Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania Plc, Philip Besiimire, akipeana mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Heart Team Africa Foundation (HTAF), Dkt. Naizihijwa Majani, mara baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano wa kuchangia asilimia 30 ya gharama za matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo, huku serikali ikigharamia asilimia 70. Hafla hiyo, iliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 29 Septemba 2025 sambamba na Maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani chini ya kaulimbiu “Don’t Miss a Beat”, ilishuhudiwa na Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge.Mange Mwandishi Wetu.
Dar es Salaam, 29 Septemba 2025: Vodacom Tanzania Foundation imeingia makubaliano ya ushirikiano na Heart Team Africa Foundation, asasi inayofanya kazi chini ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), katika hatua ya kuongeza nguvu kwenye mapambano dhidi ya magonjwa ya moyo kwa watoto nchini. Hafla ya utiaji saini imefanyika sambamba na maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani 2025, chini ya kaulimbiu “Don’t Miss a Beat.”
Kwa mujibu wa utafiti wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, watoto 2 kati ya 100 huzaliwa na ugonjwa wa moyo wa kuzaliwa nao (Congenital Heart Disease – CHD), huku asilimia 3 ya watoto wenye umri kati ya miaka 5–15 wakiathiriwa na ugonjwa wa moyo wa Rheumatic (RHD) unaoweza kuzuilika kwa matibabu mapema ya maambukizi ya koo.
Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watoto 4,000 huhitaji upasuaji wa moyo kila mwaka, lakini huduma hizo bado hazipatikani kwa urahisi. Ingawa serikali inagharamia asilimia 70 ya matibabu, asilimia 30 iliyosalia ni mzigo mkubwa kwa familia nyingi, huku watoto zaidi ya 350 wakiwa kwenye foleni ya kusubiri upasuaji katika JKCI.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Dkt. Peter Kisenge, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, alisema:
"Kila takwimu inawakilisha mtoto mwenye ndoto na mzazi mwenye matumaini. Ushirikiano huu utapunguza pengo kati ya uhitaji na upatikanaji wa huduma, ili watoto wengi zaidi wapate nafasi ya kuishi maisha yenye afya njema."
Naye Dkt. Naizihijwa Majani, Mkurugenzi Mtendaji wa Heart Team Africa Foundation, alibainisha kuwa gharama za matibabu zimekuwa kikwazo kikubwa:
"Ushirikiano huu sio tu msaada wa kifedha, bali ni njia ya kuokoa maisha. Tunataka kila mzazi awe na hakika kwamba mtoto wake atapata huduma bila kuchagua kati ya umasikini na mustakabali wa mtoto wake."
Mapema mwaka huu, Vodacom Foundation ilizindua Amini Initiative huko Zanzibar, ikiahidi kugharamia asilimia 30 ya gharama zinazobaki za watoto 150 wanaohitaji upasuaji. Mpaka sasa watoto 38, wenye umri wa kati ya miezi miwili na miaka 14, wamefanyiwa upasuaji kwa mafanikio.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya kutafsiri imani kuwa vitendo:
"Makubaliano haya ni ishara thabiti ya kuchukua hatua. Kwa kushirikiana na JKCI na Heart Team Africa Foundation, tunafungua kesho ambayo hakuna mtoto atakayepoteza maisha kwa kukosa huduma za kitabibu zinazoweza kuokoa maisha."
Vodacom Foundation, JKCI na Heart Team Africa Foundation wamewataka serikali, kampuni binafsi na watu wote kuungana nao katika juhudi hizi.
"Huu ni wito wa kitaifa," alisema Besiimire. "Ni jukumu letu kuhakikisha mtoto wa Kitanzania hapotezi maisha kwa sababu ya kuchelewa kupata upasuaji wa moyo unaookoa maisha."





Toa Maoni Yako:
0 comments: