●Wanafunzi 200 wapatiwa vyeti baada ya mafunzo ya mazingira

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa ushirikiano na Taasisi ya Mazingira Plus, leo Julai 25, 2025, limekabidhi rasmi Mradi wa Taka Sifuri kwa Shule ya Sekondari Maalum ya Wasichana ya Dar es Salaam, huku wanafunzi 200 wakikamilisha mafunzo na kutunukiwa vyeti.

Hafla ya makabidhiano ilihusisha maonesho ya ubunifu na matokeo ya mafunzo hayo, yakiwemo bustani za kiorganiki, utengenezaji wa mbolea kutokana na mabaki ya chakula, mabanda ya kutenganisha taka, pamoja na kazi za sanaa zilizoonesha athari za uharibifu wa mazingira kwa viumbe hai.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria kutoka NEMC, Bi. Amina Kibola, aliwapongeza wanafunzi kwa kufanikisha mafunzo hayo, akisisitiza kuwa elimu waliyoipata inawapa uwezo wa kuchangamkia fursa za kiuchumi kupitia uhifadhi wa mazingira.

“Mradi huu ni dira ya mabadiliko. Unawajengea vijana uwezo wa kubadili taka kuwa rasilimali kupitia mbinu bunifu na endelevu,” alisema Bi. Kibola. Alisisitiza umuhimu wa dhana ya “Punguza, Tumia Tena na Rejeleza” kama njia ya kupunguza uchafuzi na kuchochea uchumi wa kijani.
Naye Mratibu wa Programu ya Taka Sifuri Mashuleni, Bw. Suleman Mang’uro, aliwataka walimu wa shule hiyo kuhakikisha mradi huo unaendelezwa kwa maslahi ya wanafunzi na mazingira ya shule kwa ujumla.

Mradi wa Taka Sifuri unalenga kujenga uelewa na kuwashirikisha vijana katika utunzaji wa mazingira kupitia mbinu shirikishi, bunifu na zenye tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: