Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameunda Tume Huru ya kufanya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025. Hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi leo, Novemba 18, 2025, imeeleza kuwa Rais Samia amemteua Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman, kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Aidha, wajumbe walioteuliwa kushiriki katika Tume hiyo ni:
• Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania;
• Balozi Ombeni Yohana Sefue, Mwanadiplomasia na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu;
• Balozi Radhia Msya, Mwanadiplomasia na Balozi Mstaafu;
• Balozi Lt. Gen. Paul Meela, Mwanadiplomasia na Balozi Mstaafu;
• IGP (Mstaafu) Said Ally Mwema, Mkurugenzi Mstaafu wa Jeshi la Polisi;
• Balozi David Kapya, Mwanadiplomasia na Balozi Mstaafu;
• Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax, aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa SADC.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tume ina dhamana ya kuchunguza kwa kina chanzo na mwenendo wa matukio yote yaliyosababisha uvunjifu wa amani, pamoja na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kurejesha na kuimarisha utulivu wa Taifa.
Taarifa hiyo imetolewa na Balozi Dkt. Moses M. Kusiluka, Katibu Mkuu Kiongozi.



Toa Maoni Yako:
0 comments: