Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) leo, tarehe 23 Julai 2025, imetoa rasmi leseni ya mwaka mmoja kwa Kampuni ya Society of Music Advocacy Limited (SOMA) kwa ajili ya ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha ya kazi za muziki nchini.
Leseni hiyo inahusu kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, ambapo kampuni hiyo itakuwa na jukumu la kukusanya na kugawa mirabaha kwa niaba ya wamiliki wa kazi za muziki, huku COSOTA ikiendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa majukumu hayo kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa leseni, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa COSOTA, Ndugu Philemon Kilaka, aliitaka SOMA kuanza kazi mara moja kwa kuhakikisha ukusanyaji wa mirabaha unafanyika katika maeneo yote yanayotumia kazi za muziki ikiwemo hoteli, baa, migahawa, kumbi za starehe na maeneo mengine husika.
Aidha, alisisitiza kuwa utekelezaji wa jukumu hilo unapaswa kuzingatia Sheria ya Hakimiliki pamoja na Kanuni za Usimamizi wa Kampuni ya Ugawaji wa Mirabaha ya mwaka 2023, ili kulinda haki za wasanii na wadau wote wa kazi za muziki nchini.
Kwa hatua hii, Tanzania imepiga hatua muhimu katika kuhakikisha wasanii wananufaika ipasavyo na kazi zao kupitia mfumo rasmi wa ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha.




Toa Maoni Yako:
0 comments: