NAIROBI, KENYA – Rais William Ruto ameipongeza timu ya taifa ya soka ya wanawake, Harambee Starlets, kwa ushindi wa mabao 3-1 walioupata dhidi ya Gambia katika mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) unaotarajiwa kufanyika nchini Morocco mwaka 2026.
Kupitia ujumbe wake kwa taifa, Rais Ruto alisema ushindi huo ni ushahidi wa nidhamu, vipaji na ari ya kupambana iliyooneshwa na wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
"Hongera kwa Harambee Starlets kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Gambia, ushindi unaotuvusha hatua moja karibu zaidi na kufuzu WAFCON 2026," alisema Rais Ruto.

Aidha, alisifu uwekezaji na usimamizi wa timu, akibainisha kuwa mafanikio ya Starlets ni sehemu ya kuimarika kwa nafasi ya Kenya katika michezo ya wanawake barani Afrika.
"Ushindi huu unaonesha nidhamu, kipaji na dhamira ya wachezaji wetu, pamoja na uongozi madhubuti wa benchi la ufundi. Mmeliletea taifa letu heshima na kutuonesha ukuaji wa nguvu ya michezo ya wanawake nchini," aliongeza.
Rais Ruto aliwahimiza wachezaji kuendeleza ari hiyo wanapojiandaa kwa mchezo wa marudiano, akisisitiza kuwa taifa lote lipo nyuma yao.
"Tunaposubiri mchezo wa marudiano, tambueni kwamba taifa zima lipo pamoja nanyi. Ushindi wenu ni fahari yetu. Endeleeni kung’ara, endeleeni kushinda, na roho ya Harambee iendelee kutuunganisha kama taifa," alisema.
Rais alimalizia kwa ujumbe wa hamasa, akisema: "Hongera Starlets! Kama nilivyoahidi, nitacheza kama mimi."












Toa Maoni Yako:
0 comments: