Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM – Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesaini mikataba minne ya uwekezaji wa utalii kupitia mpango wa Uwekezaji Mahiri (SWICA) na kampuni ya Kitanzania ya Uhusiano International ICT Ltd, yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 281.5 (sawa na TZS bilioni 719) kwa kipindi cha miaka 20.

Mikataba hiyo, iliyosainiwa leo Agosti 12, 2025 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, inahusu uwekezaji katika vitalu vinne vya Burko Open Area (Monduli – Arusha), Selous MHJ1, Selous MHJ2 na Selous ML1 (Liwale – Lindi).

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, uwekezaji huo unatarajiwa kuingiza wastani wa TZS bilioni 36 kwa mwaka, pamoja na kuchochea ajira, kuboresha huduma za jamii na kuchangia miradi ya maendeleo kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo husika. Miradi hiyo ya kijamii inakadiriwa kugharimu TZS bilioni 4.6 kwa miaka 20.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana, alisema hatua hiyo itaimarisha sekta ya uwindaji wa kitalii na utalii wa picha, sambamba na kuongeza mapato ya Serikali.

“Tunampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuitangaza Tanzania kupitia filamu za Amazing Tanzania na The Royal Tour, ambazo zimeongeza mwamko wa watalii na wawekezaji kuja nchini,” alisema Dkt. Chana.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA, Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis R. Semfuko, alisema mikataba hiyo mipya inafanya idadi ya mikataba ya SWICA kufikia 13 kati ya 14 iliyopangwa, sawa na asilimia 92.3 ya lengo, na imewezesha ukusanyaji wa zaidi ya TZS bilioni 27.4 tangu Januari 2024.

Aliongeza kuwa TAWA ipo kwenye mazungumzo ya mwisho kusaini mkataba na GBP Trading Ltd (GTL) kwa ajili ya ujenzi wa kambi za kudumu za kitalii katika hifadhi za Kijereshi, Mpanga-Kipengere na Wami-Mbiki, hatua itakayoongeza vitanda 240 na kupunguza uhaba wa malazi kwa watalii.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: