Na “Mzee wa Atikali” ✍️✍️✍️
Simu: 0754 744 557
Ijumaa, Novemba 7, 2025
Utangulizi
Katika taarifa iliyochapishwa na Nyasa Daily, Mwanasheria Mkuu wa Malawi, Mhe. Thabo Nyirenda, ametunukiwa tuzo ya “Mwanasheria Mkuu Bora Barani Afrika” kwa mchango wake katika kuimarisha utawala wa sheria, uadilifu, na ushujaa katika kusimamia haki.
Hata hivyo, kwa kuzingatia historia ndefu ya bara letu, kuna majina mengine yaliyowahi kung’aa kwa ubora na uadilifu katika taaluma ya sheria. Miongoni mwao ni marehemu Bashiru Swanzy wa Ghana, Charles Njonjo wa Kenya, na kwa heshima kubwa, Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba wa Tanzania.
Makala hii inamchambua Mhe. Warioba kama kielelezo cha ubobevu, uadilifu, ujasiri, na uzalendo wa kweli katika kutetea misingi ya kisheria na maadili ya kitaifa.
Mwanasheria wa Uadilifu na Ujasiri
Mhe. Warioba, ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 1976 hadi 1985, ni miongoni mwa viongozi waliotambulika kwa uthabiti wa maadili, bidii ya kazi, na ushujaa wa kusimamia ukweli bila woga.
Ni mwanasheria mwenye weledi wa hali ya juu ambaye amewahi kuhudumu hadi ngazi ya kimataifa kama Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa. Heshima kubwa anayopata kitaifa na kimataifa ni matokeo ya maisha yake yaliyosimama imara katika misingi ya haki, ukweli, na uwajibikaji.
Uthabiti Mbele ya Nguvu ya Kiongozi
Wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, viongozi wengi walikuwa na heshima kuu na wakati mwingine woga kwa Rais huyo mwenye hekima na uthabiti wa kimaamuzi. Hata hivyo, Mhe. Warioba alisimama tofauti. Alimheshimu Rais Nyerere kwa dhati, lakini hakuwahi kuogopa kumwambia ukweli pale alipoona sheria inavunjwa.
Mfano wa wazi ni kisa cha “Msala wa Majaji”, ambapo Mhe. Warioba alikataa shinikizo la Rais Nyerere kutumia dissenting opinion kumwondoa jaji ambaye kamati ya uchunguzi ilikuwa imemwachia huru. Kwa uthabiti na ujasiri, alisisitiza kuwa kufanya hivyo kungekuwa kinyume na Katiba ya mwaka 1977.
Uthubutu huo wa kisheria unamtofautisha na wanasheria wengi wa bara hili. Ni nadra kupata Mwanasheria Mkuu mwenye ujasiri wa kumweleza Rais wake asivunje Katiba.
Uadilifu Katika Uteuzi
Kisa kingine ni lile la Mhe. Chediel Mgonja, aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga mwaka 1983 baada ya kuvuliwa ubunge na Mahakama ya Rufaa kwa kosa la rushwa. Mhe. Warioba alipoona tangazo hilo, alikwenda moja kwa moja Ikulu kumwonya Rais Nyerere kuwa uteuzi huo ni kinyume cha Katiba.
Awali, Rais Nyerere alikasirika, lakini baadaye alitafakari na kukubali hoja za kisheria za Mhe. Warioba, akatengua uteuzi huo na hata kumuomba radhi hadharani mbele ya Waziri Mkuu Edward Sokoine.
Kitendo hicho si tu kilionesha uadilifu wa Mhe. Warioba, bali pia kilidhihirisha namna alivyopata heshima ya kweli kutokana na ujasiri na ukweli wake.
Upinzani Dhidi ya Sheria Kandamizi
Mwaka 1984, wakati Baraza la Mawaziri likijadili Muswada wa Sheria ya Uhujumu Uchumi, Mhe. Warioba alikosoa kwa uwazi vifungu vilivyokuwa vinavunja haki za binadamu, akisisitiza kwamba sheria hiyo ilikuwa na mapungufu makubwa.
Alipokosa kusikilizwa, alitishia kujiuzulu, akiamini kwamba utekelezaji wa sheria isiyo na haki ni kinyume na misingi ya utawala bora. Baadaye, kwa ujasiri uleule, aligoma kutekeleza agizo la Rais na Waziri Mkuu la kutoa dhamana kwa mtuhumiwa, akisisitiza kuwa sheria hairuhusu. Hatimaye, hoja zake zilizingatiwa, na Bunge likafanya marekebisho ya haraka Juni 1984 — ikiweka rekodi kama mojawapo ya sheria zilizorekebishwa ndani ya muda mfupi zaidi.
Hitimisho
Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba ni mfano halisi wa Mwanasheria Mkuu anayekidhi vigezo vyote vya ubora: ubobevu wa taaluma, uadilifu wa hali ya juu, bidii, ujasiri, na uthabiti katika kutetea sheria.
Kwa weledi wake, ujasiri wake mbele ya mamlaka, na uaminifu wake usiotetereka, Mhe. Warioba amejijengea heshima isiyofutika katika historia ya Afrika.
Katika enzi za sasa ambapo baadhi ya viongozi wanayumbishwa na maslahi binafsi, historia ya Mhe. Warioba inabaki kuwa somo kwa vizazi vijavyo kuhusu maana halisi ya utumishi wa umma, uadilifu, na utii wa Katiba.
With permission from:
“Mzee wa Atikali” ✍️✍️✍️
Simu: 0754 744 557
Ijumaa, Novemba 7, 2025
“God bless you with great health, Mhe. Warioba — you remain an enduring inspiration.” 🌿



.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments: