Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga (PhD), amempongeza John Elisha, maarufu kama Boneka, kwa kushinda Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Mwaka 2025 kupitia tamthiliya maarufu ya Kombolela inayorushwa katika chaneli ya Sinema Zetu ya Azam TV.

Tuzo hiyo imetolewa na East Africa Youth Panel Awards tarehe 19 Oktoba 2025, ikitambua mchango wa Elisha katika kukuza ubunifu na ubora wa tasnia ya filamu Afrika Mashariki.

Akiwa katika ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania, Kivukoni jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 23, 2025, Elisha aliwasilisha rasmi tuzo hiyo kwa Bodi kama ishara ya heshima na ushirikiano kati ya wasanii na taasisi hiyo.

“Tuzo hii ni matokeo ya jitihada, ubunifu na kujituma kwa wasanii wetu. Tunampongeza John kwa mafanikio haya na tunamhimiza aendelee kufanya kazi kwa weledi na ubunifu,” alisema Dkt. Kasiga.
Aidha, Dkt. Kasiga aliwataka wasanii wote wa filamu nchini kuhakikisha wanajisajili na Bodi ya Filamu Tanzania, na kuwasilisha kazi zao kwa ukaguzi na vibali ili kujenga sekta ya filamu yenye nidhamu na mazingira bora ya kazi.

“Bodi itaendelea kuwatambua na kuwapongeza wasanii wanaofanya vizuri, pamoja na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za kukuza soko la filamu zetu,” aliongeza Dkt. Kasiga.

Kwa upande wake, John Elisha alishukuru Bodi ya Filamu kwa kumtambua, akisema tuzo hiyo ni motisha kwake na kwa wasanii wengine kuendelea kutangaza utamaduni wa Tanzania kupitia sanaa ya filamu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: