Articles by "KILIMO"
Showing posts with label KILIMO. Show all posts
Na Mwandishi Wetu.

KAMPUNI ya Mati Super Brands Ltd kupitia tawi lake la Mati Technology imezindua teknolojia mpya ya ndege nyuki (drone) zinazotengenezwa nchini, zenye uwezo wa kuboresha sekta ya kilimo na huduma nyingine za kijamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mati Group of Companies, David Mulokozi, amesema kampuni hiyo imeamua kuwekeza katika uzalishaji wa drone zinazotumika kunyunyizia dawa mashambani, kupima maeneo, kupanda mbegu, kusafirisha mizigo na kusaidia kaguzi mbalimbali.

Mulokozi ameeleza kuwa drone hizo zitauzwa kuanzia Shilingi milioni 17, bei ambayo ni nafuu ukilinganisha na gharama kubwa za kuagiza kutoka nje ya nchi. Pia, kampuni ipo katika mazungumzo na benki ili kuwezesha wakulima kupata mikopo kwa ajili ya kumudu teknolojia hiyo.


“Tumeona changamoto kubwa inayowakabili wakulima hasa kwenye upuliziaji wa dawa. Kwa kutumia drone hizi, hekari moja inaweza kunyunyiziwa dawa ndani ya dakika saba pekee, jambo linaloongeza ufanisi na kulinda afya za wakulima,” alisema Mulokozi.

Aidha, amebainisha kuwa uzalishaji wa drone hizo utatoa ajira kwa wahandisi wa Kitanzania na kufanikisha uhamishaji wa teknolojia kutoka kwa wataalamu wa kigeni
Kwa upande wake, Afisa Ushirika kutoka ofisi ya Msajili mkoa wa Manyara, Godamen Merinyo, amesema teknolojia hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wakulima wa mazao kama mbaazi ambayo hukua kwa urefu na kufanya unyunyiziaji wa dawa kuwa mgumu na wa gharama kubwa.

“Hii itasaidia kuongeza uzalishaji kwa gharama nafuu na kuimarisha vyama vya ushirika. Tutaanza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya teknolojia hii,” alisema Merinyo.
Naye Afisa Kilimo wa mkoa wa Manyara, Paulo Eugine, amesema drone hizo zitasaidia kuwalinda wakulima dhidi ya madhara ya kiafya yaliyokuwa yanawapata kutokana na kutumia pampu za mgongoni.

“Sasa mkulima ataweza kutumia remote control bila kuingiliwa na sumu, jambo linaloimarisha usalama na afya zao,” alisisitiza Eugine.

Hatua hii ya Mati Technology inatarajiwa kuchochea mapinduzi ya kilimo nchini na kuunga mkono jitihada za serikali katika kukuza tija kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Na Ferdinand Shayo, Arusha.

Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) kimetoa mafunzo ya utengenezaji wa majiko ya nishati safi pamoja na miundombinu yake kwa Maafisa wa Jeshi la Magereza kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania ili kuwawezesha kutumia nishati hiyo na kuondokana na matumizi ya mkaa na kuni ambayo yanasababisha uharibifu wa mazingira .

Akizungumza katika hafla ya kufunga Mafunzo hayo ,Mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania ambaye ni Mkuu wa Magereza Mkoa wa Manyara Felichisim Masawe amempongeza Mkuu wa Jeshi hilo kwa kutoa Maafisa waliopatiwa mafunzo na CAMARTEC ili waweze kutengeneza majiko yanayotumia gesi ya bayogesi pamoja na sufuria.

Masawe amesema kuwa Jeshi hilo limekua mstari wa mbele kutekeleza agenda ya nishati safi kwa kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Samia Suluhu Hassan ya kuzitaka taasisi zenye watu Zaidi ya 100 kuanza kutumia nishati safi ambapo magereza wameanza tangu mwaka 2024.

Kaimu Mkurugenzi wa CARMATEC Boniface Chatila amelitaka Jeshi la Magereza kuendelea kushirikiana na kituo hicho ili kupata mahitaji yote muhimu ya mitambo ya nishati safi pamoja na kutoa ujuzi kwa Maafisa Magereza ili kueneza Teknolojia hizo.

Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo CAMARTEC Peter Mtoba amesema kituo hicho kimesaini makubaliano ya kutengeneza majiko Zaidi ya 300 ya nishati safi yatakayosambazwa kwenye magereza mbali mbali nchini ili kuhakikisha wanatumia nishati safi na kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa.

Na Mwandishi Wetu.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ametumia ziara yake nchini Belarus kunadi fursa za uwekezaji katika maeneo manne ya kipaumbele ya Serikali ya awamu ya sita ambayo ni kilimo, afya, madini na ulinzi & usalama.

Mhe. Waziri Mkuu katika siku mbili za ziara yake, tarehe 22 na 23 Julai 2025 ametembelea kampuni kubwa nane zenye nguvu ya mitaji jijini Minsk na kuzihakikishia utayari wa Serikali ya Tanzania kushirikiana nazo kwa kuzipatia kila aina ya msaada zitakapokuja Tanzania kuwekeza.

Kwenye eneo la kilimo, Mhe. Waziri Mkuu alikutana na viongozi wa kampuni ya AFTRADE ambayo tayari ipo nchini na kuwasisitiza kuongeza kasi katika kuendeleza kilimo hususan kuwa na programu za kuwasaidia wakulima wadogo mitaji, utafiti na mafunzo ili kilimo kiweze kuwa na tija, kizalishe ajira na kuongeza usalama wa chakula nchini.

Katika eneo hilo la kilimo, Waziri mkuu pia alitembelea chuo cha kilimo cha Belarus na viwanda vya matrekta na kuvishawishi viwanda hivyo kufungua matawi nchini Tanzania.

Kuhusu chuo cha kilimo ambacho mafunzo yake huyafanya kwa vitendo zaidi, Waziri Mkuu aliomba Watanzania wapatiwe fursa za masomo katika chuo hicho ili waweze kuendeleza sekta ya kilimo nchini, watakapomaliza masomo yao.

Kuhusu Afya, Mhe. Waziri Mkuu alitembelea kampuni ya kuzalisha na kusambaza dawa na vifaa tiba ya Belmedepreparaty ambayo ni moja ya kampuni kubwa nchini Belarus. Kampuni hiyo inayozalisha bidhaa tofauti tofauti zaidi ya 1700 na kuuza ndani na nje ya nchi katika mataifa zaidi ya 24, iliridhia maombi ya Mhe. Waziri Mkuu na kuahidi kufanya ziara nchini Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji.

Mhe. Waziri Mkuu alisema Belmedepreparaty ni kampuni sahihi kuja kuwekeza nchini kutokana na kutumia teknolojia ya kisasa ya kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya kimataifa.

Kwa upande wa sekta ya madini, Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kutengeneza mitambo inayotumika kuchimba madini migodini na kukishawishi kiwanda hicho kuja kuwekeza nchini Tanzania.

Kuhusu suala la Ulinzi na Usalama, Mhe. Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kutengeneza vifaa vya ukoaji na kuzima moto na kusisitiza umuhimu wa kushirikiana na kiwanda hicho ili kuondoa tatizo la uhaba wa vifaa hivyo nchini.

Waziri Mkuu amemaliza ziara yake na aliondoka Julai 24, 2025 kurejea nyumbani.
Na Mwandishi wetu- Morogoro

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepongezwa kwa kuendelea kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji, tija na faida kwa wakulima na wananchi kwa ujumla.

Pongezi hizo zimetolewa na, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua warsha kuhusu kuimarisha Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Kilimo leo tarehe 16 Julai, 2025 katika Ukumbi wa Mbaraka Mshee - Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, mkoani Morogoro.

Dkt. Yonazi alisema, hatua hiyo ni kutokana na Serikali kuongeza najeti ya Kilimo kwa miaka mitatu mfululizo kutoka bilioni 294 (2022/2023) hadi trilioni 1.241 (2025/2026) ambapo katika kufanikisha hilo Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imezindua Programu na Mipango ya kufanikisha malengo hayo ambayo ni pamoja na Programu ya BBT, Agenda 10/30 na Agricultural Transformation Master Plan.

