Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam.

Mashabiki wa urembo nchini sasa watapata fursa ya kipekee kushuhudia safari ya warembo wanaowania taji la Miss Universe Tanzania 2025, kupitia vipindi maalum vinavyotarajiwa kuanza kurushwa leo, Julai 25, 2025, kupitia king’amuzi cha Startimes Tanzania katika Chaneli ya ST Swahili.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kipindi hicho, Mkurugenzi wa Kampuni ya Millen Privé & Co. Lifestyle Bespoke Luxury Lifestyle & Hospitality Management, ambaye pia ni Mwanamitindo wa Kimataifa, Millen Happiness Magese, alisema mwaka huu mashabiki wataweza kuona kwa mara ya kwanza mchakato mzima wa maandalizi ya Miss Universe Tanzania.
“Watu wengi wamekuwa wakiona warembo wanaingia kambini na kutoka bila kuelewa kilichojiri kati ya hapo. Mwaka huu tumeamua kufungua milango. Mtashuhudia jinsi tulivyowachagua, tulivyowafundisha, na namna walivyokuja kuiva mpaka siku ya mwisho,” alisema Millen.

Alibainisha kuwa vipindi hivyo vitatoa nafasi kwa Watanzania kuona kwa karibu namna tasnia ya urembo inavyoendeshwa kwa weledi, nidhamu na maadili ya hali ya juu.

Lengo kuu, kwa mujibu wa Millen, ni kuwapa wananchi uelewa mpana wa mchango wa mashindano ya urembo katika kuibua vipaji, kuhamasisha uthubutu kwa vijana na kuchochea maendeleo ya sekta ya mitindo na burudani nchini.

Mashindano ya Miss Universe Tanzania kwa mwaka huu yanatarajiwa kuvuta hisia za wengi si tu kwa uzuri wa washiriki, bali pia kwa maudhui ya vipindi ambavyo vinajielekeza katika kukuza thamani ya mwanamke, kujenga uwezo binafsi na kukuza taswira ya Tanzania kimataifa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: