Na Mwandishi Wetu.

Msanii nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Mbwana Yusuph maarufu kama Mbosso, amewashukuru uongozi na mashabiki wa Simba Sports Club kwa kumpa nafasi ya kipekee kuwa headliner wa Tamasha la kihistoria la SIMBA DAY lililofanyika hivi karibuni.

Kupitia barua yake ya wazi aliyoiandika kwenye mtandao wa Instagram, Mbosso alisema uongozi wa Simba SC uliweza kumpa nafasi hiyo adhimu ambayo ingeweza kupewa msanii mwingine yeyote, lakini badala yake walimchagua yeye kuongoza burudani ya tamasha hilo kubwa.

“Kwangu mimi hili ni tamasha langu kubwa la kwanza kufanyia kwenye uwanja linalohusiana na mpira wa miguu katika maisha yangu ya muziki. Ndiyo maana nilijitahidi kwa uwezo wangu wote kuhakikisha nawapa furaha mashabiki na wadau wa Simba SC,” aliandika Mbosso.

Ameeleza kuwa SIMBA DAY kwake haikuwa tu tamasha, bali pia jukwaa la kuonyesha vipaji vyake vingine ambavyo huenda havijawahi kuonekana, ikiwemo kuigiza kwa uhalisia, kuimba na kuwasilisha ubunifu kwa kiwango cha juu.

Aidha, Mbosso alibainisha kuwa licha ya kutumia gharama kubwa kuhakikisha onyesho lake linafanikiwa, hakufanya hivyo kwa faida binafsi bali kwa mapenzi yake makubwa kwa Simba Sports Club na mashabiki wake.

“Nina imani mlifurahi, na kama kulikuwa na sehemu nilikosea au kulikuwa na mapungufu, naomba mnisamehe kwa kuwa mimi ni mwanadamu na siwezi kufanya vyote kwa ukamilifu,” alisema Mbosso huku akimalizia barua yake kwa kutia sahihi ya jina lake la kisanii Mad Max Mbosso Khan.

Tamasha la SIMBA DAY ni tukio la kila mwaka la Simba SC linalokutanisha mashabiki kutoka maeneo mbalimbali nchini, likiwa na lengo la kutambulisha kikosi kipya cha wachezaji na kutoa burudani ya muziki.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: