Iringa, Septemba 30, 2025: Kanisa Katoliki Jimbo la Mafinga limeweka wazi sintofahamu kuhusu Padre Jordan Kibiki, aliyeripotiwa kujiteka wiki iliyopita, na kufafanua kuwa tukio hilo lilitokana na changamoto ya afya ya akili, hususan msongo wa mawazo.Kwa mujibu wa taarifa ya Kanisa hilo, Jeshi la Polisi limefuta tuhuma dhidi ya Padre Kibiki na kumwachia huru baada ya uchunguzi kuthibitisha ukweli huo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Askofu wa Jimbo la Mafinga, Mhashamu Vicent Mwagala, alisema Padre Kibiki ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Afya Nyololo na Paroko Msaidizi wa Parokia hiyo, alitarajiwa Septemba 18, 2025 kuhudhuria kikao cha afya katika ofisi za Halmashauri ya Mufindi, lakini hakuwasili licha ya kuondoka nyumbani asubuhi.
Askofu Mwagala alieleza kuwa gari lake lilipatikana limeegeshwa barabarani bila dereva na juhudi za kumpata ziligonga mwamba, hali iliyosababisha hofu kubwa miongoni mwa waumini na viongozi wenzake.
Kwa mujibu wa maelezo ya Polisi, Padre Kibiki alikiri kujitenga kutokana na msongo wa mawazo uliosababishwa na shinikizo la kifedha baada ya kupoteza fedha alizokuwa amekopa kwenye biashara ya mtandao (online scam).
“Baada ya uchunguzi wa kitabibu, madaktari walithibitisha kuwa Padre Kibiki alikuwa anakabiliwa na depression. Kwa ushauri wa wataalamu, amepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Tosamaganga kwa uangalizi wa karibu na matibabu ya afya ya akili,” alisema Askofu Mwagala.
Aliongeza kuwa Jimbo la Mafinga linaendelea kufuatilia afya ya Padre Kibiki ili aweze kurejea katika hali ya kawaida na kuendelea na majukumu yake ya kiroho.
“Tunawaomba waumini na jamii kwa ujumla waendelee kumwombea Padre Jordan ili apone haraka,” alisema, huku akilishukuru Jeshi la Polisi na vyombo vya habari kwa ushirikiano katika kipindi hicho kigumu.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO, 2023), msongo wa mawazo ni moja ya changamoto kubwa za kiafya duniani, na unaweza kumpata mtu yeyote bila kujali nafasi, kazi au wito wake wa kidini.


Toa Maoni Yako:
0 comments: