Articles by "WAZIRI MKUU"
Showing posts with label WAZIRI MKUU. Show all posts

Na. Mwandishi wetu - Kilimanjaro


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa siku 100 kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Wafanyakazi wa Umma (PSSSF) Ndg. Abdul-Razaq Badru kuhakikisha Awamu ya Pili ujenzi wa kiwanda cha kuchakata Bidhaa za Ngozi Kilimanjaro unakamilika na kuanza kufanya kazi ifikapo Julai 2024.
Agizo hilo amelitoa leo Februari 22, 2024 alipo fanya ziara ya kukagua ujenzi katika kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kilimanjaro International Leather Industries Ltd (KLICL) ikiwa ni sehemu ya kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na serikali kupitia Ofisi hiyo.
Mhandisi Luhemeja amesema kukamilika kwa kiwanda hicho kutaongeza thamani ya zao la ngozi ghafi, kufungua fursa za soko la uhakika la Ngozi kutoka kwa wafugaji, kuongeza ajira kwa vijana na mapato ya fedha za ndani na za kigeni.


Aidha, amefurahishwa na ubora wa bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo na kutoa wito kwa watanzania kuwa na tamaduni za kuthamini bidhaa zinazo zalishwa nchini.


Awali akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Ndg. Abdul-Razaq Badru amesema amepokea maagizo hayo ya Katibu Mkuu Mhandisi Luhemeja na kuahidi kuwa PSSSF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza watahakikisha wanafanya kazi kwa weledi kama ilivyo elekezwa ili watanzania waanze kunufaika na mradi huo.


Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho Mhandisi Saiba Edward amesema mradi huo pamoja na mambo mengine, utaongeza kipato kwa wakazi wa Kilimanjaro na Mikoa jirani kupitia fursa za uzabuni, uwakala na usambazaji wa bidhaa.


Kwa upande wake Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Magereza Frank Mwakijungu amebainisha kuwa Magereza ni mbia wa utekelezaji wa Mradi huo hivyo watasimamia ujenzi wa kiwanda hicho ili kikamilike kwa wakati kwa manufaa ya watanzania.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhandisi Cyprian Luhemaja (kushoto) akikagua bidhaa zinazozalishwa na Kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kilimanjaro International Leather Industries Ltd (KLICL) leo Februari 22, 2024 ikiwa ni mwendelezo wa kukagua miradi inayotekelezwa na serikali kupitia Ofisi hiyo.




















Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa wakati alipokagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) ya Dodoma katika eneo la Mkonze jijini Dodoma
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa (kulia) wakati alipokagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) ya Dodoma katika eneo la Mkonze jijini Dodoma,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) iliyopo eneo la Mkonze jijini Dodoma,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRC, Profesa John Kondoro (kulia) wakati alipokagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) katika eneo la Mkonze jijini Dodoma
Baadhi ya mafundi waoshiriki katika ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR) katika eneo la Mkonzi jijini Dodoma wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao baada ya kukagua ujenzi huo,
Muonekano wa Jengo la Makao Mkuu ya Shirika la Reli Tanzania TRC jijini Dodoma ambalo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua ujenzi wake, Novemba 24, 2022. Mheshimiwa Majaliwa pia alikagua ujenzi wa Setesheni Kuu ya Reli ya Kisasa SGR katika eneo hilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongoza Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongoza Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 06 Septemba, 2022.

PICHA NA IKULU
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akifuatilia Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) unaoendelea katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Palais des Congres mjini Tunis,Tunisia, Agosti 27, 2022. Waziri Mkuu anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Tunisia Kais Saied alipowasili katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Palais des Congres kuhudhuria Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8), mjini Tunis,Tunisia, Agosti 27, 2022. Waziri Mkuu anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana na Rais wa Tunisia Kais Saied alipowasili katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Palais des Congres kuhudhuria Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8), mjini Tunis,Tunisia, Agosti 27, 2022. Waziri Mkuu anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
---
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemshukuru Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida kwa misaada ambayo nchi yake inaipatia Tanzania ili kuleta unafuu kwenye maisha ya wananchi wake.

“Tanzania tunaishukuru sana Serikali ya Japan kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwakwamua wananchi wake kiuchumi na kuwezesha ujenzi wa miundombinu hadi vijijini,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Agosti 27, 2022) wakati akizungumza naye kwa njia ya mitandao kwenye ukumbi wa Palais des Congres, jijini Tunis, Tunisia. Mheshimiwa Kishida ameshindwa kuhudhuria mkutano kwa sababu ya maambukizi ya UVIKO 19.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye anamwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa TICAD ulioanza leo, alimweleza Waziri Mkuu huyo kwamba Tanzania bado inaomboleza na wananchi wa Japan kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Shinzo Abe na akatumia fursa hiyo kuwapa pole.

Akigusia miradi ambayo Serikali imeisaidia Tanzania, Waziri Mkuu amesema: “Iko miradi mingi ambayo imetekelezwa na Japan kupitia taasisi ya JICA, wako wawekezaji wanafanya biashara nasi na pia yako makampuni ambayo yamejitoa kusaidia sekta muhimu.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuiomba Japan ikamilishe ahadi yake ya kutekelza miradi waliyoiahidi kwenye mkutano wa TICAD 7 ambayo inahusu ujenzi wa barabara ya Arusha mpaka Holili mkoani Kilimanjaro, mradi wa maji wa Zanzibar, ujenzi wa bandari ya Kigoma na bandari ya uvuvi Zanzibar.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan, amemtumia salamu Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote na akataka uhusiano wa nchi hizo mbili kupitia taasisi yao ya JICA.

Mapema, akitoa tamko kwa niaba ya Rais Samia kwenye mkutano huo wa wakuu wa nchi na Serikali, Waziri Mkuu alisema bara la Afrika linakabiliwa na matatizo ya kiuchumi ambayo kwa kiasi kikubwa chimbuk lake ni UVIKO 19.

“Nimewaeleza madhara ya UVIKO 19 ambayo yanaikumba Afrika Tanzania ikiwemo, matatizo ya vita ya Ukraine na Urusi ambavyo vimesaabisha bei za bidhaa nyingi kupanda. Nimewaambia ujko umuhimu wa mataifa makubwa ya G20 kuungana na Japan ambayo ni ya tatu kwa ukubwa kiuchumi ili kuzisaidia nchi za Afrika.”

Amesema iko haja ya kuziwezesha nchi za Afrika kujitegemea ili ziweze kuwasaidia wananchi wake kupata fursa za elimu, kujenga uweza wa shughuli za kilimo, utalii ili waweze kukuza uchumi wao.

Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Rais Tunisia, Mhe. Kais Saied ambapo Rais wa Senegal, Mhe. Macky Sall alitoa hotuba ya ufunguzi na Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Kishida Fumio akahutubia kwa njia ya mitandao kutokea Japan.

Pamoja na masuala mengine, mkutano huo wa siku unatarajiwa kukubaliana kuhusu namna ya kuiwezesha Afrika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Dunia ili kuiwezesha kufikia Agenda ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika (Agenda 2063).

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na janga la UVIKO 19, amani na usalama, mabadiliko ya tabia nchi, upatikanaji mgumu wa malighafi na mfumuko wa bei kwa bidhaa zinazotegemewa na nchi za Afrika kama vile gesi, mafuta na pembejeo za kilimo ambazo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Bara la Afrika.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inatambua mchango wa michezo shuleni, hivyo itaendelea kuhamasisha ufundishaji wa michezo katika shule za msingi na sekondari ili kuibua vipaji vipya vya michezo nchini.

Amesema katika kuwaandaa vijana kuwa na afya bora ya akili na mwili, Mheshimiwa Rais Samia ameahidi kuwa Serikali anayoiongoza itaendelea kuimarisha na kuongeza miundombinu ya shule pamoja na mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari.

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Alhamisi, Agosti 4, 2022) wakati akizindua mashindano ya Michezo na Taaluma kwa shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) wanafunzi, yanayofanyika katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mkoani Tabora.

“Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya michezo katika shule teule 56 nchini ikiwa ni wastani wa shule mbili kwa kila mkoa. Nimefurahi kuona utekelezaji wa mradi huu kwa mkoa wa Tabora tayari umeanza katika Shule za Sekondari Tabora Wavulana na Tabora Wasichana na viwanja vilivyojengwa vitatumika katika mashindano ya mwaka huu 2022.”

Amesema ujenzi wa miundombinu ya michezo utafanyika kwa awamu katika shule nyingine ili kuhakikisha kunakuwa na shule zenye miundombinu bora ya kuwezesha wanafunzi kusoma somo hilo kwa nadharia na vitendo. “Lengo ni kuzalisha wataalamu watakaobobea katika eneo hili la michezo.”

Amesema pamoja na ujenzi wa viwanja, Serikali itajenga kumbi kubwa katika shule hizo zitakazotumika kwa kazi za sanaa na michezo ya ndani. “Sambamba na hayo, Serikali imeendelea kuajiri walimu wa michezo ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 walimu wa michezo 83 wameajiriwa.”

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa michezo na utamaduni katika ukuaji na maendeleo ya wanafunzi kiakili na kijamii, kwa sababu michezo na sanaa ni miongoni mwa stadi muhimu zinazochangia ukuaji wa kiuchumi na kijamii ikiwemo kutengeneza fursa za ajira.

“Ni jukumu letu kuhakikisha kuwa tunajenga msingi imara wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa somo la elimu kwa michezo ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa vipaji vya michezo kwa wanafunzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari hadi vyuo vya elimu ya juu.”

Ili kufanikisha azma ya kuboresha michezo na taaluma nchini, Waziri Mkuu amewaelekeza viongozi wa elimu katika ngazi ya shule, kata, shehia, Halmashauri na Mkoa wafuatilie ufundishaji na ujifunzaji shuleni na kushauriana na walimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata umahiri uliokusudiwa kwa masomo yote badala ya kukaa muda mwingi ofisini.

“Kila mwalimu ahakikishe anajiwekea malengo yake binafsi katika masomo anayofundisha na kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayeshindwa kupata umahiri uliokusudiwa katika somo lake ifikapo mwishoni mwa kila mwaka.

Pia, Waziri Mkuu ameagiza uteuzi wa viongozi wanaopewa dhamana ya kusimamia Elimumsingi na Sekondari katika ngazi za Shule, Kata, Shehia, Halmashauri na Mkoa uzingatie umahiri, weledi, ubunifu na uzoefu kama ilivyobainishwa kwenye mwongozo waliouandaa.

Mbali na kufungua mashindano ya michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwa mwaka 2022, Waziri Mkuu pia amezindua vitabu vya miongozo na mikakati kwa ajili ya kuboresha elimu nchini inayolenga kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoathiri sekta ya elimu na kuongeza uelewa wa pamoja.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, David Silinde amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya kugharamia michezo hiyo na kwamba ofisi yake itahakikisha inafanyika kwa ufanisi mkubwa.

Naye, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul amesema katika kuhakikisha elimu kwa michezo inaendelea kutolewa vizuri shuleni Serikali imetenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya michezo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akipokea Maandamano ya Wanamichezo wanaoshiriki Mashindano ya UMITASHUMTA mwaka huu 2022 leo Agosti 04, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora, alipowasili kuzindua mashindano hayo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Julai 27, 2022 amezungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Nchini Marekani (CDC) Dkt. Rochelle Walensky (kulia kwake) alipokutana nae Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam
Katika mzungumzo hayo Mheshimiwa Majaliwa amemuhakikishia Dkt. Walensky kuwa Tanzania itaendelea kukipa ushirikiano Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Nchini Marekani (CDC)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa Mkoa na Wilaya za Mkoa wa Lindi wakati alipowasili kwenye uwanja wa Ndege wa Nachingwea akielekea Ruangwa, Desemba 28, 2021. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Ampongeza Rais Samia kwa kutafuta fedha hizo kwa bidii

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameridhishwa na hatua iliyofikiwa kwenye ujenzi wa madarasa yanayotokana na fedha za maendeleo mkoani Lindi.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Desemba 28, 2021) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa huo kwenye uwanja wa ndege wa Nachingwea mara baada ya kupokea taarifa ya kila wilaya.

“Nimefurahi kusikia kuwa kuna maeneo kazi imekamilika kwa asilimia 100, wilaya nyingine zimefikisha asilimia 97, nyingine asilimia 75, na kikubwa zaidi ni kuweza kubakiza fedha baada ya kazi kukamilika,” amesema.

“Wilaya moja imebakiza shilingi milioni 35, nyingine shilingi milioni 33, na nyingine zaidi ya shilingi milioni 10. Hii ni dalili njema kwamba kazi hii ilisimamiwa vizuri, nawapongeza viongozi wote wa mkoa na wilaya, na pia wananchi waliojitokeza kuchangia nguvu kazi yao.”

Waziri Mkuu amemshukuru Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kutafuta fedha hizo ambazo zimekuwa mkombozi mkubwa kwenye kutatua changamoto mbalimbali katika huduma za kijami.

“Kwa fedha hii ambayo Mheshimiwa Rais ametumia jitihada kubwa kuzitafuta, na tumezipata tena kwa masharti nafuu, ni lazima tuzitumie ipasavyo. Nimefurahi sana kusikia nyie mmetumia vizuri fedha zenu kujenga madarasa na zimebaki.”

Waziri Mkuu amesema kutokana na mfano uliooneshwa na mkoa wa Lindi, anataraji kusikia mikoa mingine pia ikiwa imekamilisha kazi na fedha zimebakia hasa kwenye mikoa ambayo malighafi na vifaa ni rahisi ama haitoki mbali.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na viongozi wa Serikali na CCM wa mkoa na wilaya za mkoa huo, Mkuu wa Mkoa Lindi, Bibi Zainab Tellack alisema hatua za ujenzi uliobakia ni hatua za kumalizia kuweka madawati, nyingine kupakaa rangi na chache sana ni kuezeka.

Alisema licha ya kazi kubwa iliyofanyika, baadhi ya wilaya zimebakiza fedha lakini nyingi zimebakiza vifaa vya ujenzi kama nondo, saruji na rangi. “Tunataka tuombe kibali maalum cha kutumia hizi fedha zilizobaki na vifaa vilivyobakia ili kuboresha miundombinu kwenye maeneo mengine,” alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Bw. Shaibu Ndemanga alisema alipokea sh. bilioni 2.26 ambapo kati ya hizo, sh. bilioni 1.1 zilikuwa ni za ujenzi wa madarasa 56 katika Manispaa ya Lindi na mengine 58 katika Halmashauri ya Mtama kwa thamani ya sh. bilioni 1.16.

“Katika Manispaa ya Lindi, tulikuwa na madarasa 35 ya shule za sekondari na madarasa 21 ya shule shikizi. Yote yameshakamilika kwa maana ya kuwekewa gypsum, marumaru na madirisha ya aluminium. Tumebakiza sh. milioni 35,” alisema.

Alisema katika Halmashauri ya Mtama madarasa 27 kati ya 58 yamekamilika kabisa na 31 yaliyobakia yako kwenye hatua tofauti. Alisema hapa hawajafikia hatua ya kubaini kiasi cha fedha kitakachobakia hadi wamalize kabisa kazi ya ujenzi na kuweka madawati madarasani.

Wilaya nyingine iliyofikisha asilimia 100 ya ujenzi ni ya Nachingwea. Wilaya hiyo ilipokea sh. bilioni 1.1 kwa ajili ya madarasa 69 ambapo madarasa 57 ni ya sekondari na 12 ni ya shule shikizi. Wilaya hiyo imebakiwa jumla ya sh. milioni 33.7.

Wilaya ya Liwale bado haijakamilisha sababu ya changamoto ya umbali lakini Mkuu wa wilaya hiyo ameahidi kuwa atakamilisha kabla ya Desemba 31, mwaka huu kama ilivyoelekezwa na Serikali.

Wilaya ya Kilwa ilipokea sh. bilioni 2.06 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 103 ambapo madarasa 28 yamekamilika kwa asilimia 100 na yaliyobakia yako kwenye asilimia 75 ya ujenzi wake.

Waziri Mkuu amewasili jimboni kwake Ruangwa kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara, tawi la Mbeya katika eneo la Iganzo jijini humo, Novemba 30, 2021. Wa pili kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujezi wa Chuo cha Elimu ya Biashara tawi la Mbeya katika eneo la Iganzo jijini humo, Novemba 30, 2021. Kulia kwa Waziri Mkuu ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homela.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujezi wa Chuo cha Elimu ya Biashara tawi la Mbeya katika eneo la Iganzo jijini humo
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye eneo kinapojengwa Chuo cha Elimu ya Biashara tawi la Mbeya , eneo la Iganzo jijini humo kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo hicho, Novemba 30,2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Azitaka taasisi zinazokusanya mapato ziweke mipango endelevu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi zote zinazokusanya mapato nchini zihakikishe zinaweka mipango endelevu itakayoziwezesha kusimamia matumizi ya mapato hayo kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kusimamia taasisi zote zinakusanya mapato na kuweka mifumo imara ya kusimamia matumizi yake.

Ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Novemba 30, 2021) baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Mbeya. Mradi huo unajengwa katika kata ya Iganzo jijini Mbeya unagharimu sh. milioni 852.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha inaweka mipango madhubuti na usimamizi sahihi wa biashara na wafanyabiashara ili waweze kunufaika zaidi na shughuli wanazozifanya.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa uongozi wa chuo cha CBE uendelee kuweka mipango ya kuwafikia wanyabiashara wa ngazi zote na hata wale ambao hawajaanza kufanya biashara ili waweze kuwatoa uoga wa uanzishaji wa biashara.

“…CBE endeleeni kuweka mpango mzuri wa kuwafikia na kuwapa elimu ya biashara wafanyabiashara wakubwa, wakati na wadogo ili kuwawezesha kufahamu namna bora ya kuzifanya biashara zikue zaidi na kuongeza tija.”

Amesema katika kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi, Serikali iliwaagiza viongozi wa Serikali za Mitaa kwa kushirikiana nao watafute maeneo mazuri na kuyawekea miundombinu muhimu.

Naye, Mkuu wa Chuo cha CBE, Profesa Emmanuel Mjema amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Juni mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu, ambapo chuo hicho kimetoa sh. milioni 502 na Serikali Kuu imetoa sh. milioni 350 kwa ajili ya ujenzi huo.

Amesema Chuo cha CBE kampasi ya Mbeya kilianza mwaka 2013 kikiwa na wanafunzi 44 na sasa kina wanafunzi 947. Ongezeko hilo linaonesha kuwa chuo hicho kinaendelea kuaminika zaidi katika utoaji wa elimu ya biashara na ujasiriamali nchini.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amefungua kiwanda cha Raphael Group cha kuongeza thamani zao la mpunga na mazao mengine kilichopo katika eneo la Uyole jijini Mbeya na kumpongeza mwekezaji huyo kwa hatua hiyo.

“Nampongeza Mkurugenzi wa kiwanda hiki Bw. Raphael Ndelwa kwa kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Samia za kuhamasisha uwekezaji sambamba na ujenzi wa viwanda ili kuwezesha bidhaa mbalimbali kuzalishwa nchini.”

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa taasisi za Serikali zinazojihusisha na sekta ya uwekezaji kutowasumbua wawekezaji bali wawaelimishe na kuwasaidia ili waweze kukuza zaidi shughuli zao. “Wawekezaji hawa wanaweka pesa nyingi sana kwenye eneo hilo, ni lazima tuwaunge mkono.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw. Ndelwa amesema kampuni yao inafanyakazi kwa mfumo wa kilimo cha mkataba na wakulima zaidi ya 14,000 ambao kati yao 7,800 wamejiajiri katika kilimo cha mpunga na 5,800 wanalima maharage.