“Ninapenda kumshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuboresha muundo wa Taasisi za Umma na kuanzisha Idara ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu na Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini katika ngazi zote nchini kwa lengo la kupima utendaji wa Serikali,” alisema Dkt. Yonazi.


Pia aliongeza kwamba, warsha hiyo itakayofanyika kwa siku tano itawezeshwa na wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwa kushirikiana na Mtaalam Mbobezi kutoka Benki ya Dunia kuhusu dhana mbalimbali zikiwemo muundo wa kitaasisi wa Ufuatiliaji na Tathmini nchini, Mwongozo Elekezi wa Mwongozo Jumuishi wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali (M&E Operational Manual).
“Mpango mwingine ni Mpango wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Mpango kazi wa Mwaka wa Wizara na Taasisi (M&E Plan), Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (M&E Strategy) na Moduli ya kupima utendaji wa Wizara na Taasisi husika (M&E Performance Model). Aidha, ni muhimu kupima hali ya utayari wa kila Wizara na Taasisi zake,” alieleza .

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu imekasimiwa jukumu la kuratibu, kufuatilia, kutathmini na kupima utendaji wa serikali nchini hivyo ofisi imeendelea kuratibu shughuli hizo kwa kuandaa na kuwasilisha nyaraka muhimu zitakazowezesha ubora na ufanisi wa kazi za ufuatiliaji na tathmini.

“Ni muhimu kuvisimamia vitengo vyenu kutekeleza majukumu yao kwa kufuata miongozo ili kazi zetu ziwe na ubora unaotakiwa. Aidha, ni matarajio yangu kuwa nyaraka hizo zitawaongoza kuandaa nyaraka elekezi na tendaji kwa kuzingatia muktadha wa Wizara yenu ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yenu,” alibainisha.

Aidha, Dkt. Yonazi aliwasihi washiriki wa warsha hiyo kujadili masuala yote ikiwemo changamoto zinazoweza kusababisha kuwa na utekelezaji usioridhisha katika Wizara mbalimbali na Taasisi zake ikiwemo Wizara ya Kilimo pamoja na kupendekeza namna bora ya kuondokana na changamoto hizo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Mweli akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Chama cha Wakulima Tanganyika (TFA) .uliofanyika Jijini Arusha.
Wanahisa wakifuatilia Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Chama cha Wakulima Tanganyika (TFA).
Mkurugenzi Wa chama cha Wakulima Tanganyika (TFA) Jastin Shirima akizungumza na Wanahisa
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Mweli akipewa maelekezo ya pembejeo zinazotolewa na TFA kwa wanachama wake
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Mweli akiwasili Kweye mkutano Mkuu wa Wanahisa TFA.
Baadhi wa wadau wakilimo wakifuatilia Mkutano Mkuu wa Wanahisa TFA.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mkulima Crop ambayo iko chini ya kampuni za Kilimo za Peter & Burg yenye makao makuu Nchini Ukraine Bakari Duchi Ame akieleza ushirikiano wao na TFA katika kuzalisha mbegu bora za alizeti
Mwanzilishi wa kampuni ya Coastal Biotech Ltd Steven Sillah akieleza alivyojipanga kushirikiana na TFA kuzalidha mbolea hai
Mwenyekiti wa TFA Waziri Barnabas akifafanua jambo kwa katibu Mkuu Wizara ya Kilimo.

Na Mwandishi Wetu , Arusha.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Mweli amekipongeza Chama cha Wakulima Tanganyika (TFA) kwa kutoa huduma bora za upimaji wa afya ya udongo na pembejeo kwa wakulima ambao ni wanachama kwa lengo la kuchochea uzalishaji bora wa mazao ya chakula na biashara ili kuongeza mapato ya wakulima na kuchangia ukuaji wa Uchumi wa Taifa.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa TFA,Katibu Mkuu ameipongeza bodi ya chama hicho kwa juhudi za kupima afya udongo kwa wakulima ili waweze kujua aina ya udongo walionao na kutumia pembejeo kulingana na aina ya udongo wa mashamba yao ili kupata mazao mengi na bora.

“Sisi kama Tanzania malengo yetu kwa miaka ijayo ni kuhakikisha kila mtu anapewa mbolea na kutumia viuatilifu na pembejeo zinazoendana na afya ya udongo ya eneo husika.Tayari tumeanza kupima afya ya udongo kwenye mikoa 8 na ndani ya miaka 2 tutakamilisha nchi nzima” Anaeleza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo .

Mkurugenzi wa TFA Jastin Shirima amesema kuwa TFA itendelea kutoa huduma bora kwa wanachama na kwasasa imejipanga kuwekeza katika viwanda vya kuzalisha mbegu bora za alizeti ili kuwawezesha wakulima kupata mbegu za uhakika na kuongeza kasi ya uzalishaji wa mafuta ya kula hivyo kupunguza uagizaji wa mafuta hayo kutoka nje ya nchi.

Shirima amesema kuwa watashirikiana na wadau kutoka nchi za Ujerumani na Ukraine ili kuzalisha mbegu bora za alizeti na kupunguza uhaba wa mbegu za alizeti.

Kwa upande wao wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mkulima Crop ambayo iko chini ya kampuni za Kilimo za Peter & Burg Bakari Duchi Ame yenye makao yake Makuu nchini Ukraine amesema watashirikiana na TFA kuhakikisha wanazalisha mbegu bora za alizeti na uzalishaji utaanza mwakani 2025.

Mwanzilishi wa kampuni ya Coastal Biotech Ltd Steven Sillah amesema tayari wana mpango wa kushirikiana na TFA kuzalisha mbolea hai ili kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao na kukua kiuchumi.

Mwenyekiti wa TFA Waziri Barnabas ameiomba serikali iendelee kudhibiti mbegu feki katika soko ili kuwalinda wakulima na kuongeza kuwa TFA itaendelea kutoa pembejeo bora kwa wakulima wake wakati wote.

Hata hivyo Wakulima ambao ni wana hisa akiwemo Simon Marunda wameiomba serikali itoe maeneo kwa TFA iliiweze kuzalisha mbegu bora badala ya kutegemea mbegu kutoka nje ya nchi zinazouzwa kwa bei kubwa ambayo wakulima wengi wanashindwa kuimudu.
Ferdinand Shayo , Arusha.

Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dadi Kolimba amekipongeza Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia vijijini (CAMARTEC) kwa kusambaza teknolojia na mashine mbali mbali za kulima ,kuvuna na kuchakata mazao pamoja na kuyaongezea thamani ili yaweze kupata bei nzuri katika masoko ya ndani na nje ya nchi hivyo kuwakomboa wakulima.

Akizungumza mara baada ya kutembelea kituo kihandisi cha Teknolojia za Kilimo kilichoanzishwa na CAMARTEC katika kijiji cha Gongali Wilayani Karatu ambapo amejionea zana mbali mbali ikiwemo mashine za Kupukuchua mahindi,maharage,alizeti na matrekta ,Mkuu wa Wilaya hiyo amesema kuwa kituo hicho kitawasaidia wakulima kulima kwa kisasa na kuchakata mazao yao kwa kutumia zana za kisasa.

Kolimba ameipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuiwezesha Camartec kufungua kituo kijijini hapo na kuwafikia wakulima wengi na kuongeza kuwa uhitaji wa mashine hizo bado ni mkubwa kwa wilaya hiyo yenye wakulima wengi zaidi.

Kaimu Mkurugenzi wa CARMATEC Mhandisi Godfrey Mwinama amesema wataendelea kufanya utafiti na kutengeneza mashine ambazo zitakua mkombozi kwa wakulima kwa kuwokolea muda na gharama lunwa walizokuwa wakitumia kutokana na teknolojia duni.

"Tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dr
Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kuwasogezea wakulima wa vijijini mashine mbali mbali " Anaeleza Godfrey Mwinama Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa CARMATEC.

Kwa upande wao wakulima wakiwemo Rogati Israel na Musa Hussein wamesema kuwa mashine walizozipata kutoka CAMARTEC Zimewasaidia kupukuchua mahindi na maharage kwa muda mfupi bila kuharibu ubora wa mazao hayo.
Veronica Simba – WMA

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Albogast Kajungu, amefanya ziara ya kushtukiza katika mashamba ya wakulima mbalimbali eneo la Mang’ola wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha na kuridhishwa na namna wakulima hao wanavyozingatia matumizi ya vipimo sahihi.

Akiongoza Timu ya Wataalamu wa WMA katika zoezi hilo, Agosti 9, 2024, Kajungu amesema lengo ni kujiridhisha ikiwa wananchi wanazingatia elimu inayotolewa na Wakala wa Vipimo kuhusu matumizi ya vipimo sahihi ili kuzilinda pande zote yaani wakulima, wafanya biashara na walaji.

Katika ziara hiyo, Timu hiyo ya Wataalamu wa WMA walihakiki uzito wa mazao aina ya vitunguu yaliyofungashwa katika vifungashio vya aina mbalimbali tayari kwa kuuzwa pamoja na kuzungumza na wakulima, wafanyabiashara na wasafirishaji wa mazao hayo.
“Niwapongeze sana kwa kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi maana katika mazao yote yaliyofungashwa ambayo tumepima, hakuna yaliyozidi uzito unaoelekezwa kisheria. Nawasihi muendelee hivyo kwani kila upande utapata faida stahiki,” amesema Kajungu.

Akifafanua zaidi kuhusu maelekezo ya kisheria kwa uzito wa mazao ya shamba yaliyofungashwa, Kajungu amesema mkulima yuko huru kufungasha kwa kutumia aina yoyote ya kifungashio isipokuwa azingatie uzito wake usizidi kilo 100.

Ametoa ufafanuzi huo kutokana na uelewa tofauti kwa baadhi ya watu wanaotafsiri kuwa sheria inakataza kufungasha mazao kwa kuongeza kishungi katika vifungashio.

“Niendelee kuwaelimisha na kuwaelewesha kuwa tafsiri sahihi ya lumbesa siyo kishungi bali ni uzito uliozidi kilo 100 kwa mazao yaliyofungashwa, Na katika hili niseme wazi huwezi kuthibitisha lumbesa kwa macho, ni lazima upime kujiridhisha kuwa mazao yaliyofungashwa yamezidi kilo 100,” amesisitiza Kajungu.

Katika hatua nyingine, Kajungu ameendelea kutoa ushauri kwa Halmashauri zote nchini kutumia mizani kupima mazao yaliyofungashwa ili kuondoa utata na manung’uniko yanayojitokeza kwa baadhi ya wakulima na wafanyabiashara kwamba wanatozwa faini kwa mazao yaliyofungashwa na kuwa na kishungi yakitafsiriwa kama lumbesa.

“Mwarobaini wa changamoto hiyo ni kutumia mizani kama sheria inavyoelekeza na siyo kutizama kwa macho.”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima na wafanyabiashara wa vitunguu katika eneo la Mang’ola wamekiri kunufaika zaidi kwa kila upande baada ya kuanza kuzingatia elimu ya vipimo sahihi waliyopatiwa na Serikali kupitia Wakala wa Vipimo.

Marieta Tlemai, mkulima wa vitunguu, kwa niaba ya wenzake, ametoa pongezi kwa Serikali kupitia Wakala wa Vipimo kwa kuwajali wakulima na kuweka sheria ya ufungashaji mazao inayolenga kulinda maslahi yao.

Awali, Timu hiyo ya Wataalamu kutoka WMA, ilitembelea Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu ili kueleza dhamira ya ziara yao na kupokelewa na Katibu Tawala, Dkt. Lameck Karanga ambaye aliwahakikishia kuwa Ofisi yake inaunga mkono jitihada za kutokomeza lumbesa ili kulinda maslahi ya wananchi wake ambao wengi hujishughulisha na kilimo cha vitunguu.