Articles by "HABARI ZA BIASHARA"
Showing posts with label HABARI ZA BIASHARA. Show all posts
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Upendo Wella (kushoto), na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania, Bi. Fatma Abdalla (kulia), wakipanda na kumwagilia mti katika Shule ya Msingi Usule, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, ikiwa ni sehemu ya shughuli za uwajibikaji kwa jamii zilizotekelezwa na Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania wakati wa hafla ya uzinduzi wa kituo chake cha 100 cha huduma za mafuta nchini, kilichozinduliwa mkoani Tabora tarehe 22 Julai 2026. Kama sehemu ya uzinduzi huo, Kampuni hiyo pia ilikabidhi madawati 100 kwa Shule ya Msingi Usule kwa lengo la kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati na kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora na salama ya kujifunzia, pamoja na kutoa magodoro 100 kwa Kituo cha Kulelea Watoto cha Istiqaama kwa ajili ya kuboresha mazingira ya maisha ya watoto wanaoishi katika kituo hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Upendo Wella (katikati), akikata utepe kuzindua rasmi kituo cha 100 cha huduma za mafuta ya rejareja cha Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania nchini, kilichopo eneo la Usule, Mkoa wa Tabora. Kituo hicho ni cha kwanza cha Kampuni hiyo mkoani Tabora na kitawawezesha wakazi wa Tabora na maeneo jirani kupata huduma za mafuta, vilainishi vya Puma, gesi ya kupikia ya PumaGas pamoja na fursa za kujipatia pointi kupitia mpango wa Puma Pris. Uzinduzi huo ni sehemu ya upanuzi wa mtandao wa huduma za mafuta wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania unaolenga kuimarisha upatikanaji wa nishati salama na ya uhakika nchini. Hafla hiyo iliyofanyika tarehe 22 Julai 2026 ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Meya wa Manispaa ya Tabora, Mheshimiwa Gulam Dewji (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania, Bi. Fatma Abdalla (wa pili kushoto), Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora, Bi. Asha Churu (wa pili kulia), pamoja na mmiliki wa kituo hicho, Bw. Kishimba Kibera (kulia).
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Upendo Wella (kushoto), akipokea dawati kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania, Bi. Fatma Abdalla (kulia), ikiwa ni sehemu ya madawati 100 yaliyotolewa na Kampuni hiyo kwa Shule ya Msingi Usule, iliyopo Kata ya Mbugani, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora. Msaada huo unaolenga kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati na kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora na salama ya kujifunzia ni sehemu ya shughuli za uwajibikaji kwa jamii zilizotekelezwa na Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania wakati wa uzinduzi wa kituo chake cha 100 cha huduma za mafuta nchini, kilichozinduliwa mkoani Tabora tarehe 22 Julai 2026.

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Nishati ya Puma Tanzania imezindua rasmi kituo chake cha 100 cha huduma za mafuta nchini, huku ikifungua kituo chake cha kwanza mkoani Tabora katika hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa nishati salama na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Kituo hicho kilichopo mjini Tabora kilizinduliwa Julai 22, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, akishirikiana na viongozi wa serikali, wawakilishi wa wananchi, wateja pamoja na menejimenti ya kampuni hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Tanzania, Fatma Abdalla, alisema kufikisha vituo 100 ni ishara ya imani ya kampuni katika uchumi wa Tanzania na dhamira yake ya kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya nishati.

Alisema uwekezaji huo utarahisisha upatikanaji wa mafuta ya uhakika, kuimarisha biashara, kuchochea shughuli za usafirishaji na kuongeza fursa za ajira, hususan katika mkoa wa Tabora ambao unaendelea kukua kwa shughuli za kilimo na biashara.

"Kuanzisha kituo chetu cha 100 si tu kupanua mtandao wa huduma, bali ni kuimarisha ushirikiano wetu wa muda mrefu na Tanzania. Tunaamini upatikanaji wa nishati ya uhakika unafungua fursa za maendeleo kwa wananchi na uchumi wa taifa," alisema Abdalla.

Mbali na uwekezaji huo, kampuni hiyo ilitekeleza shughuli mbalimbali za uwajibikaji kwa jamii (CSR), ikitoa magodoro 100 kwa Kituo cha Kulelea Watoto cha Istiqaama, madawati 100 kwa Shule ya Msingi Usule pamoja na kupanda miti 100 kwa kushirikiana na wananchi ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhifadhi mazingira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, aliipongeza Puma Tanzania kwa kuendelea kuwekeza nchini, akisema hatua hiyo itaongeza ajira, kuimarisha biashara za ndani na kuchangia maendeleo ya mkoa huo.

Alisema uwekezaji wa kampuni hiyo unaonesha imani ya wawekezaji katika mazingira ya biashara nchini na kuwataka wawekezaji wengine kutumia fursa zilizopo mkoani Tabora.

Puma Tanzania ni sehemu ya Kampuni ya Nishati ya Puma inayofanya shughuli zake katika zaidi ya nchi 34 duniani, ikitoa huduma za usambazaji wa mafuta, mafuta ya anga, vilainishi na lami kwa kuzingatia viwango vya usalama, ubora na maendeleo endelevu.

Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Tanzania Plc, Joseph Sayi (katikati) akizungumza wakati wa kutangaza udhamini wa Mashindano ya Golf ya Vodacom Corporate Masters 2026, yaliyoandaliwa kwa ushirikiano na Lugalo Golf Club kwa lengo la kuunganisha jumuiya ya wafanyabiashara nchini Tanzania, kuimarisha mahusiano ya kibiashara, kukuza ushirikiano na kuleta fursa zenye tija kwa wateja, washirika wa kibiashara na wadau muhimu nchini. Mashindano hayo yatakayofanyika tarehe 1 Agosti 2026 yanaendelea kuimarisha nafasi ya Vodacom kama mshirika wa kuaminika katika teknolojia na huduma za mawasiliano kwa taasisi na mashirika yanayoendelea kukua katika mazingira ya uchumi wa kidijitali. Uzinduzi huo umefanyika tarehe 16 Julai 2026 jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Katibu wa Corporate Masters, Maryanne Mugo (kushoto) pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Corporate Masters, Ken Mbaya (kulia).

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Vodacom Tanzania PLC imezindua rasmi mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 yatakayofanyika katika Uwanja wa Gofu wa Lugalo kuanzia Agosti 1, 2026, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kukuza ushirikiano na kufungua fursa mpya kwa wateja, washirika na wadau wa sekta mbalimbali.

Mashindano hayo, yanayoandaliwa kwa kushirikiana na Oakwood Holdings Limited kupitia kitengo cha Vodacom Business, yatawakutanisha viongozi wa makampuni, wafanyabiashara, wataalamu wa sekta mbalimbali na wapenzi wa mchezo wa gofu kwa lengo la kujenga mitandao ya biashara na kubadilishana uzoefu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Tanzania PLC, Joseph Sayi, alisema kampuni hiyo imeendelea kudhamini mashindano hayo kwa mwaka wa tatu mfululizo kwa kuwa yanaendana na dhamira ya kuimarisha mahusiano ya muda mrefu na jumuiya ya wafanyabiashara.

Alisema mashindano hayo si ya michezo pekee, bali ni jukwaa linalowakutanisha viongozi wa biashara, wabunifu na watoa maamuzi ili kujadili fursa mpya za uwekezaji na kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.

Sayi alisema katika kipindi chote cha mashindano hayo, Vodacom Business itaonesha suluhisho mbalimbali za kidijitali ikiwemo huduma za mawasiliano, usalama wa kidijitali na teknolojia za biashara zinazosaidia taasisi kuongeza ufanisi, kukuza biashara na kuimarisha ushindani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Corporate Masters, Ken Kariuki, alisema mashindano hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la makampuni kujitangaza, kujenga mitandao ya kibiashara na kuzalisha fursa mpya za biashara huku yakiimarisha ushiriki wa wateja.

Mashindano hayo yatashirikisha timu 10 za makampuni zitakazowania taji la Vodacom Corporate Masters 2026, sambamba na maonesho ya biashara, burudani, maonesho ya vitu vya kale na eneo maalumu la watoto, hatua inayolenga kuwafanya washiriki na familia zao kufurahia tukio hilo katika mazingira rafiki.

Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji, Vodacom Tanzania Plc, Joseph Sayi (kulia) na Mkuu wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani wa kampuni hiyo Happiness Shuma (kushoto), wakiwa wameshika tuzo zilizotolewa kwa Vodacom Tanzania kutambua mchango wake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (SABASABA). Maonesho hayo yaliyofanyika Juni 28 hadi Julai 13, 2026, yaliipa Vodacom Tanzania fursa ya kuonyesha namna teknolojia inavyobadilisha maisha, kuwezesha huduma za kidijitali na kuimarisha nafasi yake kama kinara wa huduma za mawasiliano nchini.
Meneja Masoko wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani wa Vodacom Tanzania Plc, Caleb Majo (kushoto), akitoa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Vodacom Tanzania wakati wa mahojiano maalumu na Azam Media katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (SABASABA). Maonesho hayo yaliyofanyika Juni 28 hadi Julai 13, 2026, yaliipa Vodacom Tanzania fursa ya kuonyesha namna teknolojia inavyobadilisha maisha, kuwezesha huduma za kidijitali na kuimarisha nafasi yake kama kinara wa huduma za mawasiliano nchini. Wengine ni Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania Plc, Alex Bitekeye (wa pili kushoto), Mkuu wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani wa Vodacom Tanzania Plc, Happiness Shuma (wa pili kulia), na Mtangazaji wa Azam Media, Jafar Mponda (kulia).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi (aliyekaa katikati), Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga (aliyekaa kushoto), na Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Latifa Khamis (aliyekaa kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa kampuni mbalimbali, akiwemo Mkuu wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani wa Vodacom Tanzania Plc, Happiness Shuma (aliyevaa tisheti nyekundu), muda mfupi baada ya kufungwa kwa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (SABASABA). Vodacom Tanzania Plc ilitambuliwa kama mshirika muhimu wa maonesho hayo baada ya kupewa tuzo mbili; Tuzo ya Nafasi ya Tatu kwa Mshindi wa Jumla wa Maonesho na Tuzo ya Nafasi ya Pili ya Udhamini, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika kufanikisha maonesho hayo.
Mkuu wa idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Tanzania Plc, Joseph Sayi (wa sita kulia), na Mkuu wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani wa kampuni hiyo Happiness Shuma (wa sita kushoto) wakiwa katika picha ya Pamoja na wafanyakazi wengine wa Vodacom wakiwa wa wameshika tuzo zilizotolewa kwa Vodacom Tanzania kutambua mchango wake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (SABASABA) muda mfupi baada ya kufungwa rasmi kwa maonesho hayo. Kwa siku zote 13 za maonesho hayo Vodacom Tanzania ilishiriki fursa ya kuonyesha namna teknolojia inavyobadilisha maisha, kuwezesha huduma za kidijitali na kuimarisha nafasi yake kama kinara wa huduma za mawasiliano nchini.

Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Kampuni ya Tanzania Breweries Public Limited Company (TBL) imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuunga mkono maendeleo ya jamii na uchumi wa ndani kupitia kampeni yake ya Cheers to Bars, inayotambua mchango mkubwa wa baa katika kuwaleta watu pamoja, kukuza biashara ndogo ndogo na kuimarisha shughuli za kiuchumi nchini.

TBL imesema kuwa baa zimekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku ya Watanzania, zikitoa nafasi kwa marafiki na majirani kukutana, mashabiki wa soka kushuhudia mechi pamoja na wafanyabiashara wadogo kuendesha shughuli zao. Kampeni hiyo inalenga kuzisherehekea baa kwa mchango wake katika kujenga mshikamano wa kijamii na kuchochea maendeleo ya uchumi.

Mbali na kuwa sehemu za burudani, TBL imeeleza kuwa baa zimeendelea kutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania, wakiwemo wamiliki wa baa, wahudumu, wauzaji wa chakula, wasambazaji wa bidhaa, walinzi, wasafishaji pamoja na watoa huduma za usafiri, hali inayochangia kuongeza kipato kwa watu wengi na kuimarisha mzunguko wa fedha katika jamii.

Kampeni ya Cheers to Bars pia imeangazia nafasi ya baa wakati wa matukio makubwa ya michezo, hususan soka, ambapo mashabiki wengi hupendelea kutazama mechi kwa pamoja katika mazingira yanayowapa fursa ya kushirikiana, kushangilia na kujenga kumbukumbu za pamoja.

Hali hiyo ilijidhihirisha katika Baa ya Kitambaa Cheupe jijini Dar es Salaam, ambapo mashabiki walikusanyika kushuhudia mechi ya robo fainali kati ya Hispania na Ubelgiji. Mechi hiyo iligeuka kuwa zaidi ya mchezo wa soka, huku ikiunganisha watu wa kada mbalimbali walioshiriki kushangilia na kufurahia burudani kwa pamoja.
Akizungumza kuhusu kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Sheria na Masuala ya Ushirika wa TBL, Neema Temba, alisema Cheers to Bars si kampeni inayolenga soka pekee, bali ni jukwaa la kutambua mchango wa baa na watu wanaoziendesha katika maendeleo ya jamii na uchumi wa Tanzania.

"Baa ni sehemu muhimu ya maisha ya kijamii na kiuchumi ya Watanzania. Zinasaidia kujenga maisha ya watu, zinatoa fursa kwa biashara ndogo ndogo na zinatoa nafasi kwa jamii kukutana na kuimarisha mahusiano. Kupitia Cheers to Bars, tunazisherehekea baa hizi pamoja na watu wanaoziendesha, huku tukiwahamasisha watumiaji kufurahia vinywaji kwa kuwajibika," alisema Neema.
Aliongeza kuwa wakati wa mechi kubwa za soka, shughuli za biashara huongezeka kwa kiasi kikubwa katika baa na maeneo yanayozizunguka. Wauzaji wa chakula, wasambazaji wa bidhaa, madereva wa usafiri na watoa huduma wengine wote hunufaika kutokana na ongezeko la wateja, jambo linaloifanya sekta ya ukarimu kuwa kichocheo muhimu cha uchumi wa ndani.

Kwa mujibu wa TBL, mafanikio ya kampeni hiyo yanaonesha kuwa baa za kienyeji zimeendelea kuwa sehemu muhimu zinazochangia maendeleo ya jamii kwa kuunganisha watu kupitia michezo na burudani, huku zikitoa fursa za ajira na biashara kwa makundi mbalimbali.

Kampuni hiyo imewataka Watanzania kuendelea kuunga mkono baa za kienyeji na kushiriki burudani katika mazingira salama kwa kutumia vinywaji kwa uwajibikaji. TBL imeeleza kuwa itaendelea kutekeleza kampeni ya Cheers to Bars kama sehemu ya juhudi zake za kuthamini mchango wa baa katika ukuaji wa uchumi, maendeleo ya jamii na ustawi wa sekta ya ukarimu nchini.

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akikabidhi Tuzo ya Rais ya Walipakodi Bora katika Sekta ya Uzalishaji kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Breweries Public Limited Company (TBL), Michelle Kilpin wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Mlimani City, Dar es Salaam, Jumatano tarehe 1 Julai 2026.

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam, Tanzania – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipatia Tanzania Breweries Public Limited Company (TBL) Tuzo ya Rais ya Walipakodi Bora katika Sekta ya Uzalishaji (Manufacturing), ikiwa ni kutambua mchango wa kampuni hiyo katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia ulipaji sahihi wa kodi, uzalishaji wa ndani, uwekezaji na uundaji wa ajira.

Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Mlimani City, Dar es Salaam, Jumatano tarehe 1 Julai 2026.

Uamuzi wa Mheshimiwa Rais kuongoza binafsi utoaji wa tuzo hizo kwa mwaka wa pili mfululizo unaonesha umuhimu ambao Serikali inaweka katika kuhimiza ulipaji wa kodi na kutambua mchango wa sekta binafsi katika kufanikisha maendeleo ya nchi.

Kwa TBL, tuzo hii ni uthibitisho wa mchango mpana wa kampuni katika maendeleo ya Tanzania. Mbali na kulipa kodi kwa wakati na kwa usahihi, kampuni inaendelea kuchangia maendeleo kupitia ajira inazozalisha, ushirikiano wake na wakulima, wasambazaji, wafanyabiashara pamoja na jamii mbalimbali zinazozunguka shughuli zake.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Breweries Public Limited Company, Michelle Kilpin, alisema kuwa tuzo hiyo ni ishara ya dhamira ya kampuni ya kuendesha biashara kwa uwajibikaji na kuchangia maendeleo ya Taifa.

"Tunajivunia kupokea heshima hii kutoka kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kulipa kodi kikamilifu na kwa wakati ni wajibu wetu kama kampuni ya Kitanzania na sehemu ya mchango wetu katika maendeleo ya nchi. Tuzo hii ni ya wafanyakazi wetu, wakulima, wasambazaji, wauzaji, washirika wetu wa biashara na wadau wote katika mnyororo wetu wa thamani. Tutaendelea kuwekeza nchini na kuwa mshirika wa kuaminika katika safari ya maendeleo ya Tanzania," alisema Kilpin.

Kupitia shughuli zake za uzalishaji wa ndani, TBL inaendelea kuzalisha manufaa yanayovuka mipaka ya viwanda vyake kwa kusaidia wakulima, wasafirishaji, wasambazaji, wafanyabiashara wadogo na wa kati pamoja na wadau wengine wa biashara nchini. Aidha, kupitia ununuzi wa mazao ya ndani kama shayiri (barley) na mtama (sorghum), kampuni inachochea maendeleo ya sekta ya kilimo, kuongeza kipato cha wakulima na kuhakikisha thamani kubwa zaidi ya uchumi inabaki nchini.

Mbali na mchango wake wa kiuchumi, TBL inaendelea kuwekeza katika miradi ya uendelevu ikiwemo usimamizi wa rasilimali za maji, kuwawezesha wakulima, ununuzi wenye uwajibikaji, matumizi ya mifumo ya ufungashaji unaorejelezwa pamoja na programu za urejelezaji wa taka, hatua zinazolenga kuhifadhi mazingira na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali zinazoiwezesha kampuni kuendesha shughuli zake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria na Masuala ya Kampuni wa TBL, Neema Temba, alisema kuwa biashara yenye uwajibikaji hupimwa kwa kuzingatia utekelezaji wa sheria pamoja na athari chanya inayozalisha kwa jamii.

"Heshima hii inaakisi msingi wa maadili unaotuongoza kila siku. Tunaamini katika kufanya biashara kwa uwazi, kutimiza wajibu wetu wa kisheria na kushirikiana na Taifa ambalo limekuwa makazi ya biashara yetu kwa miongo mingi. Kampuni zinapolipa kodi stahiki, kuwekeza katika maeneo zinayofanyia kazi na kulinda rasilimali zinazowezesha shughuli zao, nchi nzima hunufaika na kusonga mbele," alisema Temba.

Tuzo hii inaongeza orodha ya mafanikio ambayo TBL imeendelea kuyapata katika maeneo ya ulipaji wa kodi, uendelevu wa biashara na uwajibikaji wa kampuni kwa jamii.

Kadiri Tanzania inavyoendelea kutekeleza agenda ya ukuaji wa viwanda na mageuzi ya uchumi, TBL imesisitiza kuwa itaendelea kuwekeza nchini, kushirikiana na jamii pamoja na kuunda thamani ya kudumu kupitia biashara inayozingatia uwajibikaji.

●Yatwaa tuzo mbili ikiwemo mshindi wa tatu wa jumla
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Chapo wakipokea maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania PLC, Philip Besiimire, kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (SABASABA) walipotembelea banda la Vodacom muda mfupi kabla ya ufunguzi rasmi wa maonesho hayo. Maonesho hayo yamefunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Chapo Julai 3, 2026, katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam ambapo Vodacom Tanzania ilitunukiwa tuzo mbili, ikiwemo Tuzo ya Nafasi ya Tatu kwa Mshindi wa Jumla wa Maonesho yote na Tuzo ya Nafasi ya Pili ya Udhamini, ikiwa ni utambuzi wa mchango wake mkubwa kama mshirika muhimu wa Maonesho hayo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Chapo (kushoto) wakipata maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania PLC, Philip Besiimire (kulia), kuhusu huduma ya simu mpya ya smati kitachi inayouzwa na kampuni hiyo ili kuwawezesha Watanzania kuingia katika ulimwengu wa kidijitali wakati Marais hao walipotembelea banda la Vodacom muda mfupi kabla ya ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (SABASABA). Katika hafla hiyo, Vodacom Tanzania ilitunukiwa tuzo mbili ikiwemo Tuzo ya Nafasi ya Tatu katika Kundi la Washindi wa Jumla wa Maonesho hayo na Tuzo ya Nafasi ya Pili ya Udhamini, ikiwa ni kutambua mchango mkubwa kama mshirika muhimu wa Maonesho hayo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitazama huduma mbalimbali zilizokuwepo ndani ya banda la Vodacom, wakati wa kutembelea banda hilo muda mfupi kabla ya ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (SABASABA), baada ya kupata maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania PLC, Philip Besiimire, kuhusu huduma zinazotolewa na kampuni hiyo. Rais Samia aliambatana na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Chapo, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho hayo. Katika hafla hiyo, Vodacom Tanzania ilitunukiwa tuzo mbili ikiwemo Tuzo ya Nafasi ya Tatu katika Kundi la Washindi wa Jumla wa Maonesho hayo na Tuzo ya Nafasi ya Pili ya Udhamini, ikiwa ni kutambua mchango mkubwa kama mshirika muhimu wa Maonesho hayo. Tukio hilo lilifanyika Julai 3, 2026, katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam
Wafanyakazi wa Vodacom Tanzania PLC wakiwa katika picha ya pamoja kwenye banda la kampuni hiyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (SABASABA), wakifurahia ushindi baada ya kampuni yao kutunukiwa tuzo mbili: Tuzo ya Nafasi ya Tatu kwa Mshindi wa Jumla wa Maonesho yote na Tuzo ya Nafasi ya Pili ya Udhamini, ikiwa ni utambuzi wa mchango wake mkubwa kama mshirika muhimu wa Maonesho hayo. Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi Julai 3, 2026, na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Chapo, ambaye kabla ya hafla ya ufunguzi aliambatana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutembelea banda la Vodacom na kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo.

Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Tanzania Breweries PLC (TBL) imeendelea kuonyesha uimara wa biashara yake baada ya wanahisa kupitisha Ripoti ya Wakurugenzi, Ripoti ya Wakaguzi wa Hesabu na taarifa za fedha zilizokaguliwa za mwaka ulioishia Desemba 31, 2025, huku kampuni ikirekodi ongezeko la mapato na faida kutokana na ukuaji wa mauzo na uwekezaji wa kimkakati.

Maamuzi hayo yalifikiwa katika Mkutano Mkuu wa 53 wa Wanahisa uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, ambapo wanahisa walithibitisha pia mgao wa muda (interim dividend) uliolipwa kwa mwaka huo na kuidhinisha kampuni ya PricewaterhouseCoopers kuwa wakaguzi wa hesabu wa nje kwa mwaka wa fedha 2026.
Taarifa ya kampuni inaonyesha kuwa mwaka 2025 ulikuwa wa mafanikio makubwa, huku mapato yakiongezeka kwa asilimia 13 na faida ya uendeshaji kupanda kwa asilimia 35. Ukuaji huo umechangiwa na kuongezeka kwa mahitaji ya bia na vileo vikali, usimamizi madhubuti wa gharama, uwekezaji katika chapa mbalimbali pamoja na maboresho ya mfumo wa usambazaji wa bidhaa nchini.

Mwenyekiti wa Muda wa Bodi ya Wakurugenzi wa TBL, Balozi Ami R. Mpungwe, alisema Mkutano Mkuu wa Wanahisa umeendelea kuwa jukwaa muhimu la uwazi na uwajibikaji, huku ukitoa fursa kwa wanahisa kujadili utendaji wa kampuni na mwelekeo wake wa baadaye. Alisema Bodi itaendelea kusimamia kampuni kwa kuzingatia misingi ya utawala bora ili kulinda maslahi ya wanahisa na kuhakikisha ukuaji endelevu wa biashara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle N. Kilpin, alisema mafanikio ya mwaka 2025 yametokana na nguvu ya chapa za kampuni, imani ya wateja, ushirikiano wa wadau na utekelezaji makini wa mikakati ya biashara. Alibainisha kuwa kampuni itaendelea kuwekeza katika mifumo ya kidijitali, kuongeza matumizi ya malighafi zinazozalishwa nchini na kuboresha ufanisi wa shughuli zake ili kuimarisha ushindani sokoni na kuongeza thamani kwa wanahisa.

Mbali na matokeo ya kifedha, TBL iliendelea kuimarisha mchango wake katika uchumi wa ndani kupitia Kiwanda cha Kimea cha Kilimanjaro ambacho sasa kina uwezo wa kuzalisha tani 8,000 za kimea kwa mwaka, hatua inayoongeza matumizi ya shayiri inayolimwa na wakulima wa Tanzania. Kampuni pia imeendelea kupanua mfumo wa kidijitali wa kuagiza bidhaa, kuimarisha ushirikiano na wafanyabiashara wa rejareja na kuwawezesha wakulima wa shayiri na mtama kupitia mnyororo wa thamani.

Katika eneo la uendelevu, TBL ilieleza kuwa asilimia 92 ya vifungashio vyake sasa vinaweza kurejeshwa au kutengenezwa kwa malighafi zilizorejelewa, huku matumizi ya maji yakiendelea kuboreshwa katika shughuli za uzalishaji. Kampuni pia imeendelea kuhamasisha matumizi yenye uwajibikaji ya bidhaa zake na kutekeleza programu mbalimbali za maendeleo ya jamii na biashara, ikisisitiza dhamira yake ya kujenga thamani ya muda mrefu kwa wanahisa, wateja, wakulima na uchumi wa Tanzania kwa ujumla.
Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam. Kampuni ya Puma Energy Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake katika sekta ya nishati baada ya kutunukiwa Tuzo ya Rais ya Mlipa Kodi Bora katika kipengele cha Muagizaji Bora wa Mizigo ya Vimiminika (Best Wet Cargo Importer) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa hafla ya Tuzo za Rais kwa Walipa Kodi Bora iliyofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alimkabidhi tuzo hiyo mwakilishi wa kampuni kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hafla hiyo iliwakutanisha walipa kodi bora kutoka mikoa yote 35 ya Tanzania kwa lengo la kuhamasisha ulipaji wa kodi na kutambua mchango wao katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, alisema mafanikio hayo yanadhihirisha misingi imara ya uwajibikaji, uadilifu na uzingatiaji wa sheria ambayo imeendelea kuiongoza kampuni katika shughuli zake nchini. Alisema tuzo hiyo ni motisha wa kuendelea kuendesha biashara kwa uwazi, kulipa kodi kwa wakati na kushirikiana na Serikali katika kukuza uchumi wa taifa.
Fatma alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kampuni imechangia zaidi ya shilingi trilioni 1.4 kupitia kodi na tozo mbalimbali kwa Serikali, hatua iliyoifanya kutambuliwa mara kadhaa na TRA kwa utii wa sheria za kodi na mchango wake mkubwa katika kuongeza mapato ya ndani. Aliongeza kuwa kampuni itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya nishati na kupanua huduma zake ili kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali za uzalishaji.

Mbali na ulipaji wa kodi, Puma Energy Tanzania imeendelea kuimarisha uwekezaji wake kwa kuendesha zaidi ya vituo 100 vya huduma za mafuta, maghala ya kuhifadhi mafuta na usambazaji wa mafuta ya ndege katika viwanja vinane vya ndege, ikiwemo viwanja vyote vya kimataifa nchini. Kampuni pia inaongoza matumizi ya nishati safi kupitia Kituo Kikuu cha Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG Mother Station) pamoja na mtandao unaokua wa vituo vya CNG jijini Dar es Salaam na Morogoro.

Aidha, kampuni inaendelea kupanua huduma za gesi ya kupikia kupitia Puma Gas, biashara ya vilainishi na maduka ya Shop Express, huku ikiendelea kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji, ajira na huduma za nishati zenye ubora. Tuzo hiyo imeongeza hadhi ya Puma Energy Tanzania kama mmoja wa walipa kodi wakubwa na washirika muhimu wa Serikali katika kufanikisha ajenda ya maendeleo ya Taifa.

Na Mwandishi Wetu

IRINGA – Mbunge wa Jimbo la Ismani, Mhe. Emmanuela Mtatifikolo, amezindua rasmi maonesho na sherehe za Sabasaba zinazofanyika katika Kata ya Ilolo Mpya, Tarafa ya Pawaga, wilayani Ismani, huku akiwataka wananchi kutumia maonesho hayo kujifunza, kufanya biashara na kuimarisha mshikamano wa kijamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Mtatifikolo alisema maonesho ya Sabasaba ni fursa muhimu kwa wananchi kukutana, kubadilishana uzoefu, kuuza na kununua bidhaa mbalimbali pamoja na kujifunza fursa za maendeleo kutoka kwa washiriki na wageni wanaotoka maeneo mbalimbali nchini.


Aliwahamasisha wananchi wa Kata ya Ilolo Mpya na Jimbo la Ismani kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika shughuli hizo, akieleza kuwa mbali na burudani, maonesho hayo yana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wananchi na kuimarisha mahusiano ya kijamii.

"Mnatakiwa kutumia maonesho haya kama jukwaa la kujifunza, kufanya biashara na kujenga mahusiano yatakayochochea maendeleo ya Ismani na wananchi wake," alisema Mtatifikolo.

Mbunge huyo pia aliwataka vijana kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira ya amani.



Aidha, aliwahimiza wazazi na walezi kuendelea kuwalea watoto katika misingi ya maadili, uzalendo na uwajibikaji ili kujenga kizazi kitakachochangia maendeleo ya taifa.

"Malezi bora ndiyo msingi wa kujenga taifa lenye vijana wenye nidhamu, uzalendo na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi," alisisitiza.

Maonesho hayo ya Sabasaba yanajumuisha shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, zikiwemo maonesho ya bidhaa, michezo ya mpira wa miguu, ngoma za asili pamoja na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali.



Waandaaji wa maonesho hayo wamesema lengo ni kutoa fursa kwa wananchi kuonesha bidhaa na huduma zao, kuhamasisha biashara ndogondogo na kukuza vipaji vya vijana kupitia michezo na sanaa.

Sherehe hizo hufanyika kila mwaka baada ya wananchi kumaliza shughuli za uvunaji, zikiwa sehemu ya kuimarisha mshikamano wa jamii, kuchochea biashara na kutoa burudani kwa wakazi wa Ismani na maeneo jirani.

Wananchi waliohudhuria uzinduzi huo walieleza kufurahishwa na maandalizi ya maonesho hayo, wakisema yameendelea kuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Jimbo la Ismani.