
Na Mwandishi Wetu
Dodoma — Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema (HH), ametoa wito kwa wananchi wa Tanzania kudumisha amani na utulivu, akisisitiza kuwa tofauti za kisiasa na kijamii hazipaswi kutatuliwa mitaani bali kupitia mazungumzo na mifumo rasmi ya kidemokrasia.
Kauli hiyo ameitoa wakati akihutubia katika sherehe za kuapishwa kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mara baada ya kuapishwa rasmi kuwa Rais wa Tanzania, katika hafla iliyofanyika kwenye Viwanja vya Gwaride, Jijini Dodoma, ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Rais Hichilema alisema kuwa Tanzania imekuwa mfano wa amani na utulivu tangu ilipopata uhuru, na akasisitiza kuwa urithi huo haupaswi kuharibiwa kwa migawanyiko au vurugu.
“Amani, usalama na utulivu ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa. Mara nchi inapopoteza hali hiyo, kuirejesha huwa ni jambo gumu na lenye athari kubwa kwa familia, watoto, uchumi na mustakabali wa taifa,” alisema Rais Hichilema.
Alionya kuwa historia ya Bara la Afrika imeonyesha namna baadhi ya mataifa yalivyodumu katika migogoro kwa miaka mingi baada ya matukio ya vurugu, hivyo akahimiza umuhimu wa kulinda amani kwa gharama yoyote.
Rais Hichilema alibainisha kuwa maendeleo, ajira na ustawi wa wananchi haviwezi kupatikana katika mazingira yasiyo salama, na akasisitiza kuwa meza ya mazungumzo ndiyo njia bora ya kusuluhisha tofauti.

“Panapotokea tofauti, meza ya mazungumzo ndiyo mahali pekee pa kutafuta suluhu. Hilo ndilo somo kubwa tulilojifunza Zambia,” aliongeza.
Akitolea mfano uzoefu wake binafsi, alisema chama chake cha United Party for National Development (UPND) kilikaa miaka 23 katika upinzani, huku yeye mwenyewe akiongoza kwa miaka 15, lakini licha ya kushindwa mara kadhaa katika chaguzi, hakuwahi kuhamasisha wafuasi wake kuandamana au kuvuruga amani.
“Ningeliwaambia watu waende barabarani, tungepoteza mali, maisha na utu. Niliwaambia wasubiri, maana demokrasia inahitaji uvumilivu,” alisema Rais Hichilema.
Aidha, alisisitiza kuwa Zambia sasa inafaidika na matokeo ya uongozi wa amani, na akawahimiza Watanzania kuchagua njia ya fursa badala ya uharibifu, akisema changamoto ni sehemu ya safari ya maendeleo na kwamba “muda wa Mungu ndiyo bora zaidi.”
Katika hotuba yake, Rais Hichilema pia aligusia uhusiano wa kihistoria kati ya Zambia na Tanzania, akitaja miradi ya pamoja kama Tazama Pipeline na Tazara Railway iliyojengwa kwa ushirikiano wa waasisi wa mataifa hayo, Mwalimu Julius Nyerere na Dkt. Kenneth Kaunda.
Aliongeza kuwa ushirikiano huo unaendelea kupitia miradi ya kuboresha miundombinu ya usafiri na biashara kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Katika hitimisho lake, Rais Hichilema aliwapongeza viongozi wa Tanzania na kuwataka wananchi wote — wakiwemo wasiomuunga mkono Rais aliye madarakani — kushirikiana katika kujenga taifa moja lenye umoja, usawa na matumaini.
“Ni lazima kujenga mifumo inayowafikia wananchi wote bila ubaguzi. Tukilinda amani na utulivu, tutafungua milango ya maendeleo, ajira, na ukuaji wa biashara kwa vijana wetu, hususan kizazi cha Gen Z,” alisema.
Rais Hichilema alimalizia kwa kusisitiza dhamira ya Zambia kuendeleza uhusiano wa kindugu na Tanzania, akisema mataifa hayo mawili yana historia, malengo na ndoto zinazofanana za ustawi wa pamoja.




Toa Maoni Yako:
0 comments: