
Baada ya kuangazia kwa ufupi historia za maaskofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mario Epifanio Abdallah Mgulunde katika makala zilizopita, leo tunaangazia kwa ufupi maisha na utume wa Askofu Mkuu Norbert Wendelin Mtega.
Mhashamu Askofu Mkuu Norbert Wendelin Mtega alikuwa Askofu Mkuu wa pili wa Jimbo Kuu la Songea, akichukua nafasi hiyo baada ya kifo cha Askofu Yakobo Yafunani Komba.
Askofu Mtega alizaliwa Agosti 17, 1945 katika Kijiji cha Kinyika, Parokia ya Lupanga, Wilaya ya Ludewa katika Jimbo la Njombe. Baba yake aliitwa Wendelin Mbwatilo Paulo Mtega na mama yake aliitwa Martha Msafiri Petro Mtweve.
Alibatizwa Septemba 9, 1945 na Padre Leonhard Wuesst OSB, mmisionari Mbenediktini kutoka Uswisi. Baada ya miaka kumi, mwaka 1955, alipokea Sakramenti ya Kitubio na Komunio ya Kwanza katika Kigango cha Lupanga. Mwaka uliofuata, Oktoba 2, 1956, alipokea Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Madunda kutoka kwa Askofu Eberhard Spiess OSB.
Elimu yake ya msingi aliipata katika Shule ya Msingi Lupanga kuanzia mwaka 1953 hadi 1957. Baadaye alijiunga na Seminari ya Kigonsera kwa masomo ya sekondari kabla ya kuendelea na masomo katika Seminari ya Likonde mwaka 1962. Baada ya kumaliza masomo huko, alichaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari ya Serikali ya Tosamaganga mkoani Iringa, ambako alihitimu Kidato cha Sita mwaka 1967.
Mwaka huohuo wa 1967 alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kambi ya Kitai, Wilaya ya Mbinga, kisha Mafinga, ambako alipata namba ya kijeshi A0468. Alimaliza mafunzo hayo kwa mafanikio na kutunukiwa cheti cha Best Trainee.
Mwaka 1968 alijiunga na Seminari Kuu ya Peramiho kwa masomo ya Falsafa kwa kipindi cha miaka miwili na kuhitimu Novemba 1969. Kuanzia Januari 1970 hadi Novemba 1973 aliendelea na masomo ya Teolojia katika seminari hiyo hiyo. Baadaye alipata Stashahada ya Teolojia katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda.
Baada ya masomo hayo, alipokea Daraja la Ushemasi katika Seminari ya Peramiho na baadaye Daraja Takatifu la Upadre katika Parokia ya Lupanga. Madaraja yote mawili alipewa na Askofu Raymond Mwanyika wa Jimbo la Njombe wakati huo.
Baada ya kuwekwa wakfu kuwa padre, alitumika katika majukumu mbalimbali ya kichungaji na kitaaluma, ikiwemo kuwa Mkurugenzi wa Caritas, Mkurugenzi wa Miito, mwalimu wa dini katika Shule ya Sekondari Njombe, mlezi wa YCS (Young Catholic Students) na Paroko Msaidizi wa pili wa Parokia ya Njombe.
Mwaka 1976 alitumwa kwenda kusoma katika Chuo cha Kipapa mjini Roma, Italia, ambako alianza kwa kujifunza lugha ya Kiitaliano kabla ya kuendelea na masomo ya Falsafa. Mwaka 1978 alipata Shahada ya Falsafa kwa daraja la Magna Cum Laude, na mwaka 1981 alihitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) kwa daraja la Summa Cum Laude.
Aliporejea Tanzania, alifundisha katika Seminari Kuu ya Peramiho kama mhadhiri wa Falsafa.
Mwaka 1985 aliteuliwa kuwa Askofu wa tatu wa Jimbo Katoliki la Iringa na kuwekwa wakfu rasmi Januari 1986 mjini Roma na Baba Mtakatifu John Paul II.
Baadaye Julai 1992 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea, akichukua nafasi ya marehemu Askofu Yakobo Yafunani Komba, na hivyo kuwa Askofu Mkuu wa pili wa Jimbo hilo.
Baada ya kulitumikia Kanisa kwa miaka mingi, Mei 15, 2013 Askofu Mkuu Mtega alitangaza rasmi kujiuzulu wadhifa wake kutokana na sababu za kiafya. Mei 19, 2013 aliwaaga rasmi waamini katika Kanisa Kuu la Songea kwa kuongoza misa maalumu ya kuaga.
Katika hotuba yake alisema:
“Kwa kuzingatia hali yangu ya afya na jinsi nilivyoona uwezo wangu wa kuendelea na majukumu ya uongozi unavyopungua, niliamua kwa hiari yangu kumuandikia Baba Mtakatifu nikiomba ruhusa ya kustaafu kabla ya kufikia umri wa kisheria. Nimepokea majibu yake akiridhia ombi langu, hivyo leo mbele yenu natua jukumu la uongozi wa Jimbo Kuu la Songea.”
Alieleza pia kuwa katika kipindi cha mpito, Baba Mtakatifu alimchagua Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kuwa msimamizi wa kitume wa Jimbo hilo hadi uteuzi wa Askofu Mkuu mpya utakapofanyika.
Katika hitimisho la ujumbe wake kwa waamini, Askofu Mtega aliwaomba waumini waendelee kumuombea huku naye akiendelea kuwaombea.
Makala hii imetoa muhtasari mfupi wa maisha na utume wa Askofu Mkuu Norbert Mtega. Wasomaji wanahimizwa kuendelea kutafiti kwa kina zaidi historia yake na mchango wake katika Kanisa.


Toa Maoni Yako:
0 comments: