Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza rasmi kuwa hali ya amani na utulivu nchini imerudi katika hali yake ya kawaida, na shughuli zote za kijamii, kiuchumi na utalii zinaendelea kama kawaida baada ya kudhibitiwa kwa vurugu zilizoripotiwa kutokea kati ya Oktoba 29 hadi Novemba 1, 2025.
Katika taarifa iliyotolewa jana, Novemba 4, 2025, na kusainiwa na Nteghenjwa Hosseah, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, wizara hiyo imewahakikishia wananchi, wadau wa utalii na wageni kutoka ndani na nje ya nchi kwamba Tanzania inaendelea kuwa nchi salama, tulivu na yenye mazingira rafiki kwa shughuli za utalii, uwekezaji na biashara.
“Tanzania kama mwanachama wa Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism), inaendelea kutekeleza mwongozo wa utalii wa kimataifa unaolenga kuhakikisha usalama wa wageni, ikiwemo wasafiri na watalii wanaotembelea maeneo mbalimbali nchini,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Wizara imeeleza kuwa vituo vyote vya kuingia nchini kupitia usafiri wa anga, barabara, reli, maji na vivuko vinaendelea kutoa huduma kwa utaratibu wa kawaida, sambamba na usafiri wa umma ambao unaendelea kufanya kazi bila changamoto yoyote.
Aidha, imeelezwa kuwa huduma zote za utalii na shughuli za kibiashara kwa wageni zinaendelea kutolewa kama kawaida, huku sekta binafsi ikiendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha wageni wanafurahia huduma bora na salama.
“Wasafiri wanahimizwa kuendelea na mipango yao ya kutembelea na kufurahia vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Tanzania bila hofu yoyote,” imeongeza taarifa hiyo.
Serikali pia imetoa wito kwa mataifa rafiki, wawekezaji na wadau wa utalii duniani kuendelea kuiamini Tanzania kama kitovu cha amani na utulivu barani Afrika, huku ikisisitiza kuwa hatua zote za ulinzi na usalama zimeimarishwa katika maeneo yote ya kitalii.
Taarifa hiyo imesisitiza kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuwa mwenyeji salama kwa wageni wote, ikitumia fursa hii kuwakaribisha watalii, wawekezaji na washirika wa maendeleo kuendelea kufika nchini.



Toa Maoni Yako:
0 comments: