Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizindua Kiwanda cha Majaribio cha Kuchenjua Urani cha Mantra Tanzania Limited kilichopo katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, tarehe 30 Julai, 2025.●Ajira 8,700 zatarajiwa; Tanzania yajiimarisha kuwa kinara wa rasilimali za nishati safi Afrika
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma.
Ruvuma, Tanzania – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Kiwanda cha Majaribio cha Uchenjuaji wa Madini ya Urani kilichopo Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, mradi unaoendeshwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited. Uzinduzi huu ni hatua kubwa katika dira ya taifa kufikia maendeleo ya viwanda ifikapo mwaka 2050.
Akihutubia wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia alisema kuwa mradi huo unaonesha dhamira ya Serikali kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa, teknolojia na rasilimali za ndani. “Tunataka Watanzania waone manufaa ya moja kwa moja kutoka mradi huu. Ni wajibu wetu kuhakikisha ajira zinatolewa kwa wananchi, hasa kutoka maeneo yanayozunguka mradi, na kwamba mapato yake yanaimarisha huduma za kijamii,” alisema Rais Samia.
Mradi huo unakadiriwa kugharimu Dola za Kimarekani Bilioni 1.2 na kuzalisha ajira zaidi ya 8,700. Serikali inatarajia kunufaika na mapato yatokanayo na kodi, mirabaha na gawio kutokana na umiliki wake wa asilimia 20 ndani ya mradi huo.
Kwa mujibu wa Rais Samia, Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache barani Afrika yenye akiba kubwa ya madini ya urani, ikiwemo hifadhi ya zaidi ya tani 60,000 ya madini hayo katika eneo la Mto Mkuju pekee. Aidha, Serikali inaendelea kujifunza kutoka kwa nchi rafiki kama Namibia ambayo imekuwa ikichimba urani kwa muda mrefu ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unazingatia viwango vya kimataifa vya usalama wa afya na mazingira.
Katika hatua nyingine, Rais Samia aliitaka Kampuni ya Mantra kuzingatia wajibu wa kijamii na ushirikishwaji wa Watanzania katika kila hatua ya mradi huo, huku akiagiza Wizara na Taasisi husika kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uendelevu.








.jpeg)




.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments: