Na Mwandishi Wetu, Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, amewahakikishia wananchi, wageni na watalii wote kuwa hali ya ulinzi na usalama katika Mkoa wa Arusha ni shwari, na kwamba shughuli zote za kijamii na kiuchumi zimeendelea kama kawaida.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Novemba 4, 2025, mara baada ya kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mhe. Makalla alisema vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha ulinzi unakuwepo muda wote ili kuruhusu shughuli za kila siku kuendelea bila wasiwasi.
“Nataka kuwahakikishia wananchi wa Arusha, wageni na watalii wetu kwamba mkoa uko salama. Shughuli zote za kijamii na kiuchumi zinaendelea kama kawaida, na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vipo kazini masaa 24 kuhakikisha hali hiyo inabaki kuwa tulivu,” alisema Mhe. Makalla.
Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa serikali imechukua hatua za haraka kuhakikisha mkoa unarejea katika utulivu kamili, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa mapema za viashiria vya uvunjifu wa amani.
Aidha, Mhe. Makalla aliwataka wamiliki wa vituo vya mafuta kufungua vituo vyao na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi, sambamba na wamiliki wa biashara mbalimbali kufungua maduka na maeneo yao ya kazi ili uchumi wa mkoa usisimame.
“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea. Kwa hiyo naagiza vituo vyote vya mafuta vifunguliwe, na huduma zote za kijamii zirudi katika hali ya kawaida,” alisisitiza Makalla.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amewaagiza Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zote mkoani humo, chini ya usimamizi wa Katibu Tawala wa Mkoa, kuhakikisha usafi wa mazingira unazingatiwa ipasavyo, hasa kwenye masoko na maeneo ya makazi ya watu.
“Lazima kuhakikisha taka zote zinaondolewa mara moja kwenye maeneo ya masoko na makazi ya wananchi ili kuepuka magonjwa ya mlipuko. Huduma za usafi ni sehemu ya ulinzi wa afya na usalama wa jamii,” alisema CPA Makalla.
Amewataka pia viongozi wa serikali za mitaa na vijiji kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu kwa kuhakikisha hali ya usalama inaimarika katika maeneo yao na kutoa taarifa za matukio yote ya uvunjifu wa sheria kwa mamlaka husika.
Kwa mujibu wa Mhe. Makalla, Serikali ya Mkoa wa Arusha inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya usalama na ustawi wa wananchi, huku akisisitiza kuwa mkoa huo unaendelea kuwa kitovu cha utalii na uchumi wa kanda ya kaskazini.



Toa Maoni Yako:
0 comments: