Vatican.
Misa ya mazishi ya Askofu Mkuu Novatus Rugambwa imefanyika Septemba 25 katika Basilika ya Mtakatifu Petro, ikiendeshwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican. Katika hotuba yake, Kardinali Parolin alimsifu marehemu kwa maisha ya uchaji, unyenyekevu na uadilifu aliouonyesha katika safari yake ndefu ya kuhudumu katika diplomasia ya Vatican.
Kardinali Parolin alikumbusha safari ya maisha ya Askofu Rugambwa, aliezaliwa Bukoba, Tanzania, tarehe 1 Oktoba 1957, na kupewa daraja la upadre mwaka 1986. Kuanzia mwaka 1991, aliutumikia muda mrefu utumishi wa diplomasia ya Vatican, akiacha alama kubwa ya upendo na imani.
Katika hotuba yake, Kardinali alisisitiza ushuhuda wa marehemu wakati wa ugonjwa alioupitia, akisema kuwa aliukabili kwa imani na moyo wa upendo, na hivyo kugeuza mateso yake kuwa fursa ya kumtegemea Mungu na kuimarisha imani ya watu wa Mungu waliomzunguka.
Mfano wa upendo na uaminifu wa kidiplomasia
Kardinali Parolin alieleza kuwa Askofu Rugambwa alitoa mfano bora wa utumishi katika diplomasia ya Kanisa, ambayo aliiita “njia ngumu ya kichungaji inayodai uaminifu wa Injili na heshima ya watu wa mataifa mbalimbali.” Alisema marehemu alitenda kwa uchaji, busara na uthabiti katika kutetea haki na heshima ya binadamu, mambo ambayo ni nguzo ya amani ya kweli.
Kwa mujibu wa Kardinali, Askofu Rugambwa aliweza kutengeneza uhusiano thabiti na wa kujenga, akiwa na moyo wa kichungaji uliojaa subira na upendo wa kibaba.
Mshuhuda wa kweli wa maisha matakatifu
Aidha, Kardinali Parolin aliongeza kuwa sifa nyingine kubwa ya marehemu ilikuwa ni “uadilifu wa maisha” uliomfanya kuwa shahidi wa kweli na anayeaminika wa ukweli aliohubiri. Akinukuu maneno ya Mtakatifu Paulo VI, alisema: “Binadamu wa leo husikiliza zaidi mashahidi kuliko walimu.”
Alisisitiza kuwa mfano bora wa maisha matakatifu ni silaha muhimu zaidi kwa wachungaji wa Kanisa, hasa wale wanaotumikia kama mabalozi wa Papa.
Urithi wa upendo na unyenyekevu
Kardinali pia aligusia huruma na mshikamano wa marehemu na maskini, akisema ulikuwa ni “mzizi wa maisha yake ya kikristo na njia ya pekee ya kukutana na Mungu.”
Alihitimisha mahubiri yake kwa maneno ya Mtakatifu Leo Mkuu, akisema kwamba wale wanaokaa katika upendo na umoja wa Roho hawatashindwa na vikwazo vyovyote, bali baada ya mapambano ya maisha ya duniani, watapata pumziko la amani ya Mungu.
Kardinali Parolin aliomba neema hiyo itimizwe kwa Askofu Rugambwa, na pia kwa waamini wote, ili kwa unyenyekevu na mshikamano, wawe vyombo vya wokovu kwa kila mmoja, hadi watakapokutana tena nyumbani mwa Baba wa mbinguni.



Toa Maoni Yako:
0 comments: