NAIROBI, KENYA – Rais William Ruto ameongoza hafla ya kihistoria katika Ikulu ya Nairobi kuadhimisha kuwasili kwa Ngao ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), tukio ambalo linatajwa kuwa ishara ya nafasi muhimu ambayo Kenya inazidi kuchukua katika ramani ya michezo ulimwenguni.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Ruto alisema kuwa Kenya imejaa vijana wenye vipaji na uwezo wa kuleta heshima ya kimataifa endapo watawekewa mazingira bora kupitia uwekezaji makini katika miundombinu ya michezo.
"Sisi ni taifa lenye vipaji vya kiwango cha juu vinavyostahili jukwaa la dunia. Vijana wetu wana uwezo mkubwa, na jukumu letu kama serikali ni kuhakikisha tunawawezesha kufikia kilele cha mafanikio," alisema Rais Ruto.


Rais alibainisha kuwa serikali yake imeanza na inaendelea kuboresha viwanja vikubwa na madogo kote nchini. Alisema ujenzi wa viwanja vipya, ukarabati wa vile vilivyopo na uwekezaji katika programu za mafunzo kwa vijana ni sehemu ya mpango mpana wa kuandaa mabingwa wa kesho.
"Tunajenga miundombinu ya kisasa ya michezo katika kila kona ya nchi. Hii ni pamoja na viwanja, vituo maalum vya mafunzo, na ushirikiano na mashirika ya kimataifa ili kuhakikisha vijana wetu wanapata fursa sawa na wenzao duniani," aliongeza.
Kuwasili kwa kombe hilo nchini kumetajwa kama tukio linalolenga kuongeza hamasa miongoni mwa vijana na wadau wa michezo, huku likiwaalika kuona kwamba mafanikio ya kiwango cha kimataifa yanapatikana kupitia nidhamu, mafunzo bora, na juhudi za pamoja.
Wadau wa michezo wamepongeza hatua za serikali wakisema ni ishara ya mwelekeo mpya unaotegemea matokeo, hali inayoweza kuifanya Kenya kuwa kitovu cha vipaji barani Afrika.







Toa Maoni Yako:
0 comments: