Articles by "TANZIA"
Showing posts with label TANZIA. Show all posts
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Tasnia ya burudani nchini imegubikwa na majonzi makubwa baada ya msanii na mshereheshaji mashuhuri, Emmanuel Mathias ‘MC Pilipili’, kufariki dunia ghafla leo mchana wakati akiwa safarini kuelekea jijini Dodoma kwa ajili ya shughuli za kazi.

Taarifa za kifo chake zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii majira ya saa moja jioni kupitia ujumbe kutoka kwa baadhi ya watu wake wa karibu, zikizua wasiwasi na maswali mengi kutoka kwa mashabiki na wadau wa sanaa.

Akithibitisha msiba huo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya General jijini Dodoma, Dkt. Ernest Ibenzi, amesema MC Pilipili alifikishwa hospitalini hapo tayari akiwa ameshafariki dunia.

“Ni kweli tumempokea akiwa tayari amefariki,” alisema kwa kifupi Dkt. Ibenzi, akibainisha kuwa taratibu za kitabibu zinaendelea.

MC Pilipili alikuwa mmoja wa vipaji vilivyochangamsha sanaa ya uchekeshaji na ushereheshaji nchini, na kifo chake kimeacha pengo kubwa kwa mashabiki na wenzake katika tasnia.

Familia yake inatarajia kutoa taarifa zaidi kuhusu mipango ya mazishi na hatua nyingine za maombolezo.

 

Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ametoa wito kwa Wakenya kuendeleza misingi ya haki, uhuru na demokrasia aliyoisimamia marehemu Raila Odinga, akisisitiza kuwa mapambano hayo hayawezi kurudi nyuma.

Akizungumza katika shughuli ya kuuaga mwili wa Odinga kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Uhuru alisema, “Hatutakubali kama Wakenya haki za binadamu, demokrasia na mambo yote ambayo Raila alitetea yarudi nyuma. Tutasonga mbele tukiyalinda kwa ajili yetu na vizazi vijavyo.”

Uhuru pia alikumbushia uhusiano wake wa karibu na Raila, akimtaja kama kiongozi shupavu aliyepigania haki za wananchi bila woga.

Mazishi ya Raila Odinga yanatarajiwa kufanyika Jumapili, Oktoba 19, 2025, nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya, magharibi mwa Kenya.

Na Mwandishi Wetu, Nairobi

Mwili wa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Mhe. Raila Amollo Odinga, umelazwa leo katika Jumba la Bunge, ikiwa ni heshima ya kitaifa kwa kiongozi huyo ambaye kwa zaidi ya miongo mitano aliweka alama kubwa katika historia ya siasa na demokrasia nchini. Hatua hiyo inalenga kutoa nafasi kwa mihimili yote mitatu ya dola — Serikali Kuu, Bunge na Mahakama — pamoja na wananchi kwa ujumla, kutoa heshima zao za mwisho kwa mzalendo huyo.

Kwa miaka 20, Raila aliwatumikia wananchi wa Jimbo la Lang’ata kama Mbunge, akijulikana kwa msimamo wake thabiti katika kutetea haki, demokrasia na maendeleo. Aidha, mchango wake mkubwa ulionekana wakati wa uongozi wake kama Waziri Mkuu, ambapo alihusishwa moja kwa moja na mageuzi makubwa ya kisheria na kisiasa, hususan kupitishwa kwa Katiba ya mwaka 2010.

SSerikali imesema kuwa kumlaza Raila bungeni ni ishara ya heshima na shukrani kwa mchango wake mkubwa kwa taifa. “Ni heshima stahiki kwa kiongozi ambaye maisha yake yote yalijikita katika kutafuta demokrasia, usawa na mshikamano wa kitaifa,” ilisomeka sehemu ya taarifa rasmi.

Wananchi wanatarajiwa kupewa fursa ya kuuaga mwili wake baada ya viongozi wa kitaifa, huku maandalizi yakiendelea kuelekea mazishi ya kitaifa yatakayofanyika nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya Prof. Kithure Kindiki, wakati alipowasili Uwanja wa Nyayo Jijini Nairobi kushiriki Mazishi ya Kitaifa ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya, Raila Amolo Odinga, leo tarehe 17 Oktoba 2025.












Na Mwandishi Wetu, Nairobi

Kenya leo imeungana kama taifa kushiriki ibada kuu ya kitaifa ya kumbukumbu kwa heshima ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Mhe. Raila Amolo Odinga, aliyeaga dunia akiwa na miaka 80. Ibada hiyo imefanyika kwa majonzi na mshikamano wa kitaifa, ambapo viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini, wageni mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na maelfu ya wananchi walijitokeza kuenzi maisha ya kiongozi huyo wa kipekee.

Katika hotuba zilizotolewa, Raila Odinga ametajwa kama mwanasiasa shupavu na mzalendo aliyeishi maisha ya ujasiri, amani na imani thabiti kwa taifa lake. Walisema urithi wake hautafutika, kwani maisha yake yaliandikwa kwa mfano wa kujitoa katika haki, demokrasia, mshikamano na maendeleo ya taifa.

"Patriotism, he showed us, is not about what the country gives to us, but about what we are willing to sacrifice and give for the betterment of our nation," ulisomeka ujumbe wa pamoja wa viongozi wa kitaifa.

Zaidi ya hayo, Raila ametajwa kama kiongozi mnyenyekevu, mwenye uvumilivu na imani thabiti katika mustakabali wa Kenya, ambaye hakuchoka kusimamia mabadiliko ya kikatiba na kidemokrasia yaliyoiweka Kenya katika ramani ya dunia kama taifa linaloenzi haki na mshikamano.

Ibada hiyo imetajwa kama tukio la kihistoria, sio tu kwa Kenya bali kwa Afrika nzima, kutokana na nafasi kubwa aliyokuwa nayo Raila katika harakati za ukombozi wa kisiasa na umoja wa bara.