Na Mwandishi Wetu, Michezo

Nyota wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, amezungumza kwa uwazi kuhusu hali yake ya kifedha, akisema licha ya kutajwa kuwa bilionea, bado anajiona “maskini” kwa sababu ya majukumu makubwa anayobeba kwa familia na jamii inayomtegemea.

Akihojiwa na mwandishi maarufu Morgan, Ronaldo alifichua kuwa alifikia hadhi ya kuwa bilionea akiwa na umri wa miaka 39, lakini bado anaendelea kutafuta fedha kwa bidii kila siku.

“Mwezi mmoja uliopita watu walisema mimi ni bilionea, lakini ukweli ni kwamba nilikuwa bilionea nikiwa na miaka 39,” alisema Ronaldo. “Ninaheshimu mali zangu, fedha zangu na kila kitu ninachomiliki. Nina HR wangu ambaye tunawasiliana mara mbili kwa siku — asubuhi na usiku — kujua nini kimeingia, kimepungua na nini cha kufanya kuongeza zaidi.”

Hata hivyo, Ronaldo alisisitiza kuwa pamoja na utajiri huo, bado hajitoshelezi kifedha kwa sababu ana wajibu mkubwa wa kusaidia watu wengi wanaomtegemea.

“Mimi ni baba, lakini pia nina jamii kubwa nyuma yangu. Kila mwezi nachangia zaidi ya milioni 450 za Tanzania kusaidia familia na watu wanaonihitaji. Hivyo, siwezi kusema nina pesa nyingi, maana bado nina kazi ya kutafuta zaidi,” alisema nyota huyo wa Al-Nassr.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, Ronaldo ndiye mchezaji anayelipwa zaidi duniani, akiwa na mkataba wa mamilioni ya dola kwa mwaka, lakini kauli yake imeonyesha upande wa utu na uwajibikaji wa kijamii unaokwenda mbali zaidi ya umaarufu na fedha.

Mashabiki wengi mitandaoni wameitafsiri kauli hiyo kama somo muhimu kuhusu unyenyekevu na kujituma, huku wengine wakisema Ronaldo amethibitisha kwamba “tajiri wa kweli ni yule anayejua kutumia utajiri wake kusaidia wengine.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: