

Mradi huo unakadiriwa kugharimu Dola za Kimarekani Bilioni 1.2 na kuzalisha ajira zaidi ya 8,700. Serikali inatarajia kunufaika na mapato yatokanayo na kodi, mirabaha na gawio kutokana na umiliki wake wa asilimia 20 ndani ya mradi huo.

Kwa mujibu wa Rais Samia, Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache barani Afrika yenye akiba kubwa ya madini ya urani, ikiwemo hifadhi ya zaidi ya tani 60,000 ya madini hayo katika eneo la Mto Mkuju pekee. Aidha, Serikali inaendelea kujifunza kutoka kwa nchi rafiki kama Namibia ambayo imekuwa ikichimba urani kwa muda mrefu ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unazingatia viwango vya kimataifa vya usalama wa afya na mazingira.

Katika hatua nyingine, Rais Samia aliitaka Kampuni ya Mantra kuzingatia wajibu wa kijamii na ushirikishwaji wa Watanzania katika kila hatua ya mradi huo, huku akiagiza Wizara na Taasisi husika kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uendelevu.