
Na Mwandishi Wetu, Arusha.
Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC imeadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake kwa kuandaa bonanza la michezo jijini Arusha mwishoni mwa wiki, likikusanya wateja, mashabiki wa michezo na familia mbalimbali kusherehekea robo karne ya mafanikio.
Katika shamrashamra hizo, mpira wa miguu ulikuwa kivutio kikuu ambapo timu ya Kuza FC ilitwaa ubingwa baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Kitambi Noma FC. Kapteni wa Kuza FC, Gabriel Mwandembwa, alipokea kombe la ushindi kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Arusha (ARFA), Jame Rugagila.


Mbali na soka, bonanza hilo liliibua burudani nyingine ikiwemo michezo ya video ya FIFA, mashindano ya magari yanayoendeshwa kwa simu, kuvuta kamba, pamoja na mbio za magunia, hali iliyoongeza shamra shamra na kufurahisha washiriki wa rika zote.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Vodacom, George Venanty, pamoja na Meneja Masoko na Mikakati, Hamida Hamad, walibainisha kuwa lengo la kampuni hiyo ni kuendelea kujenga ukaribu na jamii kupitia shughuli za kijamii na burudani sambamba na huduma bora za mawasiliano.



“Sherehe hizi ni sehemu ya kusherehekea safari yetu ya miaka 25 ya kuunganisha Watanzania. Tunataka tuendelee kushirikiana na wateja wetu si tu kupitia huduma za kidijitali, bali pia kwa kutengeneza kumbukumbu za pamoja za furaha na mshikamano,” alisema Venanty.
Vodacom imesisitiza kuwa itaendelea na mfululizo wa matukio ya kusherekea miaka 25 yake katika mikoa mbalimbali nchini, ikilenga kuimarisha uhusiano wa karibu na wateja wake.


Toa Maoni Yako:
0 comments: