Nairobi. Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dkt. William Ruto, amemtunuku mwanaharakati wa mazingira Truphena Muthoni Medali ya Head of State Commendation (HSC) kwa mchango wake wa kipekee katika kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Tuzo hiyo imetolewa kufuatia hatua ya kihistoria ya Muthoni ya kutumia saa 72 mfululizo akikumbatia mti wa asili, tukio lililovunja rekodi na kuvutia hisia za kitaifa na kimataifa kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira.
Rais Ruto alisema alifurahishwa na ujasiri, uthubutu na dhamira ya dhati aliyoionesha Muthoni, akieleza kuwa vitendo vyake vinaakisi roho ya uzalendo na uongozi unaohitajika katika kukabiliana na changamoto za mazingira.
“Hatua yake ni ujumbe mzito kwa dunia nzima kuhusu wajibu wetu wa kulinda mazingira kwa vizazi vijavyo,” alisema Rais Ruto.
Katika kutambua mchango huo, Rais amemteua Truphena Muthoni kuwa Balozi wa Kampeni ya Kitaifa ya Kupanda Miti Bilioni 15, mpango mahsusi wa serikali unaolenga kurejesha misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini Kenya.
Aidha, Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya (KWS) kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Kenya (KTB) limempa Muthoni pamoja na timu yake likizo iliyodhaminiwa kikamilifu kama sehemu ya kuthamini juhudi zake za kuhamasisha jamii.
Wakati huo huo, Wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu imetangaza kuunga mkono ndoto ya Muthoni ya kutembelea Brazil ili kupata uzoefu wa kimataifa kuhusu uhifadhi wa mazingira na uongozi wa kimazingira.
Hatua ya serikali kumuenzi Truphena Muthoni inaonesha dhamira ya Kenya ya kuwa mstari wa mbele katika mapambano ya kulinda mazingira, huku ikiendelea kuhimiza ushiriki wa vijana katika kulinda rasilimali za taifa.








Toa Maoni Yako:
0 comments: