Dar es Salaam, Oktoba 13, 2025: Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limekanusha vikali waraka ulioenezwa kwenye mitandao ya kijamii ukidai umetolewa na Baraza hilo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Katika taarifa iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa TEC, Rev. Fr. Charles Kitima, Baraza hilo limesema waraka wenye kichwa cha habari “Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Kuhusu Amani kwa Taifa Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Utakaofanyika Tarehe 29 Oktoba 2025” siyo halali na haujatolewa na TEC.
“Tunapenda kuwatangazia Waamini na Watanzania wote kwa ujumla kuwa waraka huo si wa kweli, na Baraza halihusiki na maudhui yaliyomo ndani yake,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
TEC imeeleza kusikitishwa na tabia ya baadhi ya watu kutumia jina la Taasisi hiyo kusambaza jumbe zisizotokana na Baraza, na kuwataka wahusika kuacha mara moja.
“Tabia hii mbaya ya kutumia Taasisi ya Maaskofu kupitia jumbe za uongo lazima ikome,” iliongeza taarifa hiyo.
Baraza hilo limewataka Watanzania kupuuza taarifa hiyo feki na kusisitiza kuwa tamko lolote rasmi kutoka kwa TEC litatolewa kupitia vyanzo vyake halali.


Toa Maoni Yako:
0 comments